Monday, November 5, 2012

UNALIJUA JIJI LA MWANZA?


                                      TAHADHARI!!
 *Mwanza kuendelea kubugia  kinyesi na kemikali za sumu wasipodhibitiwa kwa sheria kali
 
WAZIRI WA ARDHI,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Kajumlo Tibaijuka, aliwahi kusema kwamba, Mwanza ni miongoni mwa miji iliyojengwa pasipokuzingatia sheria za makazi na ulinzi wa mazingira.
Jiji hili lilijengwa na Mjerumani, Emin Pasha,mwaka 1892,ili kuwa kituo cha ununuzi wa mazao ya biashara kama pamba,katika ukanda wa ziwa.
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Daniel Ole Njoolay, Machi 5,mwaka 2004 wakati akizindua Mradi wa   Majitaka jijini Mwanza,alisema Jiji hili linaongoza kuwa na watu wengi wanaoishi katika eneo  eneo dogo(high population density),kiasi cha kuchafua mazingira,hususan vyanzo vya maji.
Jiji la Mwanza sasa hukadiriwa kuwa na wakazi takriban milioni moja, ambao kwa siku hunywa maji safi kiasi cha mita za ujazo 70,000.Wakazi wa Mwanza,kwa siku huzalisha maji taka,zaidi kinyesi,kiasi cha lita milioni 38.Asilimia  90 ya maji taka hurejea Ziwa Victoria bila kutibiwa.
Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Majisafi na Taka Mwanza(MWAUWASA),Robert Masunya,katika mahojiano na safu hii juzi, anasema wakazi wa Mwanza kwa siku hunywa maji yenye ujazo wa lita milioni 70.
Hii ni sawa na kusema,kwa siku wakazi wa Jiji hili,ambao wao wenyewe huita,” The Rock City” hunywa kiasi cha mapipa 350,000 ya maji safi ya MWAUWASA. Maji taka wanayozalisha(kinyesi,uchafu na kemikali za sumu) ni sawa na mapipa 200,000 ambayo humwagwa ziwani kila siku.
Afisa Uhusiano wa MWAUWASA,Robert Nasunya, ameiambia safi hii kwamba,ifikapo mwaka 2020,uwezo wao ni kuzalisha maji safi na salama yenye viwango vya ubora wa kimataifa kufikia mita za ujazo 108,000 ambazo ni sawa na lita milioni 108, ama mapipa 549,000 kila siku.
MWAUWASA wana matangi matano yenye uwezo wa kuhifadhi maji yenye ujazo wa mita 27,000,sawa na lita milioni 27.
 Kutokana na ujenzi holela usiozingatia sheria za makazi,MWAUWASA wanapozalisha maji mengi hata kiwango kisichotumika(Idle Capacity),yapo maeneo ambayo hayapati maji ya bomba yaliyotibiwa na kusafishwa.
Maeneo hayo hayafikiwi na maji ya bomba; mengi yako katika miinuko mikali,vilimani,kwa sababu maji ya bomba hutiririka kwa ‘gravity’,hayapandi mlima mpaka yasukumwe kwa mashine kama pampu.
Maeneo ya vilimani(Mwanza huzungukwa na vilima,miamba na mawe)yasiyopata maji ni pamoja na Kabuhoro, Ibanda,na Mji Mwema.Mengine ni Sangabuye,Kayenze na Bugogwa.
Afisa Uhusiano wa MWAUWASA,Masunya anasema, wakati wakazi wa Mwanza wanakunywa maji safi lita 70 milioni kwa siku moja, na wakati uwezo wa MWAUWASA ni kuzalisha lita milioni 108 kwa siku moja, lita 30 milioni hubaki-hushindwa kuwafikia watu.
Masunya anasema, wakazi hawa wa Mwanza huzalisha lita milioni 40 za taka zikiwemo kemikali za majumbani, hospitalini,viwandani,madukani na hata kinyesi cha binadamu na mifugo.
Serikali na Jumuiya ya Ulaya(EU) wamejenga mfumo wa kusukuma maji taka kutoka lita 35 hadi lita 170 kwa sekunde.Maji haya taka husukumwa hadi katika mabwawa 10 yaliyoko Butuja,Ilemela ambako hutibiwa kabla ya kurejeshwa Ziwani Victoria.
Mradi huu ulifadhhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani(KfW) na ukakamilika Oktoba mwaka 2010.Una uwezo wa kukusanya majitaka ya kiwango cha  asilimia 15 tu ya wakazi wa Jiji linalokuwa kila siku. Ukiamka asubuhi,unakuta vijumba vimeota milimani,pasi na ruhusa ya Mipango miji!
Asilimia 9 ya wakazi wa  Jiji hili la miamba,ndiyo waliounganisha maji yao katika mfumo huu wa maji taka,nao hawazidi wateja 2,000. Hawa ndiyo kinyesi chao na kemikali zao husafishwa na kurejeshwa ziwani.
Nimezungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA,Anthony Sanga, Alhamisi iliyopita, akasema mfumo wa MWAUWASA wa kutibu maji taka,hufanya kazi chini ya kiwango,kwa sababu wakazi wa jiji wameshindwa kuunganisha makaro yao ya maji machafu kwenye mfumo huo wa kutibu maji taka.
Sanga, ananiambia kwamba sasa wameanzisha mpango wa kuwakopesha wananchi ili waunganishe maji taka yao kwenye mfumo wa maji taka.Wanachotakiwa kufanya ni kulipa sh.5,000/ tu,halafu watakatwa pole pole baada ya kuingia mkataba.
Mfumo huu wa maji taka ulijengwa na Sirling International ya Italia. Na kulingana na MWAUWASA,Mwanza kuna vyanzo vya maji safi katika eneo la Capri Point,Chakula Barafu na Luchelele, ambavyo vyote hutoa maji Ziwa Victoria linalochafuliwa kwa kinyesi kisichorejezwa(recycled) kwa kutibiwa Butuja.
Kuna mpango wa kuongeza chanzo kingine cha maji chenye uwezo wa kuzalisha mita za ujazo 50,000 kwa siku ili kuondoa shida ya maji Kabuhoro,Ibanda na maeneo mengine wanakolazimika kunywa maji ya ziwani yasiyotibiwa na kupimwa kitaalam,ili kudhibiti uchafu na kiwango cha kemikali.
Kemikali zinaweza kuleta madhara ya afya kwa binadamu na wanyama.Ziwa Victoria liko kandoni mwa migodi ya dhahabu ambayo hutumia zebaki(mercury)kusafishia dhahabu,na kasha mvua zinaponyesha husomba zebaki hiyo hadi ziwani na kuua samaki,wanyama,binadamu kasha kuharibu mazingira.
Hata hivyo,licha ya MWAUWASA kuzalisha maji kwa kiwango cha ziada,Mwanza ni jiji ambalo wakazi wake hunywa maji ya chupa ya Uhai kutoka Dar es salaam, Kilimanjaro, wakati mwingine wanakunywa Rwenzori,kutoka Milima ya Rwenzori huko Uganda!
Yaani, bei ya lita moja ya maji ya kunywa Mwanza haina tofauti kubwa na bei ya lita ya petrol kutoka Arabuni,wakazi Ziwa tunalo hapa,lakini maji yamechafuliwa kwa kinyesi! Fika Mwaloni Kirumba,utajionea kinyesi majini,Ziwani…hii ndiyo Mwanza!
Sasa,Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA,Anthony Sanga, ananiambia labda sheria zitumike sasa kuwabana watu wanaotiririsha maji taka Ziwani, wanaokataa kuunganisha majitaka yao katika mfumo wa MWAUWASA,ili yakatibiwe Butuja.
Wakati wa mvua,watu hutapisha vyoo vyao na hufungulia makaro ya maji taka ambayo huingia ziwani. Kutiririsha kinyesi mitaroni Mwanza ni kitu cha kawaida. Halafu eti Mwanza ndilo jiji safi kuliko yote Tanzania!!
Zaidi ya asilimia 90 ya wakazi wa Mwanza,ambao huishi vilimani katika makazi yasiyopimwa,hhutiririsha kinyesi na kemikali ziwani. Maji ya ziwa yanapotumiwa pasipo kuchemshwa ni hatari.
Novemba, 22 mwaka 2005,aliyekuwa Mkemia Mkuu wa Serikali,  Dk.Ernest  Mashimba, alisema jijini Mwanza kuwa Sheria namba 3 ya mwaka 2003 ya Udhibiti wa Kemikali Viwandani na Majumbani,haizingatiwi na wakazi wa jiji hili.
Hayati,Dk. Mashimba alisema,Mwanza ni miongoni mwa maeneo ambayo kuna uvuvi haramu kwa kutumia kemikali za sumu.Wakati wavuvi wanapovua kwa kutumia sumu,humwaga kemikali hizo ziwani na kuhatarisha maisha ya viumbe.
Makopo ya sumu Mwanza hutupwa mitaroni na kuachwa kuingia ziwa Victoria,wakati sheria hii inawataka kuzika makopo hayo au kuyarejesha viwandani,yaharibiwe.
Kulingana na Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa(WHO)asilimia kubwa ya watu wanaodhuriwa na sumu ni kama hawa wakazi wa Mwanza,ambao huacha hata sumu za kuulia wadudu kuingia ziwani.
Maradhi yanayoongoza kuwaua watu wengi Mwanza ni minyoo,kichocho,kuhara damu,safura,homa za matumbo na hata kipindupindu-hii ni kutokana na kunywa kinyesi hiki wanachorudisha ziwani; kuliko na chanzo chao cha maji.
Mwanza,watu hubugia kinyesi chao kwa hiari!!
Ili kunusuru hali hii,Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Anthony Sanga, anasema sheria zitumike kuwafanya wakazi wa Mwanza kuunganisha maji taka yao na mfumo rasmi wa maji taka wa MWAUWASA.
0713 324 074
 
 
 
 
 
 
 
 
 

No comments:

Post a Comment