RAIS THOMAS JEFFERSON, wa
Marekani(1801-1809) aliposhambuliwa sana na magazeti, wakati wa Awamu yake ya
Tatu ya utawala wa Taifa hilo kubwa duniani, alisema hivi:
“Mtu asiyechungulia
kabisa katika kurasa za magazeti ,yu na taarifa sahihi kuliko anayesoma
magazeti hayo kila siku. Maana yake ni kwamba, asiyejua chochote yu jirani na
ukweli, ukilinganisha na yule ambaye akili zake zimejazwa uongo na upotovu”.
Hii ni barua ya Rais
Jefferson, kwa John Norvell, Juni 14, mwaka 1807.
Hapa, nakusudia kusema kwamba, mtu mzito
sana katika nchi inayoongoza kwa demokrasia duniani, na uhuru wa vyombo vya
habari, akavilaumu na kuvilaani sana vyombo hivyo, kwamba heri visingekuwepo
aslani.
Mwahahistoria wa
Kiingereza, Thomas Babington Macaulay, ndiye aliyevibatiza vyombo vya habari
wadhifa mtukufu wa “MHIMILI WA NNE WA DOLA”.
Vyombo vinavyolalamikiwa kuwaongezea
mahluki ujinga, hadi watu wakubwa namna hii wakasema, ‘Heri visingekuwepo’!
Ni vyombo hivi vinavyowapigia debe
wakubwa kuingia kwenye ulaji, halafu vinapoanza kuwaponda.vinageuka ‘Shetani’
kheri visingekuwepo duniani?
Spika wa zamani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Samwel Sitta, na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo wa zamani, George Mkuchika,
zamani kidogo walilaumu baadhi ya magazeti(siyo Mwanahabari), kana
kwamba ingekuwa heri wananchi kutojua kitu chochote, kuliko kuyasoma magazeti
hayo,ili kujazwa ujinga!
Sitta na Mkuchika
wanakubaliana na Thomas Jefferson kwamba,
“The man who never looks into newspapers is better informed than who
reads them inasmuch as who knows nothing is nearer the truth than he whose mind
is filled with falsehood and errors”.
Yapo mambo
yaliyoandikwa na magazeti ,yametia ukakasi katika vichwa vya mihimili mingine
ya Dola, yaani Bunge na serikali.
Bila shaka magazeti hayo yalibeba
ajenda za wahariri na wamiliki wake, waandishi na zaidi sana yalitafuta
kupambana na matatizo binafsi ya kisiasa(political problems) zaidi ya
kufahamisha na kuelimisha umma.
Lakini, wakubwa huwa hawataki
kuelezwa udhaifu wao,wanataka sifa tu.
Waziri mwenye
dhamana ya Habari, wakati huo George Mkuchika, alitishia kutumia ‘rungu’ alilopewa na Katiba
kutaka kufungia magazeti hayo.
Hata siku hizi za akina Fenela
Mkangala,magazeti yalishafungiwa,yanagugumia kwa maumivu,ingawa mwanzoni mwa
Kikwete yalisemwa kumlamba miguu rais!!
Kufungia vyombo vya habari?
Kwa sababu, kufanya hivyo si
kuchimbua mizizi ya tatizo la ukiukwaji wa maadili ya taaluma ya Uandishi wa
Habari nchini. Ni kufukia uoza usionekane, tena kuahirisha riha mbaya ya
uandishi isifike puani mwa wasomaji.
Lipo tatizo la msingi
la baadhi ya watu wanaotuhumiwa kuhusika na ufisadi, kwamba wamesajili magazeti
yao ili yafunike madhambi yanayosemwa sana juu yao .
Ushahidi unaoonekana ni
kwamba baadhi ya magazeti siku hizi yamekuwa yakimshambulia mtu mmoja kiasi
kwamba ni nadra kukuta ‘Maslahi ya Taifa’ ndani ya mashambulizi hayo.
Nachelea kumuunga mkono
Mfanya biashara, Reginald Mengi, na kauli zake kwamba, ‘Mafisadi wameanzisha
vipeperushi’ ili kumshambulia, kwa sababu hata yeye mageti yake ya Taifa
Letu na Sema Usikike, yametajwa na Waziri Mkuchika kuandika habari
zinazotia kichefuchefu!
Sina hakika kama
wakati ule ofisi ya Waziri Mkuchika ingeweza kuingia mkenge, ikasajili
vipeperushi zaidi ya magazeti, wakati kuna sheria, kanuni na taratibu za
kusajili magazeti.
Sheria hizo huainisha magazeti, vipeperushi,
majarida n.k
Niunge mkono hoja
kwamba yapo magazeti yaliyoanzishwa karibuni, yana lengo la kunyamazisha kelele
za umma dhidi ya ufisadi na mafisadi kwa njia ya kutangaza ‘Privacy’ za watu,
ili wasahahu kwamba kuna mafisadi.
Mengine huanzishwa na wanasiasa
kuelekea 2015.kazi ni kuudanganya umma na kuwachafua adui zao wa mapambano ya
siasa.
Magazeti ya kale
yamekuwa yakiandika kwamba kuna watu wanatumia vibaya madaraka waliyopewa,
wanakiuka maadili ya uongozi na kutumia vibaya rasilimali za umma.
Wakati, magazeti ya sasa
yanajaribu kutwambia kwamba wapigao kelele sana dhidi ya ufisadi ni ‘mabingwa
wa kuoa na kutaliki’; tena wapo vigogo ni ‘manchampioni’ wa kuwaweka kinyumba
wanaume wenzao, naam mashoga!
Bila shaka hivi ni vita
kati ya mtu na mtu, kati ya kundi moja na jingine.Yapo magazeti hayana
ajenda,ila kutangaza pumba,yanaapisha!
Hata hivyo, wapigao ‘panda sana ’ hawana
tofauti kubwa sana na kigenge cha matapeli, ambao licha ya kuendesha kampeni
dhidi ya wapigao kelele dhidi ya ufisadi, huwadhulumu sana waandishi; huwapiga
‘danadana’ kila kunapokucha.
Vyombo vya habari
vina jukumu begani mwake kufichua uovu na uhalifu. Vyombo hivi ni Kioo cha
Jamii.
Kazi ya kioo ni kuonesha uso ama
sura ya mtazama kioo.Kukosoa kwa nia ya kujenga Taifa imara na safi.
Kioo hakimsingizii mtu
makasoro yake. Kioo hakimsemi mtu kwamba ana kunyanzi ama udelele na madevu
mithili ya shamba la Miwa la Kilombelo, wakati hana.Kioo hakiwezi kusema kwamba
Shetani ni Mungu na Mungu ni Shetani ama Obama ni Osama, ingawa majina yao
hufanana na hulingana kasoro herufi ‘B’ na ‘S’ katikati ya majina yao.
Vyombo vya habari hutakiwa kuwa
makini na wakweli na walinganifu.
Kazi ya kioo ni kusema
ukweli kama fisadi anayo matongotongo, udelele, makunyanzi na hata midevu
inayotisha watoto na kuonja michuzi.
Mtazama kioo, awe na
udelele, tongotongo, makengeza ama makunyanzi, hapaswi kukasirika na kukivunja
kioo chake pindi kimwonyeshapo taswira ama mwonekano wake. Anapaswa kutumia
maji na sababuni kujitakasa.
Mafisadi hawataki
kujitakasa ili waonekane safi mbele ya kioo na mbele ya jamii.
Wanavunja kioo halisi, kisha
hutengeneza vioo feki na bandia ili kuwageza wananchi kuona makengeza na
maruweruwe!
Nataka kusema kwamba,
wakati maadili ya uandishi wa Habari yanataka habari ziwe ‘Objective, Fair na Accurate', siku hizi twasoma habari za
kushambuliana, kutetana na kulumbana wenyewe kwa wenyewe.Tunasoma
ushabiki mwingi. Upuuzi,vita uongo na chuki na uchimvi hasa kwenye mitandao ya
kijamii.
Zaidi sana , twasoma
‘kati kati ya mistari’ wamiliki wa magazeti hayo wakimwagiana uvumba, matusi na
fitina ili kuvuana nguo na kubakizana utupu-uchuro na mambo ya kijingajinga!
Tunauliza:
“How can they balance
freedom of the press with the rights of individuals to privacy and their good
names?”
Lini uhuru wa Habari
ulifikisha mwisho Haki za watu zinakoanzia, hadi tuambiwe mambo ya kupigana
denda wakati hayahusiani kabisa na ajenda ya wizi wa mali ya umma?
Waama, huu
uandishi wa ‘sensationalism’ na vita
dhidi ya mtu na mtu au kundi moja linalojidai safi dhidi ya jingine linaloitwa
fisadi, faida yake nini kwa umma wa Watanzania?
Heri magazeti haya
yasingekuwepo, kama alivyosema Rais wa Tatu wa Marekani, Thomas Jefferson..
Mhimili wa nne wa
Dola(vyombo vya habari) una dhima ya kuonyesha makosa ya watu na serikali yao
katika kujiletea mafanikio. Vyombo hivi vifanyapo kazi sawa sawa ni kama
kioo cha kuonyesha watu wapi wana mapungufu, ili wayarekebishe.
Naam, vyombo vya habari ni
sawa na kioo kikubwa ukutani, ambacho watu wote wan chi hupita kujitazama.
Ni aibu kundi
Fulani la watu( sijui ndiyo mafisadi kweli) wanapojitazama katika kioo hiki
kilichopo njia kuu, hubaini tabia zao chafu, lakini badala ya kujisafisha
udelele na tongotongo, huwaleta mafundi vishoka ili wakavunje kioo
kinachoonyesha makunyanzi na makengeza yao na kutengeneza vioo vipya
vipya feki.
Lengo ni kuwachanganya
watu wasione makunyanzi na matongotongo yao ? Lengo ni kuifanya jamii ya
Tanzania iwe makengeza?
Nakusudia kusema
kwamba, hawa hawana nia nyingine ila kutaka umma wa Watanzania useme kwamba
vyombo vya habari vya Tanzania (kioo cha jamii) havina maana kwa kuwa vimejitia
unajisi na vinachafua watu badala ya kuonyesha kasoro.
Watu hawa, wanataka
umma wa Watanzania uone kwamba ni heri kutosoma magazeti kabisa kuliko kuyasoma
na kujazwa ujinga!
Kwamba, eti mawaziri wetu
wakuu wanapostaafu, hujitwalia madume menzao kuwa ‘vimada’ wao; kwamba Tanzania
kuna ma “Retired” PM(But not tired) viwembe 'Chapa mamba' katika ngono za
jinsia moja! Uchuro.
Nazungumzia
ulazima wa kuwepo ama kutokuwepo kwa vyombo vya habari, kama habari zenyewe
zinatia ukakasi kiasi cha macho kupatwa kiwi na meno kuota ganzi!
Thomas Jefferson, kabla ya
kuwa Rais wa Marekani alimwandikia barua Kanali Edward Carrington, Januari 16,
mwaka 1787 kusema, angepewa kuamua kuhusu kuwepo au kutokuwepo vyombo vya
habari asingesita kuchaguwa kuwepo kwa vyombo vya habari hata mahali ambapo
hakuna serikali.
Vyombo vya habari
vifanyavyo kazi sahihi ni muhimu kuliko serikali.
Ewe Fisadi, unapovunja ‘Kioo’ nani
akuoneshe udelele wako? Tatizo siyo kioo, ni udelele na ufisadi(uchafu) wako.
Je, kioo bora kisiwepo ili udelele wako usionekane?
Vyombo vya habari(kioo)
ni muhimu kuonyesha uchafu wa mafisadi, ili wajisahihishe.Waache kujenga chuki
dhidi ya kioo kionyeshacho makunyanzi na udelele wao.
0786/0713-324 074
No comments:
Post a Comment