Tuesday, October 4, 2011

Achana na Igunga, tumkumbuke Prof.Wangari Maathai

KWA majuma mawili hivi,Tanzania tulikuwa tunazungumza Uchaguzi mdogo wa Igunga, utadhani hakuna kingine cha muhimu cha kuongea!
Watu wote, waliamkia vijiweni kuongea habari za uchaguzi wa Igunga,kabla ya kuelekea kazini.
“Igunga! Igunga! Igunga”, hadi karibia masikio yangu yazibe kwa kelele za Igunga. Afadhali hiyo ‘dhoruba’ ya siasa za Igunga imetua,watu wafanye kazi.
Kuna watu hapa Tanzania, hawapati kula mpaka wazungumze siasa ksms huo uchaguzi wa Igunga.
Hawawezi kuongea chochote kingine, isipokuwa siasa. Hawawezi kutabiri kwamba mvua itanyesha lini ili walime na kujipatia chakula-kuondoa njaa na umasikini, ila ni kuongea siasa tena umbeya usio na mashiko!
Kwa majuma mawili, nilitembea vijiweni mjini, lakini sikukuta watu wanongea kingine,isipokuwa uchaguzi wa Igunga.
Vituo vya redio na televisheni navyo havikuwa nyuma na Kiswahili chao kibovu cha “lisaa limoja!” badala ya saa moja, kuzungumza Igunga!
 Magazeti ndiyo usiseme: Yalitabiri hadi mshindi na atakayeshindwa,utadhani Marehemu Yahya Hussein,mwisho wa siku, sasa habari zimegeuka umbeya tu.
Nilishachoshwa na siasa,ndiyo maana sitaki kuandika siasa hizi na niliapa kutoandika neno  “Igunga” leo naandika mara ya kwanza na  ya mwisho neno hilo.
Hapa Afrika ya Mashariki, kwa kipindi hiki kulikuwa na jambo muhimu sana la kuzungumza.
 Kifo cha Mwanaharakati wa Mazingira nchini Kenya, Prof. Wangari Maathai.Hata Wakenya wenyewe hawakuadhimisha sana kifo cha Wangari Maathai, kama vyombo vya habari vya nje vilivyofanya.
Prof. Wangari Maathai ameenziwa mno na vyombo vya habari vya kigeni, hadi Wakenya wenyewe wamestuka, na kumpa siku mbili tu za bendera kupepea nusu mlingoti.
Binafsi, simpendi Wangari Maathaai kwa kuwa ni mwanamke wa kwanza kupata PhD, ama kuwa Profesa hapa Afrika Mashariki.
 Bali, Wangari Maathai alikuwa mkweli sana, mwana harakati,mwanamapinduzi,Mwafrika halisi,mzalendo wa kweli,msomi mwenye shahada ya uzamivu,lakini mwanakijiji, na mwanamke wa Kiafrika aliyebaki hivi tu, Mwafrika halisi, hata kama alisoma hadi kupata PhD!
Kwa mwanamke msomi,kupata fedha na tuzo ya NOBEL halafu akawa Mwafrika tu, bila kupaka mkorogo,wala dawa za Kichina za kuongeza makalio na “Uzungu” hewa, na bandia, mimi namlilia mama huyu!
 Ingawa aliachika kwa mumewe, Prof. Wangari Maathai, ametoweka Afrika imepata pengo la Mwanamapinduzi halisi!
Kila ninakotembea Mjini na vijijini,naona nywele za singa za kubumba, naona ‘Wazungu-pori’ wengi tu, hata wengine wanajifunika khanga,kuogopa kuungua jua!
Wangari Maathai, niliyemwona juzi kwenye kipindi cha ‘Straight Talk Africa’ cha Sauti ya Amerika(VoA) akiwa kwenye vitalu vyake vya miche ya miti kijijini,badala ya kushinda kwenye saluni akisula nywele na kusikiliza umbeya wa akina mama wasomi wa mjini!
Prof. Wangari Maathai,huyu Mwanaharakati wa Mazingira na Haki za Binadamu wa Kenya, aliyewavurumisha Marais kama Daniel Arap Moi, Dikteta wa zama za Nyayo, na Mwai Kibaki,kwa kauli za kutaka haki na demokrasia,ndiye huyu anayenifanya mimi nimlilie hapa.
Wangari Maathai aliyetoka kabila moja na Rais Emilio Mwai Kibaki, la Wakikuyu huko Central Province, lakini akataka ukweli na haki kwa watu wote,ndiye huyu ninayemwombolezea hapa.
Nadharau mambo ya huko nilikotaja kwa mara ya mwisho,ambako kura zimepigwa juzi na watu wakaanza kupigana na kudhalilishana.
Nasahau hata ushindi wa chama chochote ili nimzungumze Mwanamke huyu wa chuma, “the Iron-lady” Profesa Wangari Maathai kwa uzalendo wake kwa Afrika yetu.
Wangari Maathai alikuwa Profesa mwenye PhD,Marekani, Ujerumani na hata Chuo Kikuu cha Nairobi,lakini Mwafrika tu,aliyeshinda katika vitalu vya kuotesha miche ya miti,badala ya kushinda kwenye vilabu, kwenye saluni na kwenye miradi yake, au akinunua vitu vya thamani madukani.
Wangari Maathai alikula machungwa,badala ya Juice za Supermarket, alikula mhogo badala ya chips; alivaa gauni refu badala ya nguo fupi zenye mipasuo zinazoitwa,”Macho Pitiliza”.
Prof.Wangari Maathai alibeba mtungi mgongoni mwake kama wafanyavyo wanawake wengi wa huko CENTRAL PROVINCE na hata hapa Tanzania.
Wangari Maaathai, alisoma vitabuni mwa Wazungu lakini hakuathiriwa na kasumba ya Kikoloni, Colonial Mentality, aliongea vizuri badala ya kuongelea puani,kama vimwana wa siku hizi.
 Wangari Maathai,alizungumza Kiafrika, alipambana siasa za kiafrika, alikuwa Mwafrika hasa,alikula kiafrika,alivaa kiafrika,alitembea kiafrika,alinena kiafrika, ameondoka kiafrika!
Wangari Maathai alisema akifa, asizikwe kwa majeneza ya miti; yaani wasisumbue miti, wasikate miti kumzika kwa jeneza la mbao!
 Huyu mama aliipenda misitu. Misitu inayoleta mvua, inayoleta chakula,inaleta uchumi wa wananchi, misitu na miti ni chanzo cha maisha ya watu.
Misitu inaweza kuwepo pasipo watu,lakini watu hawawezi kuwepo pasipo misitu.Wangari Maathai alilijua hili akathamini misitu kwa dhati, alipanda miche pasipo kutandikiwa mikeka kama tunavyoona huku akina Rais Kikwete,Lowassa, Dk.Shein na wengine wengi wanatandikiwa mikeka waweke magoti wanapopanda miti!
Utamaduni wa Kiafrika kweli kupanda miti mnapotandika mikeka, mashuka na vitambaa ama majamvi wakati wa kupanda miti?
Hapa Afrika,ni viongozi miamba wawili,tu waliopanda miti bila kutandikiwa vitanda na mashuka,ili suti zao zisichafuke!
 Ni nyerere na Prof. Wangari Maathai. Nyerere alivaa magwanda yake ya JKT, na Wangari Maathai yeye alipanda miti akiwa amevaa gauni lake la kazi, hakuna kuvaa suti wala miwani ya jua!
Wangari Maathai hakuigiza; alifanya kweli!
 Huyu shujaa amekufa wakati sisi tukijadili michezo ya kuigiza huko Igung…samahani! Sitalitaja tena neno hilo,limesemwa mno hata linachusha sasa.
Nataka kusema kwamba,huyu ndiye shujaa aliyekufa juzi wakati huku wanapiga porojo za siasa huko mkoani Tabora,na mimi nataka mashabiki wa siasa wamfahamu na kumuenzi kwa kutodharau uafrika na kupaka rangi midomo wawe kama ndege ambao kwetu wanaita ‘ji-sore’.
Wangari, hakupaka Mikorogo,hakupaka dawa za Ki-China kuongeza makalio awe mrembo. Alikuwa Mwafrika-BINTI wa Afrika hata mauti yalipomkumba,kufuatia kansa ya shingo ya uzazi.
Alizaa.Siku hizi mabinti hawataki kuzaa, ni          “test-tube babies” ama watoto wa chupa, na wanafanyiwa operesheni,ili nani hii zisipanuke, wasije kuwa wazee kama mama yangu,Nyasongorwa, ama kama Prof. Wangari Maathai.
Wangari ati alisoma chuo kikuu akapata PhD bila kujiita jina la Mzungu!
‘Rose’ ama Agnes, bali Wangari Maathai tu! Wangari hakuvaa ‘Mapanga shaa!’ wala nguo za aibu za kuacha mapaja nje-nje utadhani business!
Haki za wanawake?
 Buriani Wangari Maathai.
Itaendelea
0786-324 074

No comments:

Post a Comment