Friday, April 8, 2011

Safari ya miaka 50 ya Afrika kutoka Uhuru kurejea Utumwani


    KATIKA mwaka wa A.D. Mosi, dunia ilikuwa na wakazi milioni 200 tu.Katika mwaka wa A.D 1650, dunia ilikuwa na wakazi milioni 500.
  Miaka 200 baadaye dunia ilifikisha wakazi Bilioni moja, na siku hizi duniani kuna wakazi takriban bilioni saba, wasio na chakula cha kuwatosha, hawana nishati muhimu kama mafuta ya kuendesha mitambo yao na kuwashia taa zao vijijini.
  Kuwalisha watu hawa na kuwapa mahitaji ya lazima ni vigumu. Ndiyo maana,kila dola duniani lazima lina haha kutafuta rasilimali muhimu,ili kunusuru watu wake wasife njaa.
Marekani imefika mwezini ili kutafuta nishati na kuangalia uwezekano wa raia wake kupata ukimbizi huko mambo yanapozidi kuwa mabaya.

Zamani,kulikuwa na vita vya kila dola kujitanua.Siku hizi, duniani kuna vita vya rasilimali;kugombea rasilimali muhimu sana kama mafuta, maji,madini,ardhi yenye rasilimali nyingi,mitaji, mito mikubwa,maziwa,bahari n.k
 Naam, twaishi katika zama za mataifa ya dunia kugombea rasilimali mchache zilizobaki.Rasilimali muhimu sana katika uchumi wa dunia ni pamoja na mafuta.
 Nchi zinazozalisha sana mafuta duniani, Organization of Petroleum Exporting Countries(OPEC) ni Algeria, Indonesia, Iran ,Irak ,Kuwait,Libya, Nigeria, Qatar, Saudi Arabia,Umoja wa Falme za Kiarabu(UAE) na Venezuela.
 Urusi,Canada,Mexico na Norway zinazalisha sana mafuta,lakini hazimo kwenye Umoja huu wa OPEC.
Marekani ni ya tatu kwa kuzalisha sana mafuta duniani,nyuma ya Saudi Arabia na Urusi.
 Hata hivyo, mafuta hayawatoshi kabisa, na hawayauzi nje. Marekani pekee hutumia zaidi ya mara 20 ya mafuta yanayotumiwa dunia nzima.
 Nchi nyingine zote zenye viwanda hutumia mafuta mengi mara 10 zaidi ya nchi nyingine duniani.
  Nataka msomaji ujue kwamba, ingawa Marekani huzalisha mafuta kwa wingi,ni mtumiaji wa mafuta maradufu,kuliko nchi yoyote duniani. Marekani huongoza kwa uagizaji wa mafuta.
Mameli yake makubwa,kila siku huingiza nchini humo mafuta yanayotumika kila siku.
Matokeo yake, sera za  Marekani za mafuta duniani ni ubabe,wizi,utapeli,ukoloni, ubeberu dhidi ya nchi zenye mafuta.
 Makampuni mengi makubwa ya Marekani yanayochimba na kusafisha mafuta duniani:Exxon, Mobil,Chevron,Texaco,Conoco,Phillips n.k yanaongoza kwa mikataba ya wizi na utapeli na mikataba yenye dhuluma duniani.
 Nchi nyingine zenye makampuni makubwa ya kuchimba na kuchakata mafuta ni pamoja na Uingereza,( British Petroleum au BP), Uholanzi na United Kingdom wanamiliki kampuni kubwa la Royal/Dutch Shell, Ufaransa na Ubelgiji wanamiliki kampuni la Total,na Urusi ina makampuni kama Lukoil,Yukos na Sibneft.
 Misri, alikopinduliwa punde Rais Hosni Mubarak,ina rasilimali tele ya mafuta,gesi,phosphate, matunda n.k
Mwaka 2000 Misri ilikuwa na akiba ya mafuta kama mapipa bilioni 2.9 hivi, nchi hii ina ushawishi mkubwa kwa nchi za Kiarabu zenye hazina kubwa ya mafuta  kama ulivyokwishaona hapo juu.
 Ni nchi yenye mfereji wa Suez wenye urefu wa maili 103 unaoziunganisha Bahari za Shamu(Red Sea)na Mediterranean.
Ulijengwa(ulichimbwa) kwa ushirika na Ufaransa na Uingereza mwaka 1859-69 kukatokea vita vya kuumiliki mfereji huo,kwa sababu yanapita mameli makubwa.Julai 28 mwaka 1956 serikali ya Misri ikautaifisha.Lazima Marekani iukodolee mimacho mfereji wa Suez.
 Tunakusudia kuona jinsi nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zinavyochochea maasi katika nchi zenye rasilimali nyingi na muhimu sana kama mafuta, gesi,madini muhimu kama Uranium,almasi,dhahabu, bahari,maziwa makubwa n.k
Je, msomaji, unaona uhusiano gain kati ya Marekani na washirika wake dhidi ya nchi zenye mafuta mengi kama Algeria, Iran,Irak, Kuwait.Libya,Venezuela na Misri?
 Hapa Afrika,umeona uhusiano hasi kati ya Marekani na Misri, Algeria,Libya, Guinea ya Ikweta,Angola  n.k hapa Barani Afrika?
 Nitashuhudia,ubabe uchochezi, maandamano, migomo,migogoro ya kutengenezwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe na uasi.
 Hatujasahau, wakati mtoto wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Margaret Thatcher, aitwaye Sir Mark Thatcher alipotaka kupindua serikali ya Guinea ya Ikweta mwaka 2004.
 Guinea ya Ikweta,ni nchi ya tatu Afrika kwa kuzalisha mafuta kwa wingi. Alitiwa mbaroni mjini Johannesburg,lakini hatujui alifungwa jela ipi?
Tumeona ugomvi mkubwa kati ya Marekani na nchi zinazomgomea kuwa kibaraka wake,kama Iran ya Mahmoud Ahmadnejad(Iran ya Shah ilikuwa kibaraka wa Marekani,wakaiba mafuta kwa wingi hadi watu walipomkataa miaka ya mwisho ya 70,akatimkia Marekani), kuna Irak ya Marehemu Saddam Hussein, Venezuela ya Hugo Chavez na Libya na Kanali Muammar al-Qaddafi.
Ukiyanyima mataifa haya babe duniani wanachotaka, utaanza kusikia kwamba Hosni Mubarak anamiliki utajiri wa Dola za Marekani Bilioni 70(Zaidi kumshinda Carlos Slim, Bill Gates Na Warren Buffet),utasikia baadaye kwamba Rais Yoweri Kaguta Museveni anamiliki utajiri wa Dola za Marekani Bilioni 10,siku wakikosana.
wangali bado wanamtandikia 'Red Carpet' Bush,Blair au Obama, mambo ni shwari!
  Ukiwanyanyima maslahi yao unakuwa adui yao;tena wakimaliza kukutumia kama kondomu,kama Charles Taylor,Fodday Sankoh na Jonas Savimbi,wanakutupa jela au wanakuua!
 Osama bin Laden, alikuwa mtu wao akawaasi, wanamsaka!Siku hizi hawamsemi sana,labda walishakutana, wakayamaliza!
 Rais Mstaafu wa Afrika ya Kusini, Nelson Mandela,aliwahi kusema kwamba Vita vya Ghuba vilikuwa vita vya mafuta.
 Yaani vita na migogoro ya Kuwait na Irak ya Saddam Hussein katika miaka ya 90-vita ya kwanza ya Ghuba na ile ya Pili ya 2003 iliyomsababishia Saddam Hussein kukamatwa,kufungwa jela na kunyongwa Alfajiri ya Jumamosi, Desemba 30 mwaka 2006,huko jengoni Camp Justice, mjini Baghdad,vilikuwa vita vya mafuta!
Marekani,ambao kwao hukumu ya kunyongwa ni haramu, walimnyonga Saddam nyuma ya pazia,kwa makosa ya ubinadamu ama utu, humanism.
 Aliwaasi Marekani pale alipoivamia Kuwait,mwaka 1993 akabambikiwa kesi ya kuua Washia 148 huko Dujail.
 Walimsingizia kumiliki silaha za maangamizi(Mass Destruction Weapons) n.k wakamnyonga kwa kamba nene shingoni, tena mbele ya kamera za televisheni, ili kila watukutu wanaone na kujisalimisha.
 Hivi ndivyo zama za Saddam Hussein zilizoitwa, The Dark Period, zilivyokoma kando ya Mto mkubwa uitwao Frati.
 Biblia, ilishatabiri kuuawa kwa Saddam kama  ‘kukaushwa’ kwa Mto ule mkubwa, Frati(Euphrates) ili kuzifanya nchi za Mashariki mwa ng’ambo ya Mto kuungana na mataifa ya Magharibi(NATO), angalia Ufunuo wa Yohana 16:12
Lazima NATO na soko la pamoja la Ulaya(Common Market) lifike mbali bila kizuizi.
 Marekani, ni wazoefu kuingilia nchi nyingine na kuzipindua ingawa kuna sheria ya kimataifa inayopinga nchi moja kuiingilia nyingine kijeshi., ingawa wanaimba demokrasia na Haki za Binadamu!
   Walimpindua Rais Mjamaa wa Chile, Salvador Allende, wakamweka kibaraka wao,Jose Ramon Pinochet Urgate.
 Desemba 1989 George Herbert Walker Bush(Bush Baba) alituma jeshi Panama City,likampindua Jen. Manuel Noriega na kumfunga pingu kama alivyofungwa Saddam zama za mwanaye, George W.Bush.
 Makampuni ya Marekani,Uholanzi,Uingereza n.k ya mafuta,yamechochea vita na mauaji mahali pengi,yametumikisha watu huko Burma ama Myanmar sasa, ukiwapinga Marekani unakamatwa na kufungwa jela,labda uwe kibaraka wao.
 Na viongozi wetu wengi ni vibaraka wa Marekani, wanaogopa kukamatwa au kupinduliwa! Si unasikia kwamba hata maandamano ya kupinga serikali wanachochea wao?
 Nigeria, Ken Saro-Wiwa, aliuliwa na Jen. Sani Abacha Novemba 10 mwaka 1995 kwa sababu alilipinga sana kampuni la mafuta la Royal/Dutch Shell la Uingereza na Uholanzi.
 Marekani wanajidai kuimba demokrasia na haki za binadamu,lakini ukiwapinga wanakuua wakiwa nyuma ya pazia!
 Nataka nikwambie msomaji. Orodha ya watu waliouliwa na Marekani na washirika wao na Mashirika ya Ujasusi kama CIA,MI6 na MI5,Mossad , BOSS la Makaburu,na mengine ni kubwa sana.
 Sasa, kaangalie huko Mahakama ya Uhalifu wa Kivita(ICC)The Hague,Uholanzi, wanashitakiwa akina nani?
  Orodha ya washitakiwa,kama wale wa Luis Moreno Ocampo maarufu kama “Ocampo Six” wamo Wakenya tu na Waafrika,na Wazungu adui zao kama wafuasi wa Adolf Hitler na Dikteta Slobodan Milosevic wa Serbia!
 Bush na Tony Blair hawamo,kuna Fodday Sankoh, Charles Taylor na ‘Ocampo Six’ kwa sababu hawana maslahi ya Marekani na washirika wao.
 Kanali Muammar al-Qaddafi wa Libya, siku hizi anasakwa kama nguruwe-pori,huko Benghazi na Tripoli,kisa…Marekani na washirika wake wanasema anahatarisha ubinadamu!
 Hii ni mara nyingine, Muammar Qaddafi anaposakwa. Aprili 14 mwaka 1986 mvua ya masika ya mabomu ya madege ya Kimarekani,ilinyesha Tripoli na Benghazi, wakashambulia kasri la Qaddafi, hakuwemo wakaua wanaye wa kambo.
 Qaddafi, alikuwa adui yao tangu mwaka 1988,magaidi wake wakiwemo maofisa usalama wake walipoilipua ndege ya Pan American Airways, Flight 103 huko Lockerbie, Scotland.
 Akina Abdel Basset Ali Al-Meghri wakahukumiwa kifo,baadaye wakaachwa huru lakini Qaddafi bado anatafutwa ili afuate nyazo za ‘waasi’ wenzake kama Noriega,Saddam,Hosni Mubarak, Ben Ali, Samora Moises Machel,Murtala Mohamed, Patrice Emery Lumumba-ya watu wa kufa, ni ndefu.
Akiwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika(AU),Qaddafi alitaka Afrika iwe nchi moja(Pan Afrcanism) ili kupinga ubeberu wa Magharibi.
 Visingizio vya kutaka kumumaliza ni vingi tu. Anataka kumrithisha mwanaye urais wa Libya.
 Marekani ilianza kuliona hilo lini, wakati Qaddafi aliingia madarakani zamani mwaka 1969.
 Je, ni yeye tu   anayetaka kumrithisha mwanaye urais? Vipi akina Omar Bongo?
Namna gani  Lurent Kabila? Nani alimuua Kabila? Nani alimweka Joseph Kabila?
Ati Hosni Mubara alitaka kumrithisha mwanaye, Gamal!
 Mbona inasemwa Museveni anataka kumsimika mwanaye,Muhozi,huko Uganda? Kuna wengi,lakini Marekani inawatazama kwa makengeza.
  Qaddafi, alitaka kuwapinga mabeberu wasisombe rasilimali za Afrika,kama ingeundwa AU kuwa nchi moja nay eye akawa Rais.
Alihatarisha mipango ya mabeberu ya kusomba rasilimali za Afrika,kama mafuta,dhahabu,gesi,almasi,pembe za ndovu,uranium, samaki kama sangara n.k
 Marais wenzake wakiona hivi,roho inauma, AU wanakurupuka usingizini huko mjini Addis Ababa, wanatoa tamko, wanalaani mashambulizi dhidi ya Muammar al-Qaddafi,lakini Too Late!
  Safari ya Bara la Afrika kutoka Uhuru uliopatikana miaka ya 60 kurejea utumwani,ilishaanza zamani.
SAFARI ya Bara la Afrika kutoka Uhuru kurejea Utumwani,ilianza kushika kasi mara baada ya viongozi waliopigania uhuru kuondoka.
 Ahmed Sokou Toure,Kwame Nkrumah, Gamal Abdel Nasser,Julis Nyerere, Patrice Emery Lumumba,n.k walioondoka madarakani wengine kwa hujuma za mabeberu,Afrika ikarudi kule ilikotoka.
Fikra huru za kuendeleza Afrika kwa maliasili zake nyingi zilihafifsishwa, ama na        Madola makubwa kwa njia za vikwazo,au fikra hizi pevu ziliyeyushwa na kutiwa kiza hadi tukakubaliana na utumwa na kuwategea wakoloni na mashirika yao waliyoanzisha baada ya Vita Vikuu vya pili vya Dunia, kwamba ndiyo utakaokuwa ufumbuzi wa matatizo ya maendeleo yetu.
 Abdul Rahman Mohamed Babu,katika kitabu kiitwacho, “African Socialism or Socialist Africa?”(Tanzania Publishing House,1981) anasema katika ukurasa wa 35 kwamba, kuwategemea wafadhili hawa kulikuwa kujiingiza kichwa-kichwa katika ukoloni mamboleo, neo-colonialism.
Wapo viongozi wa Afrika waliogoma kunyoosha mikono ya urafiki kwa hawa wakiloni:Agostino Neto, Cabral, do Santos, Samora Machel na wenzao wakadhaniwa ni wajamaa wa Ki-Marx, waliopinga ukoloni na kutaka kueneza siasa hatarishi za kijamaa kwa madola ya Magharibi.
Walihujumiwa, hawapo na mawazo na njozi zao zilishapotezwa na hawa viongozi wa leoambao hawana jipya,sispokuwa kutenda kama mawakala wa ukoloni.
 Afrika, haina tena njozi za kuendelea kwa kutumia maliasili zake au rasilimali zake. Bali, ni kutegemea misaada ya tashtiti(myth of aid) kutoka Ulaya,Marekani kwa upande mmoja, na Japan,Uchina ama Urusi,kwa upande wa pili.
 Tumewekewa akilini kasumba na wakoloni,kwamba, “If no Aid, No Development” sasa, tunadhani misaada yao ni Haki Yetu, kumbe ni utumwa kwetu.
    Nimewahi kuwasikia viongozi wa Tanzania wakijisifu mno kwa ‘kusaidiwa’ sana na kufutiwa misaada, badala ya kujisifu kwa kuwaendeleza wananchi kwa kutumia fursa zetu na rasilimali zetu wenyewe.
 Hawa vigogo wetu, wanaona kiongozi anayesaidiwa sana kupita wenzake, ndiye ‘kipenzi’ cha Mabwana Wakubwa,kumbe ndiyo “Uchangudoa” mamboleo unaowauza       Waafrika, kwa kutumia utajiri na mitaji wakoloni waliyopora kwetu zama za Ukoloni mkongwe.
 Misaada kwa Bara hili ina makusudi mahsusi: Kwa njia za moja kwa moja au kupitia kwingine,misaada na hisani,huwanufaisha zaidi hawa wafadhili na wahisani,wakiloni mamboleo,kuliko sisi.
 Taasisi za Breton Woods,Fuko la Fedha la Kimataifa(IMF)na Benki Kuu ya Dunia(WB) wamegeuka miungu kwa kutuamria kila kitu. Nasi tunafuata bila kupinga,hata kama ni kubinafsisha mashirika yaliojiendesha kwa faida,viwanda vilivyoongeza thamani ya mazao yetu na kutupa ajira, matokeo yake tumefilisika,tunauza mazao ghafi kwa bei chee bila kuyachakata.
 Viwanda vya ngozi vimegeuka maghala, viwanda vya kusindika mazao vimekufa, na vingine kama Bora Shoe Company,vilivyoleta tija kwa Watanzania,vilishakwenda kuzimu.
 Imekuwa sasa, hawa wakoloni kwa kutumia IMF na Benki ya Dunia,wamejivika jukumu letu la kufikiri na kuamua kwa niaba yetu,nasi tumeaachia jukumu hilo la msingi-tumejiuza mithili ya machangudoa katika soko la matajiri. Siku hizi tunaitwa, Nchi za Dunia ya Tatu(Third World Countries) ingawa tuna rasilimali nyingi na muhimu sana, kama tulivyoona katika sehemu ya kwanza ya makala hii.
 Tuna mafuta,gesi,uranium,dhahabu,almasi,maziwa makubwa,mito,Bahari,milima mirefu,wanyamapori na misitu isiyopatikana popote duniani ila hapa Afrika.
 Naam, Wakoloni wanafikiri na kuamua chochote watakacho kwa niaba yetu. Hii ni kusema kwamba,ubongo wetu wa mbele(The Frontal Lobe) umeshindwa kufikiri na kuamua kwa niaba yetu wenyewe, tumewaachia Marekani na Ulaya waamue mustakabali wetu!
 Rasilimali zetu wanachukua bila sisi kujua, wanauza na kutulipa mrabaha kidogo wanapojisikia, au wanatukopesha pesa za kununulia chandarua,na ujenzi wa zahanati, barabara,hospitali n.k huku tukiwashangalia na kuwachezea ngoma!
 Afrika tajiri, watu wake ni masikini, wenye njaa na wanaoingiliwa kisiasa,kiuchumi,kijamii na kijeshi na Ulaya na Mrekani na Asia.
 Mapinduzi,yalishashindwa kwa sababu wanamapinduzi walishatoweka,wenye fikra huru walishanyofolewa ubongo wa mbele-Frontal L obe-sasa tumekabidhi maamuzi na hatima yetu kwa Marekani na washirika wake!
 Nyerere, Patrice Lumumba, wa Congo, Ben Barka wa Morocco, Amilcar Cabral wa Guinea Bissau na wenzao wametoweka,jua limekuchwa.
 Afrika, ime ‘asilishwa’ hadi kubatizwa utoto bandia wa Ulaya na Marekani, wanaita “Africa Europeanized”.
 Kinachoangaliwa siku hizi,ni maslahi ya Ulaya hapa Afica, na siyo maslahi ya waafrika. Hakunavyama kama TANU, FRELIMO, M.P.L.A,UNIP na ANC vyenye kupinga utumwa na ubaguzi wa rangi na matabaka ya watu.
Matokeo yake, Umoja wa Afrika(AU) hauna turufu katika masoko, hauna maamuzi wa kura moja katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, hivyo hauna meno waka kauli hata juu ya yanayotokea hapa Barani.
   Ikitokea vita Somalia na Darfur,mpaka Marekani watutume kulinda amani na wanatulipa posho,utadhani wao walituzaa sisi!
 Marekani ndiyo yenye kusema kwa sababu ya MITAJI YAKE iliyowekeza hapa. Marekani inaweza kusema, “Gaddafi Must Go!” A.U ikiwa kimya! Ikisema ‘ Kikwete Must Go!” hata hakuna wa kupinga.
 Marekani ikiona aibu kwa kauli hizi za ubabe katika macho ya kimataifa, basi inajivua gamba,na kuwaachia washirika wake,hususan Umoja wa Kujihami wa Ulaya Magharibi(NATO), wanatushambulia tunapojidai kichwa ngumu.
   Jumatano iliyopita,(Machi 30 mwaka huu)nilipokuwa nikitazama kipindi kiitwacho, STRAIGHT TALK AFRIKA kinachorushwa na luninga Sauti ya Amerika(VoA) nikapatwa kichefuchefu,na kupiga chafya.
 Niliaona kwamba Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Rodham Clinton, alipokuwa akizungumzia Majuma Sita ya Vita nchiniLibya’ hatimaye alisema, “Gaddafi Must Go!”
 Kwamba, Gaddafi lazima aondoke Libya,utadhani Marekani ndiye mwamuzi na ofisa     habari wa watu wa Libya! Lini Walibya walimpa Clinton ubongo wao wa kufikiri na kutoa maamuzi(Frontal Lobe) ili aamue mustakabali wao kwa niaba yao?
 Kudhihirisha kiburi hiki cha Marekani, Machi 17 mwaka huu, Marekani chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa(UN) wakatoa Amri ya ndege zote za Libya kutoruka katika Anga ya Libya, ”No Fly Zone!”
  Ati, hii ni Amri ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya kiongozi wa Libya,Kanali Mouammar al-Gaddafi, asiendelee kuwashambulia waasi wan chi hiyo kwa madege ya kijeshi,ama kusababisha maafa makubwa.
   Gaddafi, kawaita wanaompinga(Waasi) kwamba ni mende, panya,mijusi,pusi-paka nyau!
 Ndipo sasa, Umoja wa Mataifa umeruhusu NATO kuishambulia Libya,utadhani Libya imetangulia kuzishambulia nchi wanachama wa Umoja wa Kujihami wa Ulaya Kaskazini mwa Bahari ya Atlantic, yaani NATO!
 Tukubaliane kimsingi, kwamba Gaddafi kaka kwenye uongozi tangu mwaka 1969,na kwamba ni Dikteta anayewaita wapinzani,mende,panya n.k
Tuchukulie kuwa kweli kwamba, Gaddafi nawaburuza raia wa Libya na wamemchoka.Sasa, Marekani,Ufaransa na Uingereza,ama NATO wamekujaje katika mgogoro huo?
 Ati, Gaddafi anatishia maisha ya watu na utu? Mbona Umoja wa Mataifa haujachukua hatua madhubuti za kuondoa vita Cote d’ Ivoire? Mbona hata huko kuna vita vinasambaa,na watu wanakufa?
 Mtayarishaji wa kipindi cha Straight Talk Africa,Dk. Shaka Ssali, Jumatano iliyopita alimuuliza swali mgeni wake studioni, Profesa Dk. Abdul Karim Bangura, ambaye ni Profesa  wa Uhusiano wa Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Howard.
 “Kwanini Marekani ichukue hatua Libya,na siyo Cote d’ Ivoire?”
    “ Ni mafuta” Prof. Abdul Karim Bangura alijibu, kwamba sababu ya Marekani kuiingilia kijeshi Libya kabla ya Cote d’ Ivoire ni mafuta ya Libya!
  Mafuta ya Libya,yanawavuta kunguru,tai, mainzi ya kijani na nyang’au wengi ili kuja kula mizoga!
 Ndivyo nilivyosema katika makala iliyotangulia,juma lililopita,kwamba mgogoro mmoja unaachwa ili kuingilia mahali kuliko na ‘uhondo’ wa mafuta.
 Wameacha suala la Laurent Gabagbo, wakaenda Libya,kwa sababu ya tabia yao ya upendeleo na macho yao yana makengengeza,ndiyo wanaita ‘double standards’.
  Suala la Marekani na Washirika wake kuona kwamba Cote d’ Ivoire hakuna taabu, wakakimbilia Benghazi na Tripoli ili kukamata visima vya mafuta, kwa visingizio kwamba Gaddafi ana madege mengi ya kijeshi na vifaru kuliko Gbagbo…ndiyo maana UN wakatuma NATO kushambulia Libya,ni uhuni na usanii ulioje?
 Kwa sababu gain Amri ya “No Fly Zone” ITANGAZWE LIBYA na wala siyo Abidjan ama Yamoussoukro?
  Ati, Libya hakuna demokrasia,hakuna katiba,kwa hiyo ni vita vya kuleta demokrasia na Haki za Binadamu. Vita dhidi ya ugaidi….Gaddafi ni gaidi kuliko akina Laurent Koudou Bagabgo, wanaoshindwa uchaguzi wanagoma kuondoka mamlakani.
 Umoja wa Afrika,mjini Addis Ababa umeshindwa kusema kwa sauti kubwa. Ulikuwa kimya wakati Hosni Mubarak akitimuliwa mjini Cairo. AU hawakusema kitu wakati Zine El Abidine Ben Ali akitimuliwa na wamachinga huko Tunis, Tunisia.
  Sasa, AU inasema polepole ikiwa chini ya makomeo ya milango na nondo za madirisha mjini Addis Ababa,kwamba Gaddafi anaonewa.
 Ni kwa sababu hii, Marekani inaidhihaki AU,kwamba  “Mfalme wa Wafalm” wa Afrika, anapaswa kutimuliwa tangu Libya hadi Afrika yote.
    Kanali Mouammar al-Gaddafi, “King of African Kings” kama wanavyomkebehi, lazima aondoke!
 Hii ni Amri ya Marekani iliyojaa dharau na kiburi dhidi ya Waafrika wa rangi zote(Pan Africanism) ili Mzungu arudi kutawala?
 Gaddafi, “King of Kings” akiwa Mwenyekiti wa AU alitaka  Afrika iwe dola moja kubwa(UNITED STATES OF AFRICA) ili yeye awe rais kwa kwanza awatoe kamasi mabeberu,na kuwanyima rasilimali tete wanazotolea udenda!
  Gaddafi, ‘King of African Kings’ aliwakufuru hawa UNITED STATES OF AMERICA kwa kutaka kuwe na USA nyingine Africa?
 Mimi najiuliza, haya mapinduzi yaliyoanzia Tunisia,Misri, sasa Libya,Yemen na Syria zinawaka moto,yakivuka   Jangwa la Sahara na kufika Kusini, Robert Mugabe atapona kweli?
 Ataendelea kuwanyang’anya walowezi mashamba na kuwagawia Waafrika?
 Hili Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,lenye wajumbe wa kudumu,Marekani, Ufaransa,Uingereza(wanaoongoza kuivamia Libya) pamoja na Uchina na Russia, wakimwondoa Gaddafi,wakapora mafuta watakwenda Cote  d’ Ivoire na kutwaa kakao, kasha watakuja Zanzibar, Uganda,Musumbiji na kwingine kwenya harufu ya mafuta,na kuleta migogoro!
 Ni kwa sababu hii,tunauona ukoloni na utumwa mpya ukirejea Afrika kwa nguvu za kijeshi, huku wakijidai kuleta Haki za Binadamu na demokrasia,kumbe ni ‘Militarization and Human Right Abuses!”.
 Waafrika tuamke.
 0754/0786-324 074



1 comment: