‘Papa’ Kabila, alikufa
Jumanne, Januari 16 mwaka 2001, kwa kupigwa risasi ndani ya Ikulu hiyo,
kufuatia mgogoro baina yake na washirika wake waliomwezesha kuwa kiongozi wa
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Waliomwezesha Kabila kuingia Ikulu
walimuua na sasa wanautafuta uhai waaaaa Kabila mtoto!
Kabla ya mauaji hayo, nchi
hiyo maarufu sana Barani Afrika, ilikwisha geuka uwanja wa vita
vilivyosababisha Mataifa ya kigeni: Rwanda , na Uganda kujipenyeza ndani
yake kwa kisingizio cha usalama wan chi zao.
Sambamba na kuyasaidia majeshi
ya waasi wa serikali katika harakati zao za kutaka kuipindua serikali kwa madai
kuwa ilikithiri kwa rushwa, ukabila,upendeleo na utawala mbovu.
Naam. Miaka 12 kamili
baada ya kifo cha ‘Papa’ Kabila, roho mchafu wa rushwa, ukabila, upendeleo na
utawala wa hovyo, angali akitafuna mataifa haya yote ya Maziwa Makuu; hata kama
mengine yana amani ya kuegesha.
Rwanda , Burundi
, Kongo yenyewe na sasa Kenya hutafunwa na ukabila; wakati majirani zetu kama
Somalia na Sudan , hususan Darfur, tatizo hilo linafanya nchi kuvunjika
vipande, na maelfu ya watu kufa, wengine makazi kutafuta hifadhi ya ukimbizi
katika mataifa mengine,
Angola , Zimbabwe na
Namibia zilijitosa kumsaidia Hayati Kabila asipinduliwe mapema na vikosi vya
waasi wakiongozwa na Watutsi wa ‘Banyamulenge’.
Licha ya kukubaliana kuacha
mapigano katika majadiliano ya siku 13 mjini Lusaka , Zambia yaliyofanyika
tangu Julai 10 mwaka 1999; vita vikaendelea katika nchi hiyo ya tatu kwa ukubwa
Afrika; na yenye utajiri wa madini ya thamani kubwa.
Mahali penye utajiri wa
nishati na madini kama almasi na dhahabu ndipo mafisadi huchochea ukabila na
vita vya kila mara ili wananchi wa kawaida, wasije wakapata fursa kusaka
maendeleo huru nay a dhati. Naam,makampuni ya Magharibi.
Kati ya Feburuari 24 na
Juni 16 mwaka 2000, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliingilia kati
mgogoro wa Kabila na Banyamulenge, na kuamuru majeshi ya kigeni kuondoka.
Tumeona Rwanda na
Uganda wakiwasaidia Banyamulenge kumwondoa ‘Papa’ Kabila madarakani, na tumeona
Namibia , Zimbabwe na Angola yakisaidia majeshi ya serikali kuvitimua vikosi
vya waasi
Hapakuwa na mafanikio.
Basi, Baraza hilo
likaamuru kupelekwa askari wa Umoja wa Mataifa wapatao 5,537 ili kusaidia
kutekeleza makubaliano na kusitisha vita.
Katika jitihada za kumwokoa Kabila,
alikutanishwa na Rais wa Rwanda , Meja Paul Kagame nchini Kenya ambako nako
siku hizi baadhi ya watu, wakiwemo watoto na akina mama wanateketea katika
miali mikali ya moto na maiti zao kuwa majivu. Unakumbuka vita vya baada ya
uchaguzi,mwaka 2007?
Kagame alikutana na
Kabila nchini Kenya Juni 13 mwaka 2000.
Mapigano yakaendelea; yakasambaa
hadi katika roho ya nchi penye utajiri wa madini na shughuli za kiuchumi.Siku
hizi wanakutana Kampala.
Naam. Utawala wa Kabila
ulikoma Januari 16, mwaka huo 2001; yeye mwenyewe akauliwa kwa risasi kutoka
kwa mlinzi wake ndani ya ikulu. Mlinzi huyo, Rashid Kasereka, aliuawa punde.
Kabila akarithiwa na mwanaye, Meja
Joseph Kabila Kabange(42), anayejaribu kurejesha amani na kuleta maelewano
miongoni mwa makabila yote ya ‘Bacongo’.
Bado kuna vita na
mauaji; na majeshi ya kigeni yangali yakichochea migogoro Kongo.
Naam, migogoro ya Kongo huchochewa
na baadhi ya waafrika wenzetu, vibaraka wa Wakoloni wa zamani, kwa tamaa ya
rasilimali za nchi.
Kabila alifanya kazi
moja…kukomesha utawala wa kibaraka mkongwe wa wazungu Afrika, Marehemu Dikteta
Kuku Mbendu wa Zabanga wa Zaire ,maana yake Buldoza,linakopita hakibaki kitu!
, koplo wa zamani Seseseko Joseph
Desire Mobutu!
Ilikuwa Mei 17, mwaka 1997.
Kabila, akaibadili
Zaire kuwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, baada ya kushika hatamu zote,
kufuatia ushindi katika vita ‘laini’ dhidi ya serikali taabani ya Mobotu.
Baadaye, Banyamulenge waanzisha uasi
dhidi ya ‘Papaa’ katika miji ya Bukavu na Goma mnamo Agosti Pili, 1998. Vikosi
vya waasi vilipata nguvu kutoka nadharia ya Kitutsi ya majeshi ya Rwanda na
Uganda .
Inadaiwa, utawala wa
Kabila uligubikwa chuki, mafarakano na uchoyo uliozaa mauti yake mwenyewe.
Alirithi utawala wa
choyo na rushwa toka kwa Mobutu, aliyesimikwa madarakani kwa masaada wa
Mabeberu wa Magharibi, baada ya mauaji ya Waziri Mkuu, Patrice Emery Lumumba,
mwaka 1961.
Tumekwishaona jambo hili,usikose
safu hii.
Kabila alipiga marufuku
vyama vya siasa Mei 20 mwaka 1997. Akamweka kizuizini mwanasiasa aliyempinga,
Etiene Tshisekedi. Tshisekedi alizuiliwa kijijini kwao Kasai, Feburuali 12,
mwaka 1998 kwa sababu zili walizonazo watawala wetu hadi sasa- za hofu ya
kuondoshwa mamlakani.
Hayati Kabila alikuwa
na uhusiano na Rwanda na Uganda tangu zamani. Biashara ya magendo ya almasi na
dhahabu pengine ilifanyika wakiwa pamoja, ili kuimarisha vikosi vyao.
Kabila aliipinga serikali ya Kongo,
Museveni alimpinga Obote na baadaye Tito Okello, na Kagame aliwahi kwenda
msituni na waasi wa RPF dhidi ya serikali ya Rwanda .
Walihitilafiana.
Museveni na Kagame wakaanza kumpinga
Kabila, wakasaidia waasi ili kumwondoa huku kukiwa na madai ya kuiba madini.
Baadaye majeshi ya Rwanda na Uganda
yalichapana ndani ya Kongo kwa sababu zinazofahamika. Kumbukumbu ya hayati
Kabila itufundishe kujua aina ya viongozi tulionao Afrika. Ni vibaraka wa adui
wa Afrika.
Uganda iliingiza jeshi
lake Kongo mwaka 1998 kwa kisingizio cha kuharibu makambi ya waasi wa serikali
wa Allied Democratic Front.
Ilidaiwa, walipata msaada toka Sudan
.
Serikali ya Kampala ikihofia kwamba
kulikuwa na makambi ya mafunzo ya waasi katika Kabaya, Kanyabayonga, Kibumba na
maeneo ya jirani na Goma.
Majeshi ya UPDF
na RPA yaliingia Kongo kupigana bega kwa bega na waasi dhidi ya serikali
ya Kabila.
Umoja wa Mataifa uliweka sharti
majeshi hayo kuiacha Kongo chini ya Jeshi lake, UN Military Observer Mission
for Congo (Monusco).
Uganda na Rwanda
zilionyesha kudharau amri hiyo wakaendelea kuwalea waasi wengi, akina Mbusa
Nyamwisi(baadaye alijiunga na serikali), Profesa Ernest Wamba dia Wamba, na
wale wa RCD Kisangani.
Mbusa Nyamwisi alikuwa Waziri wa
Mambo ya Nje baadaye. Ni vita,ili
kugawana madini ya Afrika.
Hata baada ya Kongo
kufanya uchaguzi wa Kidemokrasia, na Rais Kabila kushinda, Kongo kungali
na vita ya kikabila.
Yamefanyika mapatano kati ya Marais
Kabila na Yoweri Museveni yaliyosimamiwa na Rais Kikwete katika hoteli ya
Ngurdoto, Arusha. Hakuna kitu,vita vinaendelea kwa miaka 51.
Inadaiwa, licha ya
mapatano ya kuacha chokochoko, Rais Kabila hajamwamini sana Museveni.
Kongo, kungali na Waasi
wa Kitutsi kama, Laurent Nkundabatwale, wanaojaribu kukalia milima ya
Rumuhe na Mumba, Kaskazini mwa mji wa Ngundu. Kuna akina Bosco Ntaganda na
wenzao wa M 23.
Joseph Kabila, ambaye
aliwahi kusoma Tanzania na kupata mafunzo ya kijeshi, JKT Makutupora, na
baadaye Uchina, alimrithi babaye Januari 24, akaapishwa siku mbili baadaye,
mwaka huo wa 2001.
Baada ya kushinda
uchaguzi na kuunda serikali, anaongoza nchi kubwa yenye watu zaidi ya milioni 60.
Hii ndiyo nchi mabeberu walimuua
Patrice Lumumba Januari 17 mwaka 1961.
Ndiyo, mwezi huu
unaokwisha tunamkumbuka pia mwanamapinduzi Patrice Emery Lumumba, katika
mapambano ya kudai uhuru wa kweli, na njama za vibaraka.
Ni kipindi cha kukumbuka urais wa akina Moise
Tshombe, Juni 30 mwaka 1964.
Jenerali Mobutu
alitawala 1965, Congo ikawa Zaire mwaka 1977 kutoka Jamhuri ya Kongo toka 1966.
Kabila, aliwatumia Watutsi kupindua serikali
ya Mobutu ambaye alikuwa akitibiwa saratani, Ughaibuni, Mei 17, mwaka 1997.
Mobutu alikwenda
uhamishoni, na baadaye akafariki mjini Rabat Morocco , Septemba 7 mwaka huohuo.
Mobutu ametawala Congo miaka 33; lakini
ameondoka bila heshima sawasawa na Idi Amin, Jean Bedel Bokassa, na wengine wa
kariba hiyo. Mafisadi wanaojifanya vibaraka wa Mzungu hapa nyumbani.
Historia haiwaheshimu watawala mafisadi wa
dunia, japokuwa wataiba sana na kuwa matajiri.
Hawa hawana heshima kama
akina Nyerere, Nkrumah, Samora, Gamal Abdel Nasser, Mandela na wengine.
Tunapomkumbuka Kabila
na Lumumba, tuitazame Afrika inavyoteketea katika moto baada ya madai ya mbinyo
wa demokrasia na wizi wa kura.
Tuwatazame raia fukara dhidi ya
watawala matajiri walioshiriki kuiuza Afrika vipande thelathini vya fedha.
0786 324 074’0754
324 074
No comments:
Post a Comment