Thursday, February 7, 2013

musoma

Polisi wanapowasaka wauaji wa Musoma kwa bunduki,virungu na pingu,wanaharakati wafungue darasa la uwajibibikaji  na Haki za Binadamu
 
TOLEO nambari 852 la gazeti hili la Rai(Januari 21-27 mwaka huu), niliandika katika Mraba huu kwamba, iko haja ya wanaharakati wa Haki za Binadamu kwenda Musoma, kufundisha Haki za Binadamu.
   Niliandika kwamba, ukitembea Musoma na kusikiliza maoni ya baadhi ya watu, hutakosa kurejesha fikra zako katika zama za mauaji ya kuangamiza(genocide)huko Rwanda , mwaka 1994.
   Katika makala yenye kichwa, “Musoma vijijini uzee ni baraka au laana?” nilifananisha uwezo wa kufikiri wa baadhi ya wakazi wa huko na wauaji wa Jimbo la Darfur( Sudan ) ama huko Chad , Congo Mashariki, Somali n.k
    Nilisema hapa mrabani, kwamba maeneo niliyotaja yamesababisha vikao vingi mjini Geneva , Uswisi, kujadili namna ya kuwaokoa watu katika maangamizi.
  Geneva , ni makao makuu ya Mashirika ya kutetea wakimbizi nay ale yanayoshughulikia Haki za Binadamu. Geneva ni kitovu cha kamati ya kimataifa ya Shirika la Msalaba Mwekundu(ICRC).
     Msalaba Mwekundu kazi yao ni kulinda na kuokoa maisha ya watu. Kwamba, Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoridhia Tangazo la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu, lililotolewa Desemba 10, mwaka 1948.
    Kwamba, mikataba ya Haki za Binadamu na ile ya Geneva (The Geneva Conventions), kama ule wa mwaka 1949; hukataza mauaji.
 Hata mateka wa vita wanalindwa na mikataba hii wasiuliwe kasha wapewe matibabu na huduma za kiafya hata wawapo na majeraha ya risasi, wanapokuwa mikononi mwa adui zao vitani.
  Kinyume cha harakati zza mashirika ya Haki za Binadamu na Msalaba Mwekundu, katika kulinda na kuokoa maisha ya watu, Musoma kuja ‘Janjaweed’ mithili ya wale wanamgambo wa Kiarabu wa huko Sudan , wanaofyeka watu kwa majambia makali sana . Musoma kuna kila dalili za watu kuanza kulipizana visasi.
   Sababu za watu kuwa na majambia au mapanga, ni visasi kufuatia tuhuma za kijinga-jinga, kama uchawi, ulozi, usihiri, wizi wa mifugo na hata chuki za kikabila. Ukitazama kwa maikini, utaona mfumo wa kutoa haki Musoma, mkoani Mara, unaugua kiharusi.
  Katika makala yangu katika mraba huu, Januari 21 mwaka huu, nilitaraji serikali ingechukua hatua haraka kupeleleza na kuyasaka makundi ya wauaji wenye mapanga(Jajaweed) ambao hukodishwa na watu kwenda kutekeleza mauaji ya kinyama; naam mauaji ya kisasi.
  Walemavu wa ngozi(albino) pia huuawa na hawa hawa Janjaweed, wanapotumwa na wenye fedha, kutaka kufanya matambiko yao anuwai.
 Mauaji ya kishenzi kama hayo ya Buhare, nje kidogo ya Manispaa ya Musoma, siku chache zilizopita, bila shaka yamefanywa na Janjaweed.
   Nataka nikwamnie msomaji. Zamani kidogo, walilipwa fedha wauaji wenye pindi na mishale ya sumu. Kwenda kuua mtu yeyote aliyetuhumiwa kuwa mchawi ama mwizi kwa minajiri ya kulipa kisasi, mradi kulikuwa na aliyetangaza ‘zabuni’ hiyo kwa ujira wa pesa.
 Musoma, kuna ‘Janjaweed’ wanaoendesha maisha yao kwa kuua. Musoma kuna vikundi vya siri vya wauaji wa kukodishwa.Wamefuzu medani za kuua na hata kuangamiza kizazi na koo(genocide) kwa mapanga makali na pinde zenye mishale ya sumu kali.
   Akina mama na kina baba vikongwe wanaotuhumiwa kwa uchawi, wameuliwa wengi bila serikali kuchukua hatua. Ulegevu wa serikali-polisi na mahakama- umewapa Janjaweed kupenya mkondo wa sheria.
 Nataka kusema kwamba, polisi mkoani Mara ni wazembe; tena wazembe kuliko. Nachelea kusema ni wala rushwa, wanaoharibu upelelezi wa kesi za namna hii, wanapokuwa wamepewa chochote kitu, ama kama wamelipwa ng’ombe, kondoo, kuku, bata kama siyo fedha taslim.
 Amini usiamini, vyombo vya kutoa haki(polisi na mahakama) mkoani Mara havitendi kazi yake sawa sawa. Kwa sababu, wezi na wahalifu wengine hata wa mauaji, hukamatwa leo, kasha wakaachwa huru kesho asubuhi.
 Kisingizio, ni kukosekana kwa ushahidi ama kushinda rufaa. Rufaa za Musoma husikilizwa wapi usiku wa manane, kama siyo upenuni mwa vilabu vya pombe za kienyeji, ama baa?
 Mahakama gani hukaa usiku, siku za siku kuu na mapumziko?
     Musoma, mhalifu akifungwa jela na mahakama ya Mwanzo Ijumaa jioni, keshoye Jumamosi ama keshokutwa  Jumapili, anarejea nyumbani, kwamba kashinda rufaa!
   Hayo ndiyo ya Musoma, sasa  wana ula wa chuya! Wahalifu wanapoachiwa huru hurejea vijijini kwenda kutishia raia wema waliowasema polisi au kutoa ushahidi mahakamani.
   Musoma, ukatoe ushahidi mahakamani, mhalifu afungwe  jela siku mbili, na kurejea nyumbani baada ya juma moja; hujipendi?! Utakatwa koromeo mchana kweupe.
Raia wema na waadilifu wamekatishwa tamaa na utendaji wa vyombo vya dola.
  Siku hizi watuhumiwa huuawa na wananchi wenye hasira kali. Hufuatwa hata makwao na kuuliwa kinyama, wao, wake na ndugu na jamaa zao, nyumba huchomwa moto hata mchana kweupe.
 Hakuna kuwapeleka watuhumiwa polisi au mahakamani, kwa madai kwamba watarejea kesho! Mahakama zinaugua kiharusi;polisi wana mafua!
    Kuna mahakama 15 tu za Mwanzo mkoani Mara. Mkoa mzima wa Mwanza una mahakama za Mwanzo 20.Mahakimu ni wachache, tunaambiwa kuna upungufu wa mahakimu wa mahakama za Mwanzo 500 nchi nzima!
 Hizi mahakama ambazo ndizo huwahudumia wananchi wengi wa vijijini, zina mahakimu wachache sana . Hawana vitendea kazi, kesi zimefurika.
   Hakimu mmoja husafiri kutoka mahakama moja kwenda nyingine; na huko kuna msongamano wa kesi nyingi tena za miaka mingi.
 Nataka kusema kwamba, ni nadra kupata haki vijijini kupitia mahakama za Mwanzo. Hata mahakama za wilaya ndizo huwaachia wezi na wahalifu kwa rufaa zilizosikilizwa baa au klabuni, siku zisizo za kazi.
  Mfumo wa utoaji haki mkoani Mara, una walakini.
Kama hauugui kifaduro, una kiharusi kikali.Hakimu mmoja husafiri kutoka mahakama moja kwenda nyingine, anaposhindwa, watendaji wa vijiji na kata ndiyo wanaowasomea mashitaka washitakiwa.
   Hawa, hawana hata ‘ABC’ ya sheria. Matokeo yake, dhamana huandamana na kitita cha noti. Bila fedha hakuna dhamana hata kama ni haki ya mshitakiwa kikatiba na kisheria.
   Vituo vya polisi vya vijijini mkoani Mara, vimegeuka kuwa mahakama, kwa sababu polisi hutoa hukumu;hutoza faini vituoni.
Wauza gongo na bangi, wezi wa bata, kuku,ng’ombe n.k huachiliwa vituo vya polisi mradi wawe na pesa za hongo na rushwa!
   Kama hujawahi kuona mtu akikaa mahabusu mwaka mzima, nenda katika mahabusu za Musoma vijijini, ufanye kosa dogo kasha usiwape rushwa polisi, watendaji wa kata na vijiji.
   Hiki ni kichocheo cha watu kuchukua sheria mkononi, ama kukodisha ‘Janjaweed’ ili wakawalipie visasi, kwa kuwa polisi na mahakama walishashindwa kuwafunga jela wauaji, wezi, majambazi, kwa kuwa wana pesa za rushwa.
  Huko Musoma, ile dhana ya Robert Darwin ya “Survival of The Fittest”(ya mwenye nguvu kuua wanyonge bila kufanywa kitu) hutenda kazi. Huna kitu Musoma huna haki polisi, ofisini kwa Mtendaji wa kijiji, wa kata hata mahakamani!
  Musoma vijijini, kama huna fedha za kujaza mafuta katika pikipiki ama gari la polisi, hakuna mtuhumiwa wako kukamatwa. Hata akikamatwa na kufikishwa kituoni, huna fedha za kumlisha chakula au kumlipia nauli kwenda rumande mjini Musoma, hawezi kupelekwa!
  Mkoani Mara, ndipo hakimu mmoja wa mahakama ya mwazo hukabiliwa na kesi nyingi, kwa sababu tarafa nzima huwa na mahakama moja ama mbili. Tarafa inakuwa na takriban watu 600,000.
Kuna kesi ngapi? Kesi nyingi hazitolewi maamuzi kwa wakati; na wanasheria wanamsemo kwamba, “Justice delayed is Justice denied”(haki iliyocheleweshwa ni haki iliyopotea).
 Kwa hiyo, Musoma hakuna haki? Kwa sababu haki hucheleweshwa, haki imepotea. Katika mazingira haya, wananchi wamekata tamaa, wanaamua kuwalipa ujira ‘Janjaweed’ ili wakawalipie kisasi dhidi ya wahalifu,watuhumiwa wao ama wabaya wao hata kama ni tuhuma za kijinga kama za kishirikina.
  Mfumo wa kutoa haki unaugua kiharusi mkoani Mara.Wizi wa mifugo unaendelea kwa sababu ukiwa na fedha utakamatwa leo, kesho utaachwa huru, au utafungwa leo na mahakama ya chini na kushinda rufaa usiku wa manane!
   Wapo watu, wanaposikia Musoma kuna mauaji ya kutisha, wanadhani kuna watu wakatili sana . Hapana! Haya ni mauaji ya visasi kwa sababu mfumo wa sheria umeshindwa.
  Si kila raia mwema huuliwa, ila ukituhumiwa.Mauaji ya kinyama huandamana na visasi kwa sababu mfumo wa sheria unaugua kiharusi kikali.
  Mauaji ya juzi huko Buhare, Musoma, ambako watu 17 wa ukoo mzima walifyekwa mapanga na kuchinjwa mithili ya njiwa, ni matokeo ya kulipizana visasi, kwa sababu vyombo vya dola(polisi, mahakama, mageteza na watendaji) walishashindwa kufanya kazi yao barabara.
 Nazungumzia uwajibikaji wa vyombo vya dola, na umuhimu wa viongozi wa vyama na serikali kuhimiza watu kuishi kwa kufuata sheria za nchi-uadilifu.
   Mauaji ya kulipa visasi; naam kulipa baya kwa baya(tit-for-tat) hudhihirisha kwamba mfumo wa kutoa haki Musoma unaugua kiharusi cha ubongo na kiwili wili.
 Mahali haki inapopatikana mahakamani, watu huridhika, amani hushamiri, maendeleo huja na kuna demokrasia. Tabia ya kuchukua sheria mkononi(Mob justice) iliyoenea Musoma, ni kielelezo kwamba raia hawataki tena kupeleka kesi zao mahakamani ama polisi, kwa sababu wanadhani hakuna haki.
 Siku hizi watuhumiwa huuawa hata mbele ya polisi.Polisi wanapoaachia huru watuhumiwa, waelewe wanasababisha mauaji ya visasi namna hii.
 Niliandika mrabani hapa Januari 21 mwaka huu kwamba, Musoma ndiko wanakofanya mikutano ya hadhara kutafuta namna ya kuwadhibiti wachawi kwa kuwakata mapanga!
 Ujinga umejaa vichwani mwa viongozi wa vijiji, vitongoji, kata n.k hadi sheria na haki za binadamu ni kitenda wili.
 Haki za binadamu ni lugha ya kawaida ya ubinadamu.Haki ingalipo Musoma lakini hutindika.
   Nataka kusema kwamba, Musoma hakuna ubinadamu, kwa sababu watu huongea lugha ya kuua kwa kulipa visasi-ni kuwaondolea watuhumiwa haki ya kuishi, hata kabla ya mahakama(chombo pekee cha kutoa haki nchini)kutoa hukumu.
 Narejea wito wangu kuwataka wanaharakati wa haki za binadamu kwenda Musoma mkoani Mara, kufundisha haki za binadamu, haki za raia, itifaki ya Geneva , uwajibikaji serikalini na vyombo vya dola, ili kukinusuru kizazi hicho na maangamizi!
  Narejea kauli yangu kusema kwamba, unahitajika mkakati mzito wa kuwanusuru watu hawa katika kitisho cha uvuli wa mauti ya kuchunjana kama ng’ombe kwa mapanga utadhani Bosnia , Darfur , Rwanda ya mwaka 1994, Somalia au Congo na Chad !!
   0715-324 074  
 
  
 
  

No comments:

Post a Comment