Monday, July 22, 2013

MAGUFULI JEMBE BWANA

  Kweli Yahya Bilal, Dk.Magufuli 'Jembe'Bwana!
       Na conges mramba,Mwanza
NI JANUARI mwaka huu wa 2013, huko Uwanja wa ndege wa Mwanza.
Magufuli anafika huko kukagua miradi ya ujenzi na kuanza kuwachambua wazembe kama ilivyo kawaida yake!


WAZIRI WA UJENZI,John Pombe Magufuli,  ‘alimgonga’kiaina Waziri wa Uchukuzi,Dk.Harrison Mwakyembe,kuhusu mkandarasi kuchelewesha ujenzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza.
Dk.Magufuli, alifika Mwanza Januari 10 mwaka huu, na kukagua barabara ya kutoka Nyakato National kwenda Buswelu,itakayotumika baada ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza kuanza.
Ijumaa,Januari 11, mwaka huu 2013,Dk.Magufuli akafika uwanja wa ndege wa Mwanza,ili kukagua barabara iendayo Igombe,inayopita mita chache kutoka unapoanzia uwanja huo na kukuta mkandarasi hajaanza ujenzi; na wala hakukuwa na vifaa vilivyoletwa kuanza ujenzi huo.
Awali,kulikuwa na malalamiko kutoka kwa mkandarasi kwamba,Wizara ya Ujenzi ilikuwa ikikwamisha kuanza kwa ujenzi wa uwanja wa ndege,kwa kushindwa kuifunga barabara hiyo ya Igombe inayopita eneo ambalo  limo ndani ya ramani mpya ya uwanja huo.
Magufuli, alipoona hakuna dalili za kuanza kwa ujenzi wa uwanja huo,wakati tayari wizara yake ikilalamikiwa kwa kushindwa kuifunga barabara ipitayo ndani ya eneo la mradi wa ujenzi, akaja juu:
“Kwani barabara hii ya kwenda Igombe inamzuia nini Mkandarasi huyu kuanza ujenzi wa uwanja?
 Mkandarasi huyu tayari amelipwa malipo ya awali shilingi bilioni 8; angekwisha ‘clear site’ lakini hakuna alichofanya, wala hajaanza kupanua zile mita 500 za runway inayopanuliwa; na anasingizia kufungwa barabara!” Magufuli alisema.
Akasisitiza kuwa hawezi kuifunga barabara ya Igombe hadi mkandarasi huyo aanze kujenga uwanja huo.
Barabara itokayo katikati ya Jiji hili kwenda Igombe,hupita kandoni mwa uwanja wa ndege unaopanuliwa ili kufikia viwango wa kimataifa.Habari zilizolifikia gazeti hili zinasema,Mkandarasi anayejenga uwanja huo, Beijing Construction Engineering Group(BCEG) alikuwa amesaini mkataba tangu mwezi Juni mwaka jana,na muda wa kusafirisha vifaa(mobilizing period) wa miezi mitatu ulipita bila kuleta vifaa eneo la mradi, kwa sababu vifaa vilikuwa vingali kisiwani Zanzibar.
Kufuatia hali hiyo,Dk.Magufuli akataka maelezo kutoka BRELA,ikiwa BCEG walikuwa wamesajiliwa,na kama walikuwa na uzoefu.
Mwakilishi kutoka BRELA,akamwambia Dk.Magufuli kuwa kampuni hiyo kutoka Uchina ilisajiliwa miaka mine iliyopita,na ilikuwa imejenga uwanja wa Taifa,Dar es salaam.
“Okay,sitaifunga barabara hii,kwani inawahudumia hata akina mama wanaotaka kujifungua hospitalini.Nitafungaje barabara halafu akina mama wajifungulie barabarani hapa eti kwa sababu barabara imefungwa,wakati hata vifaa,hata toroli halijaletwa hapa ili kuanza ujenzi?”,Magufuli alisaili.
Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza uko chini ya Wizara ya Uchukuzi ya Dk.Harrison Mwakyembe,lakini Magufuli akamwambia Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi,Eng.Omar Chambo, “Miezi mitatu ya ‘mobilization’ imepita,mkataba ulisainiwa Juni mwaka jana,leo ni miezi saba hakuna kinachoendelea hapa, halafu anasema kinachomkwamisha kuanza ujenzi ni barabara hii! Sasa niifunge basi,tuone kama ataanza ujenzi wakati hana vifaa,hakuna hata  tingatinga, hata toroli!” alisema Magufuli,huku akiuliza, “Injinia Mshauri(consultant) yupo wapi?”
Akatokea mbele zake.
Magufuli akampiga maswali kama alikuwa na uzoefu wa kazi. Consultant huyo toka Zambia, akajaribu kujitetea. Magufuli akamwambia kwa kimombo: “Make sure not to compromise with that bogus Contractor… message has sent and delivered!”,
Kwamba huyo injinia toka Zambia aangalie asikubaliane na uzembe huo, akasema tena kwa umombo, “You may have a bogus contractor, but you must be very tough, otherwise this may be the last job in           East Africa”, kwamba awe makini la sivyo hii ndiyo itakuwa mara ya mwisho kufanya kazi hapa Afrika ya Mashariki!
Wakati Magufuli akimcharukia Mkandarasi huyo na mshauri wake toka Zambia, akatangaza kufungwa barabara hiyo pindi ujenzi wa uwanja ukianza.
Akasema,serikali tangu mwaka 2008 imewatimua makandarasi wazembe wanaoshindwa kuzingatia masharti ya mikataba.
Uwanja wa ndege wa Mwanza unapanuliwa kufika viwango vya kimabara kwa gharama ya shilingi bilioni 105 zinazotolewa na serikali pamoja na Benki ya Waarabu ya Maendeleo(The Arab Bank for Economic Development of Africa, BADEA).
Hatua hiyo ya Magufuli kumcharukia mkandarasi huyo imetafsiriwa kuwa ilikuwaa ‘kugongana’ na waziri Mwakyembe hadharani.
Utakapopanuliwa,uwanja huo utakuwa na njia ya kurukia yenye urefu wa mita 3,700 badala ya ilivyo sasa mita 3,300.
Utakuwa na jingo jipya la kuongozea ndege jirani na kilima(Traffic control tower),jingo jipya la abiria,maegesho na maeneo mengine muhimu pamoja na sehemu ya mafuta ya ndege,ili ndege zinazotoka Mwanza kwenda Ulaya au Asia,zisilazimike kupitia Dar es salaam kunywa mafuta.
 
 
NILIMPIGIA kura Mgombea wa chama fulani, ili awe rais  wa Jamhuri  ya Muungano wa Jamhuri ya Muungano,katika uchaguzi uliopita, 2010.
Lakini, nimepata mashaka moyoni mwangu!
Sioni mgombea wa kupigia kura mwaka 2015.
Wagombea wengi,hawana ‘a certain unique qualities’ ni kelele tu.
Rais wa NCHI YANGU ubongoni mwangu mimi, anatakiwa asiwe na mke au mume, awe hivi muda wote awapo Ikulu, na asiwe na watoto wala jamaa,rafiki,mashemeji.
Rais Dikteta,mwenye akili nyingi kama Magufuli; na hana jamaa,lakini jamaa zake na watoto wake ni sisi raia wake.
Watoto wa rais ni nywele za kila raia wake!
Mwandishi,Mike Royko, wa Chicago Sun-Times, aliwahi kuandika jambo hili zamani sana, President’s family in everyone’s hair.
Nilikuwa nikimheshimu Rais Kikwete na hata Dk. Wilbrod Slaa,lakini...
  Siyo kwamba, Kikwete ni Rais mbaya; la hasha. Si kwamba amefanya kazi mbaya.
Nafurahishwa na  baadhi ya mambo na vitu vingi anavyofanya Rais wetu; lakini ningependa Tanzania iongozwe na Rais mwenye sifa mbadala, ambazo hazijawahi kuwepo.
Nawaheshimu viongozi wa Kambi ya Upinzani, na kazi njema waliyofanya,ya kuikosoa serikali hii ya Chama cha Mapinduzi, ambayo ilishaanza kuota mapembe.
Hata hivyo, sijaona mgombea mwenye sifa za kutosha kuwa Rais wa TANZANIA NINAYOITAKA. Naam, Tanzania ya kesho niitakayo mimi lazima iongozwe na Rais asiye na watoto, asiye na mke,asiye na ndugu wala jamaa!
 Isipokuwa,ndugu,mke na jamaa zake tuwe sisi Watanzania kwa ujumla wetu,na Rais atulee mithili ya nywele zake kichwani!
   Ningependa sasa Tanzania iongozwe na Rais mwenye sifa za pekee, ili kuondokana na majanga kama haya ya viongozi kuendesha Biashara zao(japo halali) wakiwa Ikulu.
Naam, namtaka Rais ambaye ana sifa ambazo Kikwete hana!
 Hata Slaa na wanasiasa wengine kama Prof Lipumba hawana sifa ninazotaka!
   Nimeorodhesha hapa baadhi ya sifa ninazotaka Rais mpya baada ya Kikwete awe nazo:
Rais asiwe na mke, yaani awe mseja; na awe hivyo kipindi chote cha kuwa  kwake Ikulu yetu ya Magogoni, Dar es salaam !
 
   Pili, Rais atakayekuja baada ya Mhula wa Kikwete kumalizika mwaka 2015, awe yatima. Hatutaki marais wenye wake,watakaojaza mashemeji Ikulu!
Rais asiyekuwa na ndugu na jamaa wenye madhambi yanayoigubika nchi kwa kashfa; tena kashfa zenyewe kubwa zinazopamba kurasa za mbele za magazeti. Tumeshochwa na kashfa za wake na watoto wa vigogo, ambao pengine huua raia kwa risasi,lakini polisi hugwaya kuwatia mbaroni.
  Naam. Rais asiye na mke anayepenyeza pua yake katika masuala ya uongozi wan chi, wakati hakuna aliyempigia kura kufanya hivyo!

Rais mwenye mke ambaye anafungua makampuni yanayoendesha biashara pengine bila kulipa kodi.
 Mke wa Rais(First Lady) ambaye atapewa leseni na kukopeshwa fedha na mabenki kwa kasi, ili kufanya biashara kubwa kubwa, akijidai mjasiliamali.Kumbe,hata kodi halipi?
Rais asiwe na watoto ambao wanatajirika haraka haraka,baba yao anapokuwa Ikulu,wakati sisi raia tunahangaika!
    Lazima Tanzania yenye watu kama Milioni 44.9  iwe na Rais mwenye sifa za pekee, kuliko Benjamin William Mkapa, au Jakaya Kikwete.
Kuliko Dk.Slaa,Mbowe, Prof.Lipumba, ama wanaotajwa siku hizi,akina Magufuli,Membe,Mwakyembe,Lowassa n.k
 
Nataka Rais awe Mwenye hekima, mtu wa haki, mwenye akili.
Lakini, hana familia, hana jamaa wa kumharibu akili awapo Ikulu pale.Hana mashemeji.
Rais ambaye familia yake ni sisi Watanzania, na awe anatutunza mithili ya mboni ya jicho lake.
   Nimewahi kusikia tetesi za wake za Marais wastaafu, jamaa zao na watoto wao kuitumia vibaya ikulu kufanya biashara.
Nakiri, sijawahi kusikia tetesi za Mjane wa Hayati Mwalimu, Mama Maria Nyerere kutumia Ikulu kufanya biashara. Hata hivyo, simpendi Rais kama Nyerere,najua familia yake haiwezi kuwa waadilifu na wajamaa tena.
    Tetesi kwamba Benjamin Mkapa na Mama Anna Mkapa waliendesha kampuni yao , ANBEN wakiwa Ikulu, zinanivuruga akili.
Biashara hiyo ya Mkapa na Mama Anna, iwe halali au haramu, si hoja kwangu.
Lakini, napendekeza Tanzania isiwe na Marais wenye familia zinazowasukuma kufanya biashara mapema wakiwa Ikulu, ili kukimbia umasikini!
Nimesikia tetesi za utajiri wa watoto wa  mararais kama Kikwete, na Mkapa! umepatikana haraka!
    Wapo marais waaminifu na ndugu zao na watoto wao ni waaminifu; hawaitumii vibaya Ikulu.
Lakini, hatuhitaji sasa Rais mwenye mke,watoto,ndugu na jamaa na familia.
   Kadhalika, wapo wake wabaya wa marais  wenye wapambe, ndugu na jamaa wanaowashauri vibaya ili kujinufaisha na Ikulu. Wake, jamaa, wapambe na ndugu hawa nao hujigeuza maofisa wa serikali.
   Nani aliyewachagua kufanya chochote?
Nani aliwateua kuwa na sauti hadi kuwafokea mawaziri?
Unakumbuka Kenya, Lucy Kibaki aliwahi kuwachapa makonde maofisa wa serikali na kubomoa makompyuta na magazeti?
Kama ni hivyo, basi tungepewa nafasi ya kuwapigia kura hawa jamaa za marais, na wake zao  kabla hawajaingia Ikulu.
   Au, kwa sababu ndugu yao anapoingia Ikulu, wao hujigeuza ‘Mabalozi’ ama ‘Wabunge’ Fulani, basi wangepelekwa kula kiapo mahakamani, kwamba hawataitumia Ikulu kwa maslahi binafsi kipindi chote cha Bwana, Bibi, Mjomba au Shemeji yao, anapokuwa Ikulu.
   Leo, tunashuhudia mbio kali za watoto wa vigogo kutaka kuwania madaraka. Sisemi kwamba watoto wa wakubwa hawana haki ya kuwania madaraka, la hasha!
Wawe watoto wa wakubwa wenye Visheni; waachane na hadithi za kurithi damu za uchifu wenye falsafa ya kurithishana madaraka.
    Siasa si maneno matupu majukwaani.
 Ni kuzifanya sera zizae maendeleo ya watu. Je, watoto wa vigogo wanaosaka madaraka kwa udi na uvumba, kupitia vyama Tawala, wanayo Visheni hii?
    Au,wanawania madaraka  ‘kutetea’ madhambi ya baba zao pindi wanapomaliza mhula wao, baada ya kushindwa kubadili Katiba ili kurefusha muda wa kusalia madarakani?
   Licha ya wake za marais kudaiwa kufanya biashara ama kufungua vikampuni visivyotozwa kodi wakiwa Ikulu, watoto wao wamekuwa wakiwasaidia baba  au mama zao kutawala kwa mabavu. Wamekuwa wakishiriki kuwatesa raia na kukiuka Haki za Binadamu.
    Rais wa zamani wa Liberia, Charles Ghankay Taylor ambaye juzi amefungwa London miaka 50 kufuatia mashtaka ya Uhalifu wa kivita  huko The Hague, Uholanzi, mtoto wake, Charles Mc Arthur Emmanuel, au Charles Taylor Jr; ambaye Liberia alifahamika sana kama, Roy Belfast Jr, alitiwa mbaroni Desemba 15 mwaka 2005, akafunguliwa kesi mbili.
   Alitiwa mbaroni huko Miami , Marekani kwa kosa la kuwatesa kinyama waliompinga baba yake, na pia alikuwa na kesi ya kughushi Hati ya kusafiria.
   Ghankay Taylor, ambaye sasa amefungwa jela, na mahakama ya  The Hague, alishirikiana na rafikiye, Foday Sankoh, wa kikundi cha RUF kufanya unyama Sierra Leone na kuwauzia waasi hao silaha kwa kubadilishana na almasi.
    Licha ya kuwepo kwa tetesi za wake za marais kuingilia mambo ya serikali, kuwafokea mawaziri na hata kuwatwanga makofi waandishi wa habari hapa Afrika, watoto wa Marais pia wanatuhumiwa kuhusika na kashfa nzito.
Wanakuwa matajiri upesi bila kujua mitaji ya biashara walipata wapi?
    Gideon Moi, mtoto wa Rais wa zamani wa Kenya , Mzee Moi, alikuwa na tuhuma za kuhusika katika kashfa anuai za ufisadi nchini humo. Wengine, wakiwemo watoto wa wakubwa wa Dunia hii, wanatuhumiwa kubwia unga, kuuza ama kuvuta bangi na kuendesha biashara haramu hata katika Vyuo vikuu, lakini kwa sababu ya upendeleo, woga au kujikomba, vyombo vya Usalama hujikuta vikishindwa kuwachukulia hatua.
Mtoto wa Makamu wa Rais wa Marekani, AlGore, aliwahi kutiwa mbaroni kwa tuhuma za madawa ya kulevya.
   Hata kama  watoto hawa wa wakubwa waliua, au hata kama walijeruhi ama kutaharukisha umma, huachiwa mara moja, wasiyaone magereza!
   Mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Bi Margaret Thatcher(86), Mark Thatcher(60) lituhumiwa kuendesha biashara haramu na kufanya uhaini.
   Sir Mark Thatcher, mwenye vituko vya “Front Page” katika magazeti, aliwahi kupotea katika Jangwa la Sahara . Alipotea kwa siku kadhaa, wakati akishiriki Mashindano ya Paris-Dakar( Senegal ) Rally, akasababisha Bi Thatcher kuangua kilio hadharani, wakati akiwa Waziri Mkuu!
    Margaret Thatcher, alikuwa Waziri Mkuu wa Uingereza tangu mwaka 1979 hadi 1990. Lakini mtoto wake huyo aliwahi kutiwa mbaroni na polisi wa Afrika Kusini kwa tuhuma za kuongoza njama za kupindua serikali ya Guinea ya Ikweta.
    Ametiwa mbaroni na vikosi vya usalama mahali pengi Afrika; hata Zimbabwe . Polisi wa Afrika Kusini walisema, walikuwa na ushahidi wa kutumainiwa, kwamba Mark Thatcher aliwapa fedha waasi wa Guinea ya Ikweta, ili wampindue Brigedia Jenerali Mstaafu, Teodoro Nguema Mbosongo, Rais wa Baraza la Kijeshi la nchi hiyo, aliyedaiwa kuvunja Haki za Binadamu.
   Guinea ya Ikweta ni ya tatu Afrika kwa kuzalisha mafuta kwa wingi. Pengine, Mark anayetuhumiwa hata kuhusika katika biashara haramu ya silaha, alitaka mafuta ya nchi hiyo. Naam, hao ndiyo watoto wa wakubwa.
   Hata hivyo, wapo watoto wa viongozi waliopata kuwa viongozi wazuri. Waziri Mkuu wa zamani wa India , Indira Ghandhi, alikuwa Binti wa Waziri Mkuu wa Kwanza wa India , Jawaharlal Nehru. Baadaye, Sanjay na Marehemu Rajiv Ghandi nao wakafuata nyayo.
    John Quincy Adams aliyekuwa Rais wa Marekani 1825-1829, alikuwa mtoto wa Rais John Adams aliyetawala Marekani mwaka 1791 hadi 1801. Adams alikuwa Rais wa pili baada ya George Washington.
    Yupo George W.Bush ambaye baba yake George  Herbert Walker Bush, alikuwa rais miaka ya 90.
Nduguze, kama Jeb Bush ni viongozi; ni wanasiasa maarufu. Hata hivyo, katika orodha, wapo wengi viongozi watoto wa viongozi kama akina Sir Mark Thatcher  wenye tuhuma kama wahaini, wezi, wauza unga na wahujumu uchumi, wao na wapambe wao, lakini hawakamatwi wala kuhojiwa!
    Wako akina Roy Belfast Jr. wanaoghushi hati mbalimbali na  kufanya biashara haramu na halali, wanaotesa wapinzani wa serikali za baba zao, ambao pia hugeuza Ikulu kuwa ‘mapango’ ya wanyang’anyi ama ‘Mungiki’ wanao ifanyia jamii ugaidi mkubwa.
   Hayati Mwalimu Nyerere aliwahi kuwaonya watu kuiogopa Ikulu. Ikulu ni mahali Patakatifu. Si mahali pa kufanyia biashara hata ziwe halali na nyeupe kama sufi.
Rais anapoboronga, ama mkewe, jamaa au shemeji zake wanapoendesha magendo ikulu(Doing Business from Ikulu), ndipo harakati za kutafuta warithi huanza!
    Akina Umaru Yar’ Adua wa Nigeria wametafutwa na akina Obasanjo mara nyingi sana kupitia kitu ambacho si Uchaguzi, bali unyafuzi na Uchafuzi Mkuu wa Haki, Demokrasia na Uhuru Afrika!
    Ni kwa sababu hii, ningependekeza wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu, angetazamwa Mgombea ambaye jamaa, wapambe, rafiki, mke na watoto wake hawataiabisha ikulu kwa magendo, vituko, skandali na biashara zisizolipiwa kodi.
     Kama watoto, wake na wapambe wa Rais wangepelekwa Bungeni kwanza kuthibitishwa na kula viapo mahakamani, basi hofu kama ya Rais Jakaya Kikwete ya kumchunguza mtangulizi wake, isingekuwepo. Hofu ya kutafuta kubadili katiba isingekuwepo, kama wake, watoto na jamaa wa Rais wangedhibitiwa na Bunge au Mahakama.
    Lakini, pamoja na haya yote, ili kuepuka Marais kufanya Biashara Ikulu, napendekeza Tanzania ingekuwa na Rais Mseja, lakini asiye mzinzi wa kukwapua wake za raia wake; asiyekaribisha machangudoa Ikulu na kuitia unajisi nchi, rais mjane asiye na familia ya kumtia majaribuni; na yatima ambaye baba, mama na watoto wake ni sisi raia wake.
Nikijadili, agenda 2015 katika televisheni ya Star, nikamfananisha mtu Dikteta ninayemtaka kama Magufuli,kidogo!!
Kosa lake aliwahi kujitia doa katika nyumba za serikali wakati wa Awamu ya tatu,lakini Magufuli 'Jembe' kali Bwana!!
   0713 324 074
www.congesmrambatoday.blogspot,com
 
 
 
 
 

No comments:

Post a Comment