Friday, January 4, 2013

maandamano ya gesi mtwara


                                                      SAKATA LA GESI MTWARA
Na conges mramba
Maandamano yaliyofanywa na wakazi wa Mtwara kupinga gesi kusafirishwa hadi Dar esSalaam, ni mwangwi ya yaliyotokea Niger Delta,Nigeria,zama za Dikteta Sani Abacha.
Ni somo kwa Watanzania leo,kuhusu laana ya rasilimali-the resources curse.Palipo na rasilimali nyingi,watu huwa fukara,kwa nini?
Waliamka wanaharakati kupinga mafuta kuwaneemesha wenye makampuni ya kuchimba mafuta na vigogo wa serikali ya kijeshi ya Nigeria,zama za       Marehemu Dikteta Sani Abacha.
Makampuni ya mafuta,Royal/Dutch Shell la Waingereza na Waholanzi, likiwalipa polisi na jeshi mishahara na kulazimisha utawala wa Jen.Sani Abacha,lilishinikiza viongozi wa wanaharakati hao,akiwemo Saro-Wiwa,kukamatwa na kushitakiwa katika mahakama ya kijeshi(yeye alikuwa raia) kasha akauliwa na wenzake wanane kwa kupigwa risasi,Novemba 10,mwaka 1995.
Wakazi wa Niger Delta.eneo lenye kuzalisha mafuta kwa wingi, halikuwa na nafuu ya maisha,watoto hawakuwa na shule,hapakuwa na hospitali wala barabara za lami.
Hata mafuta yenyewe hayakuwepo katika ardhi ya waogoni,walilazimika kusafiri hadi Port Harcourt, ili kutafuta mafuta.
Novemba 10, kila mwaka, Ulimwengu wa wapenda haki na demokrasia unakumbuka  kifo cha mwandishi  mashuhuri na mwanaharakati wa Nigeria , Ken Saro-Wiwa.
 Saro-Wiwa, atatimiza miaka 18 tangu auawe kwa kupigwa risasi ya kichwa, na utawala wa kijeshi wa Nigeria , zama zile la Jenerali Sani Abacha itakapofika Novemba 10 mwaka huu wa 2013..
  Alipigwa risasi akiwa pamoja na wenzake wanane, Novemba 10 mwaka 1995; saa 7:30 mchana, katika Gereza la Port Harcourt , kwa makosa ya kubambikiwa.
 Aliongoza harakati za kudai kodi zaidi na mrabaha wa mafuta yanayochimbwa hata leo katika ardhi ya watu wake, yaani Waogoni.
Waogoni walipinga kwa nguvu serikali ya Marehemu Dikteta Jenerali Sani Abacha kwa kuliunga mkono kampuni la kigeni la ROYAL/DUTCH SHELL kwa kuwa na hisa kubwa ya mafuta yatokayo eneo lao, wakati wazalendo wa eneo hili wakiwa duni mno kiuchumi.
Madai kama haya ndiyo yanayotolewa na wakazi wa Mtwara,wakipinga gesi kusafirishwa kwenda Dar es salaam,wakati eneo lao likiwa duni,watoto wakiwa hawana shule na hospitali na zahanati zikiwa hazina huduma bora!
 Naam, watu walioishi katika Delta ya Mto Niger, waliazimu kufanya mapambano ya kudai mrabaha wa haki katika mgawanyo wa mapato yatokano na mafuta yaliyochimbwa katika eneo lao, wakati wao hawana barabara, hawana shule, zahanati, hospitali na hata vituo vya hayo mafuta vilikuwa havina hata tone la mafuta-mafuta yaliuzwa hapo kwa bei za kuruka.
  Nataka nikwambie msomaji, baada ya kifo cha Saro-Wiwa, harakati katika eneo la Niger Delta, zimepamba moto, makampuni ya kigeni yanashambuliwa na wenyeji, kuna vita vya silaha huko.
Jen Olsegun Obasanjo, alipoingia madarakani,ingawa anatoka  eneo hilo,hakusaidia kitu, ameingia Marehemu Yar’Adua akaacha moto unawake.Hivi sasa Goodluck Jonathana ambaye pia anatoka Kusini mwa Nigeria,amepewa muda kidogo kutatua mgogoro huo wa ‘laana ya rasilimali’ huko Nigeria. Ngoma bado mbichi,sasa “Mwangwi’ wake umeanza kusikika Mtwara,hapa Tanzania.
  Watu wa Ken Saro-Wwiwa, yaani watu wa kabila lake la Ogoni, wamefungua kesi mjini New York kuishitaki kampuni ya Royal/Dutch Shell kwa kumuua Saro-Wiwa, na madai ya haki yanapamba moto.
Wanadai mapato ya rasilimali zinazopatikana kwao,lakini wao ni fukara,hawana huduma za jamii,wakati rasilimali hizo zikiwanufaisha wengine.
  Nataka kusema kwamba, wazalendo wa eneo  lenye rasilimali za thamani kama mafuta, madini, wanyamapori, sangara, gesi n.k zinakotoka, wanapoabaini kwamba hawafunaiki na chochote kutokana na uwekezaji wa makampuni ya kigeni, basi huanza kufanya harakati za kutaka haki kama huko Niger Delta , Nigeria .
Serikali ya Tanzania,inapaswa kutambua kwamba yaliyotokea Nigeria,utandawazi umeyaleta hapa, sasa wasipige kelele,ila wazungumze na wana Mtwara na kuwathibitishia watakavyonufaika.
  Asilimia 90 ya mauzo ya Nje Nigeria , yalitokana na mafuta yatokayo katika hiyo Delta ya Mto Niger . Nigeria ni miongoni mwa mataifa ya daraja la kwanza duniani yanayosaforisha mafuta kwa wingi.
 Waogoni na Waijaw, raia wa maeneo hayo walikuwa duni sana , nimesema hawakuwa na hayo mafuta yenyewe katika vituo vyao, walilazimika kusafiri hadi mjini Port Harcourt kutafuta mafuta ya bei ya kuruka.
 Hawakuwa na hospitali, barabara, shule zao hazikuwa na mapaa.
Wiwa, ambaye alikuwa mtoto wa Chifu Beeson Wiwa wa kijiji cha Bane, hakuona furaha kuishi kwa taabu katika eneo lenye utajiri wa mafuta yanayochimbwa na makampuni ya kigeni ya Ulaya na Marekani, wakati watu wake wakiwa fukara kupindukia.
  Waliishi kwa kudura ya ya Mwenyezi Mungu, huku rasilimali walizo pewa na Bwana Mungu zikiganwa na utawala wa kijeshi wa Abacha na hao rafiki zake wa makampuni yaliyoungana ya Royal/ Dutch Shell.
  Walipojaribu kusema, walipigwa virungu na polisi waliolipwa mshahara na makampuni hayo, na walipewa hata viatu na sare za kijeshi.
 Saro-Wiwa, akajitoa mhanga kuwaokoa Waogoni, kama    Nabii Musa alivyofanya kuwakomboa Waisraeli Utumwani, Misri.
 Utajiri ulitoka katika ardhi yao , lakini wakabaki hawana elimu, walisalia masikini waliolazimika kutoa rushwa askari wa Dikteta Abacha waliozagaa mitaani kila kukicha ili kuwalazimisha raia wawape rushwa.
 Nataka nikwambie msomaji, hii rushwa iliyotolewa kwa hawa askari wa Abacha, siyo kwamba ilitolewa na wakosaji.
 Yaani, kama ulijipitia barabarani na jembe lako begani asubuhi, wakati unapokwenda shambani, ukikutana na askari wa Abacha, lazima uwape ‘mshiko’ ama posho, la sivyo utapigwa au utakamatwa, bila sababu.
  Ili uruhusiwe kufanya mambo yako, ilikuwa sharti uwape hawa askari  ‘njaa’ rushwa, ili waende zao wakuache. Hata kwenda sokoni, ukikutana na hawa askari ilikuwa sharti uwape ‘K.K’ yaani kitu kidogo ili wakuachie.
  Saro-Wiwa, na wenzake wakaanzisha Chama cha ukombozi cha Movement for Survival of the Ogoni People(MOSOP) ili kupinga unyonyaji na uzandiki katika eneo zima la Delta ya Mto Niger .
  Mafuta, ambayo yalikuwa mishipa kama veins ama artery iliyouneemesha utawala wa Sani Abacha na hayo makampuni ya kigeni , wakati raia wa kawaida walibaki masikini. Nayasema haya hapa ili kama viongozi wa serikali ya Tanzania na wanaotia saini mikataba ya madini na uwekezaji mwingine, wajifunze kitu hapa.
  Waogoni kadiri ya 500,000 walisalia fukara katika ardhi tajiri ya rasilimali ya mafuta. Na hata hapa kwetu, kule Mwadui inakotoka almasi, mambo ni yale yale ya Niger Delta, hakuna hozpitali, hakuna maji salama ya kunywa-zahatani na maji ya kunywa yanatarajiwa kama hisani kutoka kwa wawekezaji wachuma almasi.
 Hata katika dhahabu na tanzanite, katika wanyamapori, utalii  uvuvi, na uwindaji mfano ni huo huo niliotaja.Sasa hali hii imefika Mtwara,kwa hiyo dawa ni mazungumzo ya mgawo sawa wa rasilimali.
Katiba ya Tanzania inailinda serikali kutumia rasilimali zinazopatikana mahali kwa manufaa ya nchi nzima. Lakini sasa ‘Mwangwi’ wa madai ya Niger Delta umehanikiza Mtwara,watu wameandamana,kupinga gesi kupelekwa Dar,wakidhani inapelekwa Bagamoyo,nyumbani kwao Rais Jakaya Kikwete!
   Sina nia ya kuchochea maasi, bali nataka kutabiri kitu kitakachokuja hapa kama serikali haitachukua hatua mapema, maana somo tumeliona Niger Delta , Nigeria .
  Huko Nigeria , mapipa ya mafuta zaidi ya milioni 634 yenye thamani ya takriban Dola za Marekani bilioni 30 yalichimbwa mahali hapo.
 Yalitoka katika mtandao wa visima takriban 100 vilivyounganishwa katika vituo vitano. Shell Petroleum Development Corporation(SPDC) waliendesha uchumbaji mafuta kwa ubia na Shirika la Mafuta la Nigeria (MNPC), Agip na Elf.
  Wakati, Waogoni walikuwa watazamaji, wakiambulia upele kutokana na  yale mabaki ya mafuta machafu yaliyosababisha uharibifu wa mazingira hata yakatiririkia majini walipooga na kunywa au kunyweshea mifugo.
  Serikali na wawekezaji waliendelea kupuuza kilio cha Waogoni bila kuwapa mrahaba wa haki ili waondokane na kero zao, wakari rasilimali hiyo ilitoka katika ardhi yao .
Abacha alipewa gawio, askari wake walilipwa mshahara na watoto wao walisomeshwa Ughaibuni na wengine walikuwa wakurugenzi katika mashirika hayo, wakalipwa mshahara mzuri, nyumba na masurufu mazuri, kama hapa kwetu Tanzania vigogo wanavyotufanyia.
  Kampuni kubwa za dunia zilishiriki uharibifu wa mazingira na unyonyaji Nigeria .
 Kulikuwepo pia na makampuni kama Texaco, Mobil au Agip na Chevron la akina David J. O’ Reilly .
  Nikwambie kitu msomaji, Chevron ni kampuni kubwa la mafuta ambalo hata aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Dk. Condoleezza Rice, alikuwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurgenzi. Kampuni hilo lilikuwa la akina Bush.
  Mafuta ya Afrika, sangara, dhahabu, almasi, tanzanite, wanyamapori, gesi kama ya Mtwara n.k yanawavuta watu wakubwa sana hapa duniani; wanaungana kuja kuinyonya Afrika, huku wakijidai kuimba Demokrasia na Utawala Bora, sijui vita dhidi ya umasikini duniani, kumbe ni Ghilliba Bin Ghilibu tu!
 Basi, utawala wa ABACHA ukaanza kuwafagilia mbali wanaharakati wa chama cha MOSOP. Nimesema MOSOP ni Movement for Survival of the Ogoni People.Wanachama wa chama hiki wengine walikimbilia uhamishoni, wengine ndiyo akina Saro-Wiwa waliouliwa kwa risasi utadhani nyau wakomba mboga, kumbe walikuwa mashihidi wa haki waliokuwa wakitia ushahidi wao katika kesi ya kilio cha umma dhidi ya utawala wa Abacha.
 Abacha, mshitakiwa akajifanya hakimu na mwendesha mashitaka, shahidi na mlalamikaji kwa pamoja, akawaua hao mashahidi wa kweli.
  Ulishaona mshitakiwa akijigeuza hakimu na kumuhukumu kifo mlalamikaji?
Naishauri serikali,kuzungumza na wakazi wa Mtwara na kuwafundisha somo bila hasira na pupa.Maana tayari tunayoyaona huko Nigeria ya laana ya rasilimali sasa yako Mtwara!
 Raia hao wa Nigeria walihukumiwa kifo katika mahakama za kiini macho(Kangaroo Court), lakini upinzani na vita havijakoma huko Niger Delta hata leo.Makampuni ya mafuta yanatekwa huko hata miaka 18 baada ya kifo cha Saro-Wiwa.
 Hali hii inatoa hadhari hapa kwetu Tanzania , wakubwa wanapojidai kufumbia macho malalamiko ya wananchi dhidi ya wawekezaji hawa matapeli, kama nilivyotangulia kubainisha katika mfululizo wa makala zangu.
Ni kweli,gesi ni kwa manufaa ya Watanzania kwa ujumla wao,lakini bado wanamtwara wana haki ya kuona Mtwara inaonekana inafanana na mahali inapotoka gesi, si vinginevyo.
  Dola bilioni 280 zilizochumwa na Nigeria, nusu yake ilitokana na mafuta ya Niger Delta, lakini eneo hilo likawa halina miundo mbinu na huduma za jamii.
  Rasilimali zinakwenda kwa wageni, wakati serikali inapoambulia kikunja jamvi tu, na raia wao wanaambulia vumbi na upele, pengine na mamba kwa mabinti wao na ukwimwi ulioletwa na hao wawekezaji na wafanyakazi wao, maadam hata ajira watapewa wageni.
 Nenda kwenye migodi ya Tanzania , utakuta wanaajiriwa Waganda au Wakenya, kisa…Watanzania hawajui Kiingereza! Hapo upo? Serikali ijifunze kwa maandamano ya Mtwara ya amani,kabla ya matatizo kuja.
  Naam, Waogoni wa Nigeria , Waijaw, Urhobos, Itsekiris na Waafrika kwa pamoja, hawana maji safi na salama katika ardhi yao zinakovunwa rasilimali. Hawana shule, hawana huduma za Afya, wanasetwa tiki tiki kwa umasikini. Kusetwa tiki tiki ni mithili ya nafaka katika jiwe la kusagia.
  Wakati Rais Kikwete anaingia madarakani, alisema serikali yake ingepitia upya mikataba ya madini ili kuleta mazingira ya kufaidisha kila upande.
  Kitu hiki alikiita, ‘The win-win situation’
  Kama Nigeria , Dola bilioni 140 za Marekani zilichumwa eneo hilo la Niger Delta, raia wakiwa hawana hata mafuta ya kuwashia katika koroboi zao, unadhani Kikwete anafanikiwa kwa hili yeye peke yake?
 Wanigeria hawakuambulia ‘Naira’(Fedha ya NIGERIA ) ili wajenge shule, sisi tutahakikisha shilingi ngapi tunapata kutokana na madini, sangara, wanyama pori na hata misitu?
 Tuwaulize Kahama, Geita, Mwadui na hata Tarime, wamenufaikaje na madini? Halmashauri ya jiji la Mwanza ina viwanda vingi vinavyosindika sangara.
  Wawekezaji walishagoma kulipa ushuru wa shilingi saba(landing fee) kwa kiburi, kwa sababu  wenye viwanda wanajuana tu na wakubwa serikalini. Halmashauri ya Mwanza, watoto bado huketi sakafuni kwa kukosa madawati! Wanisute basi kama nasema uongo.
 Viwanda hivyo ndivyo vinavyowasomesha watoto wa vigogo na kuwalipa posho  n.k
 Wakati Fulani, mawaziri walipishana kwenda kutembelea viwanda na kuomba posho huko, Wahindi wakashituka! Posho mbili-mbili zilianza zamani…
  Ni kwa sababu ya uswaiba wa vigogo, wenye viwanda na wakubwa wetu wanakaa kimya hata ajira wanapopewa wageni, Wahindi, Wakenya na wengine hata kwa kazi ndogo za kufunga maboksi tu.
 Niliwahi kusema jambo hili, kiwanda Fulani kikataka kunirukia kwa miguu miwili. Nashukuru ujio wa serikali ya Kikwete ulipunguza kiburi cha watu hawa.
  Tanzania ni masikini kama Comoro, Timor Mashariki na Somalia , ingawa ina amani, na ardhi yake ina madini. Sisi tumekalia maneno na mitafaruku kama ya akina Edward Hosea na wabunge kutaka kutemeshwa posho mbilimbili, Richmond , IPTL, Rada kanyaboya n.k!!
  Tanzania kama Nigeria ya akina Ken Saro-Wiwa, wageni walikuwa na kiburi cha kukopeshwa mitaji na kufanya utapeli hapa, raia wakiwa watazamaji, wakisema wanaambiwa wana wivu wa kike!
 Tuna ardhi, mito , bahari, milima mirefu sana Afrika, maziwa makubwa, lakini fukara na wenye njaa.
  Hata leo Rais Kikwete akiulizwa na gazeti kama Financial Times kwamba kwanini Watanzania ni masikini wakati Tanzania ni tajiri kwa rasilimali, itakuwa mbinde kutoa jawabu!
        Chimbuko la umasikini wa Watanzania wakati Tanzania ni tajiri, ni ombwe la uongozi ambalo Kikwete alipaswa kuliziba wakati anasema umuhimu wa ‘win to win situation’ kwamba wawekezaji wanufaike kama sisi ambavyo tungenufaika.
 Kinyume chake ni wizi tu, utawala wetu hauta kuwa tofauti na Abacha alivyowafanyia akina Ken Saro-Wiwa, miaka 18 iliyopita.
  Nazungumzia ufisadi na haja ya kuwa na viongozi bora wenye mapenzi na taifa na raia, siyo wafanya siasa kama hawa wanaokataa kuhojiwa kwa posho mbili-mbili, na wengine wanaotuletea mgawo wa umeme kama  Rada mbovu, mikataba ya hovyo na madudu kibao!
  Tuangalie, mzuka wa Saro-Wiwa utaweza kuibukia Mwadui, Shinyanga, kama siyo Kahama, Mererani au popote palipo na rasilimali nyingi. Lakini, raia ni fukara, hawana hata maji ya kunywa.
Hili ndilo somo la serikali kujifunza na kufanyia kazi, na wana siasa waache kupenyeza sumu,bali hili ni darasa. Tanzania ijiepushe kuona laana ya rasilimali ikiwatafuna Watanzania.
0713 324 074

 
 
 


No comments:

Post a Comment