Thursday, September 1, 2011

BURIANI MUAMMAR AL GADDAFI




SUDAN ya Kusini, sasa ni nchi huru chini ya Rais Salva Kiir; naam ni nchi ya 54 katika Umoja wa Afrika, AU.
 ni sasa ni nchi ya 193 katika Umoja wa Mataifa(UN) uliogeuka Umoja wa Mataifa wa Marekani!

Kanali  Dk. John Garang de Mabior.
Alisafiri hadi kuzimu kwa njia ya helkopta iitwayo, M-72; ambayo awali ilitarajiwa kuruka kutoka jijini Kampala hadi Juba, Kusini mwa Sudan .
   Ilikuwa Julai 30 mwaka 2005; miaka sita  imepita  tangu   kifo chake;kifo kibaya cha ajali ya helkopta iliyopokonya tonge mdomoni.
   D.k John Garang, alikuwa akijiandaa kuwa Makamu Rais wa Sudan kufuatia Mkataba wa amani baada ya kumalizika mapigano dhidi ya serikali ya Khartoum , ya Rais Omar Hassan El-Bashir.
   Kiongozi wa Sudan People’s Liberation Army\Movement (SPLA/SPLM)alikufa katika ajali hiyo ya helkopta ya Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda ; pamoja na maofisa wake wapatao 13 mahali ambapo ni mpakani mwa Uganda na Sudan.Sababu ya ajali hiyo ilisemwa ilitokana na hali mbaya ya hewa.
  Dk. Garang, alikuwa akirejea nyumbani baada ya Mkutano na Rais Yoweri Museveni  mjini Kampala .
Agosti Mosi mwaka huo wa 2005 Salva Kiir, alirithi heshima na harakati za De Mabior za kusaka uhuru Kusini mwa Sudan , taifa la Waarabu wa Kaskazini na Weusi wakulima wa Kusini.
  Sasa, Salva Kiir ni rais wa Sudan ya Kusini iliyopata uhuru punde,kutoka kwa mabedui wa Kiarabu wa Kaskazini.
    Hayati De Mabior alianza harakati za kutafuta uhuru wa watu wake siku nyingi. Kama kawaida ya makamaradi wenzake wote, alilelewa Dar es salaam , ambako ni kitovu cha vuguvugu la uhuru hapa Barani.
   Mashujaa wengine waliowahi ‘kupikwa’ na kuiva kimapinduzi Dar es salaam ni pamoja na  hayati Samora Moises Machel wa Musumbiji, Laurent Desire Kabila wa Jamhuri ya Kongo(DRC), Rais wa sasa wa Kongo, Joseph Kabila, Profesa  Ernest  Wamba dia Wamba, Pierre Nkurunzinza wa Burundi, Yoweri Museveni, Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Omollo Odinga, na rais Mstaafu Afrika Kusini, Nelson Rolihlahla ‘Madiba’ Mandela, Rais Mstaafu wa Msumbiji, Joachim Chissano, orodhas ni ndefu.
   Hayati Kabila, Garang na Samora ni miongoni mwa wanamapinduzi walioanzisha vuguvugu la ukombozi lililokuwa na kitovu  katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam.
Bahati mbaya sana , hawa mashujaa wamepokonywa uhai kwa vifo vya aina moja.Nuru yao imezima, wakati walipokuwa  wangali wakihitajika.
   Samora Machel, alikufa hivyo hivyo katika ajali ya ndege, Oktoba 19, mwaka 1986.
  Ilikuwa ndege aina ya Tupolev-134A. Ni Jumapili, saa tano hivi za usiku, ndgd hiyo ya Kirusi ikitokea Zambia , kupitia anga ya Zimbabwe , ili kurejea nyumbani, Maputo .
   Ndege hiyo ilianguka katika ardhi ya Afrika Kusini, ubavuni mwa milima ya Lebombo; ni eneo la Mbuzini; kwenye pembe ya Transvaal Mashariki. Ni jirani kabisa na mpaka wa Musumbiji, Swaziland na Afrika Kusini.
   Watu wengine 33 waliokuwemo katika ndege hiyo, pia walifariki dunia, wakati wengine 10 walinusurika.
  Kumbuka, Garang alipokufa walinusurika 13.Mwaka 1987 wakati wa Maadhimisho ya mwaka mmoja wa kifo hicho, Rais Joachim Chissano alisema, Komredi Machel hakufa kwa ajali; bali kifo chake kilitokana na hujuma.
   Duru za kipelelezi ziliutuhumu utawala wa Makaburu wa Afrika Kusini, hususan Shirika lake la Ujasusi la BOSS, kuhusika na njama za kifo hicho.Afrika Kusini iliunda Kamati yake ya Uchunguzi wa kifo hicho iliyokuwa chini ya Jaji Cecil Margo, wakasema marubani wa Tupolev 134A walikosea;wakadhani wanatua Maputo , kumbe walikuwa porini!
  Aghalabu, njama za mauaji ya wanamapinduzi hufunikwa kwa ‘magunia’ ili kuuficha ukweli.Hata mashujaa wanapouliwa kwa risasi ya kichwa, vyombo vya Habari  huambiwa “kalamu chini” halafu umma huambiwa ti ajali, Basi!
    Naam. Hata kifo cha Kanali Dk. John Garang kilifuatwa na tetesi kwamba kilipangwa.
  Rais "Seven Batallion" ama  Museveni, aliyedhamini safari ya Garang alikanushwa kifo hicho kutokana na hujuma zozote.
  Hivyo, Garang na Samora Machel, walikufa kifo kimoja.
   Wakati Garang alikwenda mjini Kampala kufanya mkutano na Museveni, Samora alikwenda mjini Lusaka kufanya mkutano na Rais Kenneth Kaunda wa Zambia .
  Kaunda alikuwa Mwenyekiti wa Nchi za Mstari wa Mbele wa Ukombozi Kusini mwa Afrika.
    Ni wakati huo huo kundi la kijeshi la RENAMO lilikuwa nchini Malawi. Enzi hizo Malawi iliongozwa na marehemu Dk. Hastings Kamuzu(kana-ka-Mzizi)Banda.
RENAMO walitumiwa kuidhoofisha Musumbiji baada ya uhuru, kwa sababu imesemwa Banda alikuwa kibaraka wa Wazungu.
   Mlinzi wa Samora, ambaye alinusurika katika ajali hiyo, Fernando Maniel Joao,alitambaa hadi katika kituo kimoja cha polisi, kuomba msaada ndani ya Afrika Kusini ya Makaburu.
  Joao anasema, wakajichelewesha kwenda kutoa msaada kwa majeruhi; hadi wakaja kutangaza baadaye keshoye kuwa Samora alikuwa amefariki.
  Polisi wa Makaburu walifika katika eneo la ajali saa chache baada ya habari, wakaishia kuiba nyaraka muhimu na kupora mizigo na fedha.
   Samora, aliongoza chama cha Frelimo(Mozambique Liberation Front), ambacho kilifanikiwa kupata uhuru, baada ya kuwang’oa Wareno mwaka 1975.
  Rais wa Uganda, Yoweri Museveni aliwahi kupata mafunzo ya medani ya kijeshi kwa wapiganaji wa Frelimo, kabla ya kurejea Uganda muda mfupi kabla ya Dikteta Iddi Amin Dada kumpindua Dk. Milton Apollo Obote, mwaka 1971.
    Baada ya mapinduzi, ndipo Museveni alipokuwa Dar es salaam na kusoma Chuo Kikuu cha Dar es salaam, shahada yake ya Sayansi ya Siasa(political science); akakutana na akina Garang, Kabila na wengine.
    Dk. Apollo Milton Obote, alianza kutawala Uganda kama rais Mei 24 mwaka 1966 hadi alipopinduliwa Januri 25 mwaka 1971 na Jenerali Amin, aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Uganda. Obote, alirejea kutawala Uganda Desemba 1980 hadi Julai 27 mwaka 1985 alipopinduliwa kwa mara nyingine na Jenerali Tito Okello. Afrika, jua la Haki linakuchwa, zimebaki hujuma na njama za ‘makaburu mambosasa’ wanaohujumu kila haki na kila chanzo cha maendeleo ya watu.
 Leo, wanamapinduzi hawa wamepotea kuzimuni wakati harakati za mabeberu sasa wakitumia majeshi ya NATO(Northern Atlantic Treaty Organization) badala ya majeshi ya Makaburu na mashirika yao ya kijasusi kama BOSS,CIA n,k wanaipindua Afrika, ili kutwaa rasilimali zetu.
 Kisingizio ni demokrasia Afrika!
   Tunapomaliza  kuadhimisha miaka sita ya kifo cha Kanali Dk. John Garang de Mabior na uhuru wa Sudan,  tunashindwa kuthamini mchango wa baadhi ya viongozi wetu, wanaoonekana kama kondoo, lakini kumbe mbwa mwitu wakali.
  Leo,ukimwacha 'R.G' Mugabe, na Jacob Zuma Mushorozi, hakuna     tena wa kukemea ubeberu Afrika, akina Bernard Membe wanasema kwa kigugumizi juu ya uvamizi wa NATO, Afrika, naam Libya. Nani wa kuwakemea NATO dhidi ya vitendo vyao vya kupindua nchi na kuwasaidia Waasi?
   Dhana halisi ya ukombozi, haki, uhuru na maendeleo ya Waafrika husalia mbali.
Afrika itasemaje kwamba ilishinda vita vya ukombozi dhidi ya wakoloni, wakati wakoloni mamboleo wangalipo, ni vibaraka wanaoendeleza “NJAMA” mithili ya zile za Mashirika kama CIA la Marekani na BOSS, la Makaburu.
Leo, NATO wanatangaza amri ya 'No Fly Zone' hapa Barani pasipo AU kusema chochote. Mwanachama mmoja AU anapinduliwa na majeshi ya Wazungu kuanza kumsaka mithili ya panya,lakini hakuna wa kukohoa!
    Hawa, baadhi yao hufanya kinyume cha demokrasia na haki za binadamu;hufanya, “HUJUMA” na ufisadi.
Huonekana kana kwamba, ni “KIKOSI CHA KISASI” baada ya uhuru, na kuwapinga Wazungu kuendelea kujitwalia rasilimali za Bara letu na kupeleka chakula Ulaya, wakati watoto wa Afrika, wakipewa silaha wauane.
Leo, Libya kunaweza kufumuka vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa muda mrefu,kwa sababu ndivyo NATO watakavyo,Afrika kusiwepo maendeleo na utangamano.
 Wamekuwa wakiwadhamini waasi wa Angola,Musumbiji, Sierra Leone na sasa Libya.
Baadaye huwatia mbaroni akina Charles Taylor na Fodday Sankoh ili kutuziba midomo.
   Tumeona Samora akihujumiwa na Makaburu.
  tuliona Patrice Emmely Lumumba akiuliwa na vibaraka, akina Mobutu na Moise Tshombe.
Tumemwona Kanali Garang akifa kwa ajali ya helkopta ya Museveni, mpakani mwa Uganda na Sudan.
Yumeona Afrika, baada ya uhuru wa vyama vingi, sasa majeshi ya kigeni yameanza kupukutisha serikali za Afrika kwamba ni madikteta, nasi tunashangilia sana bila kujua tunarejea zama za Makaburu na chini ya bendera za kikoloni kama Union Jack!
   Orodha ya waliokufa ni ndefu, ya waliokufa wakisaka mustakabali wa watu wao. Leo, mahakama ya mjini Hague imegeuka mahali pa kuwasweka rumande wengi WAAFRIKA tu, Wazungu wauaji kama Bush na Blair, hawakamatwi!
Hadi leo hakuna utangamano, kwa sababu WAZUNGU wangali wakimezea mate madini, samaki,  mafuta, madini,misitu,wanyama na rasilimali zingine.
Huwatumia viongozi wetu kuwa mawakala wa BOSS na CIA; wasomaji wakumkumbuke mwanamapinduzi Alstablus Elvis Musiba na vitabu vyake dhidi ya majahili hawa, ambao sasa wanaweka madarakani hapa Afrika viongozi, wanaotugeuka na kuuza kila kitu kwa bei bure.Hawa wanaokubaliana na uporaji-ubinafsishaji, ugenishaji na wizi wa rasilimali, hawakamatwi,wanaopinga kuhamishia rasilimali zetu Uswisi hukamatwa.
 Hata Nyerere aliambiwa kuiba fedha na kuficha Uswisi akagoma!Leo, wenye vijisenti wanaficha Jersey, halafu baadaye Wazungu husema kinafiki kwamba kuna fedha za Libya Ulaya,kwamba Mobutu alificha fedha Uswisi, huu ni wizi na utapeli tu.
    Wameuza migodi yetu na mashirika yetu kwa NJAMA za wakoloni, kwa kutumia Mashirika kama IMF,Benki ya Dunia na wahisani wengine, wanaojulikana kama G-8 n.k
   Ni kwa sababu hii Afrika inavuja damu mbichi, kuashiria adui yetu hayuko mbali nasi.
Afrika inateketea katika miali ya moto, kwa tamaa,rushwa,hujuma,ufisadi na kukosa haki.
   Madhumuni ya serikali za Afrika, yalikuwa kukuza Amani, Imani na Tumaini; isijekuonekana hili ni Bara la watu Bwana Mungu aliwaumba bahati mbaya.
Ndiyo sababu, viongozi ama watawala wetu wamekosa shabaha katika kila lengo la fursa za maendeleo duniani.
  Akina Nyerere, Kwame Nkurumah na wenzao walikuwa na visheni ya kutumia rasilimali na fursa za Bara hili, kuondokana na utumwa. Ingawa walishindwa bahati mbaya; waliondoka na njozi na malengo yao.
   Watawala walioirithi Afrika, wanaonekana kuikabidhi kwa wakoloni walewale; huku hawa wakijigeuza wanyapala.
Hawataki kuambiwa, hawataki uchaguzi, na hawana lengo la maendeleo kwa umma.
Ni waoga, wanapokea kila amri na shurti  kutoka Uingereza na Marekani kwa utii mkubwa.
Ni kwa sababu hii kuna ufisadi na kila machafuko.Shina la ufisadi ni Ulaya na Marekani.
   Hawa ni nani; kama si Kaini aliyemuua nduguye Abili kwa sababu ya choyo na tamaa ya madaraka?
Wapo viongozi wetu vitanga vya mikono yao vinachuruzika damu mbichi, kwa kuwaua Waafrika wenzao, Congo (DRC), Darfur, Sierra Leone  na mahali pengine pasipo amani hapa  Barani.
  Hata hapa kwetu kuna nyufa. Kelele za kuvunjika nyumba yetu zimesikika, mara “Oh..Bara wanainyonga         Zanzibar”, mara “Unguja anakula peke yake, wakati Pemba akiambulia makombo chini ya meza”, n.k
Wenzetu Kenya walikaribia kumalizana kwa tamaa ya ‘machungwa’ na ‘ndizi’.Somalia wanachinjana kwa sababu ya usultani na mamlaka.Vivyo hivyo ndugu zetu  Afrika Kusini wameanza kututimua nyumbani kwao, kwa sababu chakula kidogo-unga robo.
   I wapi leo thamani ya wimbo, “UHURU NA UMOJA”?
   Hapa, kuna siri ya maisha matamu-Furaha katika hali ya hewa ya kupendeza chini ya JUA LA HAKI lililokuchwa kwa sababu ya kiza cha dhuluma, tamaa ya madaraka,ufisadi, rushwa na choyo.Wenye nguvu huwapiga raia kwa ngumi za chuma. Akina Kaini!
   Palipo na giza hapana nuru; na palipo na nuru hapana giza.
BURIANI KANALI MUAMMAR AL GADDAFI, wamekuondoa,lakini angalau wewe ni Mwana wa Afrika!
      congesdaima@yahoo.com
        0786/0754-324 074
Top of Form
Bottom of Form
Top of Form
Bottom of Form
Top of Form
Bottom of Form


No comments:

Post a Comment