Monday, January 28, 2013

Ati ulaya na marekani kuna haki za binadamu?-8


 Agosti 7 mwaka huu  2013 tutakuwa tunakumbuka miaka15 ya  mashambulizi ya magaidi yaliyofanywa katika Balozi za Marekani, Dar es salaam na Nairobi ; mwaka 1998.
    Zaidi ya watu 240 walikufa; hawa hawakuwa wa  Kenya pekee bali pia wa Tanzania . Hawakuwa wa kabila moja au wa  dini fulani, waliokuwa wakisali msikiti mmoja ama kanisa fulani.Magaidi ni hatari kwa raia wote wa dunia.
    Tunawaombolezea waathirika wa tukio hilo la Agosti 7 mwaka huo wa 1998, ambalo msingi mkubwa ni uadui kati ya Marekani na Waarabu walioamua kuisaka Marekani popote duniani, ili kulipa kisasi.
    Naam,kuisaka Marekani katika ardhi yetu, kusababisha hasara ya maisha na mali za watu wetu, ni vitu tunavyovipinga leo na kesho hata kama mbingu zishuke; ama jua litue mchana saa saba!
    Si lengo la safu kusema kwamba magaidi ni Waarabu peke yao, ama watu wa imani fulani. Nitajadili malengo ya ugaidi na chimbuko lake. Nitajadili imani inavyoupa msukumo na nguvu ugaidi duniani.
   Kuna vikundi tele vya kigaidi duniani. Usishangae, hakuna gaidi anayejiita gaidi. Wote wanajiita, wanaharakati(activists) wa ‘Haki’ za ubinadamu wao. Ugaidi unakula maisha ya watu na mali vinapopotea au kuharibiwa.
  Kila mmoja ana tafsiri yake ya ugaidi.
Sitajali kusikia Rais Mstaafu George W. Bush wa Marekani naye ni gaidi kama Osama bin Laden. Hata hivyo, najua, magaidi kama wale waliolipua Balozi la Marekani Dar es salaam na Nairobi, Agosti 7 miaka 15 iliyopita, wote ni wauaji; wanastahili adhabu kali.
   A-Qaeda ni kundi la harakati za kigaidi, bila kujali wanaharakati wake wanatokana na itikadi gani. Japan, kuna kundi moja linaitwa, “Ukweli Mkuu” kwa Kijapani, Aum shinrikyo-hawa nao hata wakifanya mauaji, watasema wameua ili kuueneza huo Ukweli(The supreme Truth). Mauaji hayaenezi haki yoyote.
   Uhispania, kuna kundi linaitwa, ETA(Freedom for The Bosque Homeland), nalo linadai uhuru. Lebanon , kuna kundi maarufu sana kama , Hezbollah(Chama cha Bwana Mungu), wakati Ireland Kaskazini kuna kundi liitwalo, Irish Republican Army(IRA).
    Nchini Israeli, kitovu cha uadui wa mgogoro wa Mashariki ya Kati, kuna kundi liitwalo, Kach and Kahane Chai, Uturuki kuna PKK(Kurdistan Peoples Party), Sri Lanka kuna, Liberation Tigers of Tamil Eelam(LTTE); wakati nchini Iran kuna Mujahedin-E-Khalq.
   Ugiriki kuna kundi linaitwa, November 17 Revolution. Juzi tulisikia kundi la FARC(Revolutionary Armed Forces of Columbia) likifanya utekaji nyara; lakini ni ‘Jeshi la Kimapinduzi’.Jeshi la kimapinduzi hupindua raia?
   Hakuna anayemaizi kuwa matendo yake ni kinyume cha sheria za nchi, za kimataifa, ama ubinadamu. Wengine wanajisingizia, wametumwa na Mungu ili kuwaua binadamu wenzao, waabudu sanamu ama wapagani.
  Wapo, Shining Path kule Peru . Columbia pia kuna National           Liberation Army(ELN), na Ufilipino kuna New Peoples Army.
    Tumjadili kidogo tu, gaidi la kale, Ilych Ramirez Sanchez, ambaye kwa utani anaitwa, Carlos The Jackal-mzaliwa wa mjini Caracas , Venezuela .
Venezuela , ni nchi anayoongoza Hugo Chavez, anayeugua kansa huko Cuba, ambaye alimtukana rais Bush, wakati anahutubia Mkutano wa Umoja wa Mataija, jijini New York , akapewa saa chache awe ameondoka nchini humo.
   Carlos, gaidi anayetumikia kifungo cha maisha   Ufaransa, ikifika Oktoba 12 mwaka huu, atakuwa anaadhimisha miaka 64 ya kuzaliwa kwake.
  Sasa, huyu jamaa katika mafaili ya uhalifu na Jinai duniani, kuna mambo yake mengi, ambayo yametokana na chuki za siku nyingi kati ya nchi za Amerika ya Kusini(zilifuata siasa za Ki- Marx) na Marekani. Carlos, ambaye baba yake alikuwa mjamaa, alimpeleka Chuo Kikuu cha Patrice Lumbumba, mjini Moscow , kusoma.
   Huko alikutana na Wapalestina, akaiva katika siasa za mrengo tofauti na ubeberu wa Kimarekani.
   Hata jina ‘Ilych’  aliitwa na babaye ili kuwaenzi ‘makomredi’ wa Urusi ya Ujamaa, akina Lenin.
   Sasa Carlos anaipinga Marekani hata huko jela, alishasema anamuunga mkono Osama bin Laden, kwa asilimia 100; na kwamba anawataka watu wasiache kujitoa mhanga ili kufa na Wamarekani, popote walipo!
   Nitajadili kauli hii baadaye kidogo.
Hata hivyo, huyu jamaa aliyetiwa mbaroni na mashushushu wa Ufaransa akiwa mjini Khartoum, Sudan alishakaa Urusi tangu 1968, amekaa Ujerumani mwaka 79, amekaa Syria 91-93, na Ufaransa. Vituko vyake unaweza kuvipata katika sinema za akina James Bond.
  Hapa, nitajadili ugaidi, si Carlos.
   Naam, ugaidi wa Agosti 7 mwaka 1998, ulileta hadithi nyingi. Lakini, tuseme kwamba wale magaidi walishambulia Balozi za Marekani Dar es salaam na Nairobi , karibia muda uleule mmoja, kwa sababu nchi hizi hazikuwa zimejiandaa.
   Wengine wanasema hata Kampala ingeshambuliwa. Kilichoiponya ati ujio wa Rais Bill Clinton wakati ule mjini Kampala , ulivifanya vikosi vya usalama vya Uganda kuwa ‘more alert’ kuliko Dar na Nairobi ! Hayo tuyaache.
     Shambulizi lingine la magaidi Afrika Mashariki lilifika Novemba 28 mwaka 2002. Magaidi waliua watu 16 mjini Mombasa, katika hoteli ya Paradise iliyoko Kikambala. Ni kilomita 25 kutoka mjini Mombasa.
   Hii hoteli ni ya Waisraeli; sasa unaweza kukisia hata wewe, kwamba ilishambuliwa na adui zao Wapalestina. Wapalestina walikuja Afrika Mashariki kuwawinda adui zao Waisraeli, katika ardhi ya Kenya. Hawakuua Waisraeli tu, waliua na Wakenya, na raia wa mataifa mengine.
   Sasa tuseme, vita vya kudai uhuru vinavyoendeshwa na Wapalestina dhidi ya Mayahudi, vina leseni ya kuua na kuumiza binadamu wengine wasio na hatia?
   Halafu, hao magaidi wa Kipalestina walifanya jaribio la kuilipua ndege ya Arkia Airlines ya Israeli, iliyokuwa ikiruka kutoka uwanja wa ndege wa Moi, mjini Mombasa. Bahati tu, lile kombora, bila shaka la Kirusi, liliikosa- kosa ndege ile iliyokuwa na abiria 271 hivi.
    Fikiria, kama kombora lile lingeipata ndege ile,wangekufa Waisraeli pekee? Hata raia wa mataifa mengine, wasiojua uadui waa Israeli na Wapalestina wangeungua katika miali ya moto wa mlipuko. Sasa ugaidi unasura ya ukombozi  au uokozi na uhuru wa wapi?
   Narejea mada yangu ya madhara ya ugaidi Afrika Mashariki. Matukio yote ya ugaidi yalisababisha watu mamia kufa, inakisiwa kulitokea hasara ya dola mabilioni. Ili kuponya majeraha ya ugaidi, zimetumika dola matrilioni, ambazo pengine zingetumiwa kuleta maendeleo-ugaidi ni adui wa maendeleo ya watu.
   Nimesema magaidi wapo Wazungu kama IRA, na wa mataifa mengine kama akina Carlos The Jackal; lakini ni magaidi. Magaidi hawana rangi, dini ama taifa moja.
   Ugaidi ni mauaji ya kinyama yanayoendana na matakwa ya ulipaji kisasi. Pengine, magaidi kama Black Banners wa Iraki, wakati ule wa vita, waliwateka jamaa watatu wa Kenya, ili kutafuta fedha kutoka kwa makampuni waliyofanyia kazi.
   Sasa nijadili jambo ambalo watu hupenda kunitolea  matusi. Watoa lugha chafu, hawana weledi juu ya lolote. Silaha yao ni matusi na vitisho. Wanadhani, ukweli ni ule unaolingana na wanavyopenda, ama wanyofikiria wao.
    Hata hivyo, ugaidi ni unyama, hata Mungu mahali popote hajawahi kusema watu walipizane visasi. Sera za ‘Jino kwa Jino’ ama ‘TIT FOR TAT’ ni za Ibilisi. Mungu anawataka watu kutong’oana meno, ili kulipa baya kwa baya?
 ungu anawataka watu wawe vibogoyo au chongo?
  Juzi, Papa Benedict XVI ameungama kwamba Kanisa Katoliki nalo lilishafanya ugaidi. Ugaidi hauna rangi, kanisa, msikiti wala watu wa kabila moja.
   Nilipata kutukanwa na hawa jamaa kwa kupinga kauli ya Carlos, kuwataka watu kufuga midevu mingi kama shamba la miwa la Kilombero, halafu  eti wasiache kujilipua ili kuwakomesha Wamarekani, popote watakapowaona!
    Sasa kama Carlos kawaambia, kwa nini wasiende kujilipua New York au Washington ? Kwa nini Mombasa , Nairobi au Dar? Huku Wamarekani hawapo! Mkijilipua huku mnatuumiza sisi, wao hawapo. Kama wapo ni mmoja tu au wawili-wafuateni Wamarekani kwenye uwanja wa mapambano! Wenye uwezo walikwenda kulipua New York na Washington, Septemba 11 mwaka 2001; hadi leo historia inaelekea kuwasahau.
   Sipendi kuamini kuwa, mtu mwenye uwezo wa kufikiri anaweza kuwa’Shahidi’ mwaminifu wa imani yake(uwe Ukristo,upagani ama Uislamu)kwa kujilipua, ili afe yeye na kumuua adui!
   Huku ni kushika dini kupita kiasi(fanaticism), kunakogeuza dini kuwa vifo na mauti, kwamba ni ushahidi(martyr). Hii si Jihad halali kuua hata watoto wasio na hatia, kwa sababu tu walikaa meza moja na adui.Kwa nini kuua adui mmoja kati ya ndugu mamia?
    Najua vita kati ya Waisraeli na Waarabu wa Mashariki ya Kati, inaitwa ‘Vita kati ya wema na uovu’. Sasa kama pande mbili zinaua hata wasiohusika, mwema nani na mwovu ana alama gani?
   George Bush na Tony Blair, wakati wanaishambulia Irak, walisema ni vita dhidi ya watu wasiostaarabika. Wakati magaidi waliposhambulia London, wakasema ni vita dhidi ya ustaarabu.Sasa tujiulize pia, kuua watu wasiohusika hata huko Irak ni ustaarabu? Ni kwa sababu hii, safu hii inasisitiza kuwa mauaji ni jinai, na kila muuaji ni Ibilisi mwenye mikia saba.
    Hakuna kitabu kitakatifu kinachotuma watu kuwaua wenzao wasioamini ama waabudu sanamu. Ndiyo maana hapa Tanzania si lazima kwa mujibu wa Katiba mtu kuwa dini fulani.Hata wapagani na waabudu sanamu ni watu; wasiuawe kwa kutokuwa na dini kwao.
   Nasema hivi kwa sababu rafiki yangu aliniambia, Allah kasema kuua hawa walao nguruwe ni kupata thawabu hata akhera!(to be elevated to a higher plane of existence, where life is an eternal bliss).
   Ni kwa sababu hii, msomi na mhadhiri, Imam  mashuhuri anasema kila siku, kwamba Kuran inakataza kabisa kuua au kujitoa mhanga-na kwamba wanaofanya hivyo, hawafanyi kwa jina la Uislam; bali wanasaliti mafundisho ya Mtume Muhammad.
    “Hatutaruhusu imani yetu adhim kutekwa nyara na wahalifu”, alisema.
 Maneno kama haya kayasema Kiongozi wa zamani wa  Upinzani Bungeni , Hamad Rashid Mohamed, alipokuwa akitoa hutuba fupi wakati wa kuaga mwili wa Chacha Zakayo Wangwe, “Rasta” wa Tarime. Buriani Chacha Wangwe.
    Hamad Rashid, alisema alikwaruzana na Marehemu Chacha Wangwe, lakini wakasameheana, kwa sababu, Kuran inasema, ‘kusamehe ni lazima’ ili upate thawabu.Samehe 7 mara 70!
  Biblia inasema kusamehe ‘saba x sabini’ maana yake siku zote za maisha. Saba ni alama ya ukamilifu wa utimilifu; hivyo tusichoke kusamehe.
 Sasa  hata hapa mtanitukana na kutishia kunipiga kwa kuhimiza amani? Mungu gani kawaambia kumpiga mwenye mawazo tofauti nanyi? Dini yenu  ni ya amani, kwa nini Jino kwa Jino?
    Nilishasema katika makala mbili zilizotangulia, kwamba kuna upendeleo na ‘double standards’. Alichofanya Bush au Blair, akikifanya Mugabe au Mpalestina, ataitwa gaidi, wao “Patriots”.
  Hili ni tatizo ambalo haliondolewi kwa watu kujilipua, lawama hizi haziondoki kwa kujifunga mabomu. Hatupambani na ‘metropolitan power’ kwa kulipua Dar, Mombasa na Nairobi.Tunatakiwa kuilipua Washington kisayansi, maana yake kumlipua Bush pekee bila raia wasio na hatia.
   Ukijifunga bomu utamlipua Blair au Bush? La hasha. Utawalipua ndugu zako wa Dar, Mombasa ama Nairobi. Tutafute njia mwafaka ya kuondoa ‘double standards’ duniani. Tusijiite, “Liberators” ama ‘in the service of’ Allah’ kumbe wauaji wa ndugu zetu wenyewe.
  Tusidhani tunakomboa, kumbe tunajiua! Kujiua ni dhambi kubwa na kosa katika sheria za binadamu na Allah. Mashahidi waaminifu wa imani, hawatoki msikiti fulani tu, hata sinagogi au kanisa.
 Je, hamjaona watu wakienda uwanja wa ndege na biblia pasipo nauli,hati za kusafiria wala visa wakadhani Mungu atawapeleka Ulaya kuhubiri? Huku nako kujifunga mabomu! Magaidi hawana dini moja.
   Nimalize, kwa kusema Kuzimu kumepanua kinywa chake. Kuna visasi vingi tangu matukio ya Septemba 11 mwaka 2001. Lakini, tuangalie faida yake nini? Nani kasema ukifa kwa kujilipua kwa bomu na kuangamiza Mzungu mmoja na Waafrika wenzako 200 ni thawabu? Imani zisitugawe;sisi ni wamoja hapa Tanzania ama Afrika.
  Tutafakari msugoano uliopo kati ya Magharibi na Mashariki. Leo, siasa za akina Hugo Chavez, zinashindwa. Akina Carlos The Jackal wanaonekana majambazi tu, hata kama walifanya kazi bega kwa bega na makomredi kama Fidel Castro, katika kuzuia ubeberu.
  Hatuwezi kuupinga ubeberu kwa kuangamizana Paradise Mombasa, au katika usafiri wa ndege kama ile ya Arkia Airline, ama wa treli London.
  Hata katika balozi za Wazungu, kama Dar, Kampala na Nairobi, ukijilipua hukosi kuua Mzungu mmoja na Waafrika wenzako 300. Kuna thawabu gani hapo?
   Tufanyeje sasa? Tufikiri kwa makini; tuepuke kutukana watu, kupandisha mizuka ili kuhuisha roho ya kisasi. Tutaushinda uadui kwa akili na imani,  si imani bila busara. Busara hutoka kwa Mungu.Kwa mungu kuna haki na thawabu. Mungu ni wa utaratibu, si wa machafuko.Palipo na machafuko, hapana Mungu. Na sheria ni msumeno.
   . Ukweli si ule unaomfrahisha mtu; ukweli ni mchungu lakini mtamu. Ukweli ni ubinadamu. Tuimarishe ubinadamu-humanity.Ndivyo tunavyoikumbuka Septemba 11 mwaka 2001
  congesdaima@yahoo.com
  0754 324 074,0786 324 074



No comments:

Post a Comment