Monday, August 5, 2013

KIKOMBE CHA BABU WA LOLIONDO KIMEINYWESHA SUMU TZ




ZAIDI ya watu 10,260 waliacha kwenda kuchukua dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi Mkoani hapa,tangu 2004 hata sasa.
Serikali ya Tanzania leo,kwa kushirikiana na Tume ya Kikristo, The Christian Social Service Commission(CSSC) na serikali ya Marekani,siku hizi wanatumia mabilioni ya Dola za Marekani kuwarejesha wenye virusi vya Ukimwi hospitalini ili kupata tiba ya kisayansi.
Mkakati huo unaitwa, ‘Back to Treatment” na unalenga kuwarejesha watu 10,262 wa mkoa wa Mwanza tu hospitalini.
Baadhi yao waliacha tiba ya kisayansi, wakatimkia Samunge,Loliondo mwaka 2011 kwa Yule ‘Babu’ wa Kikombe cha Miujiza,kilichodaiwa kuponya magonjwa sugu,ukiwemo Ukimwi kwa majuma matatu tu!
Ambilikile Mwasapila,(78),Mchungaji Mstaafu wa KKKT, alikuwa ameota ndoto ikimwambia aondoke Babati na kuhamia porini huko Samunge, ambako alianza kunywesha maelfu ya watu kutoka Afrika Mashariki,Ulaya na Asia dawa ya miujiza kutoka kwenye mti uitwao,Carisa Spinarum, ama ttuuite     Mrigariga!
Serikali ikaanza kuishabikia dawa hiyo iliyouzwa kwa shilingi 500 tu kwa kikombe, maelfu ya watu wakanywa, wakiwemo wasomi,maprofesa,wafanyabiashara na hata wakulima wa kijijini.
Vigogo wa serikalini walikuwa mstari wa mbele kuishabikia na kuibugia ili wapate tiba ya kimiujiza-Cure in the Tanzanian Bush!
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Abbas Kandolo(yuko Mbeya siku hizi) alipoulizwa na Mwandishi huyu aliyefanya mkutano kamambe ofisini kwake kuratibu safari za kwa ‘Babu’ wa Loliondo,mwaka huo 2011, “Ni kwanini serikali inahaha kushiriki ushirikina na miujiza ya uponyaji huko kwa Babu,Loliondo, kabla ya dawa hiyo kuthibitishwana taasisi husika, Tropical Pesticides Research Institute, TFDA, labda na TBS, akaniambia kwa hamaki!
“Sasa wewe mtu layman (usiye na taaluma ya kitabibu) unawazidi maprofesa wanaoinywa dawa ya Babu wa Loliondo?” akamtaja mkubwa mmoja.
Katika mkutano huo wa Mkuu wa Mkoa na wafanyabiashara wenye mabasi ya kusafirisha watu kwenda Loliondo, walikaribia kunimeza,kuona nilikuwa nikitaka kuwaharibia biashara, wakati serikali ilishamkubali huyo ‘Babu wa Kikombe’ aliyeleta neema kwa wenye mabasi mwaka 2011.
Carisa tree, ni mti uliokuwa ukitajirisha si babu huyo tu, bali na wenye vyombo vya usafirishaji na hata mama ntilie wa Samunge.Wagonjwa wengine waliopelekwa wakiwa mahututi, walifariki dunia.
Leo,serikali inameza machungu, inashirikiana na serikali ya Marekani na taasisi za dini kufanya mkakati wa kuwarejesha wenye virusi vya Ukimwi kwenye tiba uitwao kwa Kimombo, “Back  To Treatment” kwa mabilioni ya dola.
Mkakati huu, BACK TO TREATMENT, ulizinduliwa rasmi jijini Mwanza Agosti Mosi mwaka huu kwa mbwembwe, na watu wakalipana posho!
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanywa katika Hospitali ya Sekou Toure, Mkurugenzi Mkazi wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa wa Tume hiyo ya Kikristo ya Huduma za Jamii,Dk.Michelle Roland       akasema:
“Tangu 2003 serikali za Marekani na Jamhuri ya Muungano zimekuwa na ushirika kupambana na Ukimwi unaoathiri watu wote Duniani,hususan Watanzania”,Dk. Michelle Roland alisema.
Akabainisha kuwa ubia huu umewafanya wananchi wa Marekani kuchanga jumla ya Dola za Marekani bilioni 2.2 ambazo ni sawa na shilingi za Tanzania Trilioni 3.2.
Fedha hizi ni kwa ajili ya kupambana na magonjwa sugu,ukiwemo Ukimwi.
Mkuu wa Mkoa,Evarist Welle Ndikilo, akafungua mkakati huo, akisema Tanzania Bara sasa kuna zaidi ya watu 430,000 wanaopewa dawa za kufubaza Virusi vya Ukimwi kupitia Mpango huo wa Back to Treatment wa hao  Christian Social Service Commission(CSSC).
Ndikilo, akasema eti sasa Mkakati huo wa Back to Treatment utawarejesha wagonjwa kwenye tiba na utaifanya Tanzania mahali pasipo na maambukizi ya Ukimwi-AIDS-free Tanzania!
Labda, asitokee Babu mwingine kama wa Loliondo,bibi ama shangazi!
Asilimia 25 ya wenye kuishi na virusi vya Ukimwi walikimbia vituo vya kutolea dawa za Ukimwi, antiretroviral Therapy.
Wamekuwa hawapati dawa hizo ili kuwawezesha kuishi na afya njema na kushiriki ujenzi wa taifa.
Mama huyu wa Kimarekani,Michelle Roland, akaonya kuwa endapo wenye kuishi na virusi vya ukimwi hawatapata tiba sahihi,jamii nzima itaathiriwa vibaya,na maambukizi yataongezeka maradufu, na virusi vitajenga usugu-hizi ni athari za akina Abbas Kandoro kupigia debe Sangoma,kama Babu wa Loliondo!
Pia,Dk.Michelle Roland amewataka wenye virusi vya Ukimwi kwenda hospitalini kupata tiba sahihi,kando ya mfumuko wa vikombe vya babu na shangazi!
Akashauri udhaifu uliopo katika mfumo wa tiba(zikiwemo imani potofu za viongozi ba ushirikina) uepukwe,ili watu waishio na virusi vya Ukimwi warejeshwe kwenye huduma za tiba na ushauri sahihi.
Dk. Michelle akawataka watu kubadilika,na kuacha kushabikia uvumi na umizimu na masangoma.
Kampeni kama hii iliwahi kuzinduliwa Iringa na Balozi wa zamani wa Marekani nchini,Alfonso Lenhardt.Ilikuwa Septemba mwaka uliopita.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Evarist Ndikilo amesema Tanzania kuna watu 945,142 wanaoishi na Virusi vya Ukimwi.
Kati ya hawa 530,118 ndiyo walioanzishiwa dawa za kufubaza virusi vya ukimwi, watu 129,372 hapa Tanzania wamekimbia matibabu,wengine walitupa vidonge walipokunywa Kikombe cha Babu!
Hadi Machi mwaka huu watu 85,320 Mkoani Mwanza waliandikishwa kupata huduma,lakini ni 46,622 tu walioanzishiwa tiba.
Watu zaidi ya 10,000 hawajulikani walikokwenda,hawa ni pamoja na watoto 1,600 hapa Mkoani Mwanza.
Sasa  tukiulize,hizo imani za kishirikina zinazoshabikiwa na serikali na maofisa wake hata kukiuka sheria ilizoweka yenyewe kuhusu tiba ndiyo nini,kama siyo kuitesa nchi?
Imani potofu,ushirikina hata wa kuua Albino ili kushinda kura,kupata utajiri n.k
Wengine,watu wakubwa walibugizwa dawa ya babu na kuwafanya maelfu kufuata mkumbo wakaacha tiba sahihi.
Ndiyo maana tukasema, Kikombe cha Babu kimeinywesha sumu Tanzania,sasa inatumia mabilioni ya dola kurejesha wenye VVU hospitalini.
Hawa ni wenye VVU tu, saratani,kisukari,magonjwa ya moyo n.k siku hizi hupelekwa kwa sangoma kwa Baraka za akina Abbas Kandoro na serikali nzima!
0786 324 074





No comments:

Post a Comment