Monday, December 24, 2012

mwanamke kuzaa Jiwe Kunzugu,Bunda 2011



 Mnamo tarehe 25, mwaka 1978,huko Oldham,Lancashire,Uingereza, mwanamama aitwaye Louise Brown, alikuwa mtoto wa kwanza wa   Chupa(test tube baby)duniani.
Yai kutoka kwa mama lilirutubishwa kwenye maabara, na watoto namna hii hawaji kwa miujiza,bali kwa maarifa ya sayansi na teknolojia.
Wanasayansi hubuni kuchanganya vinasaba vya binadamu,wakitaka hata na nyani!
Waweza kuchanganya vinasaba Ati,akina vya chura, hata na kondoo na kuku,ukapata kiumbe Fulani,lakini siyo kusema mtu anazaa kiumbe tofauti na binadamu.
Vipi kwa mwanamke kujifungua ‘Jiwe’ dogo la mviringo,kama ilivyotangazwa na vyombo vya habari,kwamba ilitokea huko Kunzugu,Bunda huku Kanda ya Ziwa,mnamo Agosti 23 mwaka 2011?
Ngeme Makala(20),mkazi wa Kunzungu,nje kidogo ya mji wa Bunda,mkoani Mara, alitangazwa na vyombo vya habari kwamba alijifungua Jiwe     dogo la mviringo!
Wakati wa tukio hilo, yeye Ngeme na mumewe,Nyamulekela Kennedy, waliwahakikishia wanakijiji wenzao kwamba lilikuwa ‘Jiwe’ lililozaliwa mithili ya kichanga. Nge
  Ngeme Makala(kulia) akiwa na mumewe, Nyamulekela Kennedy aliyeshikilia ‘kiwe’ analodai kuzaa huko Kunzungu,Bunda mwaka jana

Wakalifunga katika gazeti na kumonesha kila aliyefika kushangaa.
Ngeme, aliwathibitishia wananchi wenzake kwamba ujauzito wake ulikuwa na matatizo tangu kutungwa,na kwamba walishaenda kwa waganga wa kienyeji wee!
Lakini, ujauzito uliendelea kuleta shida.Mimba haikuwa ikicheza.
“Mimba ilikuwa haichezi”, alisema Ngeme, “Niliamua kumfuata mganga wa kienyeji ambaye hata hivyo hakunisaidia lolote.      Baada ya kubeba ujauzito huo kwa miezi 12,hatimaye nikasikia utungu wa kuzaa”.
Ngeme, akasema kwamba aliposikia utungu,akajitahidi kujifungua,kumbe likatoka jiwe dogo la mviringo lilikuwa na matone ya damu,utadhani kichanga! Hakwenda Kliniki kujifungua,alijifungua nyumbani kwake.
Nilimtafuta Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake,Watoto na wakati baada ya Kujifungua,katika Hospitali ya Mkoa wa Mwanza,Sekou Toure,na kumuuliza swali:
“Ati,Ngeme Makala alijifunguaaa ‘Jiwe’ badala ya kichanga huko  Kunzugu,Bunda?”
Dk.Onesmo Rwakyendera, ambaye pia wakati huo,mwaka jana alikuwa Daktari Mfawidhi wa Hospitali hiyo ya Sekou Toure, akaniambia:
“Haiwezekani binadamu kujifungua Jiwe! Nani alilipima?Wataalamu wa miamba,yaani geologists? Nitakueleza”.
Ngeme Makala ,alipewa kadi ya Kliniki huko Kunzugu,ni nyuma ya Mlima Balili.Bila shaka, hakufuata ushauri aliopewa,akaenda kwa wataalam wa miti shamba.
“Kama jiwe hilo lingepelekwa kwa wataalamu wa miamba,ingekuwa ngumu kubaini kuwa kweli lilikuwa jiwe lililokaa tumbo la uzazi la Ngeme kwa miezi 12”,Dk. Rwakyendera akaniambia,katika mahojiano maalum.
Akaniambia kwamba, katika taaluma ya utabibu, inafahamika kuwa hutokea mazingira ambamo mimba change katika mfuko wa mimba wa mama mjamzito huharibika,kasha huanza kuganda.
“Mimba iliyoharibika na kuganda,wakati mwingine hutokea kuwa kitu kigumu mithili ya jiwe”,Dk. Onesmo Rwakyendera anasema,”Kwa kutumia mashine kama x-ray, unaweza kuona kitu hicho katika nyumba ya uzazi.Akipata hali hiyo hawezi kuwa hedhi,na huona ni mjamzito”.
Akasema kwamba,mwanamke mwenye dalili hizi anapaswa kuwaona madaktari ili kupata ushauri wa kitaalam,badala ya kukimbilia kwa waganga wa jadi.
Wakati mwingine mimba inapoganda tumboni mwa mama,basi kwa kuwa mama anapotunga mimba,kiumbe huwa na madini ya Calcium ambayo hupatikana katika mifupa,basi huganda na kuwa kama jiwe gumu.
“Hii tunaita kwa kitaalam “Calcification” kwa sababu hiyo mifupa ya mtoto aliyekufa tumboni inaganda,na kutokana na madini hayo ya Calcium,huganda na kuwa kama jiwe,lakini siyo jiwe halisi.
 Hivi ndivyo ilivyomtokea huyo Ngeme Makala.”,Dk. Rwakyendera Onesmo aliniambia.
Kwamba,hali kama hiyo huweza kuwatokea hata wanaume wenye matatizo ya kibofu cha mkojo wanaoshindwa kukojoa ipasavyo.
Kwamba,madini ya Calcium hujikusanya yakawa kama kitu kinachofanana na yai ndani ya kibofu.Hiku kitu hujulikana kama “Jiwe la Kibofu” na siyo kwamba kuliwekwa mawe kwenye kibofu cha mkojo,bali ya madini ya Calcium yaliyojikusanya na kuganda.
Dk.Rwakyendera Onesmo akasema,wakati mwingine mtoto anapokufa tumboni na kaganda, basi huwa kama wale Mafaraoh wa Misri waliogandishwa kwa madawa maalum na kuishi muda mrefu.
“Hawa huitwa “Mummies” na kutokana na jina hili, watoto wanapokufa tumboni wakagandishwa na madawa Fulani,hali hiyo huitwa,    “Mummifying Process” na  baadaye hutoka,na mama akadhani amejifungua jiwe”, amesisitiza Dk.Rwakyendera.
Daktari mhuyu Bingwa, anashauri akinamama kwenda Kliniki kupima ujauzito kila wanapotunga mimba,na waachane na imani za kishirikina kwamba mtu huweza kujifungua nyoka,jiwe au kiboko!
Hutokea tu mimba inapoharibika,mtoto akafia tumboni,akaganda na kukaa zaidi ya  siku 280 ambazo mtoto hukaa tumboni mwa mama.
Hata wataalam wa Jiolojia hawawezi kuthibitisha kuwa jiwe kama hilo alilozaa Ngeme na mumewe Nyamulekela Kennedy, ni jiwe halisi ama mwamba mdogo. Hii ni dhana.
Ni hapa wanahabari wanapokurupukia dhana na uvumi na kuanza kuandika kwamba mama kazaa jiwe au nyoka,badala ya kuwafuata wataalam kuthibitisha habari zile.
Hali hiyo huleta taharuki kwa jamii,hofu na tashtiti na mwisho ni kwenda kwa wapiga ramli,na ni mwanzo wa visasi na mauaji ya kinyama katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
“Katika taaluma ya udaktari,hakuna manamke kujifungua jiwe, watu waende hospitali kupata vipimo,wasiende kwa ‘Sangoma’ haisaidii”, anasema Dk. Rwakyendera.
Ni wakati sasa wanahabari kufuata taaluma ya kuandika habari sahihi na zenye kufanyiwa tafiti,kuliko kwenda ku ‘balance’ stori za uvumi namna hii kwa ‘sangoma’ na watu wa kijiweni tu!
0713 324 074


No comments:

Post a Comment