Monday, December 19, 2011

KIFO CHA KIM JONG IL KITUPE SOMO AFRIKA

Korea Kaskazini,  baada ya kifo cha Rais kuna kituko cha mchakato wa kurithishana madaraka, kutoka kwa  Marehemu Kim Il Jong kwenda kwa mwanaye wa mwisho, Kim Jong-UN. 
 Kim Jong IL naye alirithi utawala kutoka kwa babaye, Kim Il Sung, mwaka 1994.
 Wakati hata hapa Afrika Mashariki, tunayaona sana haya.
 RAIS Yoweri  Kaguta Museveni, Aliuanza mwaka 2009 kwa kumteua mkewe, Janet, kuwa Waziri wa    eneo la Karamoja.
   Watu walipompinga sana kuifanya Uganda kama kampuni binafsi ya familia, akasema Janet ndiye mtu pekee Uganda , ambaye anaweza kukabali kumsaidia kuunganisha eneo hilo lenye kero na dhiki nyingi.
  Kwamba, hapakuwa na mtu Uganda , ambaye angekubali kufanya kazi eneo lenye njaa, vita na machafuko, isipokuwa Janet Museveni. Rais Museveni pia alishalalamikiwa kuwapa vyeo kaka yake na mwanaye, kana kwamba serikali ya Uganda ni kampuni ya familia.
  Familia nyingi za Marais hapa Duniani zina kawaida ya kurithishana madaraka na vyeo serikalini, hata raia wanaposimama kupinga mtindo huo.
   Afrika, inashuhudia marais wakifa, watoto wao wanatawazwa kuchukuwa mahali pao, utadhani hakuna watu wengine wenye utashi, busara ama uwezo.Hata chaguzi za kiini macho zinapofanyika, bado hao watoto wa marais waliofariki, hushinda kwa kishindo na tsunami na kuzima ngebe za wapinzani.
  Mwaka 1979 kulikuwa na wimbi la kuwapindua madikteta.
Na mwanzoni mwa mwaka 2011 wamepinduliwa Madikteta tangu Tunisia,Libya na Misri na upepo bado unavuma Kaskazini,labda utashuka Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Ni wakati  huo  mwaka 1979  akina Amin Dada na Marcius Nguema Biyogo waliondoka madarakani ili kupisha mabadiliko.
   Nataka kusema kwamba, siyo Korea Kaskazini tu ambako Dikteta Kim Il Sung alikufa mwaka 1994 akamwachia mwanaye, Kim Jong Il madaraka na sasa hata Kim Jong Il    alipofariki akawachia Kim Jong-UN.
.Na wala siyo Uganda tu, ambako Janet Museveni amepewa uwaziri na mumewe, ili pengine akiondoka, baadaye apate kumrithi.
   Katika ulimwengu huu watu hutaka kuwarithisha wana, mabinti,ndugu, jamaa na rafiki madaraka ili kulindiana heshima kufuatia wimbi la kuumbuana na kushitakiana kama Zambia na Malawi ambako akina Frederick Chiluba na Bakil Muluzi wamekumbwa na kitisho cha kuishi nyuma ya nondo za magereza.
   Siyo neno kama Janet au jamaa yeyote wa Rais watakuwa wanamapinduzi na wazalendo waliouza mali zao kuikomboa nchi kama Fidel Alejandro na Raul Castro Ruz, huko Cuba .
  Nazungumzia hatari ya viongozi tulio nao hapa Afrika kutumia fedha za walipa kodi, kujijengea himaya za kinasaba au miliki za kifalme na kisultani, katika nchi zetu zinazoitwa eti za kidemokrasia.
   Hawa viongozi wetu hawataki kuondoka madarakani kwa sababu waliikomboa nchi kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza.
WANARITHISHANA MARAKA ili wakiondoka wao maslahi yao yalindwe kama ilivyo Zimbabwe kwa akina Morgan Tsvangirai na R.G. Mugabe.
   Ukichunguza kwa makini, utaona aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika(AU) ,Muammar al-Qaddafi wa Libya alikuwa  hajaondoka madarakani tangu apindue serikali mwaka 1969.
Hata hivyo napingana na maguvu ya NATO kumpindua Gaddafi na kumuua. Afrika yenyewe inapaswa kujadili jambo hili kwa kina,ili kuepuka ukoloni.
Huyu  Gaddafi ndiye aliyesema Uganda kwamba ingekuwa heri ‘wanamapinduzi’ kama Museveni au Mugabe wasiondoke MADARAKANI!
  Hata Misri, Hosni Mubarak aliingia madarakani baada ya Rais Anwar Sadat kuuawa kwa risasi Oktoba 6, mwaka 1981. Alikaa madarakani hadi mwaka huu 2011 alipoondoka kwa NGUVU YA UMMA.
 Kuna maneno maneno kwamba Qaddafi na Mubarak nao walitaka kuwarithisha watoto wao pindi wangeondoka, ili kuweka mambo yao sawa sawa.
   Nchini Kenya , mbio za Uhuru Kenyatta kuingia madarakani zilikitumbukia nyongo chama tawala cha zamani KANU, kikashindwa na Muungano wa Upinde wa Mvua, NARC.
   Naam, katika Tanzania yetu, uataona kitu hiki kurithishana madaraka serikalini na chama tawala baina ya ndugu, watoto na jamaa za vigogo na wenye nasaba.
  Tulishaona watoto wa vigogo wakipigana vikumbo kugombea vyeo, hususan Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM(NEC) na hata wamejaribu kuingia Kamati Kuu(CC) ya Chama ili kulinda huko maslahi, milki na himaya ya baba zao.
   WANAWANIA UBUNGE na nyadhifa nyingine, si kwa sababu wanataka sana kuwatumikia wananchi, bali wanataka kurithi madaraka ya baba zao wanapostaafu.
   Naam, Tanzania kama nchi nyingine nilizotaja, inakuwa vigumu masikini wa vijijini kugombea nafasi za uongozi, wakapata kura za kutosha.
   Kwa sababu, walioko juu wanataka kurithishana madaraka na ndugu na wapambe,kama si marafiki ama wenye nasaba.
. Wanaotaka kudumu kuwa wabunge na mawaziri ni wale wanaoitwa ‘mtoto wa fulani’ ili kulinda milki yao .
 Hawa, ni wake, jamaa, watoto na marafiki za wakubwa, ambao hata Benki Kuu(BoT) tulisikia juzi hapa wakiwa wameajiriwa bila kuwa na sifa.
   Dikteta wa zamani wa Argentina , Juan Peron alitawala mwaka 1946 hadi 55 akapinduliwa na jeshi.
   Mwaka 1973 akarejea toka uhamishoni Uhispania na kuwa rais tena. Alimfanya mkewe wa pili, Isabel kuwa Makamu wake. Huyo Isabel hakupendwa na raia kama mkewe wa kwanza, Eva ama kama walivyomwita, Evita.
   Peron alikufa mwaka 1974, Isabel akawa rais.
 Nchi ikawa ‘wizi mtupu’ kwa sababu ya utawala mbovu, watu kuingia madarakani kwa upendeleo bila uwezo. Mfumuko wa bei ulipanda hadi asilimia 500 hadi akapinduliwa na jeshi.
  Huu upendeleo na ubinafsi natawala za wapambe na unasaba, ndio unaoipeleka Afrika kaburini.
 Kwa sababu wenye uchungu na nchi wananyimwa fursa za kujitawala. Hawana fedha, hawana mvuto kwa wapiga kura wa 'kura za kula'.
Waliorithishwa utawala huwa hawana uchungu na nchi; hawana tofauti na Isabel.Nikuponda maraha tu,kwa fedha za walipa kodi, wanakwenda kujifungua Paris,London au New York wakati raia wanapolazwa wanne kitanda kimoja, ama wanapokufa kwa kukosa tiba.
Wake zao na hawa watoto wao wanakula maisha kwa jasho la walala hoi.
 
   Wana kula maraha mpaka nchi inakauka-wao hawana habari-gharama za maisha zinapanda, wizi wa fedha za umma, ufisadi unakuwa mkubwa ili kugharimia starehe.
 Hata Chadema hawako salama sana na tabia hii ya kurithishana madaraka na vyeo kinasaba-huu ni ukoloni usiovumiliwa hata chembe!
    0786-324 074
congesdaima@yahoo.com
 
 
 

No comments:

Post a Comment