Wednesday, September 14, 2011

MV SPICE ISLANDERS ILISAFIRI HADI KUZIMU MITHILI YA MV BUKOBA!

AJALI YA MV. SPICE ISLANDERS HAINA TOFAUTI NA YA MV BUKOBA

 
 Tanzania ilikuwa tayari imepitisha  miaka 15  ya kuzama kwa Meli ya Mv.Bukoba pale Mv. Spice Islanders ya Zanzibar ilipozama Bahari ya Hindi.
 Mv. Spice Islander, ilizama Septemba 10,ikifanya safari zake kati ya Unguja na Pemba na kupoteza maisha ya watu zaidi ya 200.
Watu 260 waliokolewa.
 Hadithi ni zile zile za Mv Bukoba, kwamba meli ilipakia watu wengi na mizigo kupita uwezo wake, kwamba abiria wengine walichelea kuipanda; ndivyo ilivyotokea kwa MV Bukoba huko Kemondo Bay.
   Meli ya  Mv. Bukoba,ilizama alfajiri, Mei 21, mwaka 1996 na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 800.
Ilikuwa ikitokea Bukoba, na ilizama kilomita kama 12 za majini kutoka bandari ya Mwanza, uelekeo wa Bwiru, jijini Mwanza.
     Inakisiwa kwamba, watu waliojeruhiwa katika ajali hiyo ya kihistoria ni 100; wakati mali nyingi zilipotea na thamani yake bado kujulikana.
 Mara baada ya ajali ile, serikali iliunda Tume iliyokuwa chini ya Jaji Robert Kissanga, ili kuchunguza chanzo cha ajali ile mbaya ya majini.
  Kulingana na Ripoti ya Tume hiyo, usiku wa kuamkia siku ya ajali(Mei 20 mwaka 1996),meli hiyo ilikuwa na abiria kati ya 750 na 800 na wafanyakazi 37.
Kati hao, 114 waliokolewa, na maiti 391 ndiyo walioopolewa na kuzikwa katika makaburi ya Igoma,jijini Mwanza, wakati miili mingine ilichukuliwa na ndugu zao kwenda kuzikwa.
   Kila mwaka, serikali na wananchi huwasha mishumaa na kufukiza ubani katika makaburi hayo kama kumbukumbu ya ajali ile.
  Pengine, serikali huongozana na watu wa madhehebu ya dini kwenda eneo la ajali ili kusoma dua na kumwaga mchanga majini kama ishara ya ibada ya wafu na maziko.
 Inakisiwa, jumla ya miili 332 haikupatikana.
Kwahiyo, serikali ilifanya ‘mazishi’ ziwani katika eneo la ajali,umbali wa kama maili za majini nane tu kutoka ilipo Bandari ya Mwanza.
    Mv.Bukoba, ilijengwa na kampuni ya Meli ya Kibelgiji.Wakati wa kuzinduliwa,Julai 27 mwaka 1979 ilibainika ilitaka kumtosa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere.
 Haikuwa na uwiano wa majini.
 Ilisemwa kwamba, serikali ilishaipiga marufuku meli hiyo isifanye huduma Ziwa Victoria ,  sababu haikuwa na 'sea worthness', vinginevyo lilikuwa kaburi lenye kuelea, ambali siku na saa yoyote ingesababisha maada makubwa.
  Hata hivyo, kufuatia uzembe wa serikali ama kutojali, Mv. Bukoba iliendelea kukata mawimbi ya Ziwa kutoka Mwanza hadi Bukoba, kila siku hadi ilipozama.Iliazama miaka 15 baadaye.
   Baada ya Tume ya Jaji Robert Kissanga kuwasilisha Ripoti ya uchunguzi wake, serikali ikafungua kesi Mahakama Kuu na kuwashitaki aliyekuwa Nahodha wa Meli, Jumanne Rume-Mwiru, aliyekuwa Mkaguzi wa Mamlaka ya Bandari(THA),Gilbert Mokiwa, Meneja wa Bandari ya Bukoba, Alphonce Sambo, na aliyekuwa Meneja wa Bandari ya Kemondo, Prosper Lugumila.
    Kesi hiyo nambari 22,ilifunguliwa Mahakama Kuu,Mwanza mwaka 1998, na ilianza kusikilizwa Mei 14 mwaka 2001.
   Upande wa Mashitaka ukiongozwa na mawakili wa serikali, William Magoma na Eliezer Feleshi(sasa DPP) ulidai mahakamani hapo kwamba washitakiwa kwa pamoja walisababisha vifo,kujeruhi na upotevu wa mali nyingi(hazikufahamika), kwa uzembe.
   Kesi hiyo ilitajwa mara nyingi, ikaahirishwa zaidi ya mara sita hivi, baada ya kusikilizwa kwa mwaka mzima,tangu ilipoanza kusikilzwa Mei,2001.
   Ijumaa, Novemba 29, mwaka 2002, majira ya saa sita mchana, aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Juxton ,Mlay, akasoma hukumu ya kesi hiyo.Nilikuwepo mahakani wakati hukumu ikisomwa.
  Aliwaachia huru washitakiwa wote wanne, baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuithibitishia mahakama(pasipo shaka yoyote) kwamba walisababisha ajali ile na vifo vya watu kama nilivyokwisha taja.
   Jaji Malay, alisema mahakamani wakati akisoma hukumu hiyo ya kihistoria, kwamba hoja za upande wa mashitaka kwamba washitakiwa, Jumanne Mwiru, Mokiwa, Sambo,na Prosper Lugumila walisababisha vifo,kujeruhi na upotevu wa mali, hazikuwa na ushahidi.
   Kwamba, kwa kuwa mashahidi waliiambia mahakama kuwa Rume-Mwiru alisikika asubuhi ile ya ajali, akimwamuru rubani kukata kona, maana yake ni kwamba alikuwa na nia thabiti ya kuokoa maisha ya abiria na wafanyakazi wa meli yake, na wala siyo kutaka kuwaua kwa uzembe kama ilivyodaiwa.
    Akisoma hukumu ndefu, iliyokuwa na jumla ya kurasa 118 zilizvyoandikwa kwa mkono, Jaji Mlay alitumia zaidi ya dakika 160 kufafanua vipengele vya kisheria na kuvitolea maamuzi kwa ufasaha.
   Mwishoni mwa hukumu, akasema kwamba hapakuwa na ushahidi kwamba Mv Bukoba ilizama kwa uzembe wa washitakiwa wanne: Sambo, Mwiru, Mokiwa na Lugumila peke yao !
   Madai ya upande wa mashitaka kwamba Mv.Bukoba ilipakia mizigo mingi kushinda uwezo wake yakatupiliwa mbali na mahakama.
 Kwa sababu, haikufahamika kwa yakini, kwamba MV.Bukoba ilikuwa na abiria wangapi siku ya ajali. Na ilibeba mizigo ya uzito wa kiasi gani?
 Mashahidi wa upande wa mashitaka,walikuwa wameiambia mahakama hiyo kwamba, meli ilipakia mikungu mingi ya ndizi: Lakini, kiasi gani yenye uzito gani?
Nani aliipima uzito?
    Mahakama ilihoji bila majibu. Jaji Mlay alisema, MV.Bukoba ilizama Mei 21, mwaka 1996 kwa sababu haikuwa thabiti; na haikuwa na uwiano wa majini. Hata Tume ya Jaji Kissanga ilisema hivyo.
  Kama kawaida,upande wa mashitaka ukiongozwa Eliezer Feleshi, ukaonesha nia ya kuomba rufaa mahakama ya rufaa.
   Nilikuwepo mahakamani, wakati wa kusomwa hukumu ile.
Niliwaona washitakiwa wakiganda kwa butwaa, kama waliomwagiwa barafu; hawakuamini.
 Nilitaka Jumanne Rume-Mwiru aniambie, alijiskiaje? Hakujibu.
   Miezi mingi baadaye, tulipokutana katika mitaa ya jiji la Mwanza, Mwiru aliniambia kwamba mshitakiwa mwenzake ambaye siku hiyo hakuwepo mahakamani, alipoambiwa kuhusu hukumu ile aliugua nakulazwa hospitalini, mjini Bukoba.
  Leo, ni  miaka mingi  tangu hukumu ile isomwe,rufaa haijasikilizwa, na baadhi ya washitakiwa wamefariki dunia, bila kuona hatma ya kesi yao .
  Mawakili wa upande wa utetezi walikuwa Salum Magongo na Gallati Mwantembe wa jijini Mwanza.
 Mv.Bukoba ilizama kwa sababu za uzembe wa serikali na vyombo vyake.
Haikuwa na uwiano wa majini muda mrefu, hata haikuwa na zana za uokozi kama maboya ya kutosha.
   Haikuwa na mawasiliano.
  Niliwahi kufanya mahojiano na aliyekuwa Nahodha, Jumanne Rume-Mwiru, na kumuuliza hatma ya kesi ile huko mahakama ya rufaa, na kama walikuwa na nia ya kudai mafao yao ?
 “Tunamwachia Mungu” alisema Mwiru huku akicheka bila shaka kukumbuka kilichomtokea.
Aliniahakikishia kwamba mwezao mmoja alikuwa amefariki,bila kujua hatma ya kesi ile.
 Rume-Mwiru, tayari ni marehemu, wakati hatma ya kesi yao haijulikani hadi leo.
   Hata baada ya ajali ile, zimetokea ajali nyingi Ziwa Victoria , mitoni na baharini.
 Mv.Nyamageni,iliyokuwa meli ya binafsi, ilizama miaka ya karibuni ikiwa imebeba masanduku ya soda na abiria kwa pamoja, na haikupatikana hata leo.
 Ilikuwa safari ya kwenda kuzimu.
  Naam, safari ya kuzimu!
Meli za Tanzania ni majeneza yanayosafiri kwenda kuzimu.
Uzembe! Hata ajali za magari huletwa na uzembe tu, usalama barabarani wapo, hakuna hatua. Ziwa Victoria ndipo kuna kazi, majahazi hayana hata boya moja,hakuna vifaa vya kuzima moto!
 miaka ya karibuni, Meli nyingine ya Shirika la Meli(Marine Services Company), Mv.Butiama, ilizimika majini, ikaelea kwa zaidi ya saa nne.
 Meli hiyo ati haikuwa na mawasiliano.
Mtu mmoja alikiambia kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa(RCC) Mkoani Mwanza,kuwa ingeweza kupigwa mawimbi hadi Uganda , au ikaparamia mwamba?
   Majibu hayakutolewa, aliyekuwa akiulizwa alikuwa mtaalam kutoka Mamlaka ya Bandari(TPA), kwamba asingeweza kuisemea MSC, ambao hawakualikwa katika mkutano huo.
  Abiria walihaha, Mv.Butiama ilipozima injini zake jirani tu na Bandari ya Mwanza, lakini hakukuwa na mawasiliano. Eti meli za MSC bado hazina maboya na mawasiliano!
 Je, zile za wajasiliamali zinazotia nanga katika bandari zinazomea kama uyoga, zina zana za uokozi?
Zina maboya mangapi na hufuata sheria kwa kiwango gani?
 Bila shaka, zinafanya kazi kwa mazoea kama ilivyokuwa mwaka 47!
Naam, meli za nchi hii, hata leo hii miaka 15 baada ya kuzama kwa Mv.Bukoba ni majeneza yanayosafiri majini
.Hata MV Spice ilikuwa jeneza lililoelea majini, abiria wakapanda,wakasafiri hadi kuzimu! Nawapa pole walionusurika!
  SUMATRA na vyombo vingine vya serikali wapo, wanatazama majahazi yakisafiri ama kuelea kwenda kuzimu.
Serikali huishia kufanya matambiko majini kila mwaka, kama ilivyofanya juzi.
Wengine wamekula ubani wa wafiwa, wengine hujitajirisha kwa maadhimisho haya, wapo tu.
   Wanabarizi upepo.Kufaa kufaana, sijui?
 0754-324 074,0786 324 074
 
 
 
  
  

Top of Form

No comments:

Post a Comment