Thursday, May 2, 2013

ZIARA ZA AKINA OBAMA AFRIKA HAZINA KITU(1)

NILISOMA katika gazeti la The African la Aprili 23-Mei 3 mwaka huu,hususan katia katuni ya GADO,kwamba Rais wa Marekani na mkewe,Michelle, watakuja Afrika ya Mashariki.
Naam, niliona katika katuni ile Obama na Michelle wakiteremka katika dege lile la Air Force One,huku kukiwa na maandishi, "Obama to visit Africa" huku wakipokelewa na wawekezaji wa kichina!
Utadhani Afrika, isipokuwa mali ya Mzungu,basi itaangukia katika ushawishi wa wageni hususan Wachina!
Wachina, wanafanya biashara Afrika,na wametujengea ofisi za Makao Makuu ya Umoja wa Afrika,AU, kule Addis Ababa.
Ni hapa naanza kutafakari ujio wa wakubwa hawa wa dunia hapa Afrika,hususan Tanzania yetu kama ifuatavyo:

UJIO wa Rais George Walker Bush  Afrika,  hapa Tanzania  mwaka 2008  ulifanya mfumo wa kawaida wa maisha ya watu kusimama.
   Ni kawaida kusimama. Kila kinakokwenda kivuli cha Bush, Clinton,Obama,Malkia Elizabeth na watoto ama wake zao, mfumo wa maisha ya kila siku husimama hasa wanapokaa takriban wiki nzima.
  Ni jua tu ndilo halisimami; yaani ni dunia tu ndiyo huendelea kulizunguka jua na kutufanya tuone kwamba dunia ingali inazunguka.Wakati mwingine tunapumua kwa shida. Bush, ni kama Mungu ama malaika, sijui.
   Bush, alikuja Tanzania miezi kama kumi tu kabla ya Uchaguzi Mkuu wa  nchi hiyo mwaka 2008. Naam, miezi 11kabla ya kuiacha White House kwa Rais mpya atakapoapishwa Januari 20 mwaka 2009.
   Rais wa Marekani alikuja mara ya pili hapa, baada ya miaka minane. Rais Bill Clinton alikuja Arusha, Jumatatu Agosti 27 mwaka 2000. Alialikwa na Msuluhishi wa Mgogoro wa Burundi wakati wa utiaji saini mkataba wa amani, Nelson Mandela.
   Kilichotokea wakati Clinton anashuka uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Kilimanjaro, ni kivuli cha mtu mkubwa kukanyaga ardhi ya watu wanyonge.
  Wamekuja hapa akina Madeleine K. Albright mwaka 1999 mfumo wetu wa maisha ukasimama ili kupisha wa Kimarekani kutandaa nchi masikini.Bendera ya nyota 50 ikapepea anga lote la Mtu Mweusi.
  Jumatano, Julai 13, 2005 mke wa Bush, Laura Welch Bush alitua Dar es salaam kwa ziara ya siku mbili.Julai 2003 Laura alikuwa Nairobi.
Mama huyu amekuja Dar es salaam tena na mumewe, kwake ikiwa ziara ya tatu Afrika Mashariki, na mara kama tano hapa Afrika.
   Luteni Usu, na Rubani wa dege la Jeshi(US Army) anapokuja Tanzania, wengine tunadhani kaja kutafuta namna ya kusimika jeshi la nchi hiyo ili kudhibiti ugaidi na magaidi.Na akina Obama wanakuja hapa kujipendekeza kwetu ili tuwaone rafiki,kumbe ni kuona Wachina wanapata ushawishi mkubwa Afrika,na wanapewa kandarasi,huenda wakatufundisha kichina.
  Wapo wanaodhani kivuli cha ‘kichaka’-Bush ni kutafuta kushawishi serikali za Afrika Mashariki  kuwanyanyasa Waislamu…lakini magaidi hawatambuliki kwa dini moja,
Marekani wapo Wazungu na Wachina Magaidi. Hata Ulaya, wapo magaidi kama Red Brigade, waliomuua Aldo Moro Waziri Mkuu wa Italia, Mafia, na wengine wengi.
   Hata kabla ya Osama kulikuwa na magaidi kama Black September waliowaua na kuwateka nyara wanariadha wa Israeli katika mashindano ya riadha ya Olimpiki mjini Munich, mwaka 1972.
 Magaidi hawana rangi moja, dini moja ama ukoo.
   Bush, kaja Tanzania, Benin, Rwanda, Ghana na Liberia; na mraba huu haudhani kaja kuumiza watu wa dini Fulani ambao walitaka kuandamana kupinga asije!
  Naam, sisimizi kupinga tembo asije, kwake kibarua!
   Yawezekana, Bush na Obama wakaja  kuhakikisha maslahi ya Marekani yanalindwa Afrika hii hata kabla Obama hajaondoka mamlakani.
Maslahi ya Marekani ni pamoja na makampuni ya uchimbaji madini ya (Kimarekani) hapa,  na yale ya uchimbaji mafuta kwingineko Afrika.
   Ukiacha siasa, Bush ni mfanyabiashara wa mafuta na madini. Kampuni yake ya kwanza iliyoanzishwa Midland iliitwa, Arbusto Energy. Arbusto ni neno la Kihispania lenye kumaanisha ‘kichaka’yaani Bush.
   Baadaye, Arbusto ikabadilishwa na kuitwa, Bush Exploration. Ilifilisika mwaka 1980, wakaanzisha nyingine, Spectrum 7; baadaye Harken Energy Corporation. Bush ni mwekezaji pia katika michezo.
  Yeye na matajiri wenzake walinunua timu ya Baseball, ‘Texas Rangers’ kwa dola milioni 75.
  Hii ni kusema, katika ziara yake hapa, akikumbuka kumuuliza Rais Kikwete juu ya michezo waipendayo Watanzania, Kikwete atasema Mpira wa miguu. Anaweza kumshawishi yeye Bush na Wamarekani wenzake kununua hisa katika vilabu vyetu maarufu hapa, kama Yanga!
  Kwa kuwa Bush ni mfanyabiasha wa madini, yawezekana sasa baada ya kuondoka Ikulu, akataka kuwekeza zaidi katika dhahabu, almasi, makaa ya  mawe, mafuta, gesi tanzanite, shaba n.k
   Atataka pengine kuwekeza katika utalii ama sekta ya wanyamapori. Shahada yake ya Uzamili katika Biashara anaweza kuitumia  kuchota rasilimali zetu hapa. Wengine wanasema Bush ni mabepari walewale wanaitangazia Dunia utawala bora, demokrasia na haki, wakati makampuni yao yanaongoza duniani kwa unyonyaji.
   Makampuni ya mafuta kama Chevron, au Chevron Texaco, Conoco Phillips na Exxon Mobil, ni makubwa sana duniani yanayokomba mafuta ya dunia na kutengeneza faida ya zaidi ya dola bilioni 80 kila mwaka.Haya yako Nigeria na popote.
   Hivyo, Marekani hufika sehemu zote kuliko  mafuta ili kushinikiza mambo. Ikitokea nchi ikakatalia mafuta au madini yake, mambo kadhaa, kama ugomvi na vita( kama Iran na Irak) huanza kutokea.
Na watawala wa  nchi hizo wanaokubali kuipa Marekani rasilimali au mafuta, huwa ‘watoto wazuri’ na rafiki kama Marehemu  Mohamed Reza, ama Shah(wa Iran) ama Mobutu hadi wanapotimuliwa, au wanapofariki. Usiombe kuchukiwa na akina Bush na Obama.
   Makampuni hayo ya mafuta ndiyo yanayolalamikiwa sana hata huko Niger Delta, kwa mikataba ya ovyo ya rushwa kwa viongozi wa Nigeria, kama akina Marehemu Dikteta Sani Abacha.
   Ni kwa sababu hii Bwana ‘Arbusto’(Bush) ama mrithi wake Obama  wanastahili kuchungwa sana watakapotaka kuwekeza katika rasilimali zetu.
Aulizwe Obama, kama atakubali kulipa tozo kamili na mrahaba sahihi au wa kinyonyaji kama Niger Delta?Atashinikiza mikataba iwe siri? Utawala bora upi hapo?
   Bush ni ‘pacha’ wa baba yake, George Herbert Walker Bush(84); ambaye Desemba 1989 alituma majeshi Panama na kupindua serikali na kumkamata mateka kiongozi wa nchi hiyo, Jen. Manuel Noriega.
Na Obama ndio wale wale wanaong'ata na kupuliza wakati Gereza la Guantanamo Bay,Cuba linaponyanyasa watu kwa miaka mingi bila kuwafikisha mahakamani,sasa wanasusa kula chakula,dunia kimya!
Bush  Aliingilia ugomvi wa Irak na Kuwait mwaka 1990, alivuruga uchumi uliokuja kurekebishwa na Rais Clinton.Alidhoofisha dola la Urusi(USSR) na kumfanya Mikhail Gorbachev kujisalimisha mikononi mwake mwaka 1989.
   Arbusto(Bush mtoto) aliyewahi kutiwa mbaroni na polisi mwaka 1976 kwa kuendesha gari akiwa ametutika mtindi, anafanana sana na babaye.
  Kasoma chuo kikuu kilekile alichosoma babaye, cha Yale; kaendesha madege ya jeshi kama babaye,anafanya biashara ya mafuta, amewapindua Saddam Hussein na Mullah Mohamad Omar. Mmoja amenyongwa, mwingine ni mkimbizi asiyefahamika alikokimbilia.
   Kama muda wake wa kuwepo Ikulu ungeruhusu, haikosi angemaliza kazi kwa kuwapindua  Marehemu Hugo Chavez wa Venezuela na Ahmadinejad wa Iran.
Hawa, wanakiburi cha mafuta, na marekani huhitaji kama asilimia 30 ya mafuta yote duniani.
   Naam, kwa kuwa Arbusto ‘kichaka’ Bush bado anakumbukumbu ya kuvurumisha dege la Jeshi, F-102  Fighter, kule Texas Air Nation Guard, kwa vyovyote atataka Tanzania kuwa mshirika wake wa kijeshi kwa kile kiitwacho, African Command; ama maslahi ya kijeshi na kiuchumi ya Marekani hapa Barani.
   Kwa kuwa Rais Kikwete ni mwanajeshi; tena wa enzi zile za vita baridi, tunaimani atakuwa ‘chonjo’ na jamaa huyu, kama ataleta njama zozote za kutaka kuchukua mwambao wetu kiulinzi, ama maliasili zetu kiuchumi.
   Jambo moja tunaomba Rais Kikwete alikatae: Udhalilishaji na nyodo za Wamarekani kwa mataifa anayotembelea rais wao.
 Vyombo vya ulinzi vya nchi anakotua hugeuka ‘mdoli’ ama sanamu.Ombaomba huwekwa kizuizini ili wasionekane mabarabarani wakitangatanga, barabara hupigwa deki usiku kwa magari ya zimamoto, na viongozi wetu wakuu ama hukatazwa kumkaribia, na  pengine magari ya viongozi wetu hunuswa na mijibwa ya Marekani yanayokuja kwa dege maalum kabla ya Air Force One, kutua.
   Hawa jamaa huja na magari yao ‘Bullet Proof’ ili rais wao asishambuliwe kwa namna yoyote na magaidi na wenye msimamo mkali wanaojitoa mhanga, kama walivyomuua Benazir Bhutto huko Pakistan.
  Arbusto ‘kichaka’ na Obama wanapokuwa Dar es salaam pilika pilika huwa nyingi; ni karibia kama Amri ya hatari huwa imetangazwa.
 Usafi huwa wa hali ya juu, ulinzi wa polisi na usalama barabarani wenye vyeo vikubwa; hapana tuseme FBI na makachero wengine huwa kila sehemu, kila mahali kusikiliza na kuchunguza chochote kisemwacho kumhusu jamaa huyu, Arbusto.
   Marekani inajidai sana kusemea demokrasia na haki za binadamu.
Bush aliwahi kudaiwa kumwibia kura Al(bert) Gore mwaka 2000 hadi kesi ilipohamia mahakamani, baadaye  AlGore akakubali kushindwa, kwa maslahi ya Marekani.
   Kuhusu haki za binadamu, Arbusto hana cha kusema kwa sababu anadaiwa kumiliki jela Abu-Ghraibu, mjini Baghdad na Guntanamo nchini Cuba. Juzi tumewaona wafungwa wakichechemea na kugomea chakula, lakini nani aseme?
Huko watuhumiwa wa ugaidi huteswa bila kupelekwa mahakamani….hiki nacho ni kivuli cha kichaka kinachotisha wanyonge.
   Digrii yake ya Uzamili katika Usimamizi wa Biashara aliyopata katika Chuo Kikuu cha Harvard mwaka 1975, kama ataitumia vema kumshauri Rais wetu kutowatumia akina ‘Karamagi’ katika mikataba… Buzwagi na Richmond; tutampongeza sana.
 Lengo ni kutaka wanyonge wa nchi hii kupata mgawo katika ‘kasungura’ kadogo kanakoishia mikononi mwa wajanja.Kumbuka, mfisadi huficha fedha zetu katika mabenki hata ya Marekani, baadaye hukimbilia huko, Bush akiwa kimya.
   Bush, ni wa pili kwa watoto wa Marais kutawala Marekani. Mwingine ni John Quincy Adams, mwaka 1824.Asigeuke somo hapa kwa watoto wa wakubwa kuhamia NEC ya CCM  kila unapofika msimu wa uchaguzi  ili kusaka madaraka.Watoto wa wachungaji huwarithi baba zao.
    Ni kwa sababu hii, tunamtaka Bush  na Obama wakifika Washington, wakemee mabepari wanatunyonya kwa kutumia makampuni yao ya uwekezaji hapa na kuwanyima watu ajira. Mengine hewa.
  Bila shaka, atawaona watu maskini na wenye Ukimwi hapa; atawaona ombaomba, pengine atasikia habari za machangudoa, atatembelea mbuga zetu na kutamani kujenga hoteli la nyota sita(six star hotel), afikirie kutupa ajira sisi, na si Wamarekani.
  Shime, Bush afikirie maslahi ya mtu mweusi wakati huu anapojitayarisha kuipisha White House.
   Tanzania ni taifa dogo la watu milioni 46 kulinganisha na Marekani yenye milioni 250.Bila shaka  Obama atajifunza namna tunavyopambana na akina ‘Karamagi’ huku bila kupigana ngeu, kama ‘nyumba’ ya jirani.Fujo zimeanza,lakini angalau tuna amani.
 Shime, aambiwe kutusaidia kuwatia mbaroni akina Ballali , pindi wanapotimkia huko, baada ya kutu ‘richmond’ huku!
   Mwisho, kwakuwa  Marehemu Osama Bin Laden hajawahi kukimbilia huku kwetu, na kwa kuwa watuhumiwa wa ugaidi wengi si wa dini, rangi ama ukoo Fulani tu.Obama asitufanye sisi magaidi.
  Basi, Wamarekani wanapokuja Dar es salaam(Bandarisalama), waepuke nyodo zao za ulinzi, utadhani sisi nyau –wakombamboga.
   Watuamini kuwa sisi ni rafiki tu…tafadhali Rais mwingine wa Marekani akija hapa kwetu, asiigeuze Tanzania Jehanum:
 Moja, kwa itifaki na mikogo ya ulinzi, pili kwa kuzuia mfumo wa kawaida wa maisha. Tatu, kwa kupandisha bei hata za mafuta, kukata na kuingilia mawasiliano yetu, kusumbua ombaomba wetu, machangu na kunyanyapaa viongozi, waandishi wetu na makachero.
   Mwisho, mikogo na utajiri wa Marais wa Marekani usiowaongoze katika tamaa mbaya vigogo wetu kwa fahari na utajiri wao.
Unajua Rais Bush, mbali na biashara zake za madini na mafuta  alikuwa anapokea mshahara wa dola 400,000(zinazotozwa kodi) kwa mwaka. Alilipwa alawansi ya matumizi dola 50,000(hazitozwi kodi) kwa mwaka, kwa kazi za kiofisi.
  Rais Mwai Kibaki wa Kenya alikataa kulipwa mshahara kama huo wa dola za Marekani 500,000 kwa mwaka, wakati raia wake wakingali masikini.
 Bush, alililipwa pia masurufu ya safari kama dola 100,000(hazikatwi kodi) kwa mwaka; na pia hupewa dola 19,000 za viburudisho ama burudani. Anuani yake ya barua pepe ni president@whitehouse.gov mtu yeyote aweza kumwandikia na hata kumkosoa ijapokuwa ni mbabe tu kama  madikteta wengine.
 Hata hivyo,Rais wa zamani Venezuela, Hugo Chavez alipomtukana wakati wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa(UN)  mwaka 2007,akapewa saa chache  awe ameondoka jijini New York. Nitafuatilia mshahara wa Obama na Michelle.
Siku hizi Venezuela 'Jembe' limelala, anatawala Nicolas Maduro,nchi imeanza kuwaka moto kwa ushawishi wa hawa jamaa.Sasa Obama yuaja hapa Afrika Mashariki, atatufanyia nini kama si kuja kuleta nyodo na shinikizo hapa?
Itaendelea
    0754/0785 324 074
 
 




No comments:

Post a Comment