Agosti 7
mwaka huu 2013 tutakuwa tunakumbuka miaka15 ya mashambulizi ya magaidi yaliyofanywa katika Balozi za
Marekani, Dar es salaam na Nairobi ; mwaka 1998.
Zaidi ya watu 240
walikufa; hawa hawakuwa wa Kenya pekee bali pia wa Tanzania . Hawakuwa wa kabila moja
au wa dini fulani, waliokuwa wakisali
msikiti mmoja ama kanisa fulani.Magaidi ni hatari kwa raia wote wa dunia.
Tunawaombolezea
waathirika wa tukio hilo
la Agosti 7 mwaka huo wa 1998, ambalo msingi mkubwa ni uadui kati ya Marekani
na Waarabu walioamua kuisaka Marekani popote duniani, ili kulipa kisasi.
Naam,kuisaka Marekani katika ardhi yetu,
kusababisha hasara ya maisha na mali
za watu wetu, ni vitu tunavyovipinga leo na kesho hata kama
mbingu zishuke; ama jua litue mchana saa saba!
Si lengo la safu kusema kwamba magaidi
ni Waarabu peke yao, ama watu wa imani fulani. Nitajadili malengo ya ugaidi na
chimbuko lake. Nitajadili imani inavyoupa msukumo na nguvu ugaidi duniani.
Kuna vikundi tele vya kigaidi duniani.
Usishangae, hakuna gaidi anayejiita gaidi. Wote wanajiita, wanaharakati(activists)
wa ‘Haki’ za ubinadamu wao. Ugaidi unakula maisha ya watu na mali vinapopotea
au kuharibiwa.
Kila mmoja ana tafsiri yake ya ugaidi.
Sitajali kusikia Rais Mstaafu George W. Bush wa Marekani naye ni gaidi kama Osama bin
Laden. Hata hivyo, najua, magaidi kama wale waliolipua Balozi la Marekani Dar es
salaam na Nairobi, Agosti 7 miaka 15 iliyopita, wote ni wauaji; wanastahili
adhabu kali.
A-Qaeda ni kundi la harakati za kigaidi,
bila kujali wanaharakati wake wanatokana na itikadi gani. Japan, kuna kundi
moja linaitwa, “Ukweli Mkuu” kwa Kijapani, Aum shinrikyo-hawa nao hata
wakifanya mauaji, watasema wameua ili kuueneza huo Ukweli(The supreme Truth).
Mauaji hayaenezi haki yoyote.
Uhispania, kuna kundi linaitwa,
ETA(Freedom for The Bosque Homeland), nalo linadai uhuru. Lebanon , kuna kundi maarufu sana
kama , Hezbollah(Chama cha Bwana Mungu), wakati
Ireland Kaskazini kuna kundi liitwalo, Irish Republican Army(IRA).
Nchini Israeli,
kitovu cha uadui wa mgogoro wa Mashariki ya Kati, kuna kundi liitwalo, Kach and
Kahane Chai, Uturuki kuna PKK(Kurdistan Peoples Party), Sri Lanka kuna,
Liberation Tigers of Tamil Eelam(LTTE); wakati nchini Iran kuna
Mujahedin-E-Khalq.
Ugiriki kuna kundi
linaitwa, November 17 Revolution. Juzi tulisikia kundi la FARC(Revolutionary
Armed Forces of Columbia) likifanya utekaji nyara; lakini ni ‘Jeshi la
Kimapinduzi’.Jeshi la kimapinduzi hupindua raia?
Hakuna anayemaizi kuwa matendo yake ni kinyume
cha sheria za nchi, za kimataifa, ama ubinadamu. Wengine wanajisingizia,
wametumwa na Mungu ili kuwaua binadamu wenzao, waabudu sanamu ama wapagani.
Wapo, Shining Path
kule Peru .
Columbia pia
kuna National Liberation
Army(ELN), na Ufilipino kuna New Peoples Army.
Tumjadili kidogo
tu, gaidi la kale, Ilych Ramirez Sanchez, ambaye kwa utani anaitwa, Carlos The
Jackal-mzaliwa wa mjini Caracas ,
Venezuela .
Venezuela , ni nchi anayoongoza Hugo Chavez, anayeugua kansa huko Cuba,
ambaye alimtukana rais Bush, wakati anahutubia Mkutano wa Umoja wa Mataija,
jijini New York ,
akapewa saa chache awe ameondoka nchini humo.
Carlos, gaidi anayetumikia kifungo cha maisha Ufaransa, ikifika Oktoba 12 mwaka huu,
atakuwa anaadhimisha miaka 64 ya kuzaliwa kwake.
Sasa, huyu jamaa katika mafaili ya uhalifu na
Jinai duniani, kuna mambo yake mengi, ambayo yametokana na chuki za siku nyingi
kati ya nchi za Amerika ya Kusini(zilifuata siasa za Ki- Marx) na Marekani.
Carlos, ambaye baba yake alikuwa mjamaa, alimpeleka Chuo Kikuu cha Patrice
Lumbumba, mjini Moscow ,
kusoma.
Huko alikutana na Wapalestina, akaiva katika
siasa za mrengo tofauti na ubeberu wa Kimarekani.
Hata jina
‘Ilych’ aliitwa na babaye ili kuwaenzi
‘makomredi’ wa Urusi ya Ujamaa, akina Lenin.
Sasa Carlos anaipinga
Marekani hata huko jela, alishasema anamuunga mkono Osama bin Laden, kwa
asilimia 100; na kwamba anawataka watu wasiache kujitoa mhanga ili kufa na
Wamarekani, popote walipo!
Nitajadili kauli
hii baadaye kidogo.
Hata hivyo, huyu jamaa aliyetiwa mbaroni na mashushushu wa
Ufaransa akiwa mjini Khartoum, Sudan alishakaa Urusi tangu 1968, amekaa
Ujerumani mwaka 79, amekaa Syria 91-93, na Ufaransa. Vituko vyake unaweza
kuvipata katika sinema za akina James Bond.
Hapa, nitajadili ugaidi, si Carlos.
Naam, ugaidi wa Agosti 7 mwaka 1998,
ulileta hadithi nyingi. Lakini, tuseme kwamba wale magaidi walishambulia Balozi
za Marekani Dar es salaam na Nairobi , karibia muda uleule mmoja, kwa
sababu nchi hizi hazikuwa zimejiandaa.
Wengine
wanasema
hata Kampala
ingeshambuliwa. Kilichoiponya ati ujio wa Rais Bill Clinton wakati ule
mjini Kampala , ulivifanya vikosi vya usalama vya Uganda kuwa ‘more
alert’ kuliko Dar na Nairobi ! Hayo tuyaache.
Shambulizi lingine la magaidi Afrika
Mashariki lilifika Novemba 28 mwaka 2002. Magaidi waliua watu 16 mjini Mombasa,
katika hoteli ya Paradise iliyoko Kikambala. Ni kilomita 25 kutoka mjini
Mombasa.
Hii hoteli ni ya Waisraeli; sasa unaweza
kukisia hata wewe, kwamba ilishambuliwa na adui zao Wapalestina. Wapalestina
walikuja Afrika Mashariki kuwawinda adui zao Waisraeli, katika ardhi ya Kenya.
Hawakuua Waisraeli tu, waliua na Wakenya, na raia wa mataifa mengine.
Sasa tuseme, vita vya kudai uhuru
vinavyoendeshwa na Wapalestina dhidi ya Mayahudi, vina leseni ya kuua na
kuumiza binadamu wengine wasio na hatia?
Halafu, hao magaidi wa Kipalestina walifanya
jaribio la kuilipua ndege ya Arkia Airlines ya Israeli, iliyokuwa ikiruka
kutoka uwanja wa ndege wa Moi, mjini Mombasa. Bahati tu, lile kombora, bila
shaka la Kirusi, liliikosa- kosa ndege ile iliyokuwa na abiria 271 hivi.
Fikiria, kama kombora lile lingeipata ndege
ile,wangekufa Waisraeli pekee? Hata raia wa mataifa mengine, wasiojua uadui waa
Israeli na Wapalestina wangeungua katika miali ya moto wa mlipuko. Sasa ugaidi
unasura ya ukombozi au uokozi na uhuru
wa wapi?
Narejea mada yangu ya madhara ya ugaidi
Afrika Mashariki. Matukio yote ya ugaidi yalisababisha watu mamia kufa,
inakisiwa kulitokea hasara ya dola mabilioni. Ili kuponya majeraha ya ugaidi,
zimetumika dola matrilioni, ambazo pengine zingetumiwa kuleta maendeleo-ugaidi
ni adui wa maendeleo ya watu.
Nimesema magaidi wapo Wazungu kama IRA, na
wa mataifa mengine kama akina Carlos The Jackal; lakini ni magaidi. Magaidi
hawana rangi, dini ama taifa moja.
Ugaidi ni mauaji ya kinyama yanayoendana na
matakwa ya ulipaji kisasi. Pengine, magaidi kama Black Banners wa Iraki, wakati
ule wa vita, waliwateka jamaa watatu wa Kenya, ili kutafuta fedha kutoka kwa
makampuni waliyofanyia kazi.
Sasa nijadili jambo ambalo watu hupenda
kunitolea matusi. Watoa lugha chafu,
hawana weledi juu ya lolote. Silaha yao ni matusi na vitisho. Wanadhani, ukweli
ni ule unaolingana na wanavyopenda, ama wanyofikiria wao.
Hata hivyo, ugaidi ni unyama, hata Mungu
mahali popote hajawahi kusema watu walipizane visasi. Sera za ‘Jino kwa Jino’
ama ‘TIT FOR TAT’ ni za Ibilisi. Mungu anawataka watu kutong’oana meno, ili kulipa
baya kwa baya?
ungu anawataka watu wawe vibogoyo au chongo?
Juzi, Papa Benedict XVI ameungama kwamba
Kanisa Katoliki nalo lilishafanya ugaidi. Ugaidi hauna rangi, kanisa, msikiti
wala watu wa kabila moja.
Nilipata kutukanwa na hawa jamaa kwa kupinga
kauli ya Carlos, kuwataka watu kufuga midevu mingi kama shamba la miwa la
Kilombero, halafu eti wasiache kujilipua
ili kuwakomesha Wamarekani, popote watakapowaona!
Sasa
kama Carlos
kawaambia, kwa nini wasiende kujilipua New York
au Washington ?
Kwa nini Mombasa , Nairobi au Dar? Huku Wamarekani hawapo!
Mkijilipua huku mnatuumiza sisi, wao hawapo. Kama
wapo ni mmoja tu au wawili-wafuateni Wamarekani kwenye uwanja wa
mapambano! Wenye uwezo walikwenda kulipua New York na Washington,
Septemba 11 mwaka 2001; hadi leo historia inaelekea kuwasahau.
Sipendi kuamini
kuwa, mtu mwenye uwezo wa kufikiri anaweza kuwa’Shahidi’ mwaminifu wa imani
yake(uwe Ukristo,upagani ama Uislamu)kwa kujilipua, ili afe yeye na kumuua
adui!
Huku ni kushika
dini kupita kiasi(fanaticism), kunakogeuza dini kuwa vifo na mauti, kwamba ni
ushahidi(martyr). Hii si Jihad halali kuua hata watoto wasio na hatia, kwa
sababu tu walikaa meza moja na adui.Kwa nini kuua adui mmoja kati ya ndugu
mamia?
Najua vita kati ya
Waisraeli na Waarabu wa Mashariki ya Kati, inaitwa ‘Vita kati ya wema na uovu’.
Sasa kama pande mbili zinaua hata
wasiohusika, mwema nani na mwovu ana alama gani?
George Bush na Tony Blair, wakati
wanaishambulia Irak, walisema ni vita dhidi ya watu wasiostaarabika. Wakati
magaidi waliposhambulia London, wakasema ni vita dhidi ya ustaarabu.Sasa
tujiulize pia, kuua watu wasiohusika hata huko Irak ni ustaarabu? Ni kwa sababu
hii, safu hii inasisitiza kuwa mauaji ni jinai, na kila muuaji ni Ibilisi
mwenye mikia saba.
Hakuna kitabu kitakatifu kinachotuma watu
kuwaua wenzao wasioamini ama waabudu sanamu. Ndiyo maana hapa Tanzania si lazima
kwa mujibu wa Katiba mtu kuwa dini fulani.Hata wapagani na waabudu sanamu ni
watu; wasiuawe kwa kutokuwa na dini kwao.
Nasema hivi kwa
sababu rafiki yangu aliniambia, Allah kasema kuua hawa walao nguruwe ni kupata
thawabu hata akhera!(to be elevated to a higher plane of existence, where life
is an eternal bliss).
Ni kwa sababu hii,
msomi na mhadhiri, Imam mashuhuri
anasema kila siku, kwamba Kuran inakataza kabisa kuua au kujitoa mhanga-na
kwamba wanaofanya hivyo, hawafanyi kwa jina la Uislam; bali wanasaliti
mafundisho ya Mtume Muhammad.
“Hatutaruhusu
imani yetu adhim kutekwa nyara na wahalifu”, alisema.
Maneno kama haya
kayasema Kiongozi wa zamani wa Upinzani Bungeni , Hamad Rashid Mohamed, alipokuwa
akitoa hutuba fupi wakati wa kuaga mwili wa Chacha Zakayo Wangwe, “Rasta” wa
Tarime. Buriani Chacha Wangwe.
Hamad Rashid, alisema alikwaruzana na Marehemu
Chacha Wangwe, lakini wakasameheana, kwa sababu, Kuran inasema, ‘kusamehe ni
lazima’ ili upate thawabu.Samehe 7 mara 70!
Biblia
inasema kusamehe ‘saba x sabini’ maana yake siku zote za maisha. Saba ni alama
ya ukamilifu wa utimilifu; hivyo tusichoke kusamehe.
Sasa
hata hapa mtanitukana na kutishia kunipiga kwa kuhimiza amani? Mungu
gani kawaambia kumpiga mwenye mawazo tofauti nanyi? Dini yenu ni ya amani, kwa nini Jino kwa Jino?
Nilishasema katika makala mbili
zilizotangulia, kwamba kuna upendeleo na ‘double standards’. Alichofanya Bush
au Blair, akikifanya Mugabe au Mpalestina, ataitwa gaidi, wao “Patriots”.
Hili ni
tatizo ambalo haliondolewi kwa watu kujilipua, lawama hizi haziondoki kwa
kujifunga mabomu. Hatupambani na ‘metropolitan power’ kwa kulipua Dar, Mombasa
na Nairobi.Tunatakiwa kuilipua Washington kisayansi, maana yake kumlipua Bush
pekee bila raia wasio na hatia.
Ukijifunga bomu utamlipua Blair au
Bush? La hasha. Utawalipua ndugu
zako wa Dar, Mombasa ama Nairobi. Tutafute njia mwafaka ya kuondoa ‘double
standards’ duniani. Tusijiite, “Liberators” ama ‘in the service of’
Allah’ kumbe wauaji wa ndugu zetu wenyewe.
Tusidhani tunakomboa, kumbe tunajiua! Kujiua
ni dhambi kubwa na kosa katika sheria za binadamu na Allah. Mashahidi waaminifu wa imani, hawatoki msikiti fulani
tu, hata sinagogi au kanisa.
Je, hamjaona watu wakienda uwanja wa ndege na
biblia pasipo nauli,hati za kusafiria wala visa wakadhani Mungu atawapeleka
Ulaya kuhubiri? Huku nako kujifunga mabomu! Magaidi hawana dini moja.
Nimalize, kwa
kusema Kuzimu kumepanua kinywa chake. Kuna visasi vingi tangu matukio ya Septemba 11 mwaka 2001. Lakini,
tuangalie faida yake nini? Nani kasema ukifa kwa kujilipua kwa bomu na
kuangamiza Mzungu mmoja na Waafrika wenzako 200 ni thawabu? Imani
zisitugawe;sisi ni wamoja hapa Tanzania ama Afrika.
Tutafakari msugoano uliopo kati ya Magharibi
na Mashariki. Leo, siasa za akina Hugo Chavez, zinashindwa. Akina Carlos The
Jackal wanaonekana majambazi tu, hata kama walifanya kazi bega kwa bega na
makomredi kama Fidel Castro, katika kuzuia ubeberu.
Hatuwezi kuupinga ubeberu kwa kuangamizana
Paradise Mombasa, au katika usafiri wa ndege kama ile ya Arkia Airline, ama wa
treli London.
Hata
katika balozi za Wazungu, kama Dar, Kampala na Nairobi, ukijilipua hukosi kuua
Mzungu mmoja na Waafrika wenzako 300. Kuna thawabu gani hapo?
Tufanyeje sasa? Tufikiri kwa makini; tuepuke
kutukana watu, kupandisha mizuka ili kuhuisha roho ya kisasi. Tutaushinda uadui
kwa akili na imani, si imani bila
busara. Busara hutoka kwa Mungu.Kwa mungu kuna haki na thawabu. Mungu ni wa
utaratibu, si wa machafuko.Palipo na machafuko, hapana Mungu. Na sheria ni
msumeno.
. Ukweli si ule unaomfrahisha mtu; ukweli ni
mchungu lakini mtamu. Ukweli ni ubinadamu. Tuimarishe ubinadamu-humanity.Ndivyo
tunavyoikumbuka Septemba 11 mwaka 2001
congesdaima@yahoo.com0754 324 074,0786 324 074
No comments:
Post a Comment