Sunday, December 30, 2012

AFRIKA INGALI UTUMWANI

MACHI 6 mwaka huu mpya 2013,Ghana itatimiza miaka 56 ya Uhuru,wa nchi ya kwanza Afrika kupeperusha bendera yake,baada ya kushusha  ile ya Ukoloni wa Kiingereza, Union Jack.
     MACHI 6 mwaka 1957; yaani takriban  miaka 56 kamili iliyopita, Taifa Jipya la kwanza Afrika, Ghana, lilizaliwa.
     Koloni la Waingereza lililojulikana kama Pwani ya Dhahabu(Gold Coast) likapata uhuru, na kuitwa Ghana.
    Ghana, ni jina lililotokana na Ufalme wa kale wa watu weusi, uliowahi kufanikiwa sana Afrika Magharibi, kati ya mwaka 1000AD hadi katika Karne ya 15.
 Hivyo, Ghana ni nchi ya mwanzo ya  watu Weusi katika Jumuia ya Madola, Commonwealth.Hii ni Jumuiya ya kikoloni,inayozifanya nchi 54 duniani kudhani zingali chini ya ukoloni wa Malkia,watoto wake akina Prince Phillip,na wajukuu zake,Harry na William.
     Nchi hii hujumuisha Koloni la zamani la Pwani ya Dhahabu, Ashanti, na iliyokuwa Mamlaka ya Kaskazini na Togo ya enzi ya Ukoloni wa Kiingereza.
Eneo lake ni maili za mraba 92,098,sawa na kilomita za eneo 238,533; katika Ghuba ya Guinea.
    Ghana ni maarugu katika historoia ya mtu mweusi Duniani, kufuatia Falme kama Ashanti, uliokuwa na lugha yake(Akan), huku watu wake wakishikilia tamaduni zao bila kukengeuka ama kugeuzwa na tamaduni za wageni, zikiwemo mila za kishenzi za Wazungu, kama inavyoonekana leo, takriban miaka 56 ya uhuru wa Bara zima hili.
Kichekesho:Siku hizi, eti Ashanti,badala ya kuwa Dola ya Mtu Mweusi,huko Ghana, ni Kampuni ya Mzungu ya uchimbaji wa dhahabu ambayo hata hapa Tanzania humiliki migodi ya dhahabu!
      Mfalme wa Ashanti, Asantehene,alama kuu ya mamlaka yake(ya Ufalme wa Ashanti) ilikuwa kigoda cha dhahabu.
Kigoda chenyewe kilifanana kama sahani ya dhahabu, na aghalabu, Asantehene hakupenda kukikalia. Mji mkuu wa Ufalme huu ulikuwa Kumasi.
       Naam, fahari ya Taifa huru la kwanza Afrika ilikuwa utajiri wa Dhahabu inayoburuza hata sasa thamani ya Fedha katika masoko ya Dunia, ama katika Mashirika ya Kimataifa kama   IMF, Benki ya Dunia(WB), Shirika la Biashara(WTO) iwe Marekani, katika Umoja wa Ulaya na popote pengine.
    Lakini, miaka 56 baada ya Uhuru, Ghana na mataifa mengine yenye dhahabu nyingi(ikiwemo Tanzania) ni masikini kupindukia!
    Ghana pia ina wanyamapori wengi, pamoja na nyoka na kima wanaovutia watalii.Mto Volta una mamba na viboko. Kuna samaki wengi katika maji ya Pwani ya Atlantic, kama ilivyo Tanzania, katika maziwa na Bahari.Lakini nchi hii ni watu wake bado ni fukara hata miaka 56 baada ya Uhuru.
      Watu wangali wakiishi katika vibanda vya udongo, ingawa kuna samaki, miti, madini,bahari, mito,  na ardhi yenye rutuba yenye kuzalisha mazao ya biashara na chakula.
  Wapo wafanyabishara, matajiri wenye viwanda na maduka ya Kimataifa(Shopping Malls) miongoni mwa masikini wenye vibanda vya udongo; vya mviringo-tembe.
 Vibanda hivi vimemea mithili ya uyoga kote vijijini.Je, katika Tanzania, hizi  siyo nyumba za masikini katika vijiji vya ujamaa?
   Na kilimo,ufugaji, uvuvi usio endelevu na umachinga, sasa ndizo shughuli za wazalendo tangu Ghana hadi hapa Tanzania.Ukiona majumba ya fahari na miradi yenye kumereremeta,unajua kama si ya wageni,basi inamilikiwa kwa ubia na makampuni ya kikoloni ama makaburu wa zamani wa Afrika ya Kusini.
    Miaka michache tu baada ya kufumuka kwa utapeli wenye ‘Utandawizi’ ujulikanao kama utandawazi wa soko huria(Common Market) kwa matajiri na masikini, wazalendo waliokuwa  wachimba madini kwa zana duni, wamefulushwa hata kwa mtutu wa bunduki, ili kuwapisha wawekezaji-Wazungu-katika migodi!
     Leo Afrika, miaka 56 baada ya Uhuru, vijana wengi wametimkia mijini, baada ya vijiji kutelekezwa. Huko wanatafuta japo kufanya umachinga ili kuboresha maisha. Wamekimbia kilimo, uvuvi,na ufugaji usio na tija vijijini, ili kubangaiza mijini ambako pia wamekumbana na ukinzani wa sheria za mazingira na sera za wakubwa wa Benki ya Dunia.Matokeo yake ni vurugu na vita,maandamano na mauaji kama ilivyo Mwanza,Arusha,Morogoro,Mbeya na kwingineko.
    Si Ghana tu ambako vijana wamegeukia umachinga ili kusaka “Cedi”(Fedha ya Ghana), ukipenda unaweza kuita Pesos,pesa, sendi n.k
B
ali hata katika nchi nyingi za Afrika, ambako wakoloni wamerejea kwa kupitia mlango wa nyuma wa Uwekezaji, soko huria, uhurishaji wa Biashara, Ubinafsishaji, ama Utandawazi unaopigiwa debe na Benki ya Dunia na Fuko la Fedha la Dunia(IMF), Umoja wa Ulaya(EU) na matapeli wengine, ili kusomba madini, samaki,mazao ya kilimo, rasilimali watu, na fursa nyingine hata kuzidi wakati wa ukoloni.
      Wakoloni wetu wa zamani, sasa wanasomba  fursa na rasilimali zetu kupitia mikataba ya utapeli mithili ya ile ya akina Carl Peters na Mfalme Mangungo wa Msovero!
 Miaka micheche iliyopita,rais Jakaya Kikwete akiwa Ulaya,amekaririwa akisema eti wataalamu wetu wanatia saini mikataba hii ya Ghiliba,inayotuchimbia makaburi marefu, kufuatia wataalamu wetu kutokuwa na maarifa ama ujuzi!!
    Naam, Afrika miaka 56 baada ya Uhuru, bado waliopewa dhamana ya kulinda rasilimali zetu, wangali maamuma mithili ya Mfalme Mangungo!!
Bado vigogo wa   nchi zetu wanapoingia mikataba na magabacholi, tunaibiwa sana eti kufuatia umbumbumbu. Umbumbumbu, miaka 56 baada ya Uhuru!
Je, mbumbumbu wako huru? Taifa la mbumbumbu haliko huru aslani.
    Hii ni kusema kuwa dhahabu, almasi,tanzanite, rubi, samaki, bidhaa za miti, wanyamapori na nyingine husafirishwa sana nje, lakini bila manufaa kwa mtu mweusi.
 Wakati sisi tunapoagiza toka nje, chakula ni miongoni mwa bidhaa tunazoagiza, licha ya kwamba tuna Ardhi tena yenye rutuba, tuna mito, maziwa Bahari na mabwawa kama Mtera ambayo sasa yana mwaga maji, lakini bado tunaagiza sembe!
Leo, tunakula chakula kibovu na tunaagiza hata maziwa feki toka Ughaibuni,kwa sababu ya kutekeleza sera za IMF na WB kichwa kichwa.
   Maana yake ni kwamba, miaka 56 baada ya Uhuru, tumeshindwa kuwa na sera nzuri za kilimo, tunawategemea wakoloni mamboleo watuwekee mkakati kupitia Benkia ya Dunia au IMF katika kuzalisha chakula! Huu nao ni uhuru uchwara; tena uchuro!
    Katika karne ya 15 wapelelezi wa Kireno walitua Pwani ya Dhahabu, Ghana.Baadaye, katika karne hiyo, wakaimarisha makao yaoElmina, kwa ajili ya Biashara haramu ya Utumwa. Uingereza ilikuja baadaye kuifanya Pwani hii ya Dhahabu koloni lao kuu mwaka 1874.
.Katika vita ya Kwanza ya Dunia,vikosi vya nchi hiyo vikiongozwa na vile vya Ufaransa, ndivyo vilivyoivamia Togo ya Wajerumani.
     Nataka kusema kwamba,leo miaka 56 ya Uhuru wa Afrika wakoloni wameendelea kutugawa na kutumia baadhi ya watawala wetu(vibaraka wao)kuwaua ndugu zetu na kusomba rasilimali zetu, kwa manufaa ya wakoloni haohao!
    Kwame Nkrumah, Kiongozi wa Pwani hii ya Dhahabu ya Ghana alianza kuongoza tangu 1952.Alikuwa Waziri mkuu wa kwanza wan chi hiyo. Akachaguliwa Rais mwaka 1960, kwa kutumia Katiba iliyounda Jamhuri ya Ghana.
    Mwaka 1962 Kwame Nkrumah akafanywa, “Rais wa Maisha”-heshima aliyopoteza baada ya kutupa chini uhuru wa raia, nchi ikajikwaa katika madeni mazito
Nchi huingizwa katika hali ngumu ya uchumi na hawa mabeberu wakati mwingine wanapoona viongozi waliopo wameshindwa kujali maslahi yao
.
.Jeshi lilikamata madaraka ya nchi mwaka 1966. Hapa tunapata somo gani kwa kiongozi msomi wa kwanza Afrika, Dk. Kwame Nkrumah?
Kusahau utawala wa watu na watu, kwa ajili ya watu.Dk. Kwame Nkrumah alitamani kufia madarakani.Tunapaswa Afrika kujifunza maana ya kuachia wengine utawala.
    Katika Afrika huru, tumewaona marais wa maisha wengine kama akina Idi Amin Dada wa Uganda,Dk. Hastings Kana –ka Mzizi(Kamuzu) Banda wa Malawi, Emperor Jean-Bedel Bokassa wa Guinea ya Ikweta na wengine.
  Bokassa, Amin, Tito  Okello, Mobutu Seseseko Kuku Mbendu wa Zabanga wa Zaire, Sani Abacha walikula starehe kwa fedha za walipa kodi, wakati raia wakikosa shule, chakula, hospitali, barabara n.k.
Waliwaua wapinzani wa serikali zao, Waafrika wenzao na hata wanahisiwa kula nyama za maiti! Waliiba Dola mamia ya mamilioni,wakaficha Ulaya na Marekani.
   Mbali ya unyama wao, walilindwa na wakoloni. Nataka nikwambie, ukifanya unyama bila kulindwa na Ulaya na Marekani,utawala wako hauwezi kudumu.
 Wafaransa walimlinda Bokassa asishitakiwe baada ya kung’atuliwa kwa nguvu madarakani. Unajua, Bokassa aliiba Dola milioni 170 katika Hazina za nchi.Wanawalinda hata wafalme wa Qatar,Saudia n.k hata sasa zama za vuguvugu la mapinduzi.Angalia vituko vya huyo Bokassa aliyelindwa na Ufaransa.
 Aliwahi kulazimisha wanafunzi 100 waliogoma kununua sare za shule kiwandani kwake wauawe!! Alihukumiwa kifo, ingawa kesi hiyo ya kuwaua wanafunzi na kula nyama za watu haikufika mahakamani. Alikuhukumiwa kwa makosa mengine.
     Baadaye hukumu hiyo ilibatilishwa hadi kifungo cha miaka 10 jela. Aliyetoa msamaha  huo  ni Jenerali Andre Kolingba.
Hata leo huku Afrika, wangalipo akina Bokassa; wezi, mafisadi, wauaji na wala nyama za watu, “wanaolindwa” katika mbawa za akina Jenerali Kolingba!
   Tumeona watawala wa Afrika wakibadili katiba ili wapate mhula zaidi wa kutawala. Hii imeleta machafuko na vita si Ghana tu, bali hata maeneo mengine. Nani atawang’atua watawala ving’ang’anizi Afrika?
Vyama vingi ambavyo pia viongozi wake wanafanyiwa njama?
    Labda mapinduzi ya kijeshi kama ya akina Kanali Ignatius Kutu Acheampong wa  Ghana?Afrika iendelee kuwaondoa hawa walevi wa madaraka kwa mtutu wa bunduki na mapinduzi kama ya akina Jenerali Fred W.K. Akuffo, ambaye pia alipinduliwa na waasi wanajeshi wa Anga,Juni 1979?
Nataka kuwaonya kizazi kipya cha Afrika,vita na mapinduzi siyo suluhu ya matatizo yetu.Wanaosisitiza vita ni wapumbavu kupindukia.
   Naam, mapinduzi baada ya mapinduzi, badala ya demokrasia kupitia uchaguzi huru? Ni aibu kwa Ghana inayoadhimisha miaka 56 ya uhuru kufanya mapinduzi baada ya mapinduzi. Ni aibu Afrika kuwa na mapinduzi na vurugu kama Somali,Mali,Afrika ya Kati n.k
   Ni aibu wanajeshi wanaojiita wakombozi kuingia madarakani na kukataa kupisha utawala wa kiraia, kwa kujigeuza maraisi wa Maisha ya kupiga marufuku vyama vya siasa au kuunda njama.Afrika wangalopo akina Jonas Malheiro Savimbi,
 wasiokiri kushindwa katika uchaguzi.
     Akina Jerry Rawlings waliopisha utawala wa kiraia ni wachache sana. Wanafikiri nini kupisha demokrasia ya kweli?
   Tunapoadhimisha miaka  56 ya uhuru wa Ghana tujiulize: watu weusi tumekuwa huru toka kwa nani? Wakoloni wa Kizungu kwenda kwa wakoloni weusi walioungana na wakoloni mamboleo ili kuhujumu Afrika?
Katika somo la Ghana,tumejifunza kwamba hata sasa kuna chokochoko baada ya uchaguzi mkuu uliopita punde, Mahama akashinda,na upinzani umekwenda mahakamani kupinga ushindi wake,sawa.
Tunachosema ni kwamba,Waingereza walikwenda Ghana wakawakuta Waghana na historia yao,lakini wanasema Historia ya Afrika huanza pale Wakoloni walipofika,nasi tunakubali kijinga,colonial mentality!
Hata kanisa la Kiingereza,Anglican lilikubuhu kwa unyama na ukoloni,lilikuwa na watumwa waliolima mashamba na kuteswa huko Barbados,huko Caribbean.
Askofu Mkuu wa Cantebury,Rowan Williams,Feburuari 8 mwaka 2006 akaomba msamaha kwa kanisa hilo kumiliki watumwa,hasa watu Weusi.
Wapelelezi wa Kiingereza,akina John Hanning Speke, ati walipoliona Ziwa Nyanza wakaliita Victoria kwa heshima ya Malikia wa Uingereza,utadhani jina kama Nyanza,Inyanja,Rweru, kama walivyoita Wasukuma,Wajitta na Wahaya,halikuwa jina zuri.
Ilikuwa mwaka 1860, watu weusi walipofanyiwa kila udhalilishaji hata kubadili historia yao na hata leo tunachekelea na akili hiyo na kasumba ya kikoloni.
Naam, Afrika Kizimbani!
Itaendelea
    Mwandishi wa makala hii ni mwandishi wa habari anayepatikana kwa barua pepe:congesdaima@yahoo.com ama 0754 324 074,www.congesmrambatoday.blogspot.com





No comments:

Post a Comment