Monday, August 27, 2012

LEO NI JANA YA KESHO(1)


                            
TAI NI NDEGE, anayeruka juu angani, umbali wa futi 10,000 ambazo hakuna ndege mwingine aweza kufika.
Kwa sababu hiyo, ndege tai ana uwezo wa kuona mbali kiasi cha kushangaza.Aweza kuona mawindo akiwa mbali huko angani. Tunafundishwa sisi wanadamu kuona mbali mithili ya ndege huyu. Tujifunze kufikiri kuliko kusema na kusoma, lengo ni kupima faida na hasara ya kila jambo katika maisha.
Watanzania, tumefika hapa tulipo kwa sababu hatuwezi kuona mbali kwa faida yetu. Tumewaachia wafadhili na watu wengine kufikiri kwa niaba yetu-makosa makubwa. Jicho la mtu halikuoneshi wewe hatari inayokukabili.
Sasa, wasomaji wataniuliza:Wawezaje kuona mbali mithili ya ndege tai? Jibu ni rahisi. Unatazama jana ili kujua ya kesho. Unatazama historia. Historia hutuonesha kesho kuna nini?
Historia, hutuonesha kesho kutatokea nini. Historia ni muhimu katika maisha. Historia hutuambia siri za siku za usoni.
 Mwandishi wa Kiingereza, George Orwell,ambaye jina lake halisi ni Eric Arthur Blair, aliwahi kuandika hivi:
“He, who controls the past, controls the future. He who controls the future, controls the Present”
Tafsiri yangu isiyo rasmi ni kwamba George Orwell,Yule mwandishi wa kejeli(satire) ya SHAMBA LA WANYAMA, alisema hivi:
“Anayetawala Historia,hutawala pia siku za usoni; na atawalaye siku za usoni hutawala hata leo”.
Anaongeza kusema, “Today was Yesterday’s Tomorrow”-leo ni jana ya kesho!!
Ndicho kichwa cha makala haya,kutuonesha kwamba leo ni jana ya siku za usoni. Usione leo ukadhani utakuwa hivi hivi kesho,leo itapita na itakuja kesho usiyodhani. Ukitaka kujua ya kesho,tazama jana na leo-tafakari,jifunze kufikiri kwa kina.
Naam, leo ilikuwa jana ya kesho.Ninapotazama historia nawaona watu wanaorejea tabia na makosa ya jana.
Dola ya Rumi, ilipinduliwa zamani kwa sababu ya ulevi,kukosa uzalendo,rushwa,ufisadi, raia kupenda starehe na anasa, na hata leo Tanzania tunarejea yale yale tu.
Watu wanafanya makosa yaliyowahi kutendwa katika historia, watu huchagua kufanya yale yale yaliyofanywa katika historia,na hata kesho haina tofauti kubwa. Vita vilikuwepo na hata sasa na kesho vitakuwepo,kwa sababu watu huyarejea yale yaliyotendwa katika historia.
Historia haiwarogi watu hata wayatende yale ya kale. Hatutaki kujifunza Historia,hatujui na hatujui kuwa hatujui,ndiyo maana tunafanya makosa yaliyofanywa katika historia.
 Laiti tungejifunza Historian a kubaini makosa ya wenzetu wa juzi na jana,leo tungetenda tofauti na kwa umakini na hekima.
Jumatano, Agosti 22 mwaka huu, nilikuwa nikitazama kipindi cha STRAIGHT TALK AFRICA cha Sauti ya Amerika(VOA) juu ya kifo cha Rais aliyekuwa Rais wa Ghana, John Atta-Mills.
Nilitazama kuapishwa kwa Rais Mpya, John Dramani Mahama, mahojiano kati yake na Mtayarishaji wa kipindi hicho, Dk. Shaka Ssali, kwamba anaapishwa kumalizia miezi mine iliyobaki,hadi kufikia Uchaguzi Mkuu.
 Nikamaizi kuwa, Rais Mpya wa Ghana, John Mahama, anafanana sana na wenzake waliomtangulia katika Ikulu ya mjini Accra.
Marais wote waliapa kuiongoza vema Ghana;wote waliapa kuwajali raia,kuiendeleza nchi kwa usawa na kutokuwa na upendeleo.
Naam, akina Jerry John   Rowrings ,John Kufour,John Atta=Mills, na sasa John Dramani Mahama-naam,ni Ghana na utawala wa akina John!
 Majina ni yale yale, watu walewale,kasoro ni mbwembe za kuapishwa,suti walizovaa na wapambe waliowazunguka-maisha yale yale,mambo yale yale tu,hakuna jipya.
Tujifunze kuchungulia nyuma katika historia. Wanasiasa wakubwa siyo watu wa kutegemea,kutumaini na kuegemea. Tunapaswa kuwatii,kuwaheshimu na kuwanyenyekea kwa sababu wanashikilia mamlaka ambayo ni mithili ya upanga. Lakini siyo kuwatumaini.
Mwanamuziki, Roger Whittaker, alishaimba kwamba wanasiasa ni mithili ya ndizi mbivu katika chane: Wote ni njano, wameshikilia pamoja,wanakula pamoja,wana rangi moja,lakini hakuna aliyenyooka hata mmoja!
 Nataka kuwaonya Watanzania wanaodhani wanasiasa ni “Truvada” (dawa mpya ya Ukimwi iliyovumbuliwa),kwamba watamaliza matatizo yao,wanajidanganya kuliko kawaida.
Watu wakubwa wengi wamepinda mithili ya ndizi, hawana maadili. Wakisemacho hawakitendi na wakitendacho sirini,hawakisemi. Wanapoapishwa,husema wataitii sheria na Katiba ya Nchi, mara waingiapo madarakani,hujikuta wakitenda tofauti na walivyoapa.
 Sasa, utaona watu wakivuja jasho jingi kusukuma magari yao,kutandika mavazi yao chini,ili hawa mashujaa wao, “Role Models” wapiti juu yake. Wengine wamefariki dunia kwa kukinzana na mamlaka kwa sababu hao mashujaa wao wameagiza wafe!
Maisha yako ni ya thamani kuliko ya mwenzako.
 Wanasiasa hawa watakuja na kuondoka,lakini shida zetu zitabaki ikiwa sisi wenyewe hatuwezi kukaa na kutazama namna ya kuziondoa.Wanasiasa wana kiu ya madaraka,na wala hawana nia ya kututumikia mithili ya mshumaa. Mshumaa, hujiteketeza wenyewe kwa nia ya kuwaangaza wengine. Nani mwanasiasa mshumaa?
Akiwepo kiongozi mshumaa(na hayupo) huzimika mara kunako tufani. Elton John aliimba kwamba , “Candle in Wind” mshumaa kunako upepo, wakati wa mazishi ya Princess Diana, unakumbuka?
 Naam, Candle in the Jungle! 
Mshumaa mwituni, utawaka,kunako tufani? Hata Princess Diana hajawahi kuwa mwema mithili ya mshumaa,kujiteketeza wenyewe kwa nia ya kuwaangaza wengine? Huu ni Upendo wa Agape.
 Wanasiasa hawana upendo wa Agape.
Wanaweza kuwaona raia wao mithili ya familia zao ama watoto wao wa kuzaa. Huu ni upendo uitwao kwa Kigiriki, Philos,Phileo ama Philia.
Wengine wana upendo wa kitoto,Storge, na wengine wana tamaa na ashiki za kimwili,Eros ama Erao ambazo huzitumia kupora wake za raia wao na kuondoka!
Nakwambia ukweli msomaji,amini usiamini. Usiwaamini wanasiasa hata ukajitoa mhanga .Usifanywe ngazi ya kupandia ama kukwelea mamlakani,usigeuze mabega yako kubeba wanasiasa hawa-heri kubeba zege,ili upate mlo wa usiku, sembuse wanasiasa hawa?
 Watakuja na kuondoka,dhiki zetu zitabaki. Tena wengine watakuja na kupandikiza chuki na ukabila kama Kenya,watawaachia wananchi vita,umwagaji damu na visasi vya kurithi.
Mwanafalsafa wa Athens,Ugiriki,Salon anasema hivi:
“The law is like spider’s web. The small are caught ,but the great tear it up!”
Tafsiri yangu:Sheria ni mithili ya utando(mtego) wa buibui,wadogo hunaswa humo(wanyama,wadudu n.k)
Lakini, wakubwa huutatulia mbali na kujiendea zao pasipo madhara yoyote! Nataka nikwambie msomaji,watu wakubwa mnaowategemea(mnasukuma magari yao na kutandaza mashati na khanga za akina mama ili wapiti juu yake) ni wahalifu sana. Hawana maadili myoyoni mwao bali midomoni.
Wakubwa, hujidai kuwapenda raia wao. Raia wako tayari kuwafia wanasiasa wao,lakini wanasiasa ni nadra kufa kwa ajili ya raia.Wanakubali wafe kwa sababu ya tamaa ya madaraka,na aslani siyo kwa ajili ya kuwapenda raia.
Kwa wanasiasa,wanapokuwa akigombea uongozi,raia ni ngazi zao za kukwea uongozini. Pindi wanapopata madaraka,raia hugeuka shubiri,mizigo ya kuwahoji kutimiza ahadi. Raia hugeuka ‘adui’ za wenye mamlaka.
Sasa, nani alikufa kwa ajili ya adui zake. Labda tusome Warumi sura ya 5,kwamba ni Yesu aliyekufa kwa ajili ya adui zake!
 Viongozi wengi wanaponyatia madaraka,hujidai wema mithili ya mishumaa.Lakini pindi waingiapo mamlakani,hugeuka mangimeza-hutawala  kwa kutoa amri na shuruti wakiwa mezani,kuliko kusikia kilio cha wananchi.
Uadilifu hauji kwa maneno ya mdomoni,bali matendo yatokayo moyoni(Mathayo 21:23-32) hii ni kusema, “To walk the talk”.
Watu wakubwa sana duniani ni dhaifu kupindukia-Strongest but weak.
Nakusudia kuchungulia historia ya watu wakubwa duniani kama Julius Caesar, Pharao wa Misri,Malkia Cleopatra wa Misri, Kaisari Nero,  Mfalme Herode,George Washington n.k
Hawa wote walikuwa wavunja sheria,ambao kama umma ungemaizi, walistahili kukatwa vichwa kwa uhaini, lakini kwa sababu ya wapambe, walishangiliwa sana.
 Leo, nawashauri wasomaji wangu kuwaheshimu wenye mamlaka(Warumi 13) ili ujiongezee uhai. Ni upumbavu wewe mwenye mawe kujibizana na polisi wenye SMG zenye risasi za moto,ukijidai Mfalme Daudi kwa Goriathi. Usijidanganye mwanaharakati kumtupia jiwe polisi mwenye silaha.
Mwanamuziki Muhiddin Gurumo, na wenzake waliimba hivi zama za Ndekule:
“Usimkaribie chatu, ooh chatu wee; gongo usimtupie utaukosa ushindi! Natoa onyo kwa yeyote anayemchezea chatu, ni hatari, atakuja askikose lolote la manufaa na ajali imkute bila ya kutegemea, atakuja adhirika ajute na duniaaa!”
Wanasiasa ni chatu,hasa wawapo mamlakani. Ukitumwa kuwatupia gongo,ukinaswa na chatu mwenye kiu ya damu,umejitoa kafara mwenyewe.
Najua watu wajinga wapo wengi wenye kuchochea wenzao wafe ili wapige kelele nyingi kwamba Haki za Binadamu zinavunjwa. Kila mtu atazame haki yake ya uhai kwanza.
Mara nyingi,hawa wapiga domo wanaoitwa wa Haki za Mashoga, haki za akina mama, haki sijui za Binadamu,huwavisha ngozi za kondoo raia wanaopenda kukaa-kaa vijiweni saa za kazi, ili wakararuriwe na wanyama wakali!
 Nawashauri watu kuwa ‘Busy’ na mambo yao na kazi zao,tuachane na Politiki saa za kazi,maana hakuna mtawala atayekuja kutugawia sembe na maziwa kila nyumba,bila kufanya kazi
Kanali Muammar Gaddafi, alikaribia kuwagawia maziwa raia wake kila subuhi,lakini wapo waliomkana, akauzwa kwa Wamarekani, na sasa yuko Kaburini, mtoto wake,Saif al-Islam anakabiliwa na kitanzi.tazama historia ili kujua kesho.
George Orwell anawafananisha nguruwewa SHAMBA LA WANYAMA na viongozi  na unyama wao dhidi ya raia waliojidai kuwapenda sana.
Mwanafalsafa wa Ugiriki, Salon amewafananisha viongozi ho na wanyama wakubwa wanaoichanachana sheria na katiba ya nchi na kujiendea zao wanakofuata maslahi yao.
Sisi wadogo ndiyo tunaswao na sheria. Usidanganywe kuvunja sheria na watu wakubwa-utanaswa wewe wao watabaki. Utazame utando wa buibui ujifunze somo hili,wanaonaswa humo ni akina nzi,mbu,sisimizi n.k Lakini,wakubwa hujiendea na kuuchana utando huo wa bui bui. Tembo atanaswa katika  ‘spider’s web’?
Wakubwa hukiuka maadili,na kwao si hoja.Hawnaswi na mkono wa sheria,hujiendea zao salama. Usipoteze muda kuhoji jambo hilo,kafanye kazi zako, maana ni historia,,bishana nayo upoteze muda na maisha bure!
Nawe wataka kuvunja sheria za nchi?Wewe ni nzi, utanaswa katika mtedo wa buibui(sheria),katika tawala za dhuluma, sheria wamewekewa wanyonge-wewe na mimi, kutii ni njia ya kuokoa maisha,amini usiamini.
Tunisha misuli uone,kesho utakuwa mshumaa katika tufani-Candle in Wind!
Usifuate maoni ya watu wengi wajinga, Public Opinion. Jihadhari na maneno ya kijiweni. Usimtupie fimbo chatu,utajuta. Utaumia. Usiwatupie polisi mawe wakiwa na bunduki,utavuja damu puani. Usitumiwe kama kinyangarika.
Duniani,viongozi wenye upendo na raia wao wanapokuwa madarakani,siyo wengi. Kiongozi hupenda enzi na mamlaka yake kuliko raia,kuliko mke na wanaye. Sembuse wewe?
Nikupe mfano. Karibia miaka 2,500 iliyopita,Mwanafalsafa aitwaye Euripides wa Ugiriki aliandika kisa cha Admetus mfalme wa Thesaly kukabiliwa na mauti,hadi apatikane mtu wa kujitoa mhanga ili afe badala yake.
Ndugu zake,marafiki na baba na mama yake walikataa kufa kwa ajili yake. Ni msichana mzuri,mpenzi wake aliyeitwa, Alcestis aliyekubali kufa badala ya Admetus.
 Itaendelea
0786 324 074




No comments:

Post a Comment