Monday, January 28, 2013

afrika kizimbani 10

 Mei 25 mwaka huu itakuwa siku ya kumbukumbu ya kuanzishwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika miaka 50 iliyopita.
  Umoja huo ulioitwa, Organization of African Unity(OAU) ulianzishwa Mei 25 mwaka 1963, ukiwa na jumla ya nchi 32.
   Mwaka 2001 umoja huo ulikuwa na jumla ya nchi 53. Lengo hasa la kuanzisha umoja huo lilikuwa kuimarisha amani, usalama na ustawi na maendeleo ya Waafrika. Makao yake Makuu yako mjini Addis Ababa , Ethiopia .
  Leo, Afrika iko mbioni kuwa nchi moja kama ilivyo Marekani, yaani Waafrika wako mbioni kuwa Taifa moja(United States of Africa), lengo lao likiwa kukataa kuwapigia goti mabwana wakubwa wa Magharibi na mashirika yao yaliyoanzishwa zama za Kikoloni, kama Benki ya Dunia(WB), Fuko la Fedha la Kimataifa(IMF) na vikundi kama Paris Club, G-7,8,20, WTO, Jumuiya ya Madola(Commonwealth) n.k
 Afrika, ni Bara tajiri, lakini watu wake ni fukara sana . Afrika ina ukubwa wa maili za mraba 11,667,000 sawa na kilimita za mraba 30,218,000.
Kuna milima mirefu kama Kilimanjaro wenye kimo cha futi 19,340 sawa na mita 5,895. Mlima Kenya una urefu wa futi 17,058(mita 5,199); Afrika kuna maziwa makubwa kama Victoria lenye ukubwa wa maili za mraba 26,418.
 Ziwa Tanganyika lina ukubwa wa maili za mraba 12,700. Ni miongoni mwa maziwa yenye kina kirefu zaidi Duniani, lililowahi kuwaleta wapelelezi maarufu kama David Livingston.
  Afrika kuna vivutio halisi vya kitalii, licha rasilimali zilizomo. Ziwa Nyasa lililoanza kugombaniwa na TANZANIA na Joyce Banda, lina ukubwa wa maili za mraba 11,430.
Afrika kuna mito kama Nile unaoanzia mto Kagera na kukatisha Ziwa Victoria hadi maporomoko ya Owen huko Uganda .
  Kuna Kongo, Limpopo, Zambezi , Niger , Orange , Senegal na mingine kama Tana, Kagera na Ruvuma ambayo haikauki msimu wote, lakini Waafrika tuna njaa.
  Watawala wetu waliwahi kutia saini mikataba ya hila ya mwaka 1929 na 1957 ya kuwauzia Bonde la Mto Nile watawala wa Misri, ili Waafrika wasije siku moja wakatumia maji ya Nile kwa kilimo cha umwagiliaji, wakati Misri wanalima jangwani kwa kutumia maji haya haya yanayotoka  MtoKagera.
Iko siku watatia saini Wahaya, Wajitta, Waganda, Waluo, Wasukuma n.k wasivue samaki kutoka Ziwa Victoria, ili samaki wote na rasilimali zingine view mali ya Wazungu na Wahindi wenye viwanda vya Umoja wa Ulaya(EU) vinavyosindika samaki hapa.
 Afrika ina misitu mikubwa inayozalisha mbao za thamani. Kuna mbuga kubwa za wanyama kama Serengeti, zenye mamilioni ya wanyama wakubwa ambao hawapo mahali popote pengine duniani.
  Mbuga za Serengeti zina eneo la kilomita za mraba 14,763 na wanyama wakubwa zaidi ya milioni tatu.
 Mbali na Serengeti, Tanzania kuna Ngorongoro, Tarangire, Hifadhi ya Ziwa Manyara, Ruaha, Selous, Mafia(Marine Park), Zanzibar, Olduvai Gorge anakodaiwa kuishi binadamu wa kale duniani, lakini Watanzania hawa zahanati na maji vijijini.
  Afrika nzima kuna mito , maziwa, madini, mbuga za wanyama, ardhi yenye rutuba, bahari n.k lakini Waafrika wana njaa.
 Asilimia 70 ya almasi yote duniani inatoka Afrika hasa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo , Ghana , Afrika Kusini , Botswana , Namibia , Angola , Tanzania n.k
Asilimia 55 ya dhahabu yote Ulimwenguni hutoka Afrika:Afrika ya Kusini, Ghana, Zimbabwe, Kongo, Tanzania n.k Afrika kuna Nickel, shaba za kumwaga, makaa yam awe n.k Kuna Tanzanite ambayo haipatikani popote duniani isipokuwa Mererani, lakini Wahindi na Wazungu huuza kwa wingi Tanzanite kuliko sisi.
  Mauzo ya Taninite katika soko la dunia kabla ya mtikisiko wa uchumi yalikuwa wastani wa dola za Marekani milioni 400.
Tanzania ilikuwa ikiambulia dola milioni 16 tu; hizi njama za mafisadi vibaraka wa Mzungu Barani.
Mwaka 2007 mauzo ya madini ya Tanzania nje yalikisiwa shilingi bilioni 825
Kulingana na Multilateral Investment Guarantee Agency(MIGA) serikali yetu iliambulia kama asilimia 15 ya fedha hizo bilioni 825kupitia kodi na mrabaha.
 Hali iko hivyo hata kwa rasilimali nyingine kama mafuta n.k hususan Ghana , Sudan , Nigeria , Libya , Angola , Guinea ya Ikweta. Kuna uranium na ruby. Uranium yaweza kutumiwa kuwa chanzo cha nishati ya umeme, lakini Afrika kumetanda kiza totoro. Hapa nchini Shirika la Umeme, TANESCO linatugawia kiza badala ya umeme.
Afrika kuna kila kitu, lakini hakuna manufaa, Waafrika wangali wakisubiri msaada wa chakula kutoka Shirika la Chakula na Kilimo kama FAO, WFP, na wasamaria wengine.
0786/0715-324 074
   Itaendelea
   

No comments:

Post a Comment