Monday, December 12, 2011

WABUNGE WA TANZANIA NA POSHO NA SHAMBA LA WANYAMA


WABUNGE ni wanasiasa.
Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muunganoi wa Tanzania ni wanasiasa.Wanasiasa wote(kasoro wachache tu) hufanana; hulingana na wote wana malengo mamoja ya kupata madaraka,kujiongezea vyeo na ukwasi na kasha kutumia madaraka waliyopata kwa fedha zao ili kujiongezea fedha.
Wanasiasa hutumia madaraka wanayopata ili kujiongezea utajiri, na kasha hutumia utajiri ili kujilimbikizia vyeo,madaraka na ‘uheshimiwa’. Wanasiasa wote duniani hufanana; ni wachoyo na wabinafsi.
Mwanamuziki , Roger Whittaker, alipata kuimba hivi:
“Politicians are like a bunch of bananas. They hang together, they all are yellow, and there is not a straight one”.
Kwa tafsiri yangu, Whittaker angeimba hivi kwa Kiswahili. “Wanasiasa ni mithili ya ndizi katika chana moja.Hushikana mahali pamoja; ndizi zote zina rangi moja ya njano; na kati ya hizi hakuna hata moja iliyonyooka!”.
Ndizi zote zimepinda! Na wanasiasa wote wamepinda; ni kama walizaliwa pamoja, wanashikiliwa pamoja(kwenye uchu wa madaraka,ukwasi na tama ya kila jambo)pamoja na vyeo na maslahi. Rangi yao ni moja-NJANO-ni wapenda maslahi na hawatabiriki, na hakuna hata mmoja kati yao aliyenyooka.
Lesoni ya Waadventista wa Sabato ya Oktoba-Desemba,mwaka huu 2011,ukurasa wa 105, kumeandikwa hivi:
“Politicians say one thing when seeking election, and then do the opposite once in office, all the while accepting thinly veil bribes from special interests”.
Wanasiasa wote duniani, wakisemacho wakati wanapotafuta kuchaguliwa wakati wa chaguzi anuwai, pindi wakipata madaraka hufanya kinyume chake; na wanachotazama ni maslahi yao hata kama yamekuja kwa njia haramu.
Wanasiasa, wakisemacho hawakitendi; wakitendacho hawakisemi. Unaweza kusema hivi kwa Kiingereza, “They never Walk the Talk” wana maneno matupu yasiyo na vitendo, wana ahadi hewa na matumaini ya bure kwa wale wanaowaongoza. Ghiliba Ghilibu?
Twapaswa kutowaamini wanasiasa. Tunao wengi duniani, hata hapa Tanzania wanasiasa hata wa kusoma wapo wengi,lakini hawana faida. Shida yetu ni ombwe la uongozi. Viongozi ama hawapo, au hata kama wapo hawajulikani walipo.
Kwa sababu ya kukosekana viongozi, ndiyo maana wanasiasa wale wote tunaowaita viongozi(kwa ujumla wao) wanakubalina kwa pamoja bila kujali itikadi zao kwamba wajiongezee posho za vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,kutoska shilingi 70,000 hadi 200,000 kwa siku.
Hili ni ongezeko lazaidi ya asilimia 180. Spika wa Bunge, Anne Makinda, anasema sababu ya kufanya hivi ni kupanda kwa gharama za maisha,hususan Dodoma, mahali waheshimiwa hawa(wanasiasa-wabunge) wanakoishi nyakati za vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Gharama za maisha zimepanda Dodoma(siyo nchi nzima?),halafu kwa waheshimiwa wabunge tu? Gharama za maisha hazijapanda katika maeneo mengine ya nchi wanakoishi Watanzania wengine zaidi ya milioni 42?
Majibu ya maswali haya ni rahisi mno.Kwamba, kwa tabia ya wanasiasa, wao hujijua wao peke yao, Watanzania waliobaki huwa hawajulikani.
Kila siku waheshimiwa hawa husikika wakisema, “Mimi na watu wangu!” Yaani sisi(Watanzania) ni watu wao!
Halafu husema, “Jimboni kwangu” yaani majimbo yote na watu wote ni mali zao, kwa sababu hiyo wamepewa mamlaka ya kuamua chochote kwa niaba yetu, wanafikiri kwa niaba yetu, na hata wao wakishiba wakati sisi tuna njaa kwao wanaona ni sawa sawa!
Dodoma, wakati wa vikao vya Bunge,kuna waheshimiwa na wapambe na familia zao wanapotambulishwa na Mheshimiwa spika. Kuna watu wengi wanaoandamana Dodoma na kufanya maisha yapande huko, halafu akina David Jairo wanakusanya pesa za umma na kuwalipa posho nono,kwa kile ambacho wala hakina maslahi ya taifa.
Dodoma, wakati wa vikao vya Bunge, kuna watu wengi,kuna ‘ma kaka poa’ na  ‘ma dada-poa’ wanaozengea zengea pesa za posho zitokanazo na kodi zetu. Hili niliache.
Nataka kusema kwamba, waheshimiwa Wabunge wao wanajiona ni muhimu sana kuliko wananchi wa kawaida.
Kama msomaji unabisha,nenda kasome kitabu kiitwacho, ANIMAL FARM(Shamba la Wanyama) cha Mwandishi wa Kiingereza, George Orwell.
Orwell, aliandika kejeli(satire) kwamba,katika Shamba la Wanyama, viongozi wa wanyama wao walijiona, “More equal than others” wanao usawa zaidi ya wanyama wenzao;yaani walistahili maslahi zaidi ya wanyama wa kawaida katika haka ‘kasungura kadogo’!!
Naam, waheshimiwa wabunge wetu wanafanana mno na waliokuwa viongozi wa Shamba la Wanyama wa George Orwell.Kwamba wao “ are more equal than other Tanzanians” tuseme wao ni bora zaidi kuliko sisi,ndiyo maana maisha yanakuwa magumu kwao zaidi kuliko sisi,tena ni magumu zaidi Dodoma kuliko majimboni kwao!
Nimuunge  Mkono David Kafulila, Mbunge wa Kigoma Kusini, kwamba wanalipwa mshahara kwa sababu ya vikao huko Dodoma, Bungeni, sasa posho za vikao za nini wakati tayari wamelipwa mshahara kwa kazi hiyo?
Ukiacha Kafulila na wengine wachache, wabunge wote wameweka itikadi zao pembeni kuchukua posho nono,kwa hiyo hawana tofauti sana na ‘Nguruwe’ wa George OIrwell katika Shamba la Wanyama.
George Orwell hakukusudia kumwita mtu yeyote nguruwe, hii ni kejeli name sikusudii kuwaita viongozi wetu nguruwe, ila nguruwe walikuwa viongozi katika Shamba la Wanyama la George Orwell ambalo nimechukua mfano kuwasilisha ujumbe wangu.
George Orwell, alilenga kuwasema wanasiasa ‘tamaa mbele-mauti nyuma’ na mabeberu ambao walidhani uongozi ni kujitofautisha na umma, ni kustahili heshima zaidi,maslahi,zaidi mafao manono zaidi na stahili zaidi kuliko wananchi wa kawaida.
Tunajadili Haki za Binadamu na usawa na uhuru wa kweli katika hii miaka 50 ya Uhuru iliyosherehekewa kwa mbwembwe juzi.
Tunajadili usawa, ambao tunasema Katiba yetu inasema, ‘Binadamu wote ni sawa”.
 Je, kuna usawa katika Shamba la Wanyama, wakati viongozi wanapojiona kuwa na ‘usawa zaidi’ kuliko sisi wengine?
Kwa mfano, wananchi sisi wa vijijini, ambao maisha ni magumu mara dufu kuliko mji wowote, achilia mbali Dodoma, tunaambiwa ‘kasungura ni kadogo’ hata wanafunzi wanaketi sakafuni, tuseme mchangani maana hata hiyo sakafu hakuna, wanapokuwa madarasani.
Tunaambiwa ‘kasungura ni kadogo’ wakati hatuna barabara, hospitali, zahanati,maji salama n.k
Halafu, watu wanadhani hawa wanasiasa wabaya ni wa chama Fulani tu. Kwa ujumla kwenye maslahi wote hufanana,( labda kasoro Kafulila na wenzake); ndiyo maana Whitteker akaimba kwamba, “They are like a bunch of bananas. They hang together, they all are yellow and there is not a straight one”
Siyo Mbowe, Siyo Shibuda, Mizengo Pinda na wenzao, woote ni wamoja na wameshikiliwa na moyo mmoja(maslahi ya wabunge na posho zaidi) na wote ni rangi moja-NDIZI- na hakuna aliyenyooka!!
  congesdaima@yahoo.com
0786/0754-324 074





No comments:

Post a Comment