Tuesday, September 17, 2013

wazungu wanajiandaa kuhamia mars

Wazungu wanapojiandaa kuhamia Sayari ya Mars, Mwanza,Bukoba na Musoma watahamia kuzimu!

UHARIBIFU MKUBWA wa Mzingira hapa Duniani, ni  moja ya kichocheo ama chanzo cha safari za wanasayansi katika Anga za Juu.
Tangu mwaka 1969 akina Neil Armstrong walipofanya safari katika mwezi, wanasayansi wa Mataifa makubwa wamesafiri kwenda anga za juu ili kutafuta nishati, na hata makazi huko.
Watu wenye fedha wanatafuta viwanja vya kuishi huko Mars, wengine wametafuta sehemu ya kuzika wafu wao huko!
Inakisiwa hii Dunia imeharibiwa sana kwa sumu,uharibifu wa maji na anga kiasi kwamba uhai katika dunia hii hautakuwepo miaka 40 tu ijayo!
Uharibifu wa mazingira hapa duniani, unapoongeza kitisho cha uhai katika sayari ya Dunia,matajiri wa Ulaya na Marekani, wanapanga kuitoroka Dunia, ili wakaishi katika anga za Juu,mfano katika sayari ya Mars ambako kuna kila dalili ya maji na uhai.
Viwanja vimepimwa huko, watu wenye fedha kutoka nchi mbalimbali zenye vita,migogoro,uchumi mbaya,misuko-suko yenye kutokana na uharibifu mkubwa wa kimazingira n.k wanapanga kuitoroka Dunia yenye njaa,vita na majanga ya kimazingira.
Zaidi ya watu 200,000 hapa Duniani wametuma maombi kutaka kuhamia Mars,kufuatia hofu ya majanga ya kimazingira,maradhi mabaya,njaa n.k
Hawa wanatoka takriban nchi 140 hapa Duniani wamo pia Marais wa Mataifa makubwa. Hawa wanaona wakitorokea sayari ya Mars wanaweza kuepuka kifo kinachoinyemelea sayari hii inayochafuliwa kwa mionzi ya sumu, uchafuzi wa anga,hewa, uchafuzi wa maji ya maziwa,mito na bahari n.k
Kanda ya Ziwa, haijafahamu kwamba, wakati Marais kama Barack Obama wanahaha kutafuta makazi katika Anga za Juu kama katika sayari ya Mars, huku ndiyo kwanza majumba kama mahoteli makubwa hujengwa ndani ya eneo la mita 60 za Ziwa Victoria,mito inayomwaga maji katika ziwa hili na kilimo kinafanywa mita chache toka ziwa na mito.
Imeelezwa kwamba miji ya Bunda,Mwanza, Musoma na Bukoba,kuna viwanda,mahoteli na wananchi wanajenga ndani ya eneo la mita 60 ambalo haliruhusu shughuli za binadamu kutoka vyanzo vya maji kama mito,maziwa,bahari n.k
Mahoteli yamejengwa ziwani na mengine yako mitoni, shughuli za kiuchumi zinaendeshwa kama kawaida kinyume cha sheria za Mazingira huku Kanda ya Ziwa.
Hivi karibuni, Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira(NEMC) limekusudia kubomoa sehemu ya Hoteli ya Royal Sunset Beach,iliyopo katika fukwe za Luchelele, Nyegezi jijini Mwanza,kufuatia ujenzi wa hoteli hiyo kukiuka sheria za kimazingira.
Royal Sunset Beach, inamilikiwa na Mkurugunzi wa Jiji la Dar es salaam,Wilson Mbonea Kabwe, imejengwa ndani ya mita 60 kutoka ndani ya maji ya Ziwa Victoria.
Kabla ya kuhamishiwa Dar es salaam,mmiliki wa Hoteli hiyo, Royal Sunset Beach, alikuwa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza.
Kulingana na Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Mazingira(NEMC),Manchare Suguta, kujenga ndani ya eneo la mita 60 kutoka vyanzo vya maji,ni kinyume cha sheria ya Usimamizi wa Mazingira,kifungu nambari 57.
Licha ya Mmiliki wa Hoteli hiyo kutozwa faini ya shilingi milioni 10, wadau wa Mazingira hapa Kanda ya Ziwa Victoria wanasema, Ziwa hilo ambalo ni chanzo kikuu cha uchumi, maji ya kunywa na chakula, huharibiwa kwa kiango cha kutisha.
Wakazi wa Miji ya Musoma,Bunda, Magu,Mwanza na Bukoba, wasio na mfumo wa kusafisha maji taka na taka ngumu zenyewe, wanamwaga taka zao katika Ziwa hili ama katika mito inayomwaga maji Ziwa hili.
Kulingana na Mradi wa Ulinzi wa Mazingira ya Ziwa Victoria, The Lake Victoria Environmental Management Project(LVEMP) sehemu ya Pili, wanasema watu na hata viwanda vya miji ya Mwanza,Bukoba,Musoma,Bunda,Magu n.k na wengine wa Maswa,Bariadi na Simiyu wanalima mazao katika ndani ya eneo la mita 60 kutoka maji ya mito na Ziwa hili.
Kilimo cha kando kando ya ziwa na Mito inayomwaga maji katika   ziwa Victoria,licha ya kusababisha mmomonyoko wa ardhi,husababisha utiririshwaji wa kemikali zinazotokana na mbolea na dawa za kuulia wadudu,na kusababisha hatari kwa maisha ya viumbe kama samaki, wanyama,mimea,ndege na hata binadamu wanaotegemea maji ya ziwa hilo kwa kunywa na kuoga.
LVEMP Phase II wanasema, viwanda vya kutengeneza mafuta (ya pamba) ya kula huko Bunda,mkoani Mara havikuwa na mfumo wa kuhifadhi taka kwa muda mrefu.
Viwanda hivyo,vimekuwa vikitiririsha kemikali na mabaki ya mafuta hayo ziwa Victoria ambalo liko kilomita chache kutoka Bunda, katika kijiji cha Guta.
Kulingana na wataalam wa Mazingira, kemikali za viwanda,majumbani na maduka zisipodhibitiwa,huweza kusombwa na maji ya mvua hadi katika vyanzo vya maji hata umbali wa kilomita 100.
Kutoka Bunda hadi Guta.ni umbali wa takriban kilomita 10 tu; na hali hiyo ya kutiririsha kemikali na mabaki ya mafuta ya pamba huko Bunda,huhatarisha maisha ya watu,wanyama na viumbe wanaotegemea Ziwa Victoria kwa maisha ya kila siku.
Kuna migodi inayotiririsha kemikali za hatari kama zebaki hadi katika Mito inayomwaga maji yake katika ziwa hili muhimu kwa uhai wa takriban watu milioni 30 katika Ukanda wa Mziwa Makuu.
Mifugo Mkoani Mara ilisharipotiwa kufa kwa kunywa maji ya kemikali za migodi,walkati   wananchi walishaathiriwa na kemikali hizo hadi kulazwa hospitalini na wengine kupoteza maisha.
Athari hizi za kimazingira ndizo hufanya sasa matajiri mataifa makubwa kuhaha kutaka kutorokea katika sayari nyingine kama Mars,ili kuepuka madhara ya kimazingira katika sayari ya Dunia.
Miji kama Mwanza, wakazi wake huendesha kilimo kandoni mwa Ziwa Victoria,hulima bustani kama mbogamboga na matunda ambayo huhitaji mbolea za viwandani na viuwatilifu vyenye kemikali za sumu.
Mji wa Musoma,umesemwa na LVEMP II kwamba baadhi ya wakazi wake hufanya kilimo katika Bonde la Kitaji lenye ardhi oevu,ama chepechepe.
Bonde hilo la Kitaji, zamani likitumika kama dampo la kutupia taka ngumu na Halmashauri ya MANISPAA ya Musoma.
Kemikali za mbolea za viwandani na sumu za kuulia wadudu pamoja na taka ngumu zilizokuwa zikimwagwa Kitaji,ni chanzo cha uharibifu mkubwa wa Mzingira katika Ziwa Victoria huko Mjini Musoma.
Kutokana na kemikali za sumu kutoka mashambani jirani na chanzo hiki cha maji, na kutokana na kumwaga taka ngumu,ujenzi holela ndani ya mita 60 ,ukataji holela wa miti kando ya mito kufuatia upanuzi wa mashamba, maji ya Ziwa Victoria yameharibiwa maradufu hadi samaki wamepungua na kusababisha njaa na ukosefu wa ajira mjini Musoma.
Samaki wametindika hadi bei yake imepanda maradufu.Samaki ni chanzo kikuu cha chakula aina ya Protini kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa Victoria, sasa kufuatia hali hiyo ya uchafuzi mkubwa wa mazingira,eneo la Kanda ya Ziwa linakabiliwa na hatari na majanga ya kiafya na umasikini wa kutisha.
Jijini Mwanza wakulima wa mboga na matunda hulima kando ya Ziwa na kutiririsha kemikali ndani ya maji ya ziwa.
Mamlaka ya Bandari(TPA) NAO HULALAMIKIWA kwa kutokuwa na mfumo wa maji taka ili kuzuia mafuta machafu yanayotoka melini na katika mitambo,kumwagikia ziwani.
Kuna waosha magari na wenye viwanda ambao wamekuwa wakitiririsha maji ya kemikali ziwani,na hata katika mashamba ya wananchi na kuwasababishia hasara kubwa. Maelfu ya ekari yanaharibiwa na kemikali zitokazo viwandani na migodini,na wakati mwingine mifugo wanaokula nyasi na kunywa maji yaliyoathiriwa na kemikali hufa.
Kanda ya Ziwa kuna viwanda vingi na watu wasiokuwa na Mfumo wa kusafisha maji(Sewage System) matokeo yake kemikali nyingi huwamwagwa ziwani na katika mito.
Lake Victoria Environmental Management Project(LVEMP Phase II) wanasema uchafuzi wa kimazingira unaofanywa kando ya mito na ziwa Victoria huhatarisha maisha ya mamilioni ya watu,mifugo,wanyamapori na mimea.
Matokea ya uharibifu huu ni hatari ya kiafya,umasikini uliokithiri kwa wananchi na vifo.
Baadhi ya mito inayochafuliwa sana sanjari na ziwa Victoria ni Mto Mara,Kagera,Grumeti,Mbalageti,Simiyu, na Mto Mori.
Baadhi ya migodi Kanda ya Ziwa humwaga kemikali kama Zebaki ambayo hutiririshwa hadi ziwani. Zebaki hutumiwa hata na wachimbaji wadogo wa madini kusafishia dhahabu migodini.
Zebaki inapofika ziwani hudhuru samaki na wanyama hadi walaji wa samaki wako hatarini kuugua saratani.
Upanuzi wa mashamba huko Simiyu na Bariadi umesemwa kwamba ni chanzo cha ukataji holela wa miti kandoni mwa mito, pia ni chanzo cha mmomonyoko mkubwa wa ardhi.
Wakulima wengi hulima hadi ndani ya eneo la mita 60 kutoka chanzo cha maji,kitu ambacho huharibu mazingira na ikolojia.
Kufuatia uharibifu wa mazingira katika mito na Ziwa Victoria,sasa kuna majanga yasiyosemeka.
Wakati Wazungu wakihaha kutafuta hifadhi katika Sayari ya Mars, Kanda ya Ziwa kuna uchafuzi wa mazingira na vyanzo vya maji,kuna ukataji wa miti kwa ajili ya mkaa nk
Matokeo yake eneo zima hilo mvua zitakoma kunyesha kabisa,na hata     zaweza kunyesha mvua za sumu(acid rains) zinazoweza kuleta athari kubwa kwa mimea na viumbe hai.
Ni kutokana na hali hiyo ya uchafuzi wa vyanzo ya maji(water pollution) na uchafuzi wa hewa(air pollution) Wazungu wanafanya mipango kamambe kuihama Dunia inayochafuliwa ili wakatorokee Anga za juu,hususan Sayari ya Mars
0713 324074
 
 
 

No comments:

Post a Comment