Monday, November 7, 2011

Akina David Cameron hawajaanza leo kuiburuza Tanzania


 
 KATIKA mkutano wa Jumuiya ya Madola,uliofanyika juzi  hapa, tumemsikia David Cameron,Waziri Mkuu wa Uingereza,ambayo ni koloni letu akitoa shuruti,ili tubadili katiba,na kukubali mashoga!
 Watanzania wengi wamepinga jambo hili,lakini nadhani hawaelewi kwamba nchi 54 za Commonwealth, haziko huru-huria,zingali zikiburuzwa na Uingereza na washirika wao,kwa sababu ya misaada yao kwetu!
Wanatutishia kama watoto,kwa kuwa tulishasahau kujitegemea. Akina Julius Nyerere na siasa ya UJAMAA NA KUJITEGEMEA, walipoondoka, basi tukarejea kuwategemea ‘wajomba’ wa Magharibi.
Sasa, tunapatwa na kile walichoonya akina Nyerere, tunaamrishwa kama watoto!

Mwanzoni  mwa karne ya 19, ulimwengu ulianza harakati za kupinga Ukoloni na utumwa ulioendekezwa na mataifa ya Kaskazini dhidi ya yale ya Kusini.
    Watumwa toka nchi duni hususan za Afrika, Asia na Amerika Kusini walitumika kuzalisha mali kama kilimo cha mazao ya biashara, yaliyokuwa yakihitajiwa sana na wakubwa wa Magharibi.
    Mazao hayo yalitumiwa kama mali ghafi katika viwanda vyao; wao wakanufaika sana kuliko sisi vibarua au tuseme watumwa wao, tuliosalia duni, na bila usawa katika mambo yote, ikiwemo Haki za Binadamu, na usawa katika sheria.
     Vita vya kupinga unyanyasaji  (Civil War) vilianza Marekani , Aprili 12,mwaka 1861.
Hadi karne moja baadaye nchi nyingi zikiwemo za Afrika zilikwishapata uhuru; na utumwa ulikwisha pigwa marufuku katika Ulimwengu wote.
   Raia wote wa ulimwengu walikwisha kuwa sawa katika sheria na mahitaji mengine yote ya Binadamu.
Kupitia makubaliano ya Umoja wa Mataifa, hakuna raia wa nchi moja aliyekuwa bora kuliko wenzake wa nchi zilizokuwa dhalili.
Wakoloni walianza kutuamrisha siku nyingi. Kumbuka suala la Middleton na Benjamin Mengi.
    Ni kwa misingi hii, suala la Mwekezaji wa Kiingereza, Stewart Middleton,aliyekorofishana na mwekazaji mwenzake wa Kitanzania, Benjamin Mengi,kushughulikiwa na vyombo vyetu vya dola , ni kama ada.
    Mengi na Middleton walikorofishana katika masuala ya kibiashara, kufuatia ubia wa makampuni yao ya kilimo, ya Silverdale Tanzania Limited na Mbono Farms, ya huko Hai mkoani Kilimanjaro.
    Kulingana na gazeti la Mwananchi la Jumapili, Septemba 3,mwaka 2006,Mbunge mmoja wa Uingereza wa chama cha Mahafidhina, chama cha akina Cameron, Conservative, Roger Gale,alisema Bungeni kwamba Tanzania inyimwe misaada tangu sasa kwa sababu ya Mwekezaji huyo kutiwa nguvuni, ka kutishiwa kutimuliwa nchini!
    Kwamba Tanzania itatakiwa kunyimwa misaada na Uingereza, hadi hapo itakapoonyesha mazingira bora ya uwekezaji; yasiyowanyanyasa wawekezaji, hususan Waingereza!
Misaada inatunyima uhuru jamani…misaada! Inatuweka mkao wa kuliwa na Waingereza!
   Kwa kuwa Uingereza, kupitia Shirika lake la Misaada la Kimataifa,(DFID) ndiyo inayoomgoza kutoa misaada kwetu kuliko nchi nyingine yoyote duniani, basi swala la Mzungu huyo Stewart Middleton, linaweza kututoa nyongo!

     Si kusudi la makala hii kutaka kuingilia mgogoro wa Mengi na mzungu huyo, ambao tayari vyombo vyetu vya Dola vimechukua hatua stahili. Wala si nia ya makala hii kumpendelea Mtanzania mwenzetu, Mengi, na kutaka kumuumiza Mzungu huyo toka nchi wakoloni wetu wa zamani.

     Hata hivyo, nijadili basi kwamba serikali kwa kutumia vyombo vyake ambavyo tunaamini hutenda haki kwa raia wote wa nchi hii, wakiwemo wageni kama Middleton, imetekeleza wajibu wake bila upendeleo.

    Nasema bila upendeleo kwa sababu polisi walimtia mbaroni mzungu huyo, bila shaka baada ya suala hilo kufikishwa mezani kwao.
Kitendo cha mzungu yeyote kukabiliwa na polisi wetu wakiwa na silaha si hoja; kwa kuwa hata wazalendo wa nchi hii kukamatwa na polisi wenye silaha hata kwa tuhuma ndogo tu, kama kukataa kulipa deni la shilingi 1000, au kukopa kuku na kushindwa kulipa.

 Uingereza kwenyewe, hali ni hiyohiyo, kwamba watuhumiwa (bado si washitakiwa) hukabiliwa na polisi au askari kanzu wenye silaha.
 Ulimwengu haujasahau risasi za moto za askari wa Kiingereza zilipomiminwa miilini mwa wasio na hatia, kwa sababu tu walikaidi kukamatwa!

  Uingereza ikaishia kuomba radhi kwa kitendo cha askari wake kuua raia wa kigeni, kwa kuwa tu eti alifanana na waliolipua mfumo wa reli nchini humo…naam, magaidi!
   Middleton, kama raia wengine wa hapa, aliswekwa rumande wiki mbili (siku 14) bila kupewa dhamana, ambayo ni haki ya kila raia. Hata hivyo, aliachiwa huru, baada ya  vyombo vyetu vya dola kumaizi kuwa  madai dhidi yake hayakuwa na msingi wowote.

   Yawezekana kulikuwa na makosa ya kiutendaji au kiutekelezaji; lakini angalau kilichotendeka kimeonyesha kuwa vyombo vyetu vilifanya kazi kwa usawa, bila upendeleo wowote.
     Vilimkamata Mwingereza huyo; vikachunguza madai dhidi yake, kisha vikamwachia huru baada ya kubaini kuwa hakuwa na kesi ya kujibu.
   Suala la kumnyima Mzungu huyo dhamana, kama wanyimwavyo raia wengine ni changamoto kwa vyombo vyetu, katika barabara ya kuelekea utawala bora wa haki na demokrasia; na wala si kasoro kwa Middleton kwa kuwa ni mweupe, tena kutoka kwa Mabwana wakubwa, Uingereza.
   Kulikuwa na sababu nyingi za kumnyima dhamana Middleton; kwa sababu za usalama wake au hata ili kuepuka uwezekano wa yeye kutoweka kabla ya suala lake kushughulikiwa kwa nja za haki.
   Hata hivyo, kwa kujali sana uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Uingereza, serikali yetu ikafanya mazungumzo na wafanyabiashara hao wanaozozana, kisha ikazungumza kidiplomasia na ubalozi wa Uingereza. Suala hilo tayari liko mahakamani; chombo pekee cha kutoa haki kinachotambuliwa hata na Bunge la Uingereza.
    Lakini kwa kuwa sisi ni nchi masikini; tunaendesha mambo yetu kwa ufadhili wa Mamwinyi kama Mbunge, Roger Gale, vyombo vyetu kushughulikia suala la Mwekezaji wa Kiingereza, ni tatizo kubwa, la kusababisha Waziri Mkuu, Tony Blair (wakati huo) kuombwa kukata misaada!
   Makala hii haishangai kauli za aina hiyo katika mabunge ya wakoloni wetu wa zamani, ambao hata sasa wanatutawala kwa kutumia misaada yao inayopitia katika makampuni anuai ambayo ni mawakala wao wa kutukoloni (colonize);kwa kuwa machoni pao, sisi si chochote, si lolote,isipokuwa watumwa !

   Zimbabwe, rais Robert Mugabe anaonekana dikteta wa hali ya juu sana, si na wananchi, bali anavyotazamwa na Bunge la Uingereza kwanza.
 Si Zimbabwe tu, bali popote Waigereza walipowahi kutawala, ama palipo na maslahi yao, yanayopingwa kwa nguvu na serikali husika
.Naam huu ni uchoyo wa uingereza, ubaguzi na dharau.
   Waama, kila maslahi ya Marekani au Uingereza yanapopingwa kwa nguvu, basi huonekana machoni pao kuwa ni haki za “Binadamu” zimevunjwa! Je, binadamu ni nani? Marekani na Uingereza peke yake, bila raia wa mataifa mengine?
Je, inapokuja daawa baina ya Muingereza na Mtanzania, dola ikunje mkia miguuni, mithili ya kijibwa? Iufyate!!
  Mwaka 2004, askari wawili wa nchi hiyo waliokuwa mapumzikoni nchini, wakitokea vitani  Iraki, Nigel David (23) na  Brett Richard (20), walitiwa mbaroni kwa tuhuma za kumbaka kwa zamu hadi kumuua msichana wa Kitanzania, Conjesta Ulikaye, mnamo Novemba 10, 2004.
   Tukio hilo lilitokea katika  ufukwe wa hoteli ya Siliver Sands, Dar es salaam. Shauri hilo la kesi ya mauaji, likashughulikiwa kwa siku 36 tu; wakati kesi za mauaji zinazowahusu Watanzania huchukua miaka mingi tu.
   Nigel na Brett walifikishwa mahakamani Novemba 16; yaani siku sita tu baada ya tukio.Kesi hiyo ilifutwa Desemba 22 mwaka jana, ikiwaacha ndugu wa marehemu kulalamikia mazingira hayo ya kuharakishwa kesi ya tukio la kikatili, na watuhumiwa kufutiwa shitaka upesi, kwa mujibu wa kifungu namba 91 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 1985.
      Mwandishi wa makala hii, alimuuliza Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Geofrey Shaidi, Machi Mosi mwaka 2006 jijini Mwanza, alipokuwa  akihutubia Mkutano wa Pili wa mwaka wa wanasheria wa   serikali.
    Kwamba kitendo cha ofisi yake kukimbia kuwaacha huru askari hao wa Uingereza, ilikuwa kulinda maslahi ya Uingereza au Tanzania?!
    “ Hawakuachiwa kwa ajili ya kulinda maslahi ya Uingereza au ya Tanzania…ushahidi uliokuwepo haukutosha. Wasingeendelea kushikiliwa bila ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani”, DPP Shaidi alisema.

    “Kesi hazicheleweshwi na ofisi ya DPP; zinachelewa mahakamani,zinapokuwa zikisubiri kupangiwa tarehe ya kusikilizwa. Hivyo faili la Wazungu hao lilipofika kwetu tukalishughulikia kama kawaida”, Shaidi aliendelea kufafanua.

   Akasema pia kwamba wanajeshi hao waliokuwa mapumzikoni wakitokea Iraki, vitani, hawakuachiwa huru kwa sababu ya serikali ya Tanzania kuchelea kunyimwa misaada na Uingereza, iwapo wangetiwa hatiani na mahakama na kupewa adhabu ya kunyongwa.

   Naam: Leo, baada ya kauli ya Mkurugenzi huyo wa Mashitaka nchini,Bunge la Uingereza limeombwa kuinyima misaada Tanzania kwa Muingereza  mwingine kutiwa mbaroni (kukamatwa tu) kwa shauri la kibiashara tu; si la mauaji. Na wala hajahukumiwa kifungo!
    Kwa jamaa na ndugu wa Marehemu Conjesta Ulikaye, wanaweza kupata jawabu la malalamiko yao dhidi ya vyombo vyetu vya dola. Pengine wangedhani wahusika walihongwa na wazungu hao wanajeshi, au ulikuwa woga wa bure kwa ngozi nyeupe katika kutekeleza haki.
   Kumbe picha inayoonekana leo katika nchi zetu tegemezi, ni kuingiliwa hata kuziondolea mahakama zetu uhuru wake.
 Ni hapa, kauli ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Geofrey Shaidi, inapoweza kutiliwa shaka na umma wa Watanzania leo, kwamba kesi za Wazungu, hususan Waingereza, haziishiki pabaya serikali!
     Kulingana na gazeti la Mwananchi la Jumapili, Septemba 3, mwaka 2006, misaada tunayopata toka Uingereza, imeongezeka kutoka Pauni milioni 80 (sh.Bilioni 208)mwaka 2003/2004 hadi pauni milioni 110 (sh.bilioni 286) mwaka 2006 na mwaka 2007.; huku asilimia 70 ikienda katika Bajeti.

   Naam, haya ndiyo madhara ya misaada toka kwa matajiri…kuingiliwa hadi uvunguni, chumbani na hata shukani! Uhuru wetu tuliopata Desemba 9, 1961 toka kwa Malkia wa Uingereza uko wapi?
Ati tunaadhimisha miaka 50 ya uhuru!
     Kama  Uhuru upo, kwa nini akina Roger Gale, washinikize vyombo vyetu kuchelea kuwachukulia hatua wawekezaji kama  Stewart Middleton, kama wana makosa?
Kwanini David Cameroon atuamrishe kukubali ushoga? Kwa nini tulazimishwe kwa kiwango hiki kama tuko huru?
Au wazungu hawakosei, kama si kuwa juu ya sheria za nchi walizowahi kutawala; ama wanaendelea kuzitawala kwa “remote control” kupitia mashirika ya misaada?
    Lini Waafrika tutakuwa huru dhidi ya ubeberu wa kimagharibi?
Kwa kuwa Tanzania ni nchi huru, na wala si Iraki, Afghanstan au Somalia ambako hakuna mfumo wa utawala unaoeleweka, ndiko ambako Uingereza ingetilia mashaka mfumo wa sheria na maamuzi ya haki, na kamwe si Tanzania.
    Uingereza itambue kuwa uhusiano uliopo kati yetu ni wa usawa, na wala si wa nchi moja kujiona iko juu kuliko nyingine katika jambo lolote, likiwemo la kisheria. Kama Mtanzania anavyoweza kufungwa kwa kuingia nchini humo bila kufuata taratibu, ndivyo Muingereza anavyoweza kujikuta Segerea au Butimba, kwa kukutwa na bangi.
   Kamwe, nchi yoyote isilalamike hatua za haki zinapochukuliwa dhidi ya mshukiwa au mshitakiwa.
Tumefika hapa kwa sababu ya kujikomba, laity Nyerere,Kaunda,Kenyatta,Nkrumah na wenzao wangekuwa hai leo!
Kwa kuwa hatuko huru,ndiyo maana tunaswagwa…
0786 324 074

No comments:

Post a Comment