Monday, February 4, 2013

afrika kizimbani-13

JAMII ya Kitanzania ilipewa changamoto chungu kupitia filamu ya Darwin’s Nightmare, ili ijirekebishe.
Mbali na kutiwa chumvi hapa na pale, filamu hiyo ni darasa tosha kwa uzembe, uchafu, umbumbumbu, kulindana na kukumbatia ulegevu, kunakofanywa na jamii yetu leo.
Naam,kuacha kuwategemea Wazungu,Mataifa makubwa kwa misaada na kuwachia kuchuma rasilimali zetu.
   Kwa mtu aliyewahi kuiona filamu hiyo, maarufu kama ‘Mapanki’ ataona changamoto anuai ambazo kama zitafanyiwa kazi kwa uzalendo na jamii ya Kitanzania (si serikali peke yake), athari hazitakuwepo.
  Kwanza kabisa,    Vyombbo vya usalama vya nchi yetu vinatia mashaka kama kweli vilikuwa vikifanya kazi yake sawasawa kipindi  mtengenezaji wa Darwin’s Nightmare, Hubert Sauper  alikuwepo nchini kutengeneza filamu hiyo.
     Aibu  ambayo ni changamoto ya kwanza inayotakiwa kuchukuliwa hatua kali na vyombo vyetu, ni jinsi mtu mgeni kama Sauper, alivyomudu kupiga picha chumba cha kuongozea ndege cha Mwanza, bila wahusika kujua anachofanya!
Mzungu akifika nchini hakaguliwi kama Mweusi,hiki nini kama siyo utumwa?
   Nasema bila wahusika kujua, kwa sababu mwanzoni tu mwa filamu hiyo uwanja wa ndege wa Mwanza unaonekana katika filamu hiyo: Mfanyakazi wa uwanja wa ndege anaacha kuongoza ndege, na kwenda kupiga nzi au tuseme wadudu waliokuwa wakirandaranda katika kioo cha dirisha la ofisi hiyo, kiasi cha kutia kinyaa!
   Mfanyakazi huyo mwanamume, anainuka kitini pake na kuwapiga wadudu hao kwa hasira kwa kutumia kitu kama gazeti!
   Katika hali inayosononesha sana,kishindo cha kumpiga nyuki  au tuseme mdudu yule (bila shaka mchafu sana) kinatikisa ofisi nzima ile hadi kioo cha dirisha kinakaribia kuvunjika!
Kwa mzalendo yeyote wa nchi hii aliyepata bahati ya kuiona filamu hiyo, hataacha kujiuliza: 
 
“Mainzi hadi Uwanja wa ndege?”
     Uwanja wa ndege ni usoni mwa nchi yoyote.
Wageni wanapofika katika nchi yoyote, iwe kwa mara ya kwanza au kadhaa, wanachoshuhudia uwanja wa ndege ndicho kinachowapa picha kwamba nchi wanayoingia sasa ni ya aina gani?
  Ya baridi , ama joto sana?
nchi Ya watu wacheshi, wakorofi, waungwana, wenye maringo, wazembe, wachafu wasiojijali; au hata maridadi sana.
    Lakini kinachoonekana katika filamu ile mwanzoni tu ni wadudu wanaorandaranda chumba kile cha kuongozea ndege; ambamo haiingii akilini kuwa wakati Sauper ama wasaidizi wake wanapiga picha wahusika hawakujua kuwa kitendo kile cha kizembe kingeidhalilisha nchi yetu?
   Tena tujiulize: Hubert Sauper, aliwahi kutiwa mbaroni na uongozi wa kijiji kimoja mkoani Kagera mwaka 2004. Baadaye aliachwa kwa amri ya vigogo serikalini.
Hata watu walioshirikiana naye walitiwa mbaroni kwa tuhuma za kupiga picha kambi za uvuvi, bila vibali!
   Ilielezwa kuwa kitendo hicho kilichoitwa cha kijasusi na viongozi hao kiliwafanya Sauper na wenzake kunyang’anywa vifaa vyao, zikiwemo kamera ambazo zilikuwa na picha tunazoema leo kuwa zimetudhalilisha!
   Ajabu ni kwamba licha ya baadhi ya vyombo vya habari kutangaza kuwa watu hao ‘walitekwa nyara’ waliachwa huru; na zana zao walikabidhiwa, wasipate usumbufu wowote!
   Naam, walikuwa na vibali vyote vya kazi; vilivyotolewa na Idara yetu ya Habari, Maelezo; na kwamba walikuwa na baraka zote za kufanya kazi hiyo ambayo leo imeleta kizaazaa na kiza kinene!
 
  Inadaiwa na Sauper mwenyewe na baadhi ya viongozi wa serikali kwamba mtu huyu “mwiba mchungu” kwa serikali, alikuwa akiwahonga baadhi ya maofisa wa serikakali, ili aende maeneo fulani fulani, ambako alifanikiwa kupiga picha mbaya ambazo kwa yakini zinatudhalilisha sana.
     Kama mgeni anaweza kuingia katika nchi  hii leo (miaka takriban 17 baada ya Vita Baridi) akafanya upelelezi wake kwa nguvu ya kuhonga, ni aibu na changamoto kwa kila Mtanzania kwamba nchi yetu inakwenda wapi? Uzalendo upo kwa kiwango gani dhalili katika nchi hii?
   Kila nchi, hata iwe dhalili kiasi gani; ina vyombo vyake vingi tu vya usalama. Kuna ulinzi na upelelezi wa namna nyingi tu.
Wapo wapelelezi wa siri ambao katika filamu nyingi wanaonyeshwa wakitimiza majukumu yao.
Katika vitabu vingi vya hadithi, tunawasoma wakitimiza wajibu wao kwa taifa lao.
   Kazi yao ya msingi ni kukusanya na kufafanua taarifa wanazokusanya hata za mataifa ya nje, kutazama uwezekano wa kuwepo vita na hata harakati na tamaduni mbalimbali za nchi nyingine; hususan zisizo rafiki.
  Tumewahi kujifunza kazi za mashirika makubwa ya kijasusi kama vile KGB (Komitet Gosudarstvennoy  Bezopasnosti) la Urusi ya zamani, ambalo sasa ni KFB.
Yapo mengine kama FBI na CIA ya Marekani, MI-5  na MI-6 ya Uingereza na mengine ambayo hufanya upelelezi wa ndani na nje; kwa lengo zuri la kuhakikisha usalama na ustawi wa nchi zao na watu wao.
    Linapokuja suala tete la Hubert Sauper na filamu yake ya mapanki, umma wa Watanzania unapata maswali mengi:
Kwamba vyombo vyetu vya usalama ( Intelligence Agencies) vilikuwa wapi kumnasa Sauper?
    Magazeti yaliandika habari za kutekwa kwake na wavuvi visiwani. Kwa nini aliachwa huru kwa amri toka juu, halafu miaka michache tu baadaye nchi inaombolezea picha zilizopigwa machoni mwa vyombo hivi?
   Changamoto nyingine kutokana na filamu hii ni ukosefu wa ajira kwa vijana wetu.
Mtu aitwaye Raphael ameonekana katika vipande vigi vya filanu hiyo. Amejitambulisha kama Mlinzi, bila shaka wa Chuo cha Utafiti wa samaki.
  Anasema katika fiamu hiyo: “ Ukipata kazi hata mbaya, unafanya. Kwani hivi sasa ukitafuta kazi (nzuri) hakuna”.Ajira hakuna.
Hapa anaonekana akiwa na upinde na mishale yake.
 Asilimia 80 ya Watanzania hawana ajira za moja kwa moja.
 Wanajitafutia vibarua wanavyofanya kwa malipo kidogo sana kutoka kwa hawa wawekezaji.Wanapunjwa ama kudhalilishwa tu.
   Wengi wa wakazi wa Kanda ya Ziwa ni wakulima na pia wavuvi.
Katika mikoa hiyo samaki ni chakula, fedha, tena ni ajira.Siku hizi samaki hakuna, wanakwenda Nairobi na Ulaya, hata ziwani hakuna samaki,wamekwisha.
    Hivyo kinachoonyeshwa katika filamu hiyo ni kuhoji kama samaki wanaitosheleza jamii hiyo kwa chakula; ama kama wengi wamenufaika kutokana na sekta hiyo; na pia kama wanazo fedha za kutosha kupata mahitaji yao kupitia samaki.
   Kama samaki bado wananufaisha watu wachache, tena wageni, basi ndiyo maana kuna kelele hizi za baadhi ya dada zetu kujiuza kwa marubani wa madege ya Kirusi yanayokuja kuchukua minofu ya samaki kwa ujira wa dola 10!
    Hapa kuna msichana aliyeitwa Eliza, anayesemwa kuwa ‘chakula’ cha marubani wengi (a girl friend of many pilots); pamoja na bishara hii haramu, haachi kuisifia Tanzania kwamba jina lake ni tamu sana!
      Kwamba, kama jamii hii ingekuwa imenufaika sana kiuchumi kufuatia biashara ya sangara, basi hata watoto wa mitaani walioachwa kuzagaa bila msaada, wangetafutiwa ufumbuzi. Omba-omba walioanzisha kwaya ili kujitafutia chakula kutoka kwa wapita njia, labda baada ya kutelekezwa na jamii (siyo serikali pekee) wangetazamwa na jamii hii, ili wasigeuke ajenda ya kitaifa; na si katika Darwin peke yake.
    Umasikini na ujinga wa watu wetu unawafanya wanywe gongo katika makambi ya uvuvi.
Kiongozi wa kambi aliyetambulishwa kama Mkono,anawaongoza wenzake waliohojiwa na Sauper kueleza namna wasivyonufaishwa na kazi ya uvuvi…wanaonekana wakiwa bado katika nishai ya ulevi wa gongo; tena wakiwa wachafu wenye tongotongo usoni…wanatia kinyaa.
    Kwa Mgeni ambaye hajafika Tanzania, akiwaona hao jamaa zake Mkono, bila shaka atajua samaki wale watamu sangara huvuliwa na wanywa gongo wale wasioweza hata kunawa tongotongo!
 Ni aibu, tena kinyaa!Umalaya,uchangudoa,watoto wa mitaani n.k wakati tuna rasilimali?
  Vema Watanzania tukajiuliza: Kuna vijiwe vingapi vya gongo, ambako Watanzania wenzetu huamkia hata kabla ya kupiga mswaki na kuanza kulewa chakari?
 Kuna vijiwe vingapi vya vijana wetu, wasiojua hata kufagia uwanja nyumbani, ila kula-kulala?
Tuna rasilimali nyingi,lakini watu masikini-Poverty in the midst of plentful!
  Tena vipo vijiwe vingapi vya vijana wasio na ajira, lakini huamkia kuvuta bangi, madawa ya kulevya,ulevi n.k? Mwanza kuna vijiwe vya siasa tangu asubuhi hadi jioni,nenda KEMONDO,jirani na mitaa ya Uhuru na Bantu!
Tuna ardhi,mito,maziwa na mabonde yenye rutuba lakini tungali wenye njaa na machangudoa,wakabaji,vibaka na majambazi.
    Halafu, watoto hurejea nyumbani nyakati za chakula (huitwa watoto wa mama, kula kulala!) ambao aghalabu huiba mali za nyumbani ili watimize kiu yao ya ulevi wa madawa haramu, gongo, uasherati, uchafu na ujinga, bila kuzingatia litakalotokea maishani. Hawafundishwi kujitegemea,bali kutegemea misaada ya wafadhili.
    Kuhusu madhara ya utandawazi, wakati nchi za Ulaya zikinufaika sana na rasilimali zetu kama sangara, sisi Watanzania tunaonekana kuchechemea vilivyo katika vita hiyo ya kugombea maisha ili kujinusuru na kifo.
    Wakati madege makubwa ya Kirusi, Ullyushin, yakipaa kwa kasi na shehena ya minofu yetu kwenda Ulaya, anaonekana Mtanzania mmoja jirani na Uwanja wa ndege wa Mwanza, akiwa anaendesha baiskeli yake kwa kasi, utadhani alikuwa akiifukuza!
    Bila shaka Sauper, alitaka kuuonyesha ulimwengu kwamba, wakati wenzetu wakipora rasilimali zetu kwa ndege, sisi tungali tukitumia usafiri wa baiskeli! Tutafika saa ngapi katika zama wa sayansi na teknolojia?
Tutamiliki lini zana bora, kupitia mauzo ya rasilimali zetu nje?
 Lini tutakwenda mwendo kasi kama Wazungu, katika mbio za maendeleo katika Ulimwengu wa Uatadawazi na teknolojia?
    Kila siku, marubani waliohojiwa walisema kati ya tani 500 hadi 600 za samaki husombwa na ndege kwenga Ulaya.
 Kwamba dege moja tu lilikuwa na uwezo wa kubeba tani 55. Hali hiyo huwafanya marubani hao kuwa kazini kila kukicha.
    Aliyekuwa mtoto wa mitaani, Jonathan Nathaniel ambaye ni mchora picha, anaonekana katika filanu hiyo akijitambulisha kama raia wa dunia (Citizen of the World) kufuatia jamii ya kitanzania kutochukua hatua madhubuti za kuondosha tatizo la watoto hao!
 Naam, kutowatekeleza.
    Hii ni kuonyesha kuwa baadhi ya watoto wa mitaani wamepoteza mapenzi na uzalendo wao kwa Tanzania!
 Badala yake walijitambulisha kwa Sauper kama raia wa Dunia, na wala si wa Tanzania.Watoto wa mitaani hawaoni faida kuitwa Watanzania,ila raia wa duniani.
  Kuna mashirika mangapi hapa yanayojidai kuwafadhili omba-omba na watoto wa mitaani, lakini bado wapo na jamii inaona tu bila kuchukua hatua? Wapo watu wangapi hata Mwanza kwenyewe, ambao huporwa simu za mononi na mali zingine na watoto hao?
 Je, tumekubali wawe majambazi, bila kuchukua hatua tangu leo kuhakikisha kuwa hawapo mitaani, badala yake wanawezeshwa kufanya kazi halali?
  Tena, wapo watu wangapi wanaojineemesha kwa asasi za watoto wa mitaani, wakati wao wakipata adha zinazofichuliwa na filamu hiyo tunayosema inatudhalilisha?
 Kumbe inatufunua uovu wetu pia.
    Wanaonekana wakivuta petroli ili walewe. Wanavuta gundi, wanavuta  sigara na hata bangi.
Jomathan anapohojiwa anasema wanafanya hivyo ili kujisahaulisha na madhila wanayopata mitaani! Jua kali, mvua, baridi kali na kukosa faragha…watoto hulala vibarazani na dada, kaka ,mama na baba zao wanaojamiana mithili ya ng’ombe, pasi na faragha!
 Huyo, Jonathan aliyemsaidia Sauper kutengeneza filamu hiyo, bado ni "Chokoraa" aishie hata leo mitaani jijini Mwanza, licha ya kulipwa shilingi 300,000 na huyu Hubert Sauper.
 Hiki ni kitisho kwa taifa lolote linalotaka kujenga maadili mema kuwaacha watoto wa mitaani kuzagaa ili kuwa chanzo cha mapato kwa Wazungu na aibu kwetu wenyewe.
      Kwamba wakisha lewa hulala popote bila kuogopa.
 Na kwamba kutokana na hali hiyo ya kulewa, na kutojijua (wengine huonekana katika filamu hiyo, wakiwa wamelala usingizi mitaani nyakati za usiku)   hata wale wa kiume hulawitiwa bila habari wala hadhari…Je, Tanzania tumeshindwa kukabiliana na watoto wa mitaani?
      Kuna dhana inayosemwa na marubani wa Kirusi kuwa Watanzania hawataki kufanya kazi! (These black people do not work)!
Picha inayoonekana kupitia Darwin’s Nightmare ni kwamba Watanzania walio wengi ni wavivu wanaopenda raha, lakini hawataki kazi
 Bila shaka hapa, kinachozungumzwa ni kuhusu vijiwe viwe vya kahawa, karata, ‘deal’ za mjini ,majungu, siasa au hata uongo, vinavyofanywa nyakati za kazi!
     Katika hali hii tutawanusuru watoto wetu kutopigania sufuria la wali waliopewa na mpita njia?
   Jamii ijitazame…kuna vijiwe vingapi vya" Binzala-nzala" au ‘kula kulala, hasa mijini, ambao huamkia bao, karata na ubishi wa kijinga nyakati za kazi?
  Mwisho, rubani mmoja anapohojiwa juu ya zawadi za Krisimasi, anasema anawapelekea watoto wa Ulaya  zabibu toka Afrika, wakati watoto wa Afrika wanaletewa zawadi ya bunduki toka Ulaya, ili waendelee kuuana !
    Haya ni baadhi ya matusi mazito tunayopata toka kwa Wazungu, ambayo kila mmoja wetu kwa nafasi yake anapaswa kuchukua hatua tangu sasa ili kuhakikisha kilichosemwa kama kipo tukiondoe ili kujitakasa.
   Leo Waafrika tunauana bila kusameheana.
Viongozi wetu wanapoingia madarakani, hawataki tena kutenda haki, bali kuiba mpaka wanapoondolewa kwa mtutu wa bunduki, zilizoletwa na haohao majahili, Wazungu! Hii ni aibu!
    Kwa upande mwingine matusi hayo yaliyomo katika Darwin’s Nightmare ni changamoto kwetu kuacha uchafu, ujinga ,  uzezeta wa kukubali kuibiwa kila kilicho chetu kwa ujira kidogo.
   Ifike hatua tuwe wazalendo wa kweli wa nchi yetu na Bara letu, na siyo uzalendo wa matumbo yetu.
 Hii ni changamoto kwa viongozi wetu wanaodanganya umma ili wasalie madarakani, ambako huiba na kujinufaisha huku raia wakibaki fukara, hadi waanzishe vita na mauaji kupindiua serikali..aibu!
Tangu leo Afrika ione uchungu kwa haya yaliyosemwa na Hubert Sauper, badala ya kumtafuta ili kumshitaki, tukae chini na kuvimeza ‘vidonge’ alivyo tupa…Baniani mbaya, kiatu chake dawa!
Afrika inaibiwa sana!
  Mwandishi hupatikana kwa simu 0754 324 074 au 0786 324 074
   






No comments:

Post a Comment