Thursday, June 21, 2012

israeli dhidi ya waarabu




 *Mashariki ya Kati ni “Focal Point” ya Dunia
 
VITA vya karne nzima, baina ya Waarabu na Israeli kwa upande mmoja, na mnyukano baina ya Waarabu na Mataifa Makubwa ya Ulaya na Marekani kwa upande wa pili, hatimaye madhara yake yamefika kila Bara,kila nchi.
  Katika makala nyingi zilizotangulia,nimeandika sana juu ya Misri ya Anwar Sadat alivyofanya shambulizi la kustukiza huko Israeli, Oktoba, mwaka 1973.
  Nimeandika pia mnukano wa makundi ya wanamapinduzi wa Kipalestina kumenyana na Mataifa ya Magharibi kwa staili ya ‘kigaidi’ zama za  Carlos The Jackal.
Nimeandika vita Baridi kufika hatma yake wakati wa Kuanguka kwa Ukuta wa Berlin mwanzoni mwa miaka ya 90,na kusambaratika kwa Dola la Kisovieti la USSR.
 Juma lililopita nimejadili matukio ya kigaidi ya Black September kuwasaka adui zao Waisraeli hadi Munich,Ujerumani, Septemba 5, mwaka 1972 wakati wa michezo ya Olimpiki.
  Kutoka zama za Black September, yaani Septemba ta utusitusi hadi sasa, akiina Carlos The Jackal wameishia kifungoni, akina Saddam Hussein, Muammar Gaddafi, Osama bin Laden na wenzao wamezimwa kwa mapinduzi ya kijeshi na wamelala makaburini,kufuatia jeuri na mtutu wa bunduki za rashasha.
 Tunakoelekea, mazungumzo ya Amani kama yale ya Camp David mwaka 1973 kati ya Israeli na Waarabu kwa upande mmoja, ama kati ya Waarabu na Ulaya na Marekani, hayatakuwa na maana zaidi ya kulazimishwa kusalim amri mithili ya kijibwa mbele ya dubu mwenye kiu ya damu.
  Naam, Waarabu kujisalimisha kwa njia ya kuufyata mkia mithili ya kijibwa mbele ya fisi,mbele ya Dola babe,jeuri na fisadi za Magharibi!!
Nguvu za Mataifa ya Kiarabu zinatindika sana. Nguvu hizi zilikuwa ndani ya pampu za mafuta katika miaka ya 70. Nguvu hizi zilikuwa katika majambia ya wanamgambo wa Kiarabu katika karne ya Sita hadi karne ya 15.
  Siku hizi, makampuni ya mafuta ya Marekani, Ufaransa, Uingereza, Italia,Uholanzi n.k yanahafifisha ‘nguvu’ za mataifa haya yanayozalisha sana ‘dhahabu nyeusi’ hii duniani. Majambia ya Wanamgambo wa Kiarabu yaliyofananishwa na “Mikia ya Nge”(Tazama Ufunuo 9:7-11) yamegeuka kuwa nyasi.
 Kitu kinachoweza kuonekana katika muktadha huu ni kile kiitwacho, “The Modern Middle East Oil Politics”.
   Nataka kusema kwamba, ‘Oval Office’  iliyoko White House chini ya Bwana Barack Obama, lengo lake ni kuhafifisha nguvu za uchumi(mafuta) wa Milki za Waarabu ama mataifa ya Mashariki ya Kati, huku akiibusu na kuikumbatia Israeli, wakati ‘Intifada’ nyinginezo ni maumivu kwa Mwarabu.
Shirika la Atomiki Duniani(IAEA)limearifiwa na maofisa wa Usalama wa Israeli kwamba Iran siku hizi inajidai kuweza kurutubisha zaidi ya kilogramu 630 za Uranium, ili waweze kutengeneza bomu la Nyuklia katika hatua za awali.
  Hata mataifa mengine ya Kiarabu ya Ghuba, kama Saudi Arabia na Bahrain yako tayuari kuwaunga mkono Marekani na Ulaya kuichakaza Iran ili isijitie ‘kidume’ na kughairi Amri Takatifu za Marekani,Ulaya, Israeli na NATO za kuachana na mradi wa Nyuklia.
  Iran itashambuliwa haraka sana isipojisalimisha chini ya mamlaka za Mzungu tapeli, ambaye hata sasa amezikalia Irak, Libya, Afghanistan, Misri,Libya,Syria na Mzungu anavuka Mto Frati na Tigris kuelekea kwingineko Mashariki.
  Leo, tuanze kulijadili Shirika la Ujasusi la Israeli, MOSSAD, ambalo nembo yake ni Vinara Saba vya Taa vilivyoanza kutumiwa na Waisraeli tangu zama za Nabii Musa, mwaka 1500 BC.
Mossad,ni majasusi hatari duniani ambao hujuma zao zimetamalaki hadi Afrika ya Mashariki tangu mapema mwaka 1976.
Tujadili kidogo mapambano baina ya Chama cha Ukombozi cha Palestina, POPULAR FRONT FOR THE LIBERATION OF PALESTINE (PFLP) dhidi ya Israeli na washirika wake wa Magharibi; vita vilivyopanuka hadi kufika Entebbe,Uganda miaka ya 70.
Vita kama hivyo vingalipo leo baina ya Al-Shabaab,al-Qaeda dhidi ya maslahi ya Magharibi hata hapa Afrika ya Mashariki.
   Entebbe,Uganda tuliona mapambano ya PFLP wakati ule Carlos The Jackal akiongoza hujuma tele dhidi ya Magharibi.
 Ndege ya Ufaransa, Air France Air Bus A 300,iliyokuwa na nambari za Usajili BVGG ilijikuta ikitekwa nyara Juni 27 mwaka 1976.
  Sasa, Uganda wanakumuka miaka 36 kamili ya tukio hilo la kihistoria. Ndege hiyo ilitokea Athens, Ugiriki inayofilisika, ikalazimishwa kwenda kutua Entebbe.
 Ilikuwa na jumla ya abiria 248 na wafanyakazi dazeni,ilitekwa na Wapalestina wawili walioshirikiana wa PFLP kitengo cha Operesheni za Nje kiitwacho PFLP-LEO, na walisaidiwa na Wajerumani wawili wa kikundi cha kimapinduzi  cha German Revolutionary Cells.
Wilfred Bose na Brigite Kuhlmann. Ilikuwa saa 6:30 hivi mchana, Juni 26 kama leo mwaka 1976 ndege hiyo ilipotekwa angani ikalazimishwa kwenda kutua mjini Benghazi,Libya.
 Zama za Muammar Gaddafi, ndege hiyo ikatua Benghazi na kujaza mafuta,ikapumzika kwa muda wa saa saba.
 Mwanamama raia wa Uingereza aliyekuwa mjamzito akajidai kuumwa utungu wa kuzaa mtoto, akaachiwa huru hapo Beghazi,kabla ya safari ya Entebbe,kuanza.
  Nataka msomaji atambue kwamba kuachiwa huru mwanamama huyu kulifikisha habari mjini Tel Aviv mapema, wakaanzisha mkakati kamambe wa kuwakomboa mateka wao katika ardhi ya Uganda.
  Saa tisa na robo, siku iliyofuata, yaani Juni 28 mwaka 1976 hiyo Air Bus ilitua Entebbe, wale mateka wengine ambao nao hawakuwa Waisraeli wakaachiwa huru-kosa lingine.
 Maana yake ni kwamba, serikali ya Israeli ilimaizi kuwa raia wake ambao walikuwa mikononi mwa watekaji wa Kipalestina, walikuwa mikononi mwa mauti. Hivyo, Waziri Mkuu wan chi hiyo akalazimishwa kufanya kila njia waokolewe, hata kama kufanya hivyo kulikuwa kukiuka sheria za kimataifa,kama ugaidi ama mashambulizi ya kijeshi dhidi ya nchi nyingine.Wewe ungeanza mazungunzo ya kidiplomasia ya akina Thabo Mbeki au Kofi Annan.
 Makomando wa Israeli walitua Entebbe,Uganda, na kumshikisha adabu Idi Amin Dada aliyejitia Mshindi wa Dola ya Kingereza,Mwanamasumbwi nguli na Field Marshal.
 Rais wa Maisha wa Uganda alikiona cha mtema kuni mbele ya makomando 100 wa Israeli.Wakati huo Uganda ilikuwa rafiki wa Waarabu, na walijifanya adui wa Israeli.Akina Ghaddafi na Palestina walimponza Amin,
Yule mwanamke wa Kiingereza na mateka wengine walipoachwa, wakasema kupitia vyombo vya habari,kwamba huenda mateka wale wa Israeli wangeuliwa kinyama mkononi mwa adui zao Wapalestina.
 Basi,Makomando walifanya mazoezi kwa muda mfupi wakafika Uganda usiku ili kukomesha kiburi cha Dikteta aliyejifanya mbabe katika medani ya vita. Zama za Waziri Mkuu,Menachem Begin, Shirika la kijasusi la MOSSAD likawezesha makomando wenye vinara saba vya taa(Mwangaza Mkamilifu) kutua Entebbe kwa saa moja na nusu tu na kufanikiwa kuwakomboa mateka wake.
 Hii Operesheni ina majina mengi, inaitwa Operation Thunderbolt, wengine huiita kwa jina la Komando aliyeuliwa pale, Jonathan ama  ‘Yonnie’ Huyu Jonathan Netanyahu alikuwa ndugu wa damu wa Waziri Mkuu wa sasa wa Israeli, Benyamin Netanyahu.
  Wengine tumeiona Operesheni hii kwenye Filamu ya RAID ON ENTEBBE na tumepata kusoma kitabu kiitwacho, 90 Minutes at Entebbe. Usinisumbue kuuliza wapi utakipata!!
  Luteni Kanali Jonathan ‘Yonnie’ Netanyahu alikufa Entebbe,lakini walifanikiwa kuondoka na maiti yake na akazikwa kishujaa.Abiria 103 waliokuwa mateka Waisraeli mikononi mwa adui zao Waarabu, walikombolewa hatimaye. Hawa 103 walikuwa miongoni mwa abiria 248 wa ile Air Bus ya Ufaransa.
 Ni usiku wa manane hiyo Operesheni ilipofanyika Entebbe,kilomita kama 27 kutoka Kampala, Amin hakujua aliamkia kupapasa maiti za askari wake 45 asubuhi, wakati makomando walishaondoka mapema kabla ya alfajiri.
 Uwanja wa ndege wa Entebbe uliharibiwa kwa mabomu  wakati watekanyara wote walifyekwa kwa risasi za makomandoo wa Israeli.
 Ngege iliyowaleta Makomandoo hawa iliruka kwa takriban kilomita 4000 hivi ikawaleta makomando 100 waliokata mzizi wa fitina Entebbe.
 Makomando watano walijeruhiwa,mmoja akafa lakini askari wa Amin 45 na wateka nyara wote walipigwa risasi, mateka watatu walikufa pia.
 Ndege ya Kirusi MIG-17 ilisambaratishwa vibaya.
 Itaendelea




0786 324 074

No comments:

Post a Comment