Monday, September 23, 2013

MAGAIDI WA BLACK SEPTEMBER

POLISI WA UJERUMANI walifika katika kijiji cha Olimpiki saa 11 Alfajiri.
Wale magaidi wa Kiarabu-Black September-walipoona polisi wamewasili katika mabweni ya Waisraeli, mahali walipowashikilia mateka wao, wakamtumia Kamanda wa Kikosi cha Polisi ujumbe kwa Kiingereza.
“Kuwaachilia huru wafungwa 200  Wapelestina waliokuwa wakishikiliwa katika jela la Israeli! Kama mamlaka  haitatekeleza madai haya mara moja, katika muda wa saa 3 Asubuhi, mateka(Wanariasha wa Israeli watauawa!” Ujumbe ule ulisema.
Ujumbe ule ukafafanua kuwa kila baada ya nusu saa wangekuwa wakichinjwa wawili-wawili!
Hata hivyo, muda wa nusu saa uliowkwa na hao magaidi kuwa wa mwisho(dead line)ili kutekeleza madai yao ulisogezwa mbele.
Baadaye, wateka nyara wa Kipalestina wakaongeza madai mengine kwamba,ilikuwa lazima wakubaliwe wao na mateka wao(Waisraeli) waondoke kwenda katika nchi yoyote ya Kiarabu, ambayo wangeichagua wao.
Elewa mateka wa Kiisraeli walikuwa ndani ya bweni, wakiwa wamefungwa mikono na miguu tena wakiwa wamefungiwa kitandani, wasiweze kufanya chochote, tena chini ya ulinzi wa SMG na AK-47.
Polisi wangejitia hata kuvunja mlango wa bweni lile(ulifungwa) mateka wale wangeweza kulipuliwa hata na maguruneti, pengine wangelipuliwa kwa risasi za rashasha,maiti zao zikakutwa zimetobolewa mithili ya chandarua1
 Umbali wa zaidi kidogo ya mita 220 kutoka jingo walimokuwa mateka wale wa Israeli,Mkuu wa Polisi wa mjini Munich, Manfred Schreiber, aliwaita Makomandoo 600,wakiwa na magari ya deraya.
Walitaka kuzingira bweni lile,na walikuwa na ambulance tayari kuchukua zile maiti za Yule Muisraeli aliyepigwa risasi, Moshe WEINBERG.
Schreiber, alikwenda na makomandoo wake kulihusuru lile jengo walimokuwa wale mateka wakiwa wameshikiliwa chini ya ulinzi mkali wa wateka nyara wa Kipalestina-wee uwasikie tu.
Alikutana na wale wanaume wa kazi-Black September- wakiwa wamevalia kofia nyeupe za tennis huku nyusoni wakiwa wametilia miwani myeusi ya jua, SUN GLASSSES.
Kiongozi wa Magaidi hao wa Kipalestina alikuwa mtu mwenye msimamo mkali. Schreiber aalipomtazama usoni, akaona alikuwa hatanii.Alikusudia kumtia chini ya ulinzi, akagwaya.
“Do you want to take me?”
Kiongozi wa magaidi wa Black September akamsaili Mkuu huyo wa polisi wa Mjini Munich.
Akafanya kama ananyoosha mkono wake ili labda utiwe pingu,kumbe ulikuwa na guruneti mkononi!
Kuanzia hapo simu zikaanza kupigwa mfululizo baina ya Munich, Bonn na Jerusalem.
Waziri Mkuu wa Israeli, Bibi Golda Meir na Mawaziri wake wakakaa kufikiri namna ya kufanya ili kuwaokoa mateka hao huko Munich.Mwisho, walikasirika na kuwaambia Wajerumani kwamba waliwajibika kwa uzembe wao,kwa hiyo iliwapasa kuokoa maisha ya wanamichezo hao ambao wamefanyiwa unyama katika ardhi yao!
Wakati haya yakitokea, kama umbali wa mita 400 tu kutoka hapo,michezo ya Olimpiki ilikuwa ikiendelea kama kawaida.
Wakati huo,Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Dietrich Gensncher, (nilimsikia katika taarifa za habari nikiwa mtoto, nikisoma darasa la pili)alianza mazungumzo ya kutafuta mwafaka(negotiations) kati ya wateka nyara wa Kipalestina na serikali ya Israeli na Ujerumani Magharibi zama hizo-Siku hizi Ujerumani ni moja baada ya Ukuta wa Berlin kuvunjwa mwaka 1991.
Gensncher, aliahidi magaidi wa Kipalestina kupewa KITITA CHA NOTI, kama wangekubali kuwaachia mateka wale.
Walizungumza ana kwa ana na Waziri huyo huku akiwahadaa, “Serikali ya Israeli bado inajadiliana ni mateka wangapi wa Palestina waachiliwe huru; bado kutoa jawabu” Waziri Gensncher alisema.
Black September, wakasogeza mbele tena ule muda walioweka-deadline-ya kuwaulia mbali wale mateka, kutoka Adhuhuri hadi saa 7 za mchana. Wakasogeza tena mbele deadline hadi saa tisa alasiri, hadi saa 11 jioni,ili serikali ya Israeli ikubali mateka wa Kipalestina Waachiliwe huru huko Jerusalem.
Kama msomaji unakumbuka kisa cha Iddi Amin Dada kilichosimuliwa katika gazeti hili, utakumbuka hata pale Entebbe, wakati magaidi wa Kipalestina wanawashikilia abiria wa Air France Air Bus, walitoa madai haya haya ya kutaka Israeli kuwaachia huru wanamgambo wa Kipaletina walioshikiliwa labda Tel Aviv au pengine popote katika ardhi ya Mayahudi.
Walisogeza mbele muda hadi mara sita.
Waziri Gensncher akaomba kwanza akawaone kwa maho hao mateka.Wakamchukua hadi bwenini,akawaona tisa wamefungwa watatu watatu mikono na miguu kwenye kitanda.
“Nimewaambia”,Gensncher akasema, “Kama wakikubali,basi ninyi muondoke na hawa mateka hadi nje ya Ujerumani”, wakati huo zilikuwa Ujerumani mbili,Berlin na Bonn.
Serikali ya Ujerumani ikifikiri cha kufanya ili kuwanusuru Waisraeli mikononi mwa mauti. Kama ingekurupuka,wale wateka nyara wangewaulia mbali hao mateka,halafu lawama zingekuwa pale pale,kwamba kwa uzembe wao raia wa mataifa ya kigeni waliokwenda kushiriki mashindano ya Olimpiki ya Munich, mwaka 1972 walitekwa nyara na kuuawa kinyama.
Kama ingekuwa hapa Tanzania, ungesikia kila mwanasiasa akiilaumu serikali kwa uzembe, pengine hata hapo mitaani kwenu,mngesema polisi wazembe lazima hata walipewa rushwa!
Basi,serikali ya Ujerumani ikawaleta polisi wenye shabaha, sharp shooters, wakiwa wavevalia fulana za kuzuia risasi kupenya-Bullet Proof juu ya jezi za kimichezo walizovalia.
Kamera kali sana zenye zoom zikawamulika hao makomandoo, hadi kule mateka wa Israeli walikokuwa wanashikiliwa.
Walichelea kuwafyatulia risasi wale magaidi wasije kufanya kosa moja halafu Black September wakawageukia wale adui zao na kuwalipua. Hapa kulikuwa na hesebu kali za nyoka na panya wanapokutana katika tundu dogo.
TV na Radio zikaanza kutangaza mkasa ule wa magaidi wa Kiarabu kuwateka nyara wanariadha wa Israeli hapo Munich.
Waisraeli 100 vijana wadogo wakaimba wimbo wao wa Taifa-HATIKVAH-kuwaambia Waisraeli waliotekwa nyara hapo Munich,
“Mjue hapo mlipo kwamba hamko peke yenu,tupo pamoja nanyi!”
Helkopta za polisi zikaanza kupaa angani katika vichwa vya wanamichezo wa Olimpiki.
                 
Naam, hadi wakati huo serikali ya Israeli nay a Ujerumani zilikuwa kiti moto.
Kansela Willy Brandt, BAADA YA KIKAO NA Baraza lake la Mawaziri mjini Bonn,alienda Munich ili kutafuta suluhisho la magaidi wale katika nchi yake.
Naandika kisa hiki kilichotokea mwaka 1972 leo wakati kunapokuwa na kisa kama hiki huko Jamhuri ya Kenya,baada ya magaidi labda al-Shabaab kuvamia Westgate.
Mawazo aliyo nayo Rais Uhuru Kenyatta,ni kama alivyokuwa Kansela Willy Brandt, wakati Waisraeli walipokuwa wametekwa nyara na magaidi wa Kipalestina katika bweni huko katika kijiji cha Olimpiki mjini Munich.
Nimekuambia,wakati huo Waziri Mkuu wa Israeli alikuwa mwanamama,Golda Meir, ambaye sasa alilihutubia Bunge kusema,  “Ilikuwa vema timu yetu kususia michezo ya Olimpiki iliyokuwa ikiendelea hapo Munich”.
Rais Richard Milhouse Nixon(alijiuzulu mwaka uliofuata kwa kashfa ile ya Watergate) alituma pole nyingi sana mjini Jerusalem; akaamuru Balozi za Marekani zote katika nchi za Kiarabu kushinikiza mateka wale kuachiwa huru.
Msomaji, nataka nikwambie kwamba,Rais wa Marekani ni mithili ya samba hapa duniani.
Anaponguruma ili kushinikiza jambo la muhali,dunia hukimbizana mithili ya vi-swala…Marais wa Kiarabu tumbo likawa joto!
Barozi za Kiarabu mjini Bonn-Arab League- waliwabembeleza wale wapalestina,pasipo mafanikio.
Kansela Willy Brandt wa Ujerumani,akampigia simu Rais Anwar al Sadat wa Misri, akamuunganisha na Waziri Mkuu,Aziz Sidky, aliyesema, “Hatutaki kuhusishwa na jambo hilo”.
Brandt, aliamuru wateka nyara kuondoka na mateka wao Waisraeli,wasije wakawapiga risasi bure ikifika asubuhi. Kumbuka sasa ilikuwa usiku hiyo Septemba 5,mwaka huo 1972.
Black September walisema watawaua hao mateka wa Israeli popote,kama serikali yao itajitia kichwa ngumu kutowaachilia huru mateka wa Kiarabu huko mjini Jerusalem.
Kwa msomaji anayesoma kisa hiki hapa, atapata picha kwamba,mashambulio ya kigaidi hata ya West gate, yanaweza kuandamana na madai kama haya ama wakati mwingine kikadaiwa kikombozi cha mamilioni ya fedha!
Ugaidi siyo ujambazi kama huu wa kawaida,lazima watu kuelewa.Ugaidi una sura ya kulipa visasi juu ya vuguvugu Fulani la siasa za kiulimwengu.
Kufuatia hali hiyo,Kansela wa Ujerumani ,Willy Brandt alitokwa kijacho chembamba!
“Haiwezekani kuona jambo kama hilo likitokea katika nchi yetu”,Willy Brandt alijiambia kimoyomoyo, “Tutawajibika kwa ajili ya maisha ya mateka hao Waisraeli”, alisema
Wateka nyara wakapigasimu toka humo ndani ya lile bweni kwenda mataifa ya Kiarabu.Walipiga Tunisia,hapakuwa na jibu la kuwasaidia, hata simu yenyewe haikupokelewa.
Si unajua Rais wa Marekani,Nixon alishapiga simu huko sasa nchi za Kiarabu kuonekana ziliwasaidia hao magaidi ingekuwa issue ya kupigwa hata na Drones!
Kumbuka, Marekani imetishia Balozi zote za nchi za Kiarabu kutokuwapokea magaidi hao wala kuwapa msaada.
Hata hivyo,sasa mashindano ya Olimpiki yangekuwa hatarini.Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Magharibi, Hans Dietrich Gensncher, alimwambia Willy Brandt,
“Tusiwaache hapa Munich,isije kuwa noma bure,tuwaruhusu waondoke!” alisema.
Kufuatia hali hiyo, magaidi wale na mateka wao walichukuliwa hadi uwanja wa ndege wa jirani na Munich ambako wangekwea Lufthansa 727 Jet,hadi wanakotaka? Subiri uone kasheshe kama ya al-Shabbaab, West gate.
Baada ya saa 4 usiku(saa 18 baada ya kuwateka nyara Waisraeli) magaidi wanane wa Kipalestina wakawaongoza mateka wao mikono ikiwa imefungwa nyuma mgongoni, wakatoka nje ya bweni lile,wakatembea chini ya ulinzi,wakaingia ndani ya basi la rangi ya kijivu.
Walipelekwa hadi katika helkopta ambayo wangeitumia kuondoka hapo Munich,
‘Chopper ’mbili ziliwachukua hao magaidi  tisa na mateka wao wanane,Walipaa angani dakika kama 13 hivi hadi Furstenfeldbruck,kituo cha jeshi la Anga ambacho kilikuwa umbali wa kama maili 16 nje ya Munich.
Chopper ya tatu ilishapaa mapema kabla ya hizo mbili kutua;nayo iliwachukua maofisa wa Kijerumani na mashushushu wa Kiisraeli(Mosad), na kwa vyovyote huko kungekuwa na balaa kubwa!
Kumbe, uwanja huo wa ndege ulikwishazingirwa na askari 500 wenye silaha mkononi.
Walengashabaha(sharp shooters) walijiandaa kupokea amri ya kuwafagilia mbali wale magaidi wa Kiarabu.Walitarajia magaidi wanane wauliwe ili mateka 9 wa Istraeli waokolewe.Picha ni kama hiyo ya Westgate kati ya Al Shabbab na polisi wa Nairobi na washirikwa wa usalama.
Chopper ilipotua tu, wale magaidi walitegemea wawili kati yao wangeilinda ile 727,wawili wangechupa nje ya hiyo Boeing,nikisema 727 ni hiyo ndege iliyowaleta hapo.
Ingawa waliambiwa wasithubutu kuwageuza hata Wajerumani kuwa mateka,hao magaidi waliamuru hizo Chopper kuondoka hara sana hapo uwanjani.
Kumbe,Makomandoo wa Ujerumani watatu walikuwa kwenye mnara wa kuongozea ndege,ni kama yadi 38 hivi kutoka kwenye hizo chopper,wawili walikuwa ardhini.
Haikuchukua muda,vita vikali sana vikaanza.Waarabu wakawafyatulia risasi hao Wajerumani.
Mkuu wao tayari akarukia chini ya mvungu wa helkopta akaanza kumwaga risasi.Kwa saa nzima wakabadilishana risasi,vita vikapamba moto.
Baadaye,magaidi watano na kiongozi wao walilala mauti baada ya kupigwa risasi.Walikwishawaua wale mateka Waisraeli wote tisa,kwa sababu walikuwa bado wakiwa wamefungwa mikono nyuma mgongoni ndani ya zile chopper mbili wakati vita vinapamba moto.
Wale wanne waliungulia ndani ya chopper baada ya kulipuliwa na guruneti la wale magaidi wa Kipalestina,watano walipigwa kwa SMG NA AK -47 za magaidi.
Kufuatia vita hivi,polisi waliwatia mbaroni magaidi watatu;kati yao wawili wakiwa wamejeruhiwa vi-baya.
Itaendelea
0713 324 074
www.congesmrambatoday.blogspot.com










No comments:

Post a Comment