Monday, June 24, 2013

BURIANI MANDELA

                           
Utawala wa Makaburu(Boers)ulikumbatiwa na Uingereza na Marekani;wakati watu zaidi ya 14,000 (Weusi)walipouliwa huko Zulu,katika miaka ya 1980.
Tumeona Mobutu akisaidiwa na mataifa haya ambayo siku hizi hujidai ‘Masihi’ hapa duniani,na huimba demokrasia na Haki za Binadamu kwa midomo bila vitendo.
Mobutu,na hawa,waliwasaidia Waasi wa Angola kukipinga Chama cha Ukombozi, Popular Movement for the Liberation of Angola(MPLA),uhuru usipatikane kutoka kwa Wareno,hadi nchi ikabaki vitani kwa muda mrefu.
Mobutu na hawa rafiki zake, Ungereza na Marekani, walimsaidia Jonas Malheiro Savimbi na Chama chake cha Unita, kilichopinga uhuru wa Angola.
Tumeona harakati za uhuru nchini Afrika ya Kusini chini ya African National Congress (ANC) zikiwa zimeharamishwa na utawala dhalimu sana wa Makaburu hadi Rais De Clerk alipokuja kuondoa marufuku hiyo Feburuari 1990
“Tata”Mandela aliachiwa huru kutoka Greza la Victor Verster, lililopo Paarl Feburuari 11 mwaka 1990. Ni tukio la kihistoria kuachiwa kwa Mandela; ni kama Afrika ilipata uhuru mwaka 199
Mtu huyu, “Tata” Mandela,alitangaza msamaha kwa Makaburu waliomtesa; ikaunfdwa Tume ya Ukweli na Maridhiano(THE TRUTH COMMISSION) iliyoongozwa na Askofu Desmond Tutu.
Mandela alikiri chama chake (ANC) kuunda tawi la jeshi(Umkontho we Sizwe) kwa nia ya kujilinda na kujihami dhidi ya siasa za ubaguzi wa rangi; siasa zilizoandamana na dhuluma na mauaji ya kinyama dhidi ya wazalendo na harakati za ukombozi.
Mandela na De Clerk walitunukiwa baadaye tuzo ya Nobel ya Amani,mwaka 1993.Aprili mwaka huo 1993 ndipo Mpigania uhuru Chris Hanni alipouliwa na utawala wa Makaburu,rafiki wa Uingereza na Marekani.
Mandela, ameishi siku zote kama Mwafrika halisi; akachaguliwa kuwa rais mwaka 1994   akiwa na umri wa miaka 77-na alistaafu mwaka 1999 akamwachia kiti Thabo Mvuyelwa Mbeki,mmoja wa wana wa mashujaa wa mapambano dhidi ya Kaburu jeuri.
ANC kilishinda uchaguzi wa 1994 kwa asilimia 62 ya kura.Mandela aliapishwa kuwa rais wa Kwanza Mweusi Mei 10,mwaka 1994,wakati Kiongozi wa National Party, de Clerk akiambulia Umakamu wa Kwanza wa rais;wakati Thabo Mbeki alipopewa Umakamu wa Pili katika serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Naam, tunamkumbuka ‘Tata’Mandela kwa mashati yake ya Batiki. Ama ‘Mandela Shirts’ yanayovaliwa siku hizi hata na akina Rais Jakaya Kikwete.
Uchaguzi wa kwanza huru Afrika ya Kusini ulifanyika Aprili 26-29,mwaka 1994,ANC kikapata asilimia 62,National Party cha Makaburu kikapata asilimia 20.4.Inkhata Freedom Party cha Chifu Mangusuthu Butelezi kilipata asilimia 10.5.
‘Tata’ Mandela alipata kuoa mara tatu; ni baba wa watoto sita,wajukuu 22 na vitukuu vingi. Mmoja wa wajukuu zake ni Chifu Mandla Mandela.
Mzee huyu kipenzi cha Afrika alifunga ndoa ya kwanza na Evelyn Ntoko Mase kutoka kwao Mandela huko Transkei.Walikutana Johannesburg-walizaa wavulana wawili,Thembikile ama Thembi mwaka 1946,Magkatho alizaliwa 1950 na wasichana wawwili waliopewa jina moja,Makaziwe, “Maki” mmoja alizaliwa 1947 na mwingine 1953.Mwingine alifariki dunia kabla ya kufikisha umri wa mwaka mmoja.
Ndoa ya Mandela na Evelyn Mase ilivunjika baada ya miaka 13(mwaka 1957),Mandela alikuwa haonekani nyumbani kwa muda mrefu,akiwa ‘Msituni’katika harakati za Ukombozi,mama huyo na imani yake ya kilokole ya Mashahidi wa Jehova, aliamua kwenda zake,akaachana na Mandela.
Thembi, alifariki katika ajali  ya gari mwaka 1969 akiwa na miaka 25 wakati huo Mandela alikuwa selo, Robben Kisiwani.Hawa watoto walisoma shule moja,baadaye Evelyn alifariki dunia 2004.
Ndoa ya pili ya Mandela ni ya Winnie Madikizela-Mandela, huyu ‘Iron Lady’ kutoka Transkei.Watoto wa Mandela na Winnie ni wasichana wawili:Zenani au Zeni(Feburuari 4,1958) na Zindzishwa ama Zindzi aliyezaliwa 1960.
Walitengana Aprili 1992; mwaka 1996 waliachana kabisa.Juzi, Winnie alikwenda kumtembelea  Mandela hospitalini anakolazwa.
Kaka mkubwa wa Mfalme wa Swaziland,Mswati III,Prince Thumbumuzi Dlamini alimuoan Zenani mwaka 1973,na wanaisti Boston,Marekani.
Mwaka 1998,Mandela alimuoa Graca Machel nee Simbine wakati alipokuwa akiadhimisha ‘Birth Day’ ya 80.
Mwaka 2003,Cable News Network(CNN) walitangaza tanzia ya Mandela.Mwaka 2007 pia ‘wasela’walitangaza kifo cha Mandela,wakiwataka Wazungu kwenda kwao,la sivyo wangechinjwa!
Mtu huyu, ‘Tata’ Nelson Mandela ni kielelezo cha Mzalendo wa kweli,Mwanahalisi wa Afrika aliyeitwa ‘Gaidi’ na utawala wa Makaburu wa Waziri Mkuu PW Botha, aliyejiuzulu Agosti 14, mwaka 1989 ndipo akaingia De Clerk aliyemwachia huru Mandela.
 Utawala wa Makaburu uliua watu wengi,si Afrika Kusini tu bali hata Msumbiji walifanya njama na kumuua Samora Machel mwaka 1986.
Naam,namkumbuka ‘Tata’Mandela, ambaye namba yake ya jela ilikuwa 46664. Tunawakumbuka wanamapinduzi wa Afrika ambao wamemwaga damu wakipigania uhuru wa watu wao, si ulaji wa matumbo  yao kama watu wengine wanavyotaka kuitwa leo.
Namkumbuka Samora Mises Machel,John Garang de Mabior ‘ Chris Hani na wenzao.
Obama anapokuwa Dar es salaam wakati huu makala hii inapachapwa gazetini,nataka kumwambia kwamba aslani asiweze kusahau hujuma kama hizi na zile za Kanisa la Aglican,za kuwaweka mhuri wa moto mgongoni Waafrika wenzetu waliofanywa watumwa-The Transafrica Slave Trade-waliobandika mihuri ya society migongoni!
Napenda kumwambia Barak Hussein Onyango Obama,kwamba urais wake Marekani umekuja baada ya harakati za ukombozi za akina Mandela, Malcom X,Martin Luther King Jr, na wenzao ambao walijikuta wakiuliwa na Pentagon ama kufungwa  maisha kwa uhaini.
Wakati Obama anapojitia kushutumu tawala za kiimla, Authoritarian regimes, asisahau kwamba serikali ya nchi yake imekiuka haki za msingi za Weusi kwa kuwaunga mkono majambazi kama Savimbi,majeshi ya Makaburu,Wareno na makampuni ya kifisadi kuihujumu Afrika.
Nigeria kwa mfano, inasemwa Boko Haram wameua watu 1000 wakati ukweli ni kwamba hata makampuni ya mafuta ya Magharibi kama Elf,Agip, Royal/Dutch Shell,Chevron n.k wamehujumu raia wa Niger Delta,waliodai haki zao zama za utawala wa Dikteta Sani Abacha,ambaye wao walibeba sana kwenye mbeleko hadi akawaua akina Ken Saro-Wiwa.
Makampuni ya Marekani,Ufaransa na Uingereza yameua watu wangapi Kusini mwa Nigeria kulinganisha na Boko Haram? Zaidi ya dola bilioni 400 za mafuta zimeporwa na makampuni hayo tangu zama za uhuru hata sasa huko kwa Waogoni,Igbo,(Biafra) na Yoruba.
Obama, anapozungumza utawala bora na demokrasia ana maana gani kama makampuni ya Magharibi yanashiriki unyonyaji, na dhuluma hapa Afrika?
Itaendelea
0713 324 07
www.congesmrambatoday.blogspot.com







No comments:

Post a Comment