Tuesday, December 11, 2012

HATARI ZIWA VICTORIA



               KUTOWEKA  KWA SANGARA ZIWA VICTORIA

     Watu Milioni zaidi ya  30  wa nchi za Maziwa Makuu  hatarini kufa njaa

*mamiloni wengine wamepoteza ajira;ndiyo chanzo cha maandamano na vurugu Kanda ya Ziwa
Na conges mramba,Mwanza

SAMAKI wa Ziwa Victoria wanazidi kupungua, kufuatia uchafuzi wa mazingira, uvuvi usioendelevu, na uchoyo wa watu wa Magharibi na mawakala wao Wahindi,  kuhakikisha wanasomba  hata vifaranga,hadi ziwa litakapokauka!

Taasisi ya Globefish iliyo chini ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), imesema  athari zilizoletwa na  filamu ya Darwin’s Nightmare katika masoko ya minofu ya sangara Ulaya, zilidunu kwa muda mfupi tu.
Lakini sasa, Tanzania,Kenya na Uganda wametindikiwa samaki wa kupeleka   katika masoko ya Umoja wa Ulaya,EU.
     Kulingana na ripoti  ya mwezi Agosti,mwaka 2006, iliyosainiwa na Helga Josupit; inayopatikana katika mtandao wa Kompyuta (Internet), soko la minofu ya sangara liliathiriwa haraka kiasi cha kutosha, mara baada ya filamu ya Darwin’s Nightmare kuonyeshwa katika televisheni, lakini athari hizo zilikoma baada ya kitambo kifupi.
       Ripoti hiyo ilisema,  sababu za kushuka kwa mauzo ya minofu ya sangara katika masoko ya Umoja wa Ulaya (EU)  kuanzia miaka mitano liyopita, ni uzalishaji kupungua kulinganisha na miaka ya 2000,2003, na 2004.
     Katika nchi zote tatu za Afrika Mashariki, Kenya ,Uganda na Tanzania, sangara walioagizwa Ulaya walipungua kutoka tani 56,000 (mwaka 2004 )hadi  52,800 (mwaka 2005); ingawa thamani ya minofu hiyo iliongezeka.
Hadi mwezi huu wa Desemba,mwaka 2012 bei ya samaki katika viwanda imeporomoka kwa kasi,hata kama hakuna sangara tena ziwa Victoria,kulinganisha na miaka 10 iliyopita.
    Ongezeko lilikuwa kutoka euro milioni 192 hadi milioni 210 kufuatia matatizo katika usambazaji, yaliyosababisha ongezeko la euro 3.43 kwa kilo mwaka juzi, hadi yuro 4.00 kwa kilo mwaka 2005.
Hata hivyo, bei hiyo haikufikia ,rekodi ya yuro 5.00 kwa kilo; iliyofikiwa mwaka 2002, muda mfupi baada ya Umoja wa Ulaya kuanza tena kuagiza samaki, baada ya kufungiwa.
Umoja wa Ulaya ulisusa kuagiza sangara kyoka Afrika Mashariki,kufuatia tetesi za uvuvi wa sumu.
     Kulingana na FAO, kupungua kwa sangara waliopandikizwa ziwa Victoria miaka ya 60,  sasa kumeletwa na kupungua kwa kina cha maji ya ziwa Victoria; na kwamba hali hiyo huenda ikawasababishia maelfu ya wafanyabiashara ya samaki na wavuvi kukosa kazi.
Sangara wanapopungua Ziwa Victoria, makambi ya uvuvi hufungwa na kuwakosesha watu ajira na kipato, hali inayowafanya kuingia katika uhalifu na vurugu,hususan katika mikoa ya Mwanza.
Jiji la Mwanza,halijasahau fujo za       mwaka 2011,zilizosababisha wahuni kuvamia maduka ya Wahindi,huku wakiwataka waondoke!
Mali nyingi ziliporwa na vijana waliojidai Wamachinga.
Description: Copy (2) of Picture 289sangara
Hivi sasa wavuvi hulazimika kuvua mbali, lakini mahitaji bado ni makubwa kulinganisha na kiasi kinachopatikana; hali inayowafanya wavuvi kugharimia fedha nyingi ili kumudu gharama za uendeshaji.
     Mwaka 2006,wakati huo Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Jaka Mwambi,alipokuwa akitoa tamko la chama kuiunga mkono kauli ya serikali kuilaani filamu ya Darwin’s Nightmare, iliyobatizwa jina “mapanki”  akasema ndiyo chanzo cha kupungua kwa ulaji wa minofu ya sangara katika nchi filamu hiyo ilikoonyeshwa.
Wakati huo,Chama cha Mapinduzi kilitazama hasara ya viwanda vya samaki na haikutazama athari za baadaye ambazo sasa zinaonekana kwa fujo na maandamano kila mara ya wamachinga hapa Jijini Mwanza.
     Kauli hiyo ya CCM juu ya athari za Darwin’s Nightmare ilitafsiriwa kuwa ya kisiasa zaidi, kwa kuwa imeacha kuainisha matatizo mengine yanayoikumba sekta ya samaki, hadi kusababisha mauzo kupungua, kufuatia samaki wa aina nyingi kutoweka ziwa Victoria.
     Hata hivyo, ripoti ya FAO inaonyesha kupingana na kauli hiyo ya CCM, ikionyesha dhahiri kuwa kushuka kwa mauzo ya samaki Ulaya sasa kunatokana na matatizo ya kimazingira, na wala siyo filamu ya Darwin’s Nightmare.Samaki wametoweka takriban aina 300 walioliwa na sangara ambaye pia ametoweka.
      “Madhara iliyopata minofu ya sangara mwaka jana(2005) yalitokea haraka katika nchi filamu hiyo (documentary) ilikoonyeshwa katika televisheni, hali hiyo ikasababisha  upungufu wa kutosha; lakini kwa bahati athari hizo zilidumu kwa muda mfupi,”Imesema ripoti hiyo,  ya FAO kwenye mtandao huo wa Internet, na kuongeza kwamba juhudi zinafanywa kuhakikisha hali hiyo inarekebishwa, ikiwemo kutafuta mazingira ya haki ya biashara hiyo ya minofu ya sangara ,katika masoko ya Ulaya.
   Kulingana na ripoti hiyo, kupungua kwa samaki katika ziwa Victoria hakujaifanya Tanzania isiwe nchi inayoongoza kwa mauzo ya sangara Ulaya.Kenya pia imeripotiwa mauzo yake kupungua, wakati Uganda mauzo yao yameongezeka kwa tani 5,000 na kuifanya nchi hiyo ‘kuikalia kooni’ Tanzania kwa mauzo hayo ya sangara katika masoko ya Umoja wa Ulaya mwaka huo wa 2005.
   Mwaka 2005, Uganda iliuza tani 23,793 ambazo ni tani 87 tu nyuma ya Tanzania iliyouza minofu yenye uzito wa tani 23,880.
Kenya mwaka 2005 iliuza tani 5,176.

Hata hivyo, Uganda ilinufaika zaidi kwa kupata yuro milioni 101,318; wakati Tanzania ikipata yuro milioni 87,723. Kenya ilipata yuro milioni19,087 mwaka 2005 kutokana na mauzo yake.
 Nchi zilizoongoza kwa manunuzi ya sangara  katika masoko ya Ulaya ni  Hispania, ikifuatia Ufaransa, na Italia.Wakati huo ndege 10 za Ukraine na Urusi zikisomba tani 50 za sangara kila siku kupeleka Ulaya,wakati wananchi walipokula mapanki.
Uholanzi na Ubelgiji ndiyo kituo cha kwanza cha kusambazia sangara katika masoko ya Ulaya; wakati Ufaransa na Italia siku za karibuni zilianza kuagiza sangara moja kwa moja toka Afrika Mashariki.
    Mbunge wa Ukerewe,wakati huo akiwa  Rais wa Bunge la Afrika,  na Mwenyekiti wa Chama cha Wavuvi (TAFU) na Mwenyekiti wa  Wabunge wa Mwanza,Gertrude Ibengwe Mongella, aliwahi kusema  kwamba, kama hatua za dharura hazitachukuliwa, samaki watakwisha katika ziwa hili la pili kwa ukubwa duniani.
Ni la kwanza Afrika lenye maji baridi.
Description: Copy of Picture 285 sangara
    Lina ukubwa wa eneo; kilometa za mraba 68,800.Kina chake ni wastani wa mita 40 chini, na juu mita 80; lina ujazo wa maji wa kilomita 2,760. Linachangiwa na nchi tatu za Tanzania inayomiliki kilomita za mraba 34,488 sawa na asilimia 51; Uganda kilomita 27,484 sawa na asilimia 43 na Kenya kilomita 6,828 sawa na asilimia  sita.
     Mongella aliwahi kusema katika vikao vya Kamati ya Ushauri ya mkoa wa Mwanza kuwa, kuna madai ya wavuvi kutoka nchi jirani kuvua upande wa Tanzania, kwa kutumia zana bora zaidi, zinazowawezesha  ‘kuchota’ mali asili hii na kujipatia faida wakati watu wetu wakiendelea kuwa masikini!
    Inakisiwa kuwa watu zaidi ya milioni 50  wa nchi za Maziwa Makuu wanategemea ziwa hili kwa chakula chao, uchumi wao na hata maisha yao yote.Sasa samaki husafirishwa hadi Zambia,Afrika Kusini na Msumbiji,licha ya minofu ya sangara kusafirishwa Ulaya.
Hivyo kwamba taarifa za kupungua kwa kina cha maji cha ziwa hili; na kupungua kwa samaki kunakoletwa pia na uharibifu wa mazingira, ni kitisho kikubwa kwa uhai katika Ukanda wa Maziwa Makuu.
      Mjadala  kuhusu filamu ya mapanki, Darwin’s Nightmare, kwamba nchi za Kaskazini zimeanza kutumia ukoloni Mamboleo kunyonya rasilimali za nchi za Kusini, hapa katika kuanza kupungua kwa samaki wetu, lazima kutafakari kwa kina!
    Kwamba, kwa sababu ya umasikini, ujanja-ujanja, uroho, ujinga na kukurupukia soko huria katika utandawazi, tunauza mamilioni ya tani za samaki (chakula bora na chanzo cha uhai wetu) ili kupata vijisenti; kisha baadaye watakapokwisha kabisa,tujitoe kwa hiari kuwa makoloni ya kudumu, na watumwa wa nchi za Kaskazini ya Dunia, ambao sasa hivi wanalinda sana na kuhifadhi rasilimali zao!
     Kwamba, kwa kuuza sana rasilimali zetu tena bila kusindikwa ili kuongeza thamani; au kwa kukabidhi kila tulichonacho kikiwa ghafi, kwa hao wageni, tunakubali kunyonywa sana, na hao hao tuliowahi kuwakataa miaka 40 tu iliyopita, na sasa wananyonya kwa mrija, bila jasho! Tusijivunie kuuza sana nje, tujiulize: Tunapata nini na wao wananufaikaje?
     Hawalazimiki kutumia mitaji mikubwa kutunyonya! Mashirika makubwa ya kinyonyaji, kama Benki ya Dunia (WB), Fuko la Fedha la Kimataifa (IMF) na Shirika la Biashara la Kimataifa (WTO) yamekwisha andaa sera,masharti na mikataba ya kuchota kwa mara nyingine rasilimali zetu, zaidi ya ilivyokuwa enzi za ukoloni.
Safari hii, hawa wanawatumia viongozi wetu kuwapigia debe kusomba kila tulicho nacho…mwisho wa siku tutasalia jangwa!
 Maziwa, mito na mabwawa yatakauka! Misitu itafyekwa yote, ardhi yote yenye rutuba itauzwa; mbuga za wanyama zitauzwa, sangara waliokwisha kumeza samaki wengine wote zaidi ya aina 300 nao watakwisha ziwani…hata mapanki hayatakuwepo!
Kutakuwa kilio na kusaga meno!
    Naam, madini yote yatakuwa yameuzwa yakiwa ghafi; ili faida kwetu iwe kiasi kidogo sana. Lengo ni  kutufanya tusijekuinuka na kuwa ‘super powers’ tukaanza kushindana nao kama Japan, China, India , Malaysia na mataifa mengine ambayo miaka 40 tu nyuma yalikuwa makoloni yao! Tutasaliwa na mashimo na sumu mbaya katika maziwa yetu yatakayokuwa yamekauka kiasi cha kutisha.
     Kwa sababu ya uharibifu huu wa kutisha, tutaendelea kuathiriwa na sumu zinazosafiri kwa maji ya mvua toka migodini hadi katika vyanzo vya maji.
Bila shaka wataanza kuzaliwa watoto wasio na pua au mimba zilizotungiwa nje ya nyumba ya uzazi n.k! Tutamlaumu nani?
    Aliyekuwa Mbunge wa Ukerewe, Gertrude Mongella, aliwahi kuonya juu ya hatari hii ya wawekezaji, hususan wa sekta ya samaki, kuachwa kuendelea kusomba samaki ziwani bila kuhakikiwa…samaki ni kama dhahabu, almasi, tanzanite, wanyamapori,misitu, rutuba, mito, maziwa, theluji ya milima:
Hufika muda vyote hivi vikatoweka! Kizazi kijacho tutakiambia nini?
Kwamba tuliwahi kuwa na madini kama tanzanite yasiyopatikana popote ulimwenguni, samaki wengi kuliko ukimwengu wote, wanyama pori, vyura wa Kihansi, misitu, milima mirefu na kila kitu kizuri; lakini vikatoweka baada ya kuuzwa kama wazee wa Mwadui walivyopewa shanga za kuvaa kiunoni badala ya utajiri wa almasi?
     Ni hayo hayo aliyosema mtunzi wa Darwin’s Nightmare, Hubert Sauper, kwamba rasilimali zetu zitakwenda Ulaya kwa ujira kidogo; sisi tutafanywa walinzi, vibarua: Tutalipwa kiduchu…Wahindi, Wazungu, na wageni wengine watalipwa fedha nyingi. Sisi tutakanywa, “Acheni wivu wa kijinga!”
Watachota mali yote..watabeba hata mchanga na kupeleka Japan.
Dada zetu watageuzwa malaya; na hata watoto wetu wa kiume watageuzwa ‘wake’ ili kujinusuru kwa njaa!
    Naam, baadhi ya madini na rutuba vitahamia hata Mashariki ya Mbali. Kwa kuwa baadhi ya wanaharakati wataanza kupinga madhara haya ya utandawizi, ndugu zetu walioajiliwa kazi ya ulinzi wataendelea kuwapiga risasi, ili kutetea maslahi ya bwana zao. Mwisho wa siku, tutabaki kusutana, pengine hata tutaanza kuumizana wakati wengine wakipiga hatua mbele ya maendeleo.
    Ukitazama kiasi kinachopatikana sasa kama mrahaba wa rasilimali zetu, hakilingani na kile wanachobeba hawa wawekezaji-mawakala wa wakoloni mamboleo. Huu ubishi haupo hapa Tanzania.
Hata jimbo la Ogoni, Nigeria, Waijaw hawajakoma kudai mapato zaidi     ya mafuta yao yanayochimbwa na kuuzwa Ulaya, wakati wao hawana shule, zahanati, barabara na hata mafuta yenyewe! Kitu kama hiki kuitwa ni laana ya rasilimali, The Resources Curse!
    Hali ya Niger Delta, haiko tofauti sana na wilaya ya Kishapu; ambako watu hawana maji ya kunywa au kunywesha mifugo, hawana nyumba za kuishi.
Itaendelea
0754 324 074

No comments:

Post a Comment