Monday, December 19, 2011

BURIANI KIM JONG IL

 
 KIFO CHA KIM JONG IL NI 'SHANGWE' MAREKANI?
*mwoga wa kupanda ndege amekufa ajalini ndani ya treni!
 
KULIKUWA na watawala ‘magangwe’ ambao hawajawahi kuichelea(kuiogopa) Marekani wakati wowote, katika historia ya Ulimwengu:
  Field Marshal Fidel Alejandro Castro Ruz na mdogoye, Raul Castro wa Cuba, Robert Gabriel Mugabe wa Zimbabwe, Hugo Chavez wa Venezuela, Mahmoud Ahmadnejad wa Iran na Kim  Il Sung na baadaye Kim Jong Il wa Korea Kaskazini.
   Kwa uchache, ni viongozi machachari, “magangwe” waliowahi kuitukana Marekani katika mabaraza ya Umoja wa Mataifa,huko New York, na wakati mwingine walipotukana na kuigomea Marekani wakakabiliwa na vikwazo cha kiuchumi,ndiyo kunyimwa misaada na kushindwa kuuza fursa zake n.k
   Siku za karibuni , vyombo vya habari vya kimataifa  vimekuwa vinajadili  mchakato wa kung’atuka madarakani kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Il, kufuatia afya mbaya, na mchakato wa kumrithisha mwanaye mdogo kuliko wote, Kim Jong Un.
 Ndivyo ilivyotokea, baada ya Kim Jong Il kufariki dunia Jumamosi, Desemba 17 mwaka huu wa 2011.
 Kim Jong Il, alikuwa hazungumzwi vizuri na nchi za Magharibi, kufuatia kiburi chake,wakati mwingine akakisiwa gaidi,mlevi, chakaramu,mpenda vidosho na starehe.
  Inakisiwa kwamba,kwa mwaka mmoja, Kim Jong Il alikuwa akibugia yeye peke yake, konyagi kali na mvinyo wenye thamani ya Dola za Marekani 800,000.
Ni kama  zaidi ya shilingi bilioni moja za Tanzania, alizotumia kupata ‘kilaji’.
 Mwoga wa kupanda ndege, amekuwa akisafiri mara chache mno Uchina na Russia,lakini kwa treni la fahari sana lenye ulinzi mkali. Amekufa safarini akiwa katika treni hilo hilo.
 Kim Jong Il, anatajwa kupenda sana sinema, aliwahi kuandika kitabu kiitwacho, On The Art of Cinema.
 Kim Jong Il ambaye anaachia madaraka ya kuiongoza Jamhuri hiyo ya Korea , kufuatia mauti alizaliwa Baekdu, katika kibanda katika mlima mrefu huko Peninsula ya Korea, zama za Kisovieti.
 Nyaraka za Kisovieti hueleza alizaliwa katika kijiji cha Siberia ambako babaye, Kim Il Sung alikuwa Kapteni wa Brigedi maalum ya Wachina na wakimbizi wa Kikorea.
 Amesoma Pyongyang katika shule ya watoto wa vigogo, Namsam ambako watoto wa vigogo wa vyama vya Wafanyakazi kilichoongoza Kora tangu 1948, walikuwa wakisoma.
 Akasoma chuo Kikuu cha Kim Il Sung na kutunukiwa shahada ya siasa na uchumi mwaka 1964.
 Baada ya chuo kikuu ali pandishwa vyeo katika chama cha wafanyakazi, mwaka 1974 ilishajulikana angemrithi babaye.
 Ni kweli, Julai 8 mwaka 1994 babaye Kim Il Sung akafa, yeyeakachukua madaraka.
Tabia hii hata Afrika tumeiona Gabon, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo(DRC) na mahali pengine, na tunawaona vigogo wetu hapa wakijaribu kuwakweza watoto wao katika nyadhifa nyingi.
 Huyu Kim Jong Il alitazamiwa kumritisha mwanaye wa kwanza, Kim Chul,lakini sasa upepo mwanana unamwelekea Kim  Jong Un.
Mzee huyu ameoa mara tatu, ana watoto watatu, ana dada mmoja.
 Nakupa vimbwanga vya Mzee Kim Jong Il. Aliwahi kuhusishwa na ugaidi na biashara ya madawa ya kulevya.
Kumbuka pia kuna Propaganda za Marekani kwa wale wasiotakiwa;hupakwa matope.
 Kim Jong Il mwaka 1983 alikisiwa na Korea Kusini(Korea Kusini ni adui wa Korea Kaskazini sababu ni kibaraka wa Magharibi) kwamba ndiye aliyepiga mabomu Burma(Myanmar siku hizi) na kuua viongozi 17 wa Korea Kusini waliokuwa huko.
 Mwaka 1987 pia Korea Kusini walimtuhumu kupiga mabomu ndege yao na kuua watu 115 waliokuwemo. Mawakala wa usalama(mashushushu) walitoa siri kwamba eti Kim Jong Il aliamuru ipigwe.
 Huyu jamaa anayeondoka madarakani na kumrithisha mwanaye huyo Kim Jong Un, alikuwa akiongea kwa nadra.
Wengine walidhani ni mbumbumbu ama mkichaa tu.
Aliyekuwa Waziri wa Mambe ya Nje wa zamani wa Marekani, Madeleine K. Albright alifika mjini Pyongyang, Oktoba mwaka 2000 ,akasema baadaye kwamba Kim hakuwa zoba, na siyo mwango kama walivyosema.
       Kiini cha uadui na Marekani
Alianza kurutubisha Uranium mwaka 1990.Wamekuwa wakifanya majaribio ya makombora ya Nyuklia miaka ya karibuni, Marekani kawashawishi kwa pesa nyingi waachane na mpango wao wa Nyukilia,wanasema wanataka kurutubisha Uraniu ili wapate nishati ya umeme.
 Sasa, Marekani ilitaka kuwahonga mapipa mengi tu ya mafuta, imeshindikana, wakaanza kufanya majaribio ya makombora ya Nyuklia chini ya ardhi na baharini,kitendo ambacho hakikupendwa na Korea Kusini na Japan.
 Hata hivyo, Septemba 11 mwaka 2001 Kim Jong Il alimtumia salamu za rambirambi George W. Bush kulaani kiama cha ndege zilizoangamiza WORLD TRADE CENTRE,iliyotaka kulipua Pentagon na ile iliyotua huko Pennsylvania.
 Hata hivyo,
Bush akatangaza kuiondosha Korea Kaskazini katika nchi za mhimili wa Uovu Dunini(Axis of Evil) sambamba ya Iran ya Ahmadnejad na Irak ya Marehemu Saddam Hussein.
 Mrakani iliirejesha Korea hii katika mhimili wa uovu ‘The Axis of Evil”miaka michache iliyopita, mara Korea hii ilipoanza kufanya majaribio ya Nyuklia.
Kim Jong Il alizaliwa Feburuari 16 mwaka 1942 akarithi rasmi madaraka kutoka kwa babaye Oktoba 8 mwaka 1997. Kora ina wanajeshi 1,082,000.
 Baba yake, Kim Il Sung, alikufa mwaka 1994 na aliiongoza nchi hii kwa mkono wa chuma kwa miaka 40. Utaona kwamba Kim Jong ameongoza kutoka mwaka 1994 hadi Jumamosi, Desemba 17 mwaka huu wa 2011 kwa maradhi ya moyo.
  Baba yake, alifanyiwa maombolezo ya kitaifa kwa miaka mitatu hadi 1997 ndipo huyo Kim Jong Il aliyefariki baada ya kuugua muda mrefu alipokuwa mtu wa mwanzo katika nchi za Kikomunisti kumrithi babaye katika kitu cha urais.
 Akachaguliwa kuwa rais mwaka 1998 bila kupingwa. Hata huku watu wanapita bila kupingwa hata katika chaguzi za vyama!
   Umoja wa Mataifa unasemaje?
 Mwaka 2003; ilikuwa Agosti 29 mtangazaji mahiri wa BBC, Tim Sebastian katika kile kipindi chake maarufu, HARDtalk, akamuuliza kiongozi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Nguvu za Atomiki(IAEA),Mohammed El Baradei, kwamba ni nchi ipi ya kuogofya sana duniani?
 Ni Korea Kaskazini ama Iran? Dk.El Baradei akasema nchi sita ikiwemo Marekani, zilipokutana Beijing kujadili kitisho cha Nyuklia ulimwenguni,ziliiofia sana Korea hii na mpango wake wa kurutubisha uranium.
Kwamba walitumia mpango huo kujipatia chumo duniani. Halafu alisema Iran nayo ilikuwa inaanza kurutubisha Uranium, lakini Dk. El Baradei akaitaka Iran kufuata mkataba wa NPT(Nonproliferation Treaty) unaopinga ukaguzi kufanyika wa miradi ya Nyuklia.
 
           Korea Kaskazini  hakuna Mungu ila kuna Rais tu!
 Korea Kaskazini  kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa(UN) Mwaka 2005 ilikuwa na watu milioni 29.5 katika maili za mraba 47,399.
 Hapa wanaongea Kikorea na dini zao ni Budha, Chondogyo, na wanaamini Mungu hayupo kabisa duniani, sembuse Korea?!
 Marekani wanasema huko kuna wafungwa wa kisiasa 200,000 na wapinzani wa serikali huteswa na kunyongwa na wengine husota jela kwa kipigo kama watumwa.
 Nimeleta kisa hiki ili kujifunza kwamba hata katika nchi zetu hizi bado kuna matumizi mabaya ya fedha za umma, ulevi wa vigogo kwa pesa za umma na udikteta usio na faida kwa umma.
 Watoto wa vigogo huwarithi baba zao wanapofariki kama huyo Kim Jong Un; wakati huku watoto wa vigogo hurithi kila lililojema, wakati raia wanaponyauka kama maharage wakati wa hari.
 Wakati Kim akitumia bilioni moja kupiga mtindi, huku kwetu bajeti ya shilingi bilioni 30 kwa mwaka, ni za chai ya 'wazee'.na zaidi ta bilioni 20 ni posho za wabunge,bado za vigogo!!
   0786/0754 324 074
 

No comments:

Post a Comment