Tuesday, August 28, 2012

LEO NI JANA YA KESHO(2)


TUNAJADILI ikiwa yupo kiongozi mahiri wa siasa hapa duniani, anayewapenda wananchi kiasi cha kujitoa mhanga mithili ya mshumaa. 
Mshumaa,huwaangaza wengine huku ukijiteketeza wenyewe.
Mwandishi wa Kigiriki, Euripides, aliandika takriban millennia tatu zilizopita kwamba,Mfalme kijana mtanashati wa Thesaly aitwaye, Admetus aliugua.
Miungu ya Ugiriki(Ugiriki ni nchi ya masanamu ya miungu wengi) ikawaambia nduguze kuwa lazima Admetus afe, isipokuwa kama angepatikana mtu mwingine wa kufa badala yake.
Kwa Kiingereza mtu wa kufa badala ya mwingine ni “Substitute” ambaye kama angepatikana kufa badala ya Mfalme Admetus, angeweza kupona maradhi yake na kuendelea kuishi.
Wakaulizwa baba na mama yake kama walikuwa radhi kufa badala ya Admetus,wakakataa. Ndugu zake nao waliulizwa,wakakataa. Marafiki nao walisema, “Admetus, ni kijana mzuri; ni mfalme mzuri,lakini hakuna wa kufa badala yake!”
Mwisho wa siku, mkewe msichana mrembo sana aitwaye, Alcestis, akahiari kufa kwa niaba ya Admetus,kwa sababu alimpenda na alikuwa mtu mwema.
Baada ya kifo cha Alcestis, Mfalme Admetus alitambua ‘HASARA’ iliyomkuta ya kumkosa kipenzi chake, Alcestis aliyekuwa na upendo wa dhati kwake.
  Akamwombolezea ifuatavyo:
“Nitakulilia mpenzi wangu,siyo kwa mwaka mmoja au miwili;bai katika siku zote za maisha yangu,mwanamke uliyenipenda! Baba na mama walinichukia,walinipenda kwa maneno matupu,siyo kwa vitendo”, Admetus aliomboleza.
Nataka msomaji atambue kwamba, kumpenda mtu kwa maneno matupu siyo kumpenda-ni kumchukia.Upendo wa dhati siyo wa maneno matupu; ni vitendo kama alivyofanya Alcestis.
 Naam, “Love in words, not deeds” ni unafiki mtupu, siyo upendo,kama wanavyojidai siku hizi wanasiasa na wakoloni wetu wa zamani.
Nakusudia kuwaonya Waafrika wasiwe wepesi kulaghaiwa na wanasiasa na hata wakoloni wetu wa Ulaya na Marekani, kwamba wana upendo kwa wananchi-si kweli ni unafiki na ufalisayo mkubwa!
Hata hivyo,Katika Warumi 5:7   Profesa Paulo anasema, “Ni shida mtu kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema,kama Admetus.
Biblia, katika Warumi 5:8-10, inasema, “ Lakini,Yesu Kristo alikufa kwa ajili yetu,tulipokuwa tungali “ADUI” zake.Alitupatanisha na Mungu tulipokuwa tungai adui zake”(wenye dhambi ni adui wa Mungu).
Nataka kujifunza hapa kwamba, Biblia inatwambia kwamba UPENDO ni dhidi ya adui, ambaye kwa kawaida hawezi kuwa na faida yoyote-Upendo usio na faida!
Upendo wa Alcestis kwa Admetus siyo huu usio na faida,bali ni upendo wa mke kwa mumewe, “Philos’ au Philia-upendo wa familia,upendo wa kibinadamu wa kidugu-Brotherly Love.
Baba humpenda mama,mama humpenda baba, wazazi huwapenda watoto,hata mwingine hujitoa mhanga kuwaopoa motoni.Ndugu hupendana wao kwa wao n.k
 Upendo wa mtu kumpenda adui hata kuwa radhi kufa kwa niaba yake ni Agape kwa Kigiriki, Prof. Ibrahim Lipumba, Dk.Wilbroad Slaa au Rais Jakaya Kikwete, hawawezi kuwa na upendo wa jinsi hii, wala ule wa Alcestis kwa raia.
Tuambizane ukweli.Upendo wa kweli, “TRUE LOVE” Agape au Philos ni upendo wa mtu kuumia kwa ajili ya kumpatia mema mtu mwingine. Upendo wa Agape hauna faida, “suffers long and it thinks no evil”, hata kama unamwonyesha upendo huo jambazi au adui yako!
Tujiulize:Wanasiasa wetu hawa, viongozi wa sasa wanaweza kujitoa mhanga wafe kwa ajili yetu wananchi?
Wako tayari sisi raia tuishi maisha bora kuliko wao?Wako tayari kuuza mashangingi,suti zao, briefcase zao na rasilimali zao nyingine, ili sisi wapigakura wao tuishi maisha bora?
Mtu mbumbumbu anaweza kusema kwamba jibu la maswali haya ni Ndiyo! Haidhuru. Tumjadili Mpigania Haki za Weusi wa Marekani, Martin Luther King Junior.
Kabla ya kwenda kwa mtu huyu,tujisaili: Kwanini sisi masikini hatuna shule bora kwa ajili ya elimu ya watoto wetu? Kwanini hatuna zahanati,dawa,vifaa na hatuna hospitali?
 Kwanini sisi vijijini hatuna barabara wala huduma za jamii kama umeme,maji safi na salama n.k wakati wanasiasa hawa wao wana kila kitu?Wanatembeleaje magari ya Milioni 60 wakati sisi hatuna zahanati wala dawa?
Viongozi wa dini nao siku hizi wanatembelea magari ya fahari ya zaidi ya Bilioni 2, huku waumini wao wakiwa hawana hata makubazi miguuni! Wanaimba Upendo! Mungu ni Upendoo, aaameeen! Aibu tupu!!
Yawezekana mtu “kuthubutu” kufa kwa ajili ya mtu mwema kama Admetus-huu upendo huitwa,Philosterges, kwa Kigiriki.
Lakini, kama huna nasaba na mtu,humjui, naye ni adui yako na ukahiari kufa badala yake, ndiyo AGAPE.
Wapo watu wanakesha redioni na kwenye runinga wakiimba, “Nakupenda kama nyamachoma!” Huu siyo upendo, ni tamaa za ngono(sexual drive, sexual affections, sexual love)ambazo mwisho wa ngono,hakuna chochote,bali uchungu na majuto kwa aliyedanganyika.
Kumpenda mtu usiyemjua,usiyewahi kukutana naye na hana faida kwako,ni “Impartiality Love” upendo unaoitwa Agape ama Agapao kwa Kigiriki. Huu ndiyo upendo anaopaswa kuwa nao kiongozi wa siasa-kuwapenda wananchi asiojua hata majina yao,na wanaishi pembezoni kule,Masasi ama Saragana,Masinono na Bugwema,Musoma!
Siku hizi, tunasikia kwamba kiongozi Fulani anawapenda wananchi, hadi wananchi wanakubali kupigwa virungu,kupigwa machozi ama kupigwa risasi na polisi,kwa kutii shuruti zake hata kuwapiga mawe polisi wenye SMG!
Polisi wakizuia maandamano, kiongozi wa siasa akasema, Andamaneni, watu wanatii na kupoteza maisha! Hii ndiyo Agape, watu kumfia kiongozi, siyo?
Agape, siyo watu wafe kwa ajili yako ili uende Ikulu au uukwae ubunge ama madaraka Fulani. Agape ni wewe kiongozi ufe kwa ajili ya masikini usio na nasaba nao,ili kwa kifo chako wapate faida ya kukombolewa.
Tofautisha upendo wa Alcestis,Martin Luther King Junior, Yesu na hawa jamaa. Tafakarini.
Tunajadili upendo wa dhati.Viongozi wa siasa wanaonesha upendo huu kwa wananchi? Viongozi wa kidini wanawapenda kwa dhati waumini wao? Mbona wao wanakula na kushiba, wafuasi wao ni fukara?
Kwa nini rushwa na ufisadi kama kuna upendo katika mtego uitwao siasa? Kwanini mishahara ya wabunge na wafanyakazi iongezwe maradufu,halafu mazao ya wakulima yashuke bei kwa visingizio vya kushuka kwa thamani ya shilingi au mtikisiko wa uchumi duniani?
Kwa nini hawa ambao hawajulikani kwa wanasiasa na viongozi wetu(wakulima),mazao yao yanaposhuka bei,maisha yanapokuwa duni na hawana huduma za jamii,halafu tunawachochea wafanye vurugu,wafe kwenye maandamano yaliyopigwa marufuku na polisi,badaya ya kuwasaidia waishi,wanusurike kufa?
 Tuambizane ukweli.Wanasiasa wote ni ndizi-ni rangi moja na wamepinda! Msikubali wawatumie kama ngazi, wao wanaingia kula maisha,nyie mwabaki kupigwa jua na mvua.
Acha upambe, angalia maisha yako ni ya thamani kubwa. Kwanini umpige polisi kwa mawe wakati yeye ana SMG yenye risasi 30?
Nahimiza watu kuheshimu maisha yao,nahimiza watu kuheshimu mamlaka, nahimiza usamaria wema,nahimiza utii wa sheria bila shuruti na kuheshimiana sisi kwa sisi.
 Tusikubali viongozi wa siasa kutugawa kwa misingi Fulani ili tuanze kupigana.Tukipigana wao wana mbawa,sisi tunakufa na wake na watoto wetu wanateketea wakati wao huruka kwa ndege na kwenda zao!
Vita vya wenyewe kwa wenyewe Kenya,ni mfano mzuri kwetu.Waliokufa walikuwemo watoto wa Kibaki? Hapana. Walikuwemo wa William Rutto, ama wa Raila Amolo Odinga?
Watakuwemo wa Dk.Slaa au Kikwete na wenzake? Anzisha amani, acha ujinga.
ZBIGNIEW BZEZINSKI, alikuwa Mshauri wa Usalama wa Taifa, enzi za Rais Jimmy Carter wa Marekani.
Huyu,mtu mkubwa, wa Taifa babe sana hapa duniani ambalo husemwa lina demokrasia iliyopevuka,ndiye hasa anayetuhumiwa kusimamia mradi wa kutengeneza virusi vya Ukimwi,katika maabara za kijeshi huko kilomita 75 kutoka New York, mwaka 1975.
Naam,viongozi wakubwa ni wenye ‘madudu nakubwa’.Wenye mamlaka makubwa wana madhambi makubwa sana, kinachowaokoa ni uzuzu wa wafuasi wao kueneza propaganda kwamba hao viongozi wao siyo binadamu wa kawaida,bali malaika au miungu.
Watu wadogo, hasa viongozi wa Waafrika utaona wanasemwa walifanya upumbavu huu na ule! Utaona unyama unafanywa Afrika,utadhani Ulaya na Marekani ni mbinguni!
 Martin Luther King Junior, alitiliana saini muswada wa Uhuru kwa Weusi wa Marekani,Julai 3,mwaka 1964.Mkataba huo ulikuwa kati ya Dk. Luther King na Rais Lyndon Johnson, Martin Luther aliuawa na Pentagon,Makao Makuu ya Jeshi la Marekani mwaka 1968.
Huyu, alitoa maisha yake akipigania haki za watu wake, WEUSI wa Marekani, dhidi ya ubaguzi wa rangi.
Tabia hii ingalipo Marekani, na  Ulaya. Namwonya Rais Jakaya Kikwete awe macho na Uingereza, Marekani na Ufaransa.
Siku hizi wameanza kumtumia Joyce Banda,kutaka kuleta chokochoko Maziwa Makuu,vita vinapofumuka sisi kwa sisi,wao wachote rasilimali zetu na kuondoka. Nyuma ya Joyce Banda lazima wapo hawa wameona kunaweza kuwepo mafuta ama gesi, ili tuking’amua tuache kuwategemea!
Kama alivyosema manafalsafa wa Ugiriki, Salon, sheria zilizowekwa ni ‘utando wa Buibui’. Marekani hukiuka sheria na kwenda zao pasipo kunaswa na sheria hizo. Wewe ‘mdudu’ mdogo ukicheza unanaswa.
Angalia baadhi ya wadudu wadogo walionaswa katika “Spider’s Web” ni pamoja na akina Muammar al- Qaddafi,Saddam,Osama,Charles Taylor,Laurent Gbagbo n.k
Tumjadili kidogo Charles Ghankay Taylor.Ametumwa na Marekani kufanya unyama Sierra Leone wakaja kumwacha penye mataa.
Walimtorosha wenyewe gerezani huko Boston, akakimbilia Libya, akajifunza mbinu za medani za kijeshi, akasaidiwa kupindua serikali Liberia, akaanza ‘biashara’ ya kusaidiana na Revulutionary United Front(RUF) huko Sierra Leone, wakachukua almasi na kumpa Marekani, wakapewa bunduki!
 Mwisho wa siku, Taylor amekamatwa, amefunguliwa kesi akashinda makosa yote 11, Marekani wakalazimishwa afungwe miaka 50,tena Uingereza,ili abaki kimya gerezani maishani mwake, asipate kusema siri!
BAFFOR ANKOMAH,Mhariri wa jarida mahsusi la New African la Julai mwaka huu, katika safu yake ya “Baffour’s Beefs” amesema uovu wa Marekani na mataifa babe haya(Metropolitan Powers) ambao waliwashinikiza akina Louis Moreno Ocampo na Fatou Bensouda, kumkomesha kicha maji kama Charles Taylor.
Nataka kuwaonya viongozi wa Afrika,wanaotumiwa na Marekani,Ufaransa na Uingereza,kukoma kuihujumu Afrika,la sivyo wanaelekea mahali walipo Taylor,Gbagbo, Osama, Gaddafi n.k
Marekani hawana rafiki,rafiki ni rasilimali kwa maslahi ya Marekani, siyo Afrika!
 Nawaonya pia viongozi wa vyama vya siasa hapa Afrika.Wanapewa vijisenti na silaha ili wafanye vurugu,nchi zetu zisitawalike,mwisho wa siku ni hawa Marekani,Uingereza na Ufaransa watakaofaidika na vita vya Kunguru!
Wametoka Libya,Misri,Irak,Yemen na sasa wako mbioni kuiteka Syria,wakimaliza watakwenda Iran. Qatar,Kuwait,UAE,Lebanon,Bahrain kumetulia kwa kwa sababu wamekubali ‘unono’ uende Ulaya na Marekani! Ukipinga tu,unaoneshwa mtutu wa bunduki na unapelekwa kwenye utando wa bui bui utakaokunasa.
Sisi ni wadudu wadogo,nzi-kwenye ‘spider’s web’ hatuwezi kuvuka.Tando zote za buibui kama ICC huko Hague,ni mali yao.
Sasa jidanganye kwamba Marekani na Ulaya kuna demokrasia au haki za binadamu. Wewe naye binadamu,mtu mweusi?
Kamuulize Caster Semenya, au Samuel Eto’o.
Angalia madudu ya akina Nicolas Sarkozy huko Ufaransa, amefanya ufuska,uchafu akiwa rais. Angekuwa RG Mugabe au mwingine,ungesikia maneno.Raia wangeshawishiwa kuingia barabarani na kuchoma moto magari ya serikali,majengo na matairi barabarani,kwamba ndiyo, “PEOPLES POWER”!!
Ufaransa, ‘scandal’ za akina Sarkozy za kufanyisha watoto ngono, huko Thailand na Ufaransa eti ni ‘minor thing’, lakini viongozi kama Luiz Inancio da Silva wa Barazil watasemwa hawana elimu,ni washona viatu! Hawaongei kuwa uchumi wa Brazil ulipaa wakati wa Da Silva!
Wanaona sana akina Jacob Zuma Mushorozi na Mfalme Muswati III wa Swaziland kuona vimwana kila mwaka!
 Lakini, ufuska wa akina Silvio Berlusconi huko Italia ni ‘Minor thing’! Raia hawashawishiwi kuingia barabarani na mawe na hawalipwi mishahara huko kushika bunduki,kama Syria.
Sisi ‘Madodoki’tunalishwa kila pumba na kuanza kupigana sisi kwa sisi. Hatujui mwisho wake utakuwaje? Hatutazami kesho kwa kuchungulia historia ya hawa akina Charles Taylor,Jonas Savimbi,Mobutu, Hosni Mubarak  na vibaraka wengine walivyofanyiwa.
Nataka kusema kwamba,tujiepushe na Marekani na wanasiasa wa Afrika ambao leo Marekani na washirika wake wanawalipa posho kuja kufanya vurugu Afrika,ili tupigane sisi kwa sisi,wao wachukue rasilimali.
Kumbe hata mgogoro kati yetu na Malawi haufai kuishia kuwa vita vuya silaha,tunawanufaisha hawa majahili walioanza kuchochea vita kwa kujua Ziwa Nyasa kuna mafuta au gesi!
Nawashauri Waafrika kuachana na kulishwa ‘kasumba’ ya kikoloni. Tuanze kupendana sisi kwa sisi na kutatua matatizo yetu kwa amani,bila kuwaalika majahili hawa.
 Nawaonya viongozi wa siasa hapa Afrika na wapambe wao wanaopokea posho toka Ulaya na Marekani ili wawachochee vijana kufanya vurugu kwa kisingizio cha ufisadi, na kukosa ajira!
 Fikirini vizuri. Vita vikifumuka ndiyo mtaajiriwa kwa risasi na mizinga?Ndugu zenu wakifa ama mama zenu na wadogo zenu wakiwa wakimbizi,ndiyo mtapata ajira?
 Itaendelea
0786 324 074,0754 324 074
  
                   


No comments:

Post a Comment