Monday, October 29, 2012

AKINA NANI WALIMUUA BARLOW?



                 

JAMII ya Jijini Mwanza ilisema kuwa  “motive” ya mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi,ACP Liberatus Barlow,ni wivu wa kimapenzi.
Kikosi maalum cha upelelezi(TASK FORCE) kiliundwa ili kupeleleza mauaji haya ya tashtiti.Kilihusisha makachero wa kimataifa,”Interpol”, na miongoni mwao wataalam wa Kompyuta na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano,
Kabla ya majuma mawili kwisha, tangu mauaji ya Barlow, Oktoba 13 mwaka huu,tayari watu zaidi ya 10 walikuwa wamenaswa,wengine kwa mahojiano na wengine ndiyo hasa waliomuua Barlow jijini Mwanza,wakajakutimkia Dar es Salaam.
Dorothy Moses, ama Dorothy Lymo(42) ndiye mwanamama aliyekuwa na Kamanda Barlow(55) dakika chache kabla ya mauaji ya kinyama kumkumba.Alipigwa kwa risasi ya bunduki nzito, Shotgun, “Greener”shingoni,shingo likafumuliwa kabisa.
Felix Felician(50) ama maarufu Jijini kama ‘Pepe’ alitiwa mbaroni kwa tuhuma kuwa ndiye aliyekuwa na uhusiano wa kimapenzi na Dorothy, ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi ya Nyamagana B,Jijini.
Ilihisiwa kuwa, pengine mwanamama huyu mfuauji, alikuwa akigawanya penzi la tashtiti kwa Marehemu Barlow na ‘Pepe’yumkini kiasi cha kuleta wivu na visasi.
Kufuatia tuhuma hizo ambazo polisi wangali wakifanyia kazi kwa umakini, alikamatwa pia Fumo Felician(46),mchezaji wa zamani na ‘striker’ mwenye mashuti makali katika timu ya Pamba ya Jijini Mwanza na Dar es salaam Young Africans. Pepe ni nduguye Fumo.
TASK FORCE ya makachero wa polisi iliongozwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini(DCI)Robert Manumba, iliwakamata pia Bahati Agostino na Waibe Maboto, kwa sababu Barlow alipouawa huko Kitangiri usiku wa kuamkia Oktoba 13, majahili wale walimpora redio ya upepo(Radio Call), na kasha walipora simu ya Dorothy.
Nataka kusema kuwa,bado watu hawajajifunza kwamba sasa kuiba simu ya mtu,hususan katika matukio ya ujambazi na mauaji namna hii ni kujiweka hatarini.
Nataka kuandika hapa kwamba, hisia za watu kwamba kundi hili la majambazi lilikuwa na watu werevu, ni uongo tu. Kama walitoweka na simu ya Dorothy wakaendelea kuitumia hata kama walishanyofoa laini, hawa walikuwa majambazi waliojua kufyatua risasi, na wala hawakujua chochote kuhusu teknolojia ya leo.
Hawa walivyo mazuzu, eti walitupa laini ya Dorothy, wakaendelea kuitumia simu ile wao wenyewe, ama mtu mwingine waliyemuuzia, huku wakijua simu ile ilisajiliwa na hata namba ya simu iitwayo ‘IMEI’ ilisajiliwa?
Kulingana na teknolojia ya siku hizi, ilikuwa rahisi kama nini kwa makachero wa ‘Interpol’ wenye utaalam wa hali ya juu katika ‘Information Technology’ kuiona simu hiyo na kujua mahali ilipokuwa ikiitia hata kama laini ya awali ilishanyofolewa na kutupwa.
Makachero waliifuatilia simu hiyo na kufanya mtego mdogo tu,tayari aliyekuwa nayo akatiwa mbaroni,ili akaeleze alikoipata na ilikuwa rahisi mno kuwasema waliompa au mahali wenzake walipokuwa.
Hivyo,tusiwape sifa majahili hawa kwamba walikuwa mauaji wa kimataifa, “Executioners’” kumbe majangili tu, wanaomea Tanzania kwa sababu ya uzembe wa polisi wetu na tabia ya jamii hii ya kufumbia macho watoto wao wahalifu.
Kwa kutumia IT makachero waliwanasa akina Bonge(30) na Amos Waibe Maboto; walikamatwa jijini Mwanza,kwa kutumia TEKNOHAMA.
Nataka kusema kwamba, umefika wakati sasa kutumia kompyuta kuwanasa wahalifu,badala ya kutumia mashushushu ambao wengine si waadilifu,nao hujiingiza katika usaliti na kuwaumiza raia.
ALHAMISI,Oktoba 25 mwaka huu,Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai,Kamishna Mwandamizi wa Polisi,Robert Manumba, akawaambia waandishi wa habari jijini Mwanza kwamba,kundi la watu waliokamatwa jijini Mwanza likihusishwa na mauaji ya Kamanda Barlow, hawa kuwa hasa wauaji.
Kwamba, walishikiliwa na jeshi hilo na kuhojiwa kwa sababu katika medani ya upelelezi,ni muhimu kama nini kuwahoji mashuhuda wengi,kama huyo Dorothy Lymo,ambaye alikuwa na marehemu wakati wa tukio la mauaji na hata hao ‘jamaa’ zake, akina Pepe na Fumo na wengine.
Wakikutwa hawana hatia,basi wataachwa huru.Ni muhimu polisi kuwahoji washukiwa wote na si mara moja au mbili,ili wakupe mwelekeo wa upelelezi nap engine sababu za kifo cha mtu kama huyo RPC Liberatus Barlow.
Kauli ya DCI Robert Manumba,kwamba hawa waliotajwa wangali wanapelelezwa,hata kama uchunguzi wa awali umebaini kuwa hawana uhusiano wa moja kwa maja na mauaji ya Kamanda,inaondoa tu ‘Motive’ kwamba aliuliwa kwa wivu wa kimapenzi, lakini bado tuhuma zingalipo dhidi yao.
Manumba, aliwaambia waandishi wa habari Alhamisi,Oktoba 25 kwamba waliomuua Barlow ni majambazi wazoefu(wa uhalifu,siyo weledi),na kwamba inawezekana lilikuwa tukio la ‘nasibu’ na bahati mbaya hivi.
Kundi la majahili saba, miongoni mwao watano: Muganyizi Michael Peter(36) mkazi wa Isamilo,Mwanza,Chacha Mwita(50),Edward Bugazi Kusuta,Bhoke Marwa Mwita(42)nz Magige Mwita Marwa, ambao wengine walikuwa wakazi wa Gongo la Mboto,Dar ndiyo hasa walioshiriki katika mauaji.
Watu hawa, majira ya saa nne hivi  usiku, siku ya tukio, walitangulia kupora mali za watu katika ‘grocery’ ya New Tuliza Inn,Pasiansi, waliwateka wanywaji na kuwapora vitu na simu ya mama mmoja.
Usiku huo wa Oktoba 12,Ijumaa saa sita hivi usiku walifika Kiseke katika baa iitwayo,Green Corner, waliwapora wateja,walipora hata Konyagi,wakabugia.
Sasa, wakati wanafika Kitangiri eneo lile la tukio,wakakutana na Barlow ambaye alikuwa akimsindikiza Dorothy nyumbani kwake, akawamulika kwa taa za gari.
Dorothy, anasema aliwaona wakiwa wamevalia vivazi vile vya Polisi Jamii ama Ulinzi Shirikishi, sasa Kamanda Barlow akidhani ni hao walinzi wa kijamii, akawamulika ili awaone vizuri.
Dorothy akamwambia Barlow, “Unawamulika unawajua?” Basi, kuona hivyo hgao jamaa wakamfuata Barlow haraka na kumzingira, wakaanza kufanya matata, Barlow akachukua ‘Radio Call’ ili awaite polisi.
Muganyizi Peter akamfatulia risasi ya Shotgun shingoni, ikamfumua shingo kabisa, ilimvunjilia mbali shingo lake.
Walichukua hiyo Radio Call ya Barlow na simu ya Dorothy,wakajitoma gizani.Keshoye, wakajiondokea kwenda Dar es Salaam,bila shaka walishajua walimuua nani!
TASK FORCE ya makachero wa polisi ya KIKOSI  CHA KISASI DHIDI YA MAUAJI YA BARLOW kiliwasili jijini Mwanza jioni Oktoba 13. Hata Inspekta Jenerali wa Polisi, Said A. Mwema, mtikiso wa mauaji hayo ulimleta Mwanza siku hiyo.
Makachero wa polisi, wakiwamo hao wa kimataifa, Interpol waliwasili Mwanza, wakasambaa Mara,Shinyanga,Mwanza, Geita,Bukoba na Dar es salaam, ili kufanya mtandao mkubwa katika medani ya upelelezi.
IGP Mwema, amewaambia wanahabari kuwa,waliomuua Barlow walikuwa saba, hao watano wamekamatwa tayari na wengine wawili wananyatiwa bado, na kwamba hata kama waende Uingereza watatiwa mbaroni na Interpol na watashushwa hapa nchini ili wakabiliane na mashitaka,ili kuwa fundisho kwa wenzao. Hiki ndicho KISASI alichosema Mwema, dhidi ya mauaji ya Barlow.
Nataka kusema kwamba, kulingana na Mwema,makachero wa hiki KIKOSI MAALUM CHA KISASI, walifanya kazi yao kabla ya siku 12 kwisha na kuwatia mbaroni wahusika, kama wanavyofanya kazi Federal Bureau of Investigation, Scotland Yard   ama  Military Intelligence 5(MI5)!
Majambazi hao walikamatwa Dar,Gongo la Mboto,wakakutwa na silaha mbili,Shotgun hiyo waliyotumia kumuua Barlow,ilikatwa kiatako na nyingine ni ‘Pump Action’.
Hadi Oktoba 25 redio ya upepo ya Barlow waliyopora eneo la tukio,ilikuwa bado kukamatwa,ndiyo iliyochongea Barlow kuvunjwa shingo kwa Shotgun Greener iliyofyatuliwa na huyo Muganyizi Peter,Mhaya kutoka Kagera!
Walipomuua Barlow wakatorokea Dar es salaam ambako pia hawakulala,walipora mali za raia hadi siku walipokamatwa. Nakwambia Jasiri haachi asili.
Kufuatia maelezo ya IGP Mwema na DCI Manumba, nataka kutafakari mambo machache hapa. Sina ubishi na kauli kuwa Barlow hakuuliwa kwa wivu na  visasi vya kimapenzi.
Nataka msomaji ajiulize maswali yafuatayo:
Mwanza,kuna majambazi mwazoefu wenye bunduki kama Shotgun, wanatamba tangu saa nne tu za usiku kuanzia Pasiansi,Lumala hadi Kiseke?
Polisi wa doria wanakuwa wapi hadi baa ziporwe hata Konyagi na majambazi,hata waanze kujipongeza,Kazi na Dawa, utadhani nchi haina mwenyewe?
Akina Muganyizi, walipokamatwa eti walikutwa na simu nyingi walizopora wananchi, bila shaka mchana kweupe!
Polisi walikuwa wapi wakati vibaka, wezi na majambazi wanapotishia maisha ya watu na mali zao?
Hivi Mwanza nako kuna  ‘Security Service’? Mbona raia wanatishiwa na vibaka na majambazi ambao sasa hawana hofu tena na doria za polisi?
Niliandika katika sehemu iliyotangulia kwamba, hapa Mwanza ndipo hakimu mmoja aliwahi kumtorosha jambazi sugu kwa ‘removal order’, siku ya kesi RCO Goodluck Mongi, akaambiwa na askari wake kwamba,mshitakiwa hakuwepo rumande!
Hapa Mwanza,ndipo jamaa mmoja mwaka 2005, alijipenyeza katika msitu wa wana usalama pale CCM Kirumba, akampiga mweleka Jakaya Kikwete wakati huo akiwa mgombea mteule wa Chama cha Mapinduzi! Kesi hii ilifika mahakamani,jamaa akanyeshewa mvua ya miaka jela.
Aliyekuwa Mbunge wa Shinyanga Mjini, Leonard Derefa, aliwahi kusema Bungeni kwamba jeshi la polisi livunjiliwe mbali,kwa kuwa lilishashindwa kulinda raia na mali zao-limewaacha majambazi na vibaka kutamba!
Mimi sitaki jeshi hili livunjwe,ili kuwe na “Vacuum” ama Ombwe ambalo linaweza kuleta kiama zaidi ya hapa tulipo.
Nataka kumwambia rafiki yangu Mwema ajiulize kama raia tunavyojiuliza: Kwanini Barlow alikuwa peke yake usiku wa manane,bila ulinzi? Kwanini alitembelea gari la kiraia tena lenye stika bandia ya Bima?
RPC hakuwa na walinzi? Je,polisi wa Mwanza wanafanya nini kuwakamata vibaka hata wanamiliki silaha na kumuua RPC? Polisi wanakamata wahalifu au wanafanya biashara ya daladala mjini? Kwa nini polisi wawe na vitambi? Mbona hata Bill Gates, Carlos Slim, Warren Buffett na wenzao hawana vitambi? Eti Polisi wa Mwanza wana vitambi!!
Nataka kumwambia IGP Said Mwema akumbuke kwamba, nilimuuliza katika mkutano na waandishi wa habari kwamba, Barlow aliuawa Oktoba 13, ilipofika Oktoba 25 tayari majahili hao walikwishatiwa mbaroni-siku 12 tu  za Operesheni ‘LIPA KISASI DHIDI YA MAUAJI YA BARLOW’.
Nika mkazia macho ya kidadisi IGP Mwema na kumbandika swali,
“Kwanini kasi hiyo ya majuma mawili ya kuwakomesha majambazi waliomuua Barlow isitumike pia kuwakomesha majahili wanao ua raia na kuwapora mali zao?”
Kwa nini kasi hiyo, “Supersonic Speed” isitumike katika upelelezi wa kesi nyingine za raia wa kawaida, wanaohujumiwa na majahili hawa na kuporwa mali na maisha?
Kwa nini polisi wanashindwa kufikisha kesi hata ya vibaka mahakamani, eti upelelezi haujakamilika? Kwanini kesi ya Barlow upelelezi ufanywe kwa kasi za viwango kama zile za Samuel Sitta-Standard and Speed!
“Polisi na raia wema lazima kuunganisha nguvu na talanta zao ili kuongeza ‘speed’ ya kuwakomesha wahalifu,ili nchi iwe salama”, alinijibu IGP Mwema,pale ukumbi wa Jini,Mwanza.
Said Mwema, anatishwa na jamii kukosa uzalendo kwa Taifa letu, na kushindwa kutimiza wajibu wa kizalendo kwa Taifa.
Oktoba 25,ndiyo siku nilipobaini kuwa Said A.Mwema, ni mwanafalsafa wa kiwango cha juu sana.Alianza kueleza kauli za marais wa Marekani akina John Fitzgerald “J.F” Kennedy na Abraham Lincoln, juu ya maslahi ya nchi kuwa kipaumbele cha kwanza,na uzalendo kwanza kuliko matumbo. Siku hizi Tanzania raia na polisi ni wazalendo wa matumbo yao!
Naam, Mwema akauliza hivi, “Usiulize Tanzania itakufanyia nini,uliza utaifanyia nini Tanzania?” Mwema amesema uzalendo unatoweka katika nchi yetu na maslahi ya taifa yametupwa,ndiyo maana polisi na raia wameshindwa kuunganisha nguvu na vipaji vyao ili kuwatoa kamasi majambazi!
Nitaichambua hotuba ya IGP Mwema, juma lijalo , Itaendelea.










No comments:

Post a Comment