Monday, July 22, 2013

MISRI NA DEMOKRASIA YA AFRIKA

KUNA masuala machache tunayofanana na Misri.
Msri na mataifa ya Waafrika Weusi,tunasafiri katika barabara moja kurejea katika utumwa wa kidini,kiuchumi,kitamaduni na kisiasa.
Bahati mbaya sana!
Wakati mataifa ya rasilimali nyingi yanarejea katika utumwa,wananchi wake wana kiu ya mabadiliko ya serikali zao,mabadiliko ya siasa na kijamii pasipo kujua mabadiko haya yana athari gani kwao?
Watu wengi katika Afrika wana kiu ya maisha bora pasipo kujua atayaleta shetani ama mfadhili wa aina gani! Ufadhili. Kila kitu ufadhili,hakuna ujamaa na kujitegemea tena.
Matokeo yake Afrika inakwenda kasi kurejea utumwani,inarejea katika mapinduzi baada ya mapinduzi,yawe ya raia dhidi ya serikali, ya wanajeshi dhidi ya serikali za kiraia, ama jeshi na raia kwa upande mmoja dhidi serikali za kiraia kama ilivyotokea Misri.
Naam, hii huitwa struggle for freedom, harakati ambazo sasa ni za uhuru ndani ya nchi huru,uhuru dhidi ya uhuru bandia ili kurejea katika ukoloni.
Uhuru wa kwanza(1950-1970) ulidhaniwa ungeboresha uchumi,siasa na jamii ikashindikana,leo tunasema ilikuwa uhuru wa kuondoa Wakolobi Wazungu ili waingie wakoloni Weusi!
Serikali za vyama vya uhuru zilipambana na ukoloni mamboleo ukashindwa kufikia malengo.Rasilimali za nchi hazikugawanywa vizuri.Kada ya watawala walijipa kipaumbele,wakasaua tabaka la watwana,walalahoi.
Tutaondokaje katika shida hii,vijana sasa wakipata ufadhili toka nje,wanataka kununua bunduki ili kupambana kwa lengo la kujikomboa!
Bunduki na fedha kutoka Magharibi,ili kujikomboa dhidi ya Mkoloni Mweusi! Hakuna anayejali matokeo ya Wazungu kufadhili vita na fujo Afrika,atakuja nani kutawala?
Swali,tukipigana vita kali kuondosha serikali za vyama vya uhuru kwa msaada wa Mzungu,tutamlipa nini kama siyo rasilimali hizo anazochukua sasa kupitia uwekezaji?
Ni kweli mafisadi na wakoloni weusi hutorosha mali kwenda Ulaya na Marekani,sawa. Tukiwaondoa kwa vita kama Tunisia,Misri,Libya n.k tunawalipa nini wafadhili wetu? Au tunadhani wanatupenda sana?
Tufikiri vizuri,njia bora ya uhuru wa kweli.Ndiyo tunaona vyama vya siasa vinatamani kuanzisha majeshi eti kujilinda. Ukweli ni kuanzisha majeshi ili kupambana kukamata dola na rasilimali.
Ukichunguza kwa makini unaona sote tunakumbatia utegemezi wa Metropolitan Power kufanikisha malengo ya kwenda au kusalia Ikulu,kwa lengo la kufaidi rasilimali na madaraka!
Vyama halisi vya kumkomboa Mwafrika sasa havipo.tuambizane ukweli,kuna vyama vya malengo tofauti ya kushika dola na wala siyo kuleta ukombozi wa kweli wa Bara hili na watu wake kutoka kwa wakoloni mamboleo.
Mataifa haya yanayojidai sasa wafadhili na wawekezaji hayajasahau nia yao ya kuitawala Afrika na kujichotea rasilimali na rasilimali watu.
Ubinafsishaji ni sera za IMF na Benki ya Dunia(WB) zilizoanzishwa baada ya Vita kuu ya Pili ya Dunia.
Sasa,ni vita ya sisi kwa sisi,kila mtu na staili yake ya kumpelekea Mzungu rasilimali na madini,mafuta,gesi,wanyamapori,mazao ya kilimo n.k
Umwagaji wa damu unatumiwa sasa ili kuuza bunduki na kubadilishana kwa madini ama nishati na nguvu kazi ya chee.
Watu wanaomba vita viendelee Afrika ili hata hao wanaotaka kuanzisha majeshi katika vyama wagawane maeneo ya rasilimali na kuuza Ulaya na Marekani,kama wanavyofanya Waasi wa Uganda na Rwanda huko Congo(DRC).
Ni vita kama vya RUF dhidi ya serikali ya Sierra Leone miaka ya 1990-2000 ili kuchota almasi kwa damu ya raia.
Nataka kuseka kwamba ‘social revolution’ siyo kuunda jeshi ama kuchukua silaha na kuuana! Njia sahihi ni kulinda maslahi ya taifa nay a kila mwananchi kwa njia za haki bila kunyang’anya maisha ya watu ama umwagaji damu.
Hili la kwanza,Pili National Interests siyo kupambana jino kwa jino kama Chad,Misri,Libya.Mali n.k
Hizi dola kubwa,Urusi,Uchina,Marekani,Uingereza,Ufaransa n.k wakati Fulani hukubaliana kutugombanisha ili waendelee kuchota rasilimali na kufanya biashara ya bunduki kwa kubadilishana na mafuta,pembe za ndovu,dhahabu, almasi n.k
Kama hujui hili,jiulize silaha kwa waasi wa Congo hutoka wapi? Nani hulipa mishahara ya Waasi misituni? Nani huwapelekea maji na mafuta?
Kama hujui,ni kwamba Waasi hukamata eneo lenye manufaa ya biashara haramu ya magendo.Mataifa makubwa lao moja-kutuchonganisha.
Ni hapa ninapoona haja ya Waafrika kuwa na vyama vya siasa kwa lengo la kushindana kwa sera nzuri na kamwe siyo kugombania madaraka ya kushika dola ili kugawana rasilimali.
Hiki ndicho chanzo cha mapinduzi mapya katika Afrika.
Misaada ya Ulaya, “The Myth of Aid” katika vyama hivi vya siasa ndiyo nguvu yao ya kuleta vita na kuanzisha majeshi mapya ili kuwafunza vijana vita,ili kufikia malengo ya kushika dola,na kamwe si kumkomboa Mwafrika!
Hakuna ajenda ya kuondoa rasilimali zetu mikononi mwa wageni ili kujikomboa, ni kupambana kwa namna yoyote-hata kwa gharama za damu za wananchi-ili kushika ama kusalia madarakani ili kujineemesha!
Hakuna jipya katika vyama vyenu hivi vya siasa.Ajenda za ukombozi za kweli za akina Nyerere,Mandela na wenzake hakuna siku hizi.
Adui yetu Mkoloni,pande zote zimemgeuza Mfadhili na mshauri katika medani ya vita vya umwagaji damu.Akitoka Mwingereza kumfadhili Amin kuua watu anakuja Mrusi na kambi yake!
Hakuna jipya.Mursi na Adly Mansour wote wana wafadhili wao,kama si Warusi ni Waingereza na Wamarekani na wote lengo lao ni rasilimali na cheap labour kwa wananchi wetu.
Ni kufuatia hali hii Afrika bado haiko huru na inakwenda njia isiyo sahihi,watu wanaposhangilia,vyama siyo masihi.
Bungeni,vyama vya siasa na NGOs kumejaa mafisadi wanapaza sauti kusema serikali ni mafisadi.
Utashangaa kuona vyama vya waandishi wa habari mikoa na NGO za wajanja wanaojidai vyama vya wanahabari,wajidai kukemea ufisadi, huku wenye viti wanapowaita nyumba ndogo zao na ndugu zao kugawana posho za Pres conference!
Watu wanapandia katika ulaji kwa migongo ya wanahabari,wanunua magari na kuwanunulia nyumbandogo magari ya fahari huku wakiimba, “Mafisadi!”
Kawimbo ‘Mafisadi’ huibwa na watu wanaonuka mithili ya kwapa la shetani!
Hii ndiyo tabu! Hatujui adui yetu ni nani? Shetani naye anamtukana Shetani! Mwisho tutamalizana tusipojisahihisha ili kujua adui yetu ni nani? Ni rushwa,ni ufisadi na kila fisadi katika jamii,na siyo waliomo serikalini tu,wengine tunao hata humu kweye habari.
Akitoka fisadi anaandaa mkewe naye kurithi NGO na serikali ziko hivyo.Museveni-Janet-Muhoozi Trinity Power.
Hawa madikteta wako kila mahali siyo serikalini tu, bahati mbaya sana hawajui kuwa hawajui kwamba ni mafisadi na waporaji wa haki za wenzao.Wanadhani mafisadi na madikteta ni wa serikalini tu,hata vyama vya siasa ni mali za watu Fulani,mkikosana wanakutimua!
Wanachama hawana nguvu wala sauti.Hakuna full democratic liberties.Mtoto,mjukuu,shangazi, ndiyo huruhusiwa kukamata mamlaka.Kuongoza vyama.
Akina Nasser,Obote,Nyerere,Nkrumah walijaribu kujenga usawa wakashindwa,waliondoka wakaingia akina Amin Dada katika kila Nyanja ya maisha. Kinachoendelea ni uongo wa propaganda,na hakuna hatua kuelekea uhuru wa Mwafrika! Upendeleo na unyama. Hakuna jipya.
Ni kumalizana,kukanyagana,kuandamana kila asubuhi. Utumwa ni utumwa,hauna rangi!
Itaendelea
0786 324 074
 

No comments:

Post a Comment