Aliwambwa msalabani, Dakawa,Morogoro,ili kuweka kielelezo cha kiongozi bora wa umma
 Na Conges Mramba, Mwanza
 
 NI SAA 4:30 hivi, asubuhi. Alhamisi, Aprili 12 mwaka 1984, Sokoine anatoka ofisini kweke mjini Dodoma , anaingia garini kwake, na kumwambia dereva kuwasha moto.
  Alikuwa mbioni kuanza safari kwenda Dar es salaam , baada ya kikao cha Bunge hapo Dodoma.
Mmoja wa wasaidizi wake, Harace Kolimba(naye sasa Marehemu), alikuwepo nje ya ofisi hiyo.
   “Kolimba”, anasema Sokoine, “Lini utakwenda Dar es salaam ? Ingia ndani ya gari twende”.
   “Nina tiketi ya ndege Mzee”, Kolimba anamwambia Waziri Mkuu, “Nitakuja mchana”.
     “Okay”, Sokoine anajibu; kisha akasema, “Tutaonana Dar es salaam ”.
   Baada ya kitambo, msafara wa Waziri Mkuu ukatimua vumbi kuelekea Dar. Hayati Sokoine hakufika mwisho wa safari yake.
   Umbali wa kama kilomita 40 Mashariki mwa Morogoro(Dakawa) gari aina ya Land Cruiser, iliyokuwa ikiendeshwa na mmoja wa wapigania uhuru wa Chama cha African National  Congress(ANC) cha Afrika Kusini, Dumisani Dube(23) akaingilia msafara wa Waziri Mkuu, akamgonga! Ilikuwa saa saba za mchana.
    Alipomgonga, akasababisha kifo chake. Kifo cha Sokoine kilisababishwa na ajali ya gari. Pengine, angesafiri kwa ndege, kama Kolimba, au kama wasafirivyo vigogo wetu leo, asingesafiri namna hiyo.
    Naam. Sokoine hakutaka kusafiri kwa madege ya fahari kwenda Dar es salaam. Alitaka kusafiri kama wasafirivyo Watanzania wengine.
  Kila Mtanzania, anajua anavyopitia makorongo na mahandaki mabarabarani. Wanaosafiri kwa ndege, hawajui adha za usafiri katika barabara za makorongo na mahandaki, za nchi hii.
   Nchi hii, hususan vijijini, kuna makorongo mabarabarani. Wabunge, madiwani na vigogo wetu, hata vijijini hawaendi; wanafika wakati wa msimu wa uchaguzi. Sokoine, alisafiri kama wasafirivyo Watanzania wengine; alijitolea mhanga maisha yake, kutumikia walalahoi na waamka hoi.
  Kama vigogo wetu leo wangekuwa wanaishi kama Hayati Moringe Edward Sokoine, basi hata ndege ya Rais, Gulf Stream 550 isingenunuliwa kwa bilioni 40, wakati barabara zikiwa mahandaki na mashimo matupu. Bila shaka, majengo  pacha ya BoT yaliyojengwa kwa  mabilioni ya utata, yasingekuwepo.Kashfa za EPA na Richmond nazo zisingekuwepo.
   Kama vigogo wetu wangemuenzi Sokoine hata kwa asilimia 27 tu(miaka iliyopita tangu afariki) Watanzania wasingekula majani na mizizi ya sumu, kwa kukosa chakula. Vigogo wetu walikuwa hawaachi kusisitiza, “Hata wananchi mle majani, lazima ndege ya Rais inunuliwe!” Kuna madaraja ya mabwana na watwana; watawala na watawaliwa.
   Naam; Watanzania tumemkumbuka hayati Sokoine Jumanne, Aprili 12 iliyopita
.Alikutwa na mauti Alhamisi, Aprili 12 mwaka 1984. ‘Bunduki kali’ dhidi ya wazembe, wezi na wahujumu uchumi ilitoweka ghafla, hadi sasa hakuna mbadala; hatuna spea.
 Aprili, ni mwezi wa kumbukumbu ya mauaji ya miamba duniani. Rais Abraham Lincoln wa Marekani,  Mpigania haki za Weusi wa Marekani,Martin Luther King Jr. alikufa Aprili. Rais William R. Tolbert wa Liberia, alichinjwa Aprili 12 mwaka 1980 katika mapinduzi yaliyomweka Samuel Doe madarakani.
   Pia, Aprili 6, mwaka 1994 Cyprien Ntaryamira wa Burundi na Juvenal Habyarimana wa Rwanda , waliuawa katika ajali ya ndege, ukawa mwanzo wa siku 100 za mauaji ya kimbari Rwanda . Aprili, ni mwezi wa majonzi kwa wapenda haki duniani.
 Miaka 27 ni mingi, waliokuwa watoto hawamjui Sokoine,  ‘bunduki kali’ dhidi ya wazembe, wezi wa mali ya umma, wahujumu uchumi na walarushwa.
Bunduki kubwa(Big Gun) iliyoharibika baada ya kugongwa na Land Cruiser.
 Sokoine alikuwa akisafiria, Mercedes Benz -Saloon,  iliyokuwa ikipeperusha Bendera ya Taifa, alipogongwa na kuuawa.
    Aliwasha mwanga wa kijani kwa masikini, kupita na kuendea maisha afadhali, wakati huo nchi ikitoka vitani kupambana na Nduli Idi Amin Dada wa Uganda, aliyekuwa akifadhaliwa na akina Muammar Gaddafi, wakati alipoivamia nchi yetu.
   Bahati mbaya, mwanga wa macho ya masikini ulitoweka Dakawa, Morogoro, mafisadi na majahili wanaosemwa leo wakaanza kutamba! Paka akitoka, panya hujitawala. Laiti angekuwepo…mafuriko ya ufisadi yangepita mbali.
    Enzi za uhai wake alisema,
 “Viongozi wazembe, wabadhirifu wahesabu siku zao…labda tusiwajue. Hawa, hatuna sababu ya kuwapa imani kuwa tutawalinda katika vitendo vyao viovu”. Ilikuwa Machi 26 mwaka 1983, katika Semina ya Viongozi wa Serikali na Mashirika ya umma.
 Leo, semina za hawa ni za kugawana posho; hazina maonyo makali.
    “Ole wake kiongozi mzembe na asiye nidhamu nitakayemkuta! Kiongozi wa siasa hana usalama wa aina yoyote…usalama wake ni kudra ya Mwenyezi Mungu na wananchi peke yake!”Alisisitiza hayati Sokoine. 
Huyu ndiye kipenzi cha watu. Kauli za ‘ole’ namna hii ziko wapi leo? Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, viatu vya mtu huyu vitamwenea?
   Tangu Sokoine afe, tumeona ulegevu wa hali ya juu, mafisadi wamezidi kutamba. 
Bunge, ingawa la vyama vingi, limekosa meno, yakaota ya plastiki; likageuka watia mhuri tu(rubber-stamp) wa watawala; maslahi ya wengi yamepotezwa.
   Mtu huyu, Saokoine, maisha yake yalikuwa kielelezo cha maisha safi ya utumishi wa umma; sumu kali dhidi ya mafisadi, walanguzi, wazembe, wala rushwa, majambazi wa kila rangi, enzi hizo za ulanguzi wa mali ya umma…hata leo walanguzi wapo wametamalaki. Nchi ni dampo la magendo, bidhaa na pesa bandia. Ah…tunamlilia Sokoine.
    Tumeamua kuandika katika mraba huu, kuwakumbusha wanaojilazimisha kumsahau Sokoine, watoto na vijana waliokuwa hawajazaliwa, wasiomjua vizuri na wenye  ‘akili zenye matege’ -kwamba uadilifu wake ni karipio tosha kwa viongozi wa kizazi hiki.
   Tumevunja viambaza vya woga, kusema Sokoine alikuwa bunduki kubwa(Big Gun),kali, dhidi ya mafisadi, wazembe, walanguzi wa mali ya umma, wadokozi, wala rushwa na mafisadi wa kila mbari, kila rangi na kila daraja.
   Enzi zile za ‘Big- Gun’ Sokoine, aliwakemea walanguzi akiwa Dar es salaam , wakarejesha mali walizopora…walizitupa baharini, barabarani, kichakani ama mtoni! Hata vijijini, mali za umma zilitupwa vichakani, mali za magendo zilitapikwa na wahujumu uchumi; wahusika wakichelea kukutwa na ‘Ole’ ya Sokoine!
    Walisoma maandishi ukutani, yaliyoandikwa na mtu huyu shujaa, “Mene Mene Tekeli na Peresi!” kuashiria milki ya mafisadi kutoweka ili amani itawale. Hakukuwa na kuwakingia wezi kifua, hata kama walivaa kijani!
    Tanzania inamhitaji leo kiongozi kama huyu, kuliko wakati wowote. Ili , azime jeuri ya mafisadi waliotamalaki, wengine hawajui na hawajui kuwa hawajui wanahujumu uchumi wa  nchi. Nao wanaimba, ‘mafisadii!” 
Na laiti wangekutwa na Sokoine!
    Hawajui, tena hawajui kuwa hawajui kwamba uongozi ni dhamana ya wananchi. Wao, wanajua fedha zao ndizo zinazowaweka madarakani, zinazowapa vyeo n.k Hawa, wanaoficha mabilioni katika mabenki ya visiwa vya Uingereza!
   Mtu huyu, Edward Moringe Sokoine, ‘alipiga ngoma’, akiwa Dar es salaam , ikatetemesha nchi yote- hata mafisadi wakaicheza! Vumbi likatua, na tufani za kisiasa(political storm) zikapisha njia. 
Tunamtaka mtu huyu ainuke kutoka majivu(rise from ashes) aje kurejesha tumaini lililopotea.
  Sokoine alizaliwa mwaka 1938 katika wilaya ya Monduli, Arusha. Baaada ya kumaliza masomo yake katika shule ya Sekondari ya Old Moshi(Kilimanjaro) aliajiriwa kama ofisa Utawala wa Halmashauri ya wilaya ya Maasai. Alifanya kazi hadi 1965. Alichaguliwa mbunge wa Monduli, 1965 hadi alipofariki dunia.
   Kuanzia 1967 alipanda vyeo serikalini; tangu Naibu Waziri hadi Waziri Mkuu. Aliwahi kuwa  Naibu Waziri wa Mawasiliano na Ujenzi, Naibu Waziri wa Kazi na Ustawi wa Jamii.
 Alikuwa Waziri  wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa mwaka 1972. Alikuwa Waziri Mkuu mwaka 1977, akibadilishana na Rashid Mfaume Kawawa.
   Alijiuzulu uwaziri Mkuu mwaka1980,kwa sababu ya afya mbaya; akampisha Cleopa David Msuya. Kipindi hiki alikwenda Bulgaria kusoma. Alirejeshewa wadhifa wa Uwaziri Mkuu mwaka 1983, wadhifa alioshikilia kwa ukamilifu hadi mauti yalipomkumba.Hii ndiyo ‘bunduki kali’ dhidi ya mafisadi, iliyoharibika Dakawa Morogoro, haijapata kipuri.
  Tangazo la vita kali dhidi ya mafisadi-wahujumu uchumi-alilitoa Feburuali 27 mwaka 1984. 
Alikuwa adui mkubwa wa hawa mafisadi na wala rushwa, wafanya magendo ambao leo wanajidai wafadhili wa chama,  naam waleta bidhaa bandia wanaojitia kukifadhili chama.Waendesha biashara haramu, wanaojipenyeza kila mahali ili kulinda biashara zao.
 Laiti Sokoine angekuwepo leo…hawa wangejitosa mto Pangani, Ruvuma , Ruvu, Mara, Kagera na Maragarasi, kwa pamoja!
   Alipofoka akiwa Dar es salaam wakatupa magunia ya fedha walizoiba. Walitupa mafriji, ma-TV, baharini, Musoma walitupa magunia ya ushirika vichakani…walichelea kukutwa na mtu huyu, kiboko ya mafisadi… naam, ‘Big-Gun’ Moringe Sokoine!
 Hata vibaka na machangudoa ‘waliicheza ngoma’ ya Sokoine kwa kicho.Alipo ‘kohoa’ nchi ikatetema, wala rushwa wakaogopa…wakatetemeka hadi kutabawali. Tunamlilia Sokoine, ‘kiboko’ ya mafisadi!
   Enzi hizo zimepita. Wajanja wamesoma na kupata ‘digrii’ nyingi za maarifa na ujuzi wa sheria. Na ndio wenye nyadhifa kubwa,lakini waporaji.
   Tunadhani, Rais Jakaya Kikwete hataweza kuwasweka kizuizini hawa wajanja-pasipo sheria. 
Hata mafisadi wa Richmond na EPA, hawatakabiliwa kwa staili ya Sokoine-ya kuwasweka kizuizini, pasipo ushahidi.Si unakumbuka walikimbilia mahakamani serikali ikawalipa fidia ya mabilioni?
   Kuna sheria nyingi,  uhuru wa mahakama na ule wa watuhumiwa. Shime ,sheria ichukue mkondo wake kwa haki, ili kuwaondoa hawa wezi, walanguzi, wahujumu na majahili waitwao mafisadi.Hatutarajii kukurupuka, maana maarifa yameongezeka sasa kuliko wakati ule.
 Wakati  fulani, Augostino Lyatonga Mrema, viatu vya Sokoine vilikaribia kumwenea; naye akatoweka na kuchechema, kama si kufa kifo cha mende-mafisadi wakazidi kutamba! Nani kama Sokoine sasa?
   Tuna simanzi, Edward Ngoyai Lowassa, kashindwa kuvaa viatu vya Edward Moringe Sokoine. Kila mtu atahukumiwa na historia.
  Pengine, tunataraji, Jakaya Kikwete(J.K) anaweza kuvaa viatu vya Julius Kambarage(J.K) Nyerere, sasa vikamwenea, na wafanyabiashara waliokimbilia siasa, ili kutafuta vyeo,wakati ni mafisadi na wahujumu uchumi, watazimwa. Viatu vya JK Nyerere vitamwenea JK Mrisho, au vitampwaya? 
Twangoja kusoma historia.
  0754\0786-324 074,
 congesdaima@yahoo.com