Thursday, May 2, 2013

Ziara za akina Bush na Obama Afrika hazina mashiko(2)





NILIPOWAONA, naam katika televisheni, Mke wa Rais Mama Salma Kikwete na Mke wa Rais wa Marekani, Laura Welch Bush, Jumanne Septemba 25  jijini New York, nikajisaili kimoyomoyo: Hawa, wana nini cha kufanana?
    Salma Kikwete alikuwa na mumewe jijiiini New York, Rais Jakaya Kikwete aliyekuwa akihudhuria Mkutano wa Umoja wa Mataifa, .
    Laura Bush ni mpole; si mwenye harara. Ni mtulivu; mvumilivu dhidi ya mabaya. Ni mwenye upendo kwa watu wenye dhiki, hususan wagonjwa.
      Alipofika Tanzania mwaka 2005, aliwatembelea wagonjwa wa Ukimwi; akawaona yatima na kuahidi kupoza madhila yaliyowakabili.
    Jumapili, Novemba 4 mwaka huu, Laura Welch Bush atakuwa anatimiza miaka 58. tangu azaliwe huko Midland, Texas. Alizaliwa katika familia ya kidini. Amesoma shahada ya kwanza Chuo Kikuu cha  Southern Methodist, Dallas.
        Alisoma ya pili(Masters) ya Sayansi na Ukutubi katika Chuo Kikuu cha Texas. Alikuwa mwalimu na mkutubi Texas, kabla ya kuolewa na George Walker Bush, Novemba 5, mwaka 1977.
   Kwa hakika, picha niliyoiona ya Mama Salma Kikwete na Laura Bush, katika Maktaba ya Pierpont Morgan, jijini New York, ilinikumbusha kwamba Laura ni Mkutubi na pia mwalimu kama Mama Salma. Nikajiuliza: Hawa, wanashahiana nini?
    Sijui walizungumza nini wanawake hawa wawili, walipokutana hapo Maktaba jijini New York?
      Nadhani, bila shaka Mama Salma hakusahau kumwalika Laura nyumbani Tanzania, ili aje tena kutembelea Serengeti, Mlima Kilimanjaro, Oldonyo Lengai  Pengine kukagua miradi ya harakati za kupambana na Ukimwi na kupunguza umasikini.
     Laura Welch Bush(58) amefika Afrika Mashariki mara mbili. Julai 2003 alikuwa Nairobi. Na aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Dar es salaam, DIA(sasa wa Mwalimu Nyerere) Jumatano Julai 13, mwaka 2005.
    Alikuwa katika ziara ya siku mbili chini.
   Alipokelewa na Mke wa Rais, Mama Anna Mkapa(wakati huo) na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk. Asha-Rose Migiro, ambaye sasa ni Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
    Laura Bush alipowasili Da es salaam mwaka huo, alilindwa sana na makachero wa Marekani. Alikuja na mmoja wa mabinti zake mapacha, Jenna. Walikuwa wakitokea Gaborone, Botswana. Aliandamana na ujumbe wa watu zaidi ya 30, wakiwemo waandishi wa habari 12 na maofisa wengine.
    Kufuatia ‘protokali’ ya mikogo ya Kimarekani, hakupanda gari aliloandaliwa na mwenyeji wake, Mama Anna Mkapa. Alikwea moja la gharama sana-naambiwa  MAREHEMU Michael Jackson alikuwa akitumia magari kama haya ya bei mbaya kuendea na kutoka mahakamani, wakati wa kesi yake ya kulawiti. Wamarekani wana ‘nyodo’…
     Naam, Mama Laura alikwea  Limousine, lenye milango sita. Alilindwa na mbwa maalum wa kubaini mabomu ama milipuko. Si unajua tena kitisho cha al-Qaeda? Mama Anna Mkapa alijitutumua na Mercedes Benz.
     Mbwa wa Marekani walinusa kila kitu uwanja wa ndege, saa mbili kabla ya Laura kutua. Hata mawasiliano yote ya simu yalikatika mama huyu alipokuwa akitua kwa mbwembwe za kitajiri.
    Nikakumbuka ulinzi wa Wamarekani hawa kwa Waziri wao wa Mambo ya Nje, Madeleine K. Albright, alipofika Dar sa salaam kuhudhuria maziko ya Hayati Mwalimu mwaka 1999. Leo ni miaka minane tangu Mwalimu aage Dunia St. Thomas jijini London.
    Nikakumbuka pia ‘nyodo’ za Makachero- Wamarekani- alipokuja Rais William(Bill) Jefferson Clinton mjini Arusha, Jumatatu Agosti 27 mwaka 2000.
    Clinton alitua uwanja wa ndege wa Kilimanjaro(KIA) ili kushiriki utiaji saini makubaliano ya kurejesha amani ya Burundi. Alialikwa na Msuluhishi wa mgogoro huo, Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Rolihlahla Mandela, ambaye wapenzi wake humwita, Madiba.
    Protokali ya ulinzi na mbwembe za Wamarekani zilifanya mawasiliano ya Dar es salaam na Arusha kukatika; mbwa wakanusa magari hata ya viongozi wa juu wa serikali, wakati askari wetu wa Usalama Barabarani, makachero na waandishi wa habari walitimuliwa wasikaribie kwa wakubwa hao!
   Ombaomba na wakoma waliondolewa mitaani, kisha magari ya Zimamoto tuliyozoea kuyaona yakizima moto, yakapiga ‘deki’ barabara! Kwa hakika, napendekeza Mama Salma Kikwete ayaige yote mazuri kutoka kwa Laura Bush, lakini kamwe asiendekeze ‘nyodo’ za namna hii. Aendelee kuwa mtu wa watu na mlezi wa Taifa letu.
    Wake wengine wa Marais wa Marekani ni pamoja na Jacqueline Lee Bouvier(mke wa Rais Kennedy), Claudia ‘Lady Bird’ Alta Taylor Johnson, Thelmacathy Patricia Ryan Nixon, na Elizabeth Bloomer Warren Ford, mke wa Gerald Ford.
    Wengine ni Anne Frances ‘Nancy’ Robbin Davis Reagan, Barbara Pierce Bush(mama mzazi wa George W. Bush, Hillary Rodham Clinton na Laura ‘rafikiye’ Mama Salma.
    Laura ana mabinti wawili; Barbara(alipewa jina la mama yake Bush) na Jenna, jina la mamaye Laura. Ni mapacha waliozaliwa mwaka 1981. Mama huyu hujishaghulisha na masuala ya Afya ya akina mama, hususan vita dhidi ya saratani ya matiti.
    Ni changamoto kwa Mama Salma kuepuka biashara zote awapo Ikulu, ili akazanie elimu na Afya(mama Salma pia ni Mwalimu kama Laura Bush), lengo likiwa kupunguza umasikini wa watu, magonjwa kama Ukimwi na umasikini, bila kusahau maendeleo ya akina mama.
    Wapo wake wengi wa Marais walioacha ulezi kwa taifa wakaanza kufanya hata biashara za magendo wakiwa Ikulu(si Tanzania), wapo waliowahi kuwapiga ngumi hata mawaziri na waandishi wa habari.
   Wapo wanaoishi maisha ya anasa sana kwa pesa za walipakodi, bila kulifanyia taifa kitu chochote, ia\sipokuwa nyodo na anasa!
     Pia, wapo wanaotibiwa mafua Paris, Washington na Geneva, wakati akina mama wetu hapa wakilazwa wanne kitanda kimoja, hususan wakati wa kujifungua… Mama Salma Kikwete asije kuwa miongoni mwa hawa.
    Mke wa Rais wa Maisha, Dikteta Jean-Bedel Bokassa, alilazimisha wanafunzi wote wa shule kununua sare katika moja ya duka lake! Walipogoma na kufanya maandamano, waliuawa si chini ya 100!
Mama Salma asiache kuwa kama mkewe Pilato Mrumi, alivyomtetea Yesu wa Nazareth kuwambwa msalabani..
    Tanzania ipo mifuko kama Fursa sawa kwa Wote(EOTF) ambayo haijulikani ipo kwa manufaa ya nani? Mama Salma Kikwete hastahili kufanya biashara hizo, isipokuwa awe na Taasisi ya Malezi ya Taifa(TMT).
    Salma Kikwete(kama mwalimu na mlezi wa Taifa) angeanzisha Taasisi ya Malezi ya Taifa itakayonusuru vijana katika maangamizi ya Ukimwi, umaskini, biashara ya ukahaba, madawa ya kulevya, ujinga na mmomonyoko wa maadili na Afya ya mwili na kili.
    Katika Dunia ya Utandawazi, Mama Salma Kikwete akimshirikisha Laura Bush, watawaokoa vijana dhidi ya majanga haya ya madawa ya kulevya, Ukimwi na biashara ya ngono inayofanywa sasa ili kujitafutia kipato.
    Nahisi, Mkataba wa Ushuru wa pamoja wa Afrika Mashariki(East African Customs Union Treaty) ulishaleta soko la pamoja hata la makahaba katika Afrika Mashariki. Makahaba, wakiwemo watoto wadogo kutoka hata Rwanda, Burundi, Somali na Afrika Kusini, wananyatia soko hilo ili kuendesha biashara ya ngono(sex trade) na kumomonyoa maadili licha ya janga la Ukimwi.
   Mwishoni mwa Desemba mwaka 2003, polisi wa Kenya waliwatia mbaroni wasichana wasomi wa vyuo vikuu, wakiuza mapenzi katika mitaa ya Nairobi, hususan Koinange, wao huita, ‘K-Street’! Hapa Tanzania mitaa kama hiyo huitwa Uwanja wa Fisi!
   Si muda mrefu kuanzia sasa, wasomi wa vyuo vikuu watanyatia soko hilo la biashara ya ngono; wataacha kulihudumia Taifa ili kujipatia kipato kutokana na ngono
   Hivyo, kunahitajika Taasisi yenye nguvu ya kutoa nasaha kuzuia hali hii.
   Kadiri siku zinavyokwenda, ukahaba unatazamwa kama biashara ya kawaida, inayowavutia wasomi na watu wengine, hadi wamebadili majina kutoka ‘changudoa’, ‘wauza kuku’ au makahaba na kuwa Wafanya Biashara wa Ngono, Commercial Sex Workers(CSW)!
    Ni kwa sababu hiyo, Itifaki ya Ushuru wa pamoja(EACU) itawaleta pia wauza madawa ya kulevya, ‘dada poa’ na ‘kaka poa’ wengi kutoka nchi zote za Afrika Mashariki,  pengine kutoka Afrika Kusini na Ulaya.
   Watasababisha mmonyoko mkubwa kabisa  wa maadili na gharika kwa vijana, ambao wataingilia biashara hiyo kama wafanyabiashara wa ngono, Commercial Sex Sellers!
 Ni kwa sababu hiyo, Taasisi ya Malezi anayoweza kuanzisha Mama Salma kwa kushirikiana na Lura Bush, na Michelle Obama, itapambana na biashara hiyo kwa kutoa mafunzo na ushauri-nasaha,  ili kuwaokoa wasichana wetu wakiwemo wanafunzi kuwa, Sex Seller Girls(SSG)!
     Taasisi kama hii inaweza kuendeshwa kwa msaada mkubwa wa watu kama Mama Laura Bush; yumkini ikafanikiwa kuwarejesha wasichana na wavulana masomoni, baada ya kukatisha masomo kwa mimba, au kuolewa, na wavulana  bangi na madawa ya kulevya.
    Taasisi  ikianzishwa na Laura Bush na Mama Salma, inaweza kufadhiliwa na watu maarufu sana hapa Duniani, kama Bill Clinton, Nelson Mandela, Tony Blair,  n.k. Mama Salma atakuwa mke wa kwanza wa Rais atakayejitofautisha na wenzake kwa kuokoa kizazi katika maangamizi ya Ukimwi, madawa ya kulevya na ukahaba katika zama hizi za utandawazi.
    inaweza kuwa Taasisi itakayolea na kufufua vipaji vya vijana. Badala ya biashara ya ukahaba kubadili maendeleo ya watoto kielimu, watazaliwa hapa akina Venus na Serena Williams, akina Didier Drogba, watakaoiletea Tanzania medali za heshima, badala ya hawa kugeukia biashara ya ngono kwa wageni na wawekezaji wa migodi na kubwia unga.
   Zamani, ilidhaniwa jamii na madhehebu ya dini yangeweza kuifanya kazi hii. Sasa, imegundulika, vijana na watoto hawako salama katika madhehebu ya dini, kwa kuwa hata  wachungaji, masheikh  na mapadri wameripotiwa kumomonyoa maadili kwa kiwango cha kutisha. Tunahitaji Taasisi ya Malezi.
    Hivyo, Mama Salma na Laura Bush  ama Michelle wakianzisha Taasisi ya Malezi Tanzania, wataliokoa Taifa katika maangamizi. Bila shaka Mama Salma ataibuka Shujaa wa Taifa atakayetoka pasipojulikana(from Zero to Hero) na kutoa mwanga namna Taifa linavyoweza kuokoa maisha ya watoto na vijana wake kwa kuwaandaa kuwa wazalendo na raia waaminifu.
   Taasisi hiyo pia itakemea unyanyasaji na udhalilishaji kama wa akina Mfalme Mswati III wa Swaziland, wanaooa vigoli kila mwaka, bila kujali Ukimwi na Haki za Msingi za Wanawake.
   Kwa kuwa kuna habari kuwa Michelle na mumewe walikwisha alikwa hapa nchini, t tunawakaribisha kwa moyo mkunjufu,ikiwezekana wafike kabla ya kumaliza Mhula wao mwakani.
    Naungana na Mama Salma na Watanzania wengine kumkaribisha Laura na George W. Bush, Obama na Michelle kwa wimbo, ‘Welcome  to Tanzania’ ulioimbwa na Hayati Pepe Kalle na wenzake, Djuna Bileku Mpasi, Papy Tex, Ikomo Djodjo, Lofombo na wengine wote wa Empire Bakuba… Welcome to  Tanzania!!
Itaendelea
    0754 324 074
     0713 324 074
www.congesmramba.blogspot.com

No comments:

Post a Comment