Monday, April 11, 2011

Mbwa hubwekea vivuli vya mafisadi,ama hubwekea kioo?


   Na conges mramba, Mwanza
 
MBWA, ni mnyama pekee  miongoni mwa wanyama wengine Ulimwenguni,anayeitwa rafiki wa kweli wa Binadamu.
   Siku zote hubaki mwaminifu hata mauti yanapomkumba, kutetea maslahi ya Bwanawake!
     Mbwa hajali umasikini au utajiri wa bwana wake!
 Tena, kuna hadithi nyingi za mbwa waliojitoa kafara maisha yao, ili kuwaokoa watu katika majanga ya theluji, mvua, wanyama wakali, vita, mafuriko na mengine mengi.
   Wakati mji wa Pompeii-wa jamii ya Rumi ya zamani, ulipoharibiwa na Volkano ya Mlima Vesuvio mwala 79 AD (Baada ya Kristo) na kufunikwa kabisa na majivu ya Volkano,mbwa alikutwa katika kifusi cha majivu akiwa amemlalia mtoto mchanga, kama jaribio la kumwokoa!
    Naam. Mbwa ni viumbe waaminifu mno wanaojitoa mhanga kutetea mafanikio ya bwana zao! Katika jamii nyingi mbwa hutumiwa kuwinda wanyama wa mwituni kwa ajili ya kitoweo.
    Katika jamii za Kiluo, mbwa hutumiwa kuwinda sungura, wao huita Apwoyo! Lakini mbwa anapokamata Apwoyo, bwana wake hula minofu yote, na kumwachia kwato, vichwa, ( mapanki) na matumbo, ambayo ni nadra kuliwa na mtu .
    Maeneo mengi ya nchi, mbali na mnyama huyu kujitwika dhima ya kuilinda familia na utajiri wake wote usiku kucha, bila mshahara, huishiwa kupewa makombo; tena  mwishoni,baada ya binadamu kuwa wamemaliza kula minofu.
  Pengine mbwa ,hulazimika kula makombo chini ya meza za waungwana. Hula mifupa hata kama alichinjwa ng’ombe au mbuzi kutoka boma la bwana wake; alilokuwa akilinda usiku na mchana, baridi, masika au jua kali…hakika ni laana kuzaliwa mbwa.
   Mahali pengine, ambapo mbwa hulinda mifugo isivamiwe na wanyama wakali, au kuporwa ma wezi, huishia kunyweshwa maji, tena machafu waliyonawa, badala ya maziwa. Pia hupewa mifupa badala ya minofu, au maini. Nyama nzuri huliwa na Bwana, bila kukumbuka fadhila za mbwa.
  Hakuna anayekubali kula meza moja na mbwa; achia mbali sahani moja!
  Wala hakuna anayekubali kunywea maji katika bakuli la mbwa…si ni mbwa? Nyakati za baridi, au masika mbwa huachwa kunyeshewa nje. Hulia kwa huruma mlangoni…wala hakuna anayemjali.
      Na wengine hudiriki kuwatukana wenzao, “mbwa wewe!” 
Je, mbwa hana thamani kweli? Lakini bado mbwa ni waaminifu kwa bwana wao.Bwana anapompongeza japo kinafiki; mbwa hufurahi na kurukaruka kwa furaha akizungusha mkia wake! Lakini anapopigwa na bwana wake, huondoka kwa aibu, mkia ukiwa chini ya miguu yake.
   Hawajaliwi, lakini ni waaminifu. 
Wanapobweka kuashiria hatari katika kijiji au mji, jambo baya likitokea, hulaumiwa wao kwa kukosa uzalendo; ama uzembe!
   Wengine hudiriki kusema kuwa mbwa walipewa ‘rushwa’ ya mifupa na wezi au wanyang’anyi, kabla ya kutekeleza uhalifu. Ugitokea ugonjwa, (kama kichaa cha mbwa), wengi hupigwa risasi, badala ya kupelekwa kliniki, au hospitali za mbwa! Huu ni uonevu, uchoyo, kutomthamini mbwa na kutokuwa na shukrani. Mbwa atapewaje hukunu ya kifo ( hukumu ya kihaini) badala ya kumpa kinga au tiba? dhuluma na kukosa fadhila!
  Ikitokea mbwa akachinja kifaranga ili kujinusuru kwa njaa, baada ya kusahauliwa, laana zitakazotolewa, hata Mungu atasikia! 
Wakati mwingine watoto wa Mama mbwa hutupwa na kukataliwa nyumbani. Hapa Mama mbwa hukubali kuwapoteza watoto wake, ili asipoteze uraia na uzalendo wake! Kweli mbwa ni mzalendo, amini usiamini.
 Waandishi wa habari (wana taaluma wa kweli) ni mbwa walinzi wa jamii, waliojitwika dhima ( Watch dog role) ya kuilinda jamii dhidi ya majanga. Wanabwekea hata mienendo yenye mashaka; wakati mwingine hujitoa mhanga kuokoa jamii katika maangamizi.
   Mara kadhaa, huitwa waongo, wazushi, mbumbumbu, wavivu wa kufikiri,na kila jina baya! Mara ngapi wameachwa nje munyeshewa mvua, wakati vigogo wakifakamia minofu ndani ya nyumba zenye viyoyozi?
 Mara ngapi wameambulia mchuzi, au makombo na mapanki, katika ziara za viongozi, semina, warsha au hata katika maisha yao mitaani!
   Jambo baya likiikumba nchi, kama hili la Jinamizi la Dwarwin…waandishi ndio wa kwanza kulaumiwa!
   “Oh, hawana uzalendo! Mbumbumbu!”
 Na kila kinyume cha fadhila kama afanywavyo mbwa, pusi, paka, nyau mkomba mboga!
     Waandishi hawa wa Tanzania walionya mapema juu ya hatari ya wananchi kula mapanki, na minofu ya samaki kuliwa Ulaya! 
Waliitwa wazushi, wajinga na wambea, wakafyata mkia!
 Walionya juu ya wawekezaji kuwadhulumu wazalendo katika viwanda vyao…kama kawaida waliitwa wazushi, waongo na wajinga. 
Walifikishwa katika mabaraza na kutaka kutozwa faini ya mamilioni.Wakasemwa,ni mbwa wabwekeao kioo?
    Walionya juu ya madege kubeba silaha na kutaka kuitia nchi yetu katika lawama kwamba inahujumu jirani zake; walipuuzwa kama kawaida. Waandishi walilaani ujio wa wageni kama Sauper, ambao hawakuwa tofauti sana na Majasusi wa CIA,MOSSAD,BOSS n.k waliokuwa wakitumwa kutuhujumu enzi ya Vita baridi…walipuuzwa!
   Waandishi walifichua njama za watanzania wenzetu kutumiwa kuhujumu nchi yetu, walikufa katika mazingira ya kutatanisha; wengine walitishiwa kufukuzwa nyumbani, wakanyeshewe mvua huko! Walitukanwa wezi, waongo, njaa tupu, wala makombo, na kila jina dhalili duniani.
 
   Leo Darwin’s Nightmare imetengenezwa na hao wanaotetemekewa, ikadaiwa kuhujumu maslahi ya taifa. Hatushangai waandishi (mbwa) kuanza kurushiwa maneno ya kashfa kuwa njaa zao ndizo zilisababisha Tanzania kutukanwa katika macho ya Ulimwengu.
   Wengine wanataka eti mwandishi mmoja aliyeonekana katika filanu hiyo akitoa mawazo yake, akamatwe na kufungwa jela! Ni aibu ya kutisha! Je, kubwekea majahili ni dhambi?
    Kwamba serikali zetu ziwe macho na watu wanaokuja na silaha ili kutaka kuziuza katika nchi za migogoro, wakati wanapotua kuchukua rasilimali zetu, tena kwa bei chee! Kitendo cha kushusha silaha mahali popote, katika nchi yoyote yenye vita na kisha kwenda kupakia samaki katika nchi jirani, hakijitengi na ukweli kwamba majahili huleta silaha za maangamizi Afrika, kabla ya kuhamisha rasilimali zetu kupeleka kwao!
   Mbwa anapoanza kubwakea vivuli vya majahili  hao, mwasesema, waongo, tamaa, wazandiki n.k. Mbwa, walibwekea samaki kwisha Ziwa Victoria,leo miaka sita baadaye Rais kachukua hatua za kufunga uvuvi Ziwani kwa miezi mitatu. Samaki wanakwisha Ziwa Victoria!
      Mbona hatuwasemi waliotia saini mikataba ya kuipora nchi? 
Naam, wao si mbwa; ni binadamu…laana ni stahili ya mbwa-Watch dog!!
   Mbwa, huhatarisha maisha yake kuwaokoa watu katika baridi. Mbwa hawa (waandishi) walipohisi hatari ya wenye viwanda vya samaki kushirikiana na wazungu kuwanyonya wananchi ili wabaki vibarua milele, walibweka sana , walipoona wanapuuzwa wakanyamaza, ndiyo Jinamizi la Darwin likatokea, ambalo tuna sema baadhi wamehongwa vijisenti, ili kuganga njaa yao!
     Lakini mbwa wako utampaje mapanki wakati unapokula minofu ya ng’ombe au nguruwe aliyekuwa akimlinda wakati wewe ukikoroma?
     Utampaje utumbo wa Apwoyo, wakati yeye ndiye aliyewinda, akamtia mbaroni, kisha kwa uzalendo wake, akakuletea! Mara ngapi waandishi wameokoa mali za mamilioni, kama siyo mabilioni, yaliyokuwa mbioni kuporwa na vigogo?
      Mara ngapi wamesema serikali inaibiwa mapato, kodi au rasilimali? Mara ngapi serikali imetoa tamko la kuwapuuza? Wako vigogo waliotaka serikali itoe tamko kali la kudhibiti uhuru wa habari, kwa sababu tu ya filamu ya mapanki! Uhuru wa habari siyo sababu ya mapanki; chanzo ni uzembe wa vyombo vyetu vya usalama.Tuambizane ukweli.
    Mbwa anapotumwa kupeleka nabari au barua mbaya, hugeuka kuwa msaliti? Mbwa, hata awe mdogo, kama Chihuahua   ni mbwa mwenye faida kwa bwana wake.
     Kwa nini kusema, “Hawana elimu, ni mbumbumbu, uchwara na kila kashfa! Kama mabwana ni wenye elimu, kwanini kulala usingizi na kumwacha mbwa mwenye njaa kulinda mali yako ya thamani:Gari lako, mke wako, watoto, fedha na vito vya thamani?
   Umefika wakati mbwa kuabudiwa kama miungu; ili kupambana na maadui wa ndani na nje bila kuwaonea haya. Waruhusiwe kufanya tafiti mbalimbali na kusema ukweli mtupu juu ya wizi, ufisadi na watengeneze Documentary zitakazoifanya serikali kuchukua hatua kabla ya akina Hubert Sauper, kuja kupotosha (Je, kupotosha?) jamii ya Ulimwengu juu ya Tanzania!
   Wapo waheshimiwa wanaowabeza Chihuahua.
 Wanasema ni wadogo kwa umbo, hawawezi kukabiliana na tembo! Wanataka waagizwe mbwa wakubwa toka Brazil,au wapewe mafunzo maalum katika jeshi la Marekani! Mbwa ni mbwa, bora uzalendo wake na mapenzi kwa nyumba ya bwana wake!
      Kila mbwa huridhika anaposifiwa tu. Lakini hufyata mkia na kuondoka kwa aibu anaposhushuliwa. Waandishi wameshushuliwa mara ngapi, tena  hata bungeni?
  Kwa sababu ya karama yao ya kunusa habari, waandishi wamekuwa wakinusa jinsi watu wetu wanavyonyanyaswa na wawekezaji. Wanapobweka, hutukanwa na hata Bwana mwenye kaya! 
Kumbe wafanyeje, badala ya kuufyata?
    Kuna Darwin’s Nightmare nyingi…dhahabu kutoroshwa, almasi, tanzanite, magogo, sangara na hata biashara ya madawa ya kulevya!
    Mbwa hutumiwa kunasa vyote hivi, kisha bwana wake akiona hunyaka, hula na kushiba kisha hukoroma na kumwacha mbwa kubaki na njaa yake katika lindo, iwe masika, baridi au kiangazi kikali! Ni laana kuzaliwa mbwa!
   Wakati mwingine mbwa hutumiwa kurejesha wafungwa waliotoroka magerezani.Hutumika kama macho ya wasio na macho (vipofu), huwapa sauti wasio na sauti, huongoza njia kwa mabwana wakubwa vipofu, japo kwa ubishi-ubishi, katika vikwazo au mabaa.
    Janga la Darwin’s Nightmare liwe somo kwa Bwana wetu  (serikali ) kuwapa heshima na chakula mbwa (waandishi wa habari) tangu sasa, ili wafanye kazi zao kizalendo. Ni wajibu wa mwenye mbwa kumpa chakula mbwa wake, ili kumnusuru kula sumu kutoka kwa majambazi, au kutupiwa mfupa, na kusahau jukumu lake, kama inavyodaiwa.
    Kama hatujasahau, kumekuwa na Jinamizi la kuamini kuwa mbwa hao wa nje ni bora kuliko wa ndani.
      Naam, watu wamewahi kukiri kuwa wanajisikia vizuri kuhojiwa na kina Tim Sebastian, Larry King na wengineo wa Ulaya na Marekani kuliko wa Tanzania!
Sababu kubwa ya hawa kusifiwa, ni kwa kuwa huunga mkono sera za uwekezaji, ambazo hapa hubwekewa kwa nguvu kwamba zinawashibisha wazungu wa Ulaya, wakati wenyeji wakishindia mapanki!
   Sasa kumbe, hata hao wa Ulaya ni waandishi uchwara, wanaopakazia uongo? Kumbe mwandishi uchwara ni yule asiye mzalendo; na wala si vinginevyo. Akina Sauper, bila shaka wana elimu nzuri, lakini filamu nzima  eti haionyeshi hata chembe ya maadili. Haionyeshi hata chembe ya upeo na elimu, kulingana na waheshimiwa Wabunge!
   Kama ingetengenezwa na waandishi wa hapa, sijui waheshimiwa Wabunge wangesemaje? Uchwara, mbumbumbu, njaa, kukosa uzalendo, uduni wa taaluma, uandishi pasipo elimu,mbwa koko (si mbwa?) na kejeli nyingi!
   Mwisho, katika hadithi zote hata za kale, hakuna mahali mbwa wamekosa uzalendo, katika kutetea maslahi hata yasiyo yake! Mbwa siku zote hubwekea wezi, majahili, majambazi, wawekezaji wenye hila, wageni na kila mwenendo wa mashaka.
    Wawe na njaa au wawe wameshiba, kusudi lao ni moja tu, kufichua uoza. Mbwa hata hapa wameokoa maisha ya wanadamu, kuliko wanadamu wanavyookoa maisha yao.
    Wanaowalaumu mbwa kuwa waliwakaribisha majasusi ( labda kama Sauper), wafikiri vizuri.
      Tena hakuna mbwa uchwara katika hili…Ni vema serikali imetoa tamko juu ya mapanki, lakini waandishi kama mbwa wamefanya kazi yao nadhifu, serikali ikazembea. Majahili walipotambulishwa kwa mbwa na mwenye mbwa- mbwa alipowaona rafiki wa familia, lawama zimerudi kwa mbwa kama kawaida!
     Nawahurumia mbwa, lakini wasichoke kubweka hata kama mwenzao mmoja atauawa katika hili!
    Ni kawaida kubweka kwa ajili ya maslahi ya bwana wake, hata kama mbwa atashindia mapanki! Shime mbwa, wabwekeeni hata mabwana wetu wanaotorosha magogo, almasi, tanzanite,dhahabu na sangara usiku na kuwaachia watoto mapanki, kwa madai kuwa hayajaoza!
  Mwandishi wa makala hii hupatikana kwa simu 0754 324 074 au email: congesdaima@yahoo.com

No comments:

Post a Comment