Juni 16) mwaka 2013 itakuwa siku ya Kumbukumbu ya miaka 37
ya mauaji ya vijana wa Kiafrika(Weusi) wa kitongoji cha Soweto ( South West
Township ), Afrika ya
Kusini.
Seweto, ni kitongoji
nje ya Pretoria ,
ambako Juni 16, mwaka 1976 wanafunzi zaidi ya 20,000 wa Kiafrika walifanya
maandamano kupinga mitaala ya elimu ya kibaguzi, enzi za utawala wa Makaburu.
Polisi wa Makaburu
waliwafyatulia mabomu ya machozi ili kuwatawanya, bila mafanikio. Walifyatua
risasi za moto katika kundi hilo
kubwa la waandamanaji, vijana wa Kiafrika, pasipo huruma, pasipo kicho, wala
bila kutoa hadhari.
Juni 16, pia ni siku
Rais Mstaafu, Thabo Mvuyelwa Mbeki aliapishwa kuwa Rais wa Afrika Kusini, mwaka
1999.
Waliwafyeka waandamanaji
vijana wadogo mithili ya nzi.
Yakageuka mapambano ya vijana wenye mawe, fimbo,
matofali na hata mifuko ya daftari zao dhidi ya polisi wa makaburu wenye silaha
za moto.
Mwisho wa mapambano,
walikufa vijana zaidi ya 250 katika vitongoji, mitaa na vijiji vya Weusi.
Mwaka huo wa 1976
tu, inakisiwa Wabantu 600 waliuliwa kinyama na Makaburu. Naam, siku hizi, siku
hiyo ya Juni 16 ati inaitwa, ‘SIKU YA MTOTO WA AFRIKA’.
Hapa kwetu Tanzania ,
inaadhimishwa na kulipana posho, wakati akina Waziri Mkuu, Johannes Vorster
hawapo; umesalia ukaburu mamboleo nitakaobainisha hapa.
Leo, tunatazama
matatizo, changamoto na hali ya motto wa Kitanzania, ambamo tunasema serikali
katili kama ile ya Makaburu wa Afrika ya
Kusini, iliwafyeka kwa risasi za moto.
Siku hizi, Makaburu
mamboleo wanawafyeka watoto wa masikini kwa elimu duni, na kuwageuza manamba
katika nchi yao , kama
nitakavyobainisha.
Akina P.W. Botha,
walishaondoka tangu Agosti 14 mwaka 1989, akaingia F.W. de Klerk mwaka 1990.
Nelson Rolihlahla
‘Madiba’ Mandela, aliachiwa huru Feburuari 11, mwaka 1990 baada ya kifungo
cha miaka zaidi ya 27 katika Kisiwa cha
Robben.
Siku hizi, Afrika
Kusini ni nchi huru chini ya watu Weusi, akina Jacob Zuma ‘Mushorozi’ lakini
Tanzania kuna ubaguzi wa matabaka wa watoto wa masikini, wanaopewa elimu duni,
na watoto wa vigogo wanaosoma shule bora, ili wapate elimu safi, waje kuwa
warithi wa vyeo na madaraka.
Naam. Tanzania
ungalipo mfumo katili wa kibaguzi dhidi ya watoto wa masikini. Tunasema Tanzania nchi
huru inayotawaliwa na Waafrika wenzetu.
Kwamba, hakuna Pierre
Botha na F.W de Klerk, lakini watazame watoto wa masikini wanavyosoma katika
shule duni katika vitongoji na vijiji vya masikini kuzidi Soweto ya enzi za Makaburu.
Wanaketi chini
mavumbini wawapo madarasani. Shule eti hazina madawati hata kama
kulikuwa na Mpango wa Maendeleo ya Elimu(MMEM) ambao uliishia kujaza matumbo ya
vigogo;wakanunua magari ya fahari na kujenga makasri mijini.
Madarasa ya watoto
wa masikini, hayana viti, meza, vitabu vya kiada na ziada. Wengine hukalia mawe
na matofali. Walimu wamekwenda zao.
Hawa walimu wako
katika vyumba vyao vya kupigia soga vinavyoitwa ofisi za walimu; wengine
wanadiriki kucheza bao, karata n.k
Walimu wengine wako
kwenye biashara zao za baa na vilabu vya ulanzi, wanzuki, mataptap na hata
pombe haramu ya gongo, kwa sababu wanasema mishahara haiwatoshi.
Walimu wengine wa
kike wanafuma vitambaa vyao madarasani, wanauza vitumbua vyao, maandazi,
karanga, kashata n.k saa za masomo.
Ni nadra kumkuta
mwalimu akifundisha kwa moyo kama zama za
Mkoloni.Wakaguzi wenyewe hawafiki shuleni, hadi zitolewe taarifa na walimu
waandae mbuzi na sufuria kadhaa za wali.
Laiti Bwana Mkubwa,
Albert Mnali angepandishwa cheo kuwa Mkaguzi wa Elimu, labda wangeogopa na
kuingia madarasani.
Ni kama walishagoma
kufundisha siku nyingi, ingawa tulitangaziwa juzi kwamba, sasa watagoma
kwelikweli.
Siku hizi
mwanafunzi akiwa mstarini, aghalabu hutangaziwa kwamba,
“Kesho msipoleta hela
ya Ankara ya
maji, umeme, mshahara wa mlinzi, hela ya ubani ya mwalimu kufiwa shemejie, ya
upotevu wa kitabu n.k mtakiona kilichomnyonyoa kanga manyoya”
Hata ripoti za
mtihani wa mwisho wa mhula hatupewi hadi wazazi tulipe pesa za mwalimu.
Nachukua nafasi hii
kuwahoji wanaharakati wa Haki za Watoto: Hivi, ukaburu unaovuka unyama mithili
ya ule wa Soweto ,
siyo huu wa watoto vijijini kwetu kukalishwa mavumbini tangu saa 2.00 Asubuhi
hadi saa 9.00 Alasiri?
Hawa
wanaofanya hujuma,husaidiana na makaburu na wakoloni mamboleo
kuididimiza Afrika.Zama hizo walishirikiana na majasusi wa Marekani(CIA)
na makaburu(BOSS) kuhujumu uhuru wa Afrika,leo ni uhuru wa masikini
unaohujumiwa.
Watoto wanaketi
mavumbini bila mwalimu kuingia darasani, na hakuna anayejali. Vijijini, wanafunzi
wa shule hizi hubebeshwa majembe begani ili kulima mashamba yakiwemo ya walimu.
Hawa, ni mithili wa
manamba wa mashamba ya mkonge Tanga, enzi za Jarumani. Watoto wakiwemo wa
darasa la kwanza, hubebeshwa mizigo, matofali, vyuma n.k utadhani guta au matrekta.
Ukiuliza, unaambiwa
ni mradi wa shule wa kupatia chaki, daftari, kalamu ya mwalimu n.k
Hivi serikali
inapotutoza kodi sisi wazazi, kwa nini watoto wetu wakabebe mizigo kama makuli wa Bandari ya Dar es salaam?
Je, hali iko hivi
katika shule za masikini kwa sababu watoto wa vigogo wao husoma International
schools? Watoto wao husoma Uganda ,
Kenya ,
Uingereza n.k wakati elimu ya hapa ilishavuugwa.
Kila siku utasikia
migomo ya walimu, wakati hakuna anayehangaika na migomo ya watoto wa masikini
wanaobebeshwa mizigo wakati wa vipindi, na kulimishwa mashamba, achilia mbali
kuketishwa mavumbini.
Kila kunapokucha,
watoto ni amri moja ya “Majembe beganiii weka!!”
Utadhani watumwa, au wafungwa
huko Robben Kisiwani. Ukiuliza kulikoni? Unaambiwa ni miradi ya shule maana
serikali haijaleta fedha za chaki, kalamu n.k
Sasa, mwalimu
anapohamishiwa kituo kingine cha kazi, hawa wanafunzi hugeuzwa malori na maguta
ya kubebea samani za mwalimu hadi kituo kipya cha kazi. Sijui fedha za uhamisho
huenda wapi?
Huu ni unyanyasaji
na ukaburu wa hali ya juu sana ,
watoto chini ya miaka 17 kulimishwa mashamba ya walimu na wana vijiji.
Tazama sare zao za
shule, utaona hawa watoto wana matatizo.
Wamegeuzwa malori ya kusomba samani za walimu wa Prof. Jumanne Maghembe.
Hapa lazima niondoe shilingi katika bajeti ya Waziri wa Elimu , hadi atakapokubali kutangaza
marufuku wanafunzi wa shule za msingi kulima vibarua na kubeba mizigo kama matofali, kuni, samadi n.k
Naam, walimu
huwalazimisha watoto wa kike kuwatekea maji majumbani mwao, kuwapigia deki,
kutwanga nafaka na kuwatandikia vitanda!
Huko majumbani mwa
walimu, watoto wa kike hubakwa na kugeuzwa vimada, walimu ‘mafataki’
huwanyanyasa watoto, hadi wazazi wanapolalamika walimu hulindwa katika mbawa za
maofisa elimu na maofisa wa wizara, wasichukuliwe hatua.
Kama Msumeno unasema
uongo, Waziri husika aende kijiji cha Nyawa, katika Shule ya Msingi
ya Nyawa A aulize kisa cha wasichana watatu kutorokea Mwanza,miaka michache iliyopita
Bila shaka
ataambiwa hadithi za mwalimu kubaka wanafunzi na kulipa mahali ya shilingi
100,000 ili aoe mwanafunzi chini ya umri wa miaka 16. Je, huu si ukaburu?
Amepewa adhabu gani? Walimu wanawapa ujauzito wanafunzi, na kuishia kuhonga na
kurejeshwa kazini.
Mwisho, kama hakuna
ukaburu Tanzania ,
basi serikali iseme leo kwamba watoto wa masikini vijijini ni marufuku kuketi
sakafuni au mavumbini; kasha kwamba ni marufuku kuwahamisha walimu wao au
kulima mashamba ya walimu.
Basi serikali itamke
tangu sasa kwamba walimu lazima waingie madarasani na kufundisha kila kipindi,
hata bila kutishiwa na akina Albert Mnali.
Kama Tanzania kuna usawa na umoja, basi serikali leo
itangaze kwamba, watoto wa vogogo nao watasoma shule kama
za Saragana, Rusoli, Bugoji, Kanderema n.k
Na kwamba ni marufuku
kigogo kupeleka watoto wake kusoma Uingereza na Afrika Kusini!
Kama
hili halifanyiki, ndiyo maana shule za maskini ni mavumbi tupu, hakuna kitabu
wala dawati.Hii nini kama siyo Soweto tu?
Wakati
huo,Marekani iliwaunga mkono Makaburu wa Afrika ya Kusini,kuikandamiza
demokrasia na haki za binadamu.Hata sasa wanaofanya hivi hapa Tanzania
na Afrika ni makaburu na wakoloni mamboleo ambao hatunabudi kuwapinga.
Mungu wabariki watoto
wa masikini.
0786-324 074
No comments:
Post a Comment