Thursday, January 17, 2013

MAGUFULI JEMBE KWELI KWELI

WAZIRI WA UJENZI,John Pombe Magufuli, juzi  ‘alimgonga’kiaina Waziri wa Uchukuzi,Dk.Harrison Mwakyembe,kuhusu mkandarasi kuchelewesha ujenzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza.
Dk.Magufuli, alifika Mwanza Januari 10 mwaka huu, na kukagua barabara ya kutoka Nyakato National kwenda Buswelu,itakayotumika baada ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza kuanza.
Ijumaa,Januari 11,Dk.Magufuli akafika uwanja wa ndege wa Mwanza,ili kukagua barabara iendayo Igombe,inayopita mita chache kutoka unapoanzia uwanja huo na kukuta mkandarasi hajaanza ujenzi; na wala hakukuwa na vifaa vilivyoletwa kuanza ujenzi huo.
Awali,kulikuwa na malalamiko kutoka kwa mkandarasi kwamba,Wizara ya Ujenzi ilikuwa ikikwamisha kuanza kwa ujenzi wa uwanja wa ndege,kwa kushindwa kuifunga barabara hiyo ya Igombe inayopita eneo ambalo  limo ndani ya ramani mpya ya uwanja huo.
Magufuli, alipoona hakuna dalili za kuanza kwa ujenzi wa uwanja huo,wakati tayari wizara yake ikilalamikiwa kwa kushindwa kuifunga barabara ipitayo ndani ya eneo la mradi wa ujenzi, akaja juu:
“Kwani barabara hii ya kwenda Igombe inamzuia nini Mkandarasi huyu kuanza ujenzi wa uwanja? Mkandarasi huyu tayari amelipwa malipo ya awali shilingi bilioni 8; angekwisha ‘clear site’ lakini hakuna alichofanya, wala hajaanza kupanua zile mita 500 za runway inayopanuliwa; na anasingizia kufungwa barabara!” Magufuli alisema.
Akasisitiza kuwa hawezi kuifunga barabara ya Igombe hadi mkandarasi huyo aanze kujenga uwanja huo.
Barabara itokayo katikati ya Jiji hili kwenda Igombe,hupita kandoni mwa uwanja wa ndege unaopanuliwa ili kufikia viwango wa kimataifa.Habari zilizolifikia gazeti hili zinasema,Mkandarasi anayejenga uwanja huo, Beijing Construction Engineering Group(BCEG) alikuwa amesaini mkataba tangu mwezi Juni mwaka jana,na muda wa kusafirisha vifaa(mobilizing period) wa miezi mitatu ulipita bila kuleta vifaa eneo la mradi, kwa sababu vifaa vilikuwa vingali kisiwani Zanzibar.
Kufuatia hali hiyo,Dk.Magufuli akataka maelezo kutoka BRELA,ikiwa BCEG walikuwa wamesajiliwa,na kama walikuwa na uzoefu.
Mwakilishi kutoka BRELA,akamwambia Dk.Magufuli kuwa kampuni hiyo kutoka Uchina ilisajiliwa miaka mine iliyopita,na ilikuwa imejenga uwanja wa Taifa,Dar es salaam.
“Okay,sitaifunga barabara hii,kwani inawahudumia hata akina mama wanaotaka kujifungua hospitalini.Nitafungaje barabara halafu akina mama wajifungulie barabarani hapa eti kwa sababu barabara imefungwa,wakati hata vifaa,hata toroli halijaletwa hapa ili kuanza ujenzi?”,Magufuli alisaili.
Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza uko chini ya Wizara ya Uchukuzi ya Dk.Harrison Mwakyembe,lakini Magufuli akamwambia Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi,Eng.Omar Chambo, “Miezi mitatu ya ‘mobilization’ imepita,mkataba ulisainiwa Juni mwaka jana,leo ni miezi saba hakuna kinachoendelea hapa, halafu anasema kinachomkwamisha kuanza ujenzi ni barabara hii! Sasa niifunge basi,tuone kama ataanza ujenzi wakati hana vifaa,hakuna hata  tingatinga, hata toroli!” alisema Magufuli,huku akiuliza, “Injinia Mshauri(consultant) yupo wapi?”
Akatokea mbele zake.Magufuli akampiga maswali kama alikuwa na uzoefu wa kazi. Consultant huyo toka Zambia, akajaribu kujitetea. Magufuli akamwambia kwa kimombo: “Make sure not to compromise with that bogus Contractor… message has sent and delivered!”,
Kwamba huyo injinia toka Zambia aangalie asikubaliane na uzembe huo, akasema tena kwa umombo, “You may have a bogus contractor, but you must be very tough, otherwise this may be the last job in           East Africa”, kwamba awe makini la sivyo hii ndiyo itakuwa mara ya mwisho kufanya kazi hapa Afrika ya Mashariki!
Wakati Magufuli akimcharukia Mkandarasi huyo na mshauri wake toka Zambia, akatangaza kufungwa barabara hiyo pindi ujenzi wa uwanja ukianza.
Akasema,serikali tangu mwaka 2008 imewatimua makandarasi wazembe wanaoshindwa kuzingatia masharti ya mikataba.
Uwanja wa ndege wa Mwanza unapanuliwa kufika viwango vya kimabara kwa gharama ya shilingi bilioni 105 zinazotolewa na serikali pamoja na Benki ya Waarabu ya Maendeleo(The Arab Bank for Economic Development of Africa, BADEA).
Hatua hiyo ya Magufuli kumcharukia mkandarasi huyo imetafsiriwa kuwa ilikuwaa ‘kugongana’ na waziri Mwakyembe hadharani.
Utakapopanuliwa,uwanja huo utakuwa na njia ya kurukia yenye urefu wa mita 3,700 badala ya ilivyo sasa mita 3,300.
Utakuwa na jingo jipya la kuongozea ndege jirani na kilima(Traffic control tower),jingo jipya la abiria,maegesho na maeneo mengine muhimu pamoja na sehemu ya mafuta ya ndege,ili ndege zinazotoka Mwanza kwenda Ulaya au Asia,zisilazimike kupitia Dar es salaam kunywa mafuta.
 

No comments:

Post a Comment