Tuesday, August 7, 2012



 
Nitajadili aina nne za upendo katika mwendelezo wa makala hizi. Kuna aina nne za upendo kama wasemavyo wanafalsafa wa Kigiriki: Eros, Philia,  Storge na Agape.
Hata hivyo, katika hizi, upendo halisi ni Agape ambao siyo upendo wa faida. Hili niliache kwanza.
Tuijadili kidogo demokrasia. Hawa hawa wanafalsafa wa Kigiriki wanasema, demokrasia ni ushirikishwaji wa umma katika kutoa maamuzi, “Participation of Majority”.
 Demokrasia, wanasema ni utawala wa watu na watu kwa ajili ya watu.
Siku hizi wanasema kuna tawala za kikatili sana ambazo kwao kuna serikali za wachache kwa ajili ya wachache-Government of the few by the few for the few.
Katika zama hizi, serikali ya watu na watu kwa ajili ya watu,huwa na uhuru wa kusema (chochote?)
 Ndiyo maana siku hizi duniani utaona migomo na maandamano yasiyokwisha, ambao pengine utaona virungu vya polisi na mabomu ya machozi,ili kuwatawanya waandamanaji.
 Vibaka nao hutumia mwanya huo wakijidai waandamanaji, hupora mali za raia wenzao wasio na hatia na kutokomea. Jambo hili lilitokea Mwanza,mwaka jana.
 Hakika, hakuna kiongozi au mtawala atakayekaa salama siku hizi za migomo na maandamano, ama kukosolewa.
 Na Mungu hajawahi na hata sasa haachwi bila kukosolewa. Kama ofisi ya Mungu(Elohim, Elyon,Adonai, Elshaddai, Yahweh ama Yehovah) ingejulikana ilipo, angekwisha kumbana na maandamano na watu kumgomea!
Kama Mungu nyumba yake ingejulikana, na sanduku lake la posta ama namba yake ya simu, tayari angekwisha buruzwa mahakamani kujibu mashitaka,
 “Ya kwanini alimuumba Shetani? Kwanini Shetani yupo,na anawashawishi waungwana kuzini na wake za watu,kupora mali za umma na kuwafanya wengine tajiri, wengine masikini?”
Nchini Romania, kuna kituko cha jamaa aliyemburuza Mungu mahakamani,kwa kosa la kushindwa kumlinda jamaa mmoja ili asitende makosa!
 Pavela Mircea, alimfungulia Mungu kesi hii kwa sababu ya kumuumba Shetani, ambaye alimshawishi kufanya mauaji, na kasha akajikuta nyuma ya nondo za magereza.
 Jamaa, alisema si yeye aliyeua bali ni Shetani aliyemshawishi; na wala si Shetani,bali ni Mungu aliyemuumba Shetani!
Basi, akijibu mashitaka, Mircea alisema alitiliana saini mkataba na Mungu,siku alipobatizwa Mungu amlinde hadi asifanye kosa lolote!
Mircea, akaiambia mahakama kuwa kesi ya mauaji iliyokuwa ikimkabili, haikuwa yake bali alistahili kuitwa Mungu aseme kwanini hakumlinda asitende kosa hilo?
 “Mungu alipaswa kuniepusha na maovu yote,na tamaa za wizi,rushwa,ufisadi, chuki na mauaji,lakini kwa uzembe,au kwa kutaka, Mungu amemruhusu Shetani ambaye amenisukuma kuua!” Mircea alisema mbele ya hakimu huko Romania.
Pia, alidai Mungu amlipe fidia ya mamilioni ya fedha kwa sababu alilipa sadaka, na alinunua mishumaa kanisani kwa muda wote hadi siku alipopatikana na kesi hiyo ya mauaji.
 Mircea, akaiambia mahakama kuwa,kwa sababu sadaka zake na mishumaa aliyonunua kanisani kwa muda wote wa tangu ubatizo, hazikumsaidia chochote ili aachane na tamaa mbaya,chuki hadi kupatwa kesi hii ya mauaji. Kwamba Mungu alipaswa kuzirejesha fedha zake kasha amlipe fidia!
 Upande wa mashitaka ukatupilia mbali madai ya Mircea. Kwa sababu, “Mshitakiwa” Mungu alishindwa kufika mahakamani hapo kwa muda mrefu sana,ili kujibu mashitaka haya ya Mircea.
 Jaji aliyesikiliza kesi hiyo, akatoa maamuzi ya madai hayo kwamba kwa kuwa iliipa taabu kumpata Mungu ili aje kujibu madai ya Mircea. Na kwa sababu haikujulikana wapi Mungu anaishi,nyumba namba ngapi? Mtaa gani,tena mji gani hapa duniani?
Jaji alisema: “Tumejaribu kutafuta anuani ya makazi ya Mungu,ili aitwe mahakamani, imeshindikana! Tumeshindwa kujua hata namba yake ya simu…wala hajulikani anaishi mji gani, au anuani ya nyumbani kwake”, Jaji aliwaambia waandishi wa habari wa Romania mwaka 2005.
  Mircea, alitiwa hatiani kwa kosa la mauaji, akafungwa jumla ya miaka 20 kwa kosa la mauaji,kwa sababu Mungu alishindwa kufika mahakamani,ili kubebeshwa kesi ya mauaji kwa kosa la kumuumba Shetani!
 Shetani eti ndiye husababisha wizi, tamaa,chuki,mauaji,ufisadi,rushwa n.k Kwa nini Mungu alimuumba Shetani? Ndilo suala wanalouliza watu kwa hasira siku hizi.
 Hakuna mtu anayekiri(anayekubali kuungama)makosa yake siku hizi. Kila mkosaji hutafuta mbuzi wake wa kafara(scapegoat) kufuatia makosa yake aliyotenda kwa hiari yake mwenyewe,au kwa uzembe.
Mtu akibaka katoto kachanga, au akizini na bintiye na kufumaniwa, atasema, “Ni Shetani tu!”
Shetani angeonekana mahakamani naye angesema, ‘Ni Mungu, maana bila Mungu Shetani asingekuwepo!
Akina Mircea, wako wengi Tanzania.Hawataki kukiri makosa.
Kukiri ni kutambua kosa(Confession is acknowledging of guilty),hakuna anaye tambua uhalifu wake-kila mtu humsukumia aliye karibu naye kwamba ndiye chanzo cha umasikini wake,chanzo cha matatizo yake na kuzikosa raha za dunia na wanawake wazuri!
Sisi sote tunamkasirikia Mungu,Shetani,Waziri Mkuu,Rais,Bunge,Mawaziri au wakubwa Fulani,kuwa ndiyo chanzo cha maafa Fulani.
  Katika siasa,tunadai kuwepo UHURU WA KUCHAGUA(Freedom of Choice) na uhuru wa kujieleza,kuandamana,kugoma n.k
 Linapokuja suala la mtu mmoja mmoja kufanya makosa na kupatwa na mabaya(consequences)
Kufuatia mabaya yaliyotendwa zamani, tunaruka kimanga na kumsingizia Mungu,Shetani,Rais,Waziri Mkuu,Bunge na serikali!
 Unawezaje wewe kulazimishwa na Shetani kwenda kubaka binti yako wa miezi miwili? Unawezaje kulazimishwa na Shetani kwenda kumzini kuku ama mbuzi,kuua albino na kunyofoa viungo, kupora mali za watu n.k
Wewe huna uhuru wa kuchagua? Huna uwezo wa kukataa jambo baya na kuchagua jema?
 Nimkariri Mhariri wangu wa zamani, Muhingo Rweyemamu, ambaye sasa ni Mkuu wa wilaya moja huko mkoani Pwani.
 
Kwamba, katika nafsi ya kila mmoja kuna  Nguvu Mbili zinazoshindana-nguvu ya wema na uovu-Hata Paulo katika kitabu cha Warumi sura ya 7 husema haya haya. Kuna Mbweha wawili katika nafsi ya mtu, Mbweha Mweupe na Mweusi.
 Tuchukulie kwamba falsafa hii hutwambia kuna mbweha wawili wanakushawishi nafsini mwako. Mweusi anakushawishi kutenda baya, Mweupe anakushawishi kutenda jema. Kwanini usichague jema,midhali una “Power of Choice na Freedom of Choice?”
 Tunadai uhuru,ukiwemo wa uchaguzi,tunadai uwezo wa kuchagua. Mbona tunautumia vibaya? Mbona hatuwezi kuchagua,ila kila mara tunalazimishwa kuchagua uchaguzi wa ovyo?
 
Bila shaka, ni kwa misingi hii,tunahongwa gongo, sabuni na unga,kofia na t-shirt tunawachagua viongozi wetu,halafu wakianza kuiba,tunalalamika!
 Kama ulichagua kupewa rushwa ili mtu aingie madarakani na kuamua kurejesha gharama zake alizokuhonga wakati wa kampeni ama wakati wa uchaguzi, kelele za nini sasa?
 Hii ndiyo “Consequences” ya hayo uliyochagua vibaya zamani.Sasa unataka kumtoa kafara nani?
Nani chanzo cha makosa haya,kama si wewe na uchaguzi wako mbaya?
 Meli ikizama na kuua watu,wanasema ni Mungu ametaka! Ohh ni tufani ilivuma! Abiria wakiingia kwenye boti isiyo na boya hata moja,wakiumia wengine wakifa, wanaanza kulalama, ilijaa sana! Ilibeba mizigo na hata petrol!
 Huu ni uzuzu-hamna macho, hamwoni? Hujui ukimbaka mtoto chekechea utafungwa maisha, sasa eti unamwambia Hakimu kwamba ni Shetani! Acheni utoto.
Haya ya kukataa kuwajibika kwa makosa yetu wenyewe, yamekuwepo tangu Adamu na Hawa. Hawa alipomwasi Mungu, akasingizia Nyoka(Shetani),na Adamu alipoulizwa kwa nini yeye kila alichosema mkewe akafuata bila kuhoji, akamsingizia Mungu kwamba kwanini alimuumba Hawa,na kwa nini alimuumba nyoka, yaani Shetani?
 Kwa nini dhambi iliruhusiwa? Tunauliza hivi wakati madai ya Ulimwengu sasa ni uhuru(demokrasia) ili kufanya kila jambo,kuandamana,kugoma,kukosoa hata Mungu mwenyewe n.k
 Sasa, mlitaka Mungu amuue Shetani ili aonekane Dikteta?Serikali ikimkamata Prof Lipumba au Dk. Wilbroad Slaa, kwa uchochezi,mtasema kaonewa tu.
 Je, Mungu angemfunga jela Shetani au kama angemnyonga, tungesemaje? Shetani yupo kwa misingi ya demokrasia ile ile,ili kila mtu achague cha kufanya.
Ukichagua vibaya usilalame na kusingizia watu-ebu badili mkao-Change Position- batili mtazamo,uone kwamba umekosea na sasa unatambua ulipoangukia,sawa? Acha kulalama kama chizi!
 
Tunachagua vibaya.Uchaguzi wa ovyo. Adamu na Hawa walichagua ovyo wakaanza kulalama(Mwanzo3:13,17 na Mwanzo 4:9). Binadamu hutenda mabaya na kukataa kuwajibika. Meli inazama kwa uzembe, SUMATRA wapo, serikali ipo na wewe mwenyewe unachagua kupanda meli mbovu,haina boya hata moja,ukifa kizembe,lawama zinaanza-kaa chonjo wewe,acheni uzembe na kulalamika!
Umeuza ardhi kwa mwekezaji, sasa huna chakula,unasema “Hii serikali,sijui ya CCM!” Hivi AKILI ZETU ZIKO wapi?Tumboni!
Utawala mbovu na rushwa na ufisadi,matokeo yake ni wewe na mimi. Mimi ni chanzo cha rushwa. Rushwa inapompa ndugu yangu cheo,na madaraka na pesa,mimi hufurahi kwamba sasa neema imekuja. Mwisho wa siku, nchi inafilisiwa tunaanza kulia.
 Angalia, unamsaidia mwanao kuiba mtihani, anafaulu na kupata kazi nzuri serikalini,analipwa mshahara mzuri. Hakika huyu mwanao ni mzuzu,mjinga,mbinafsi,mpuuzi na mwizi tu. Umma unapolia kwa huduma zake za ovyo nawe unalia! Unalia nini wewe uliyeshiriki kuwaweka madarakani watu wezi?
 Tukitaka kupambana na rushwa na wizi na ufisadi,tusianzie serikalini ama kwenye chama Fulani!
 Tuanzie Katina nafsi zetu, ambamo kuna nguvu mbili-naam mbweha wawili, MWEUSI na MWEUPE,tubadili mtazamo,tumchague Mbweha mweupe atutawale-UCHAGUZI.
 Naam,tunachagua vibaya sisi wenyewe. Unachagua mke mbaya,mume mlevi halafu unasumbua watu. Unachagua kunywa gongo iliyochanganywa na spirit, ukipofuka macho,unaanza lawama dhidi ya serikali.
 Kuna watu hawataki kazi halali. Ni short cut,kila kitu, shule, short cut, utajiri short cut,kuoa au kuolewa,short cut, taabu ikitokea serikali, Mungu, Shetani, sijui mafisadi n.k mradi ni lawama na maandamano na ghasia na migomo kila mahali duniani-hakuna kuwajibika!
  Katika Mwanzo 3:1-24 tunaona Adamu akiuza utawala wake kwa Shetani kwa hiari yake mwenyewe maadam alichagua kufanya hivyo.
 Matatizo yanapoanza, anayakataa. Jamii ndiyo chanzo cha rushwa,wizi,mauaji,polisi wezi,waporaji,mawaziri mafisadi wanaolala usingizi bungeni, marais na wafalme wakwapuzi n.k
 Hawa wakubwa serikalini wanatokana na jamii. Jamii bora huzaa Rais bora. Jamii safi huzaa wabunge wasafi ambao miongoni mwao huwa mawaziri wasafi na wachapakazi.
 Inawezekanaje Rais ndiye amwe mwizi eti jamii iwe safi?
Rais safi huzaliwa na jamii safi, siyo? Tuanzie wapi kufanya mapinduzi? Wajinga wanasema Rais ni tatizo, hawajui sisi raia ni tatizo na chanzo cha haya yote.
 Tunavuna tulichopanda. Tulipanda Upepo sasa tunavuna Tufani. Sasa hawa walalamishi,kazi yao ni kuchungulia Rais anafanya nini!
Iulize nafsi yako wewe unafanya nini? Umekaa kijiweni kupiga politiki, sasa leo utakula hewa? Ukikosa hela, badala ya kulaumu kwa kupoteza muda bure,unasema ni serikali hii ya mafisadi! Acha uzoba!
 Hawa unaowalalamikia nao wako kama wewe.Wewe pia ukipewa madaraka,unapora kuliko!
TAKUKURU nao siku hizi wanalalamika, polisi wanalalamika, mawaziri wanalalamika,wabunge wanalalamika,Rais wan chi analalamika!
Tunalalamika. Nchi ya walalamishi,vipofu walioshindwa kuwajibika!
 Siku hizi wabunge wanalalamikia sheria ya mafao ambao waliitunga wao! Sababu ni nini? Tumeacha maadili.
 Maadili ni nini? Maadili ya mwafrika ni yapi? Upendo! Tazama nyumbani kwako watoto unawafundisha nini?
 Matusi, ulevi,uchafu nguo fupi,chafu,vitovu nje, wakiwa Malaya na machangudoa mnasema, ‘watoto wa siku hizi’! Siku hizi hajawahi kuzaa watoto! Watoto wenu mnawalea vibaya,wakiwa majambazi wezi na waporaji mnalalama. Ukihonga pesa mwao awe polisi, anakwenda fanya nini kama siyo kuhujumu raia na kushirikiana na majambazi na wezi? Sasa una lalama serikali imeshindwa nini kulinda raia?
 Haya yalianza zamani sana. Mtu anahonga, anashinda mtihani, anapewa digrii hata ya chupi!
 Matokeo yake ‘consequences’ yakifika.tunakataa kuwajibika!
 Mrisho Mpoto anasema, “Kila siku afadhali ya jana” kweli maana kila siku kuna mbinu mpya za uporaji na uchakachuaji.
Afadhali ya jana kwa sababu ile jamii ya jana ilikuwa afadhali. Raia wa Nyerere walikuwa waadilifu kama Nyerere. Raia wa Kikwete wanafanana na Kikwete. Haiwezekani raia wawe wema eti Rais awe tapeli. Tunafanana. Tuukubali ukweli, acheni kusingizia watu, sisi tubadili tabia,tuwajibike nchi yetu itakwenda.
Shida ziko vizazi vyote,tumeona ndege zikitekwa, watu akitaka kupindua serikali,malumbano,uhujumu uchumi n.k
 Kizazi hiki hakitaki kukubali kwamba sisi ndiyo tatizo letu, wao ni chanzo cha shida zao wenyewe,mimi nina mchango mkubwa wa umasikini wangu mwenyewe-uwajibikaji,ukweli nimeuacha,muda unapotea vijiweni kujadili siasa wakati sina chakula. Mchawi wangu ni mimi,siyo Rais wala mwingine yeyote.
Wanasiasa tuachane nao-wote hufanana kama ndizi katika chale moja.
Wote ni rangi moja, wanakula pamoja,mama yao ni mmoja, na wote wamepinda-hakuna mwanasiasa aliyenyooka.
Politicians are like a bunch of bananas, they hang together; all are yellow, but there is no a straight one!”
Itaendelea
0786/0713-324 074
 
 
 
 

No comments:

Post a Comment