Thursday, January 3, 2013

AL QAEDA alifia katika ajali ya Mv.Bukoba




Ziwa Victoria, ni kiungo muhimu cha usafirishaji wa abiria na mizigo katika nchi za Mawziwa Makuu.
Gazeti moja litolewalo kila siku hapa nchini kwa lugha ya Kiingereza, katika toleo lake la Mei 23 mwaka jana, lilisema kwamba,mwaka 1996 Mv.Bukoba ilipozama na kupoteza maisha ya abiria wake takriban 1,000; miongoni mwao alikuwemo Abu Ubaidah al-Banshiri, ambaye alikuwa nambari mbili katika kundi la kigaidi la Al-Qaeda.
Kauli hii ni kuashiria kuwa malaka ya serikali sasa inapaswa kuchukua hatua thabiti za kuimarisha usalama katika ziwa hili
Naam, kundi hili la AlQaeda, lilianzishwa na Osama bin Muhammad bin Awad bin Laden,Feburuari mwaka 1998 kwa jina la WORLD ISLAMIC FRONT ,ili kuhujumu maslahi ya Marekani na washirika wake mahali popote duniani,hata kama ni Ziwa Victoria,
Osama alikuwa mshirika wa Marekani na shirika lao la Ujasusi(CIA) mwaka 1979 wakati majeshi ya Warusi walipovamia Afghanistan.CIA walimfadhili mabilioni ya Dola za Marekani kuanzisha kambi ya mafunzo ya Makhtab al-Khidamat(MAK).
Lakini,baada ya Urusi kuondoka Kabul mwaka 1989, Osama akageuka kuwa adui wa MAREKANI na washirika wao, akaungana na Taliban na Mullah Muhammad Omar kuendesha ‘Jihad’ dhidi ya Marekani na washirika.
Nataka kusema kwamba,mwaka 1996 wakati Mv.Bukoba inazama ziwa Victoria, al-Qaeda tayari walikuwepo,na wangeweza kufanya madhara hapa nchini kwa mashambulizi yenye kulenga shabaha Wamarekani ama maslahi yao hata hapa Tanzania.Tumeona Nairobi na Kampala ikishambuliwa na magaidi hawa,na hatusahau mashambulizi ya Agosti,7 mwaka 1998 yaliyoua zaidi ya watu 200 Dar na Nairobi.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Everest Ndikilo, amesema serikali imeimarisha ulinzi katika Ziwa Victoria,kwa kuwa zipo boti za doria zinazozunguka ziwani, na raia wanapaswa kutoa taarifa pindi wanapoona mienendo yenye mashaka ama kitisho cha magaidi wa al-Qaeda ama al-Shabaab!
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Nchi Kavu na Majini(SUMATRA) ndiyo wanaopaswa kusimamia ukaguzi na usalama kabla ya safari kuanza.
 “Changamoto ya SUMATRA,Mwanza kuna boti zaidi ya 10,000 zinazosafirisha abiria na mizigo kwenda visiwani na Sengerema,Ukerewe na Geita. Huwezi kusema, asilimia mia zote hufuata sheria, na kuzingatia maelekezo.SUMATRA Mwanza, tuna wakaguzi watatu tu,lakini tunao mtandao(usiotosha) wa kuwadhibiti wasafirishaji wasiopenda kutii sheria pasipo shuruti. Kumbuka, Ziwa siyo barabarani ambako utaweza vizuizi njiani na kufanya ukaguzi ili kuwabaini wakosaji”, anafafanua ofisa Mfawidhi wa SUMATRA,Mwanza, Alfred  Wariana.
  Polisi na Watendaji wa vijiji wapo katika maeneo ya vituo vya kibiashara,ambako boti hizi hutia nanga na kupeleka bidhaa,wanapaswa kuwatia mbaroni wasafirishaji wasiozingatia sheria za Usafirishaji wa Majini.
Kulingana na SUMATRA,Mwanza, ziko changamoto kuwafikia wamiliki wote wa vyombo vya majini,hususan vidogo vidogo,na kuvikagua kila mara.
 “Hata hivyo,mtandao wetu wapaswa kukagua na kuhakikisha kila chombo ni salama kabla ya kuanza safari,na kila chombo cha usafiri chapaswa kuwa na cheti cha kufaa-sea worthiness.
 Katika Ziwa Victoria,SUMATRA wana ofisi Mwanza, Bukoba na Musoma. Ziwa Victoria kuna visiwa takriban 60, Ukerewe pekee kuna visiwa 38 vingine hukaliwa na wavuvi tu.
  Mei 21, mwaka 1996,Meli iliyomilikiwa na lililokuwa Sherika la Reli(TRC) ilizama umbali wa mail inane(kilomita 12) za majini, jirani na Bandari ya Mwanza, uelekeo wa Bwiru.
 Mv. Bukoba, ilipinduka kasha kuzama,ikasababisha vifo vya zaidi ya watu 800.Wengine zaidi ya 100 walijeruhiwa,wakipoteza mali nyingi za mamilioni ya shilingi,hususan mikungu mingi ya ndizi.
 Kwa mujibu wa Ripoti ya Tume ya Jaji Robert Kissanga, iliyochunguza chanzo cha Ajali hiyo,usiku wa kuamkia siku ya ajali,Mv.Bukoba ilipakia abiria kati ya 750 na 800 pamoja na wafanyakazi 37 wa Meli hii.
  Kati ya hao, 114 waliokolewa wakiwa hai, wakati 391 waliopolewa wakiwa   wamefariki wakazikwa katika Makaburi ya Igoma,nje kidogo ya Jiji la Mwanza. Miili mingine ilichukuliwa na jamaa zao kwenda kuzikwa kwao. Jumla ya miili 332 haikupatikana.
      Kila mwaka, ifikapo Mei 21, serikali inayosema Haina Dini, huongozana na viongozi wa madhehebu ya dini na waganga kwenda eneo la ajali,kufanya ‘matambiko’ na kumwaga mchanga eneo  majini!
  Serikali iliwashitaki  katika Mahakama Kuu  aliyekuwa Nahodha wa Mv.Bukoba, Jumanne Rume-Mwiru, (ambaye sasa ni Marehemu),Mkaguzi wa Mamlaka ya Bandari(wakati huo THA),Gilbert Mokiwa, aliyekuwa Meneja wa Bandari ya Bukoba, Alphonce Sambo, na aliyekuwa Maneja wa Bandari ya Kemondo, Prosper Lugumila.
  Kesi hiyo Nambari 22 ya mwaka 1998, ilianza kusikilizwa Mei 14 mwaka 2001. Miongoni mwa waendesha mashitaka katika kesi hiyo ni Eliezer Feleshi, ambaye sasa ni Mkurugenzi wa Mashitaka nchini(DPP).
  Hukumu ya kesi hii ilitolewa Ijumaa, Novemba 29 mwaka 2002,majira ya saa sita mchana hadi saa 9 na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Juxton Mlay(amestaafu).
 Washitakiwa wote walishinda kesi hiyo,kufuatia Hukumu yenye kurasa 118 iliyosomwa kwa dakika 160 na Jaji Mlay,kusema Mv.Bukoba ilizama kwa sababu haikuwa na uwiano wa majini, na siyo uzembe wa washitakiwa.
 Serikali ikakata rufaa, hadi leo majaliwa na rufaa hiyo hayajulikani,na baadhi ya washitakiwa wamefariki dunia,bila kujua hatma ya kesi hiyo na stahili zao.
   Mv.Bukoba ilikuwa ‘Kaburi’ lenye kuelea Ziwa Victoria. Ilikwishapigwa marufuku,kwa kuwa haikuwa na viwango vya ubora-sea   worthiness.
 
Ilijengwa na Kampuni ya Kibelgiji,ikazinduliwa  Julai 27 mwaka 1979.Siku ya uzinduzi, ilibainika haikuwa thabiti,na ilikosa uwiano,ilitaka kumtosa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere ambaye alikuwa Rais wan chi wakati huo.
   Miaka michace iliyopita, meli nyingine ya MSC, Mv. Butiama, ilizimika injini zake jirani tu na Bandari ya Mwanza, lakini ikaelea kwa zaidi ya saa mbili,huku abiria wakihaha bila msaada. Ilikuja kufahamika kwamba, meli hiyo haikuwa na mawasiliano!
 Meli nyingine ya mizigo, Mv.Nyamageni,ilizama ziwa Victoria ikiwa na abiria zaidi ya 20 waliosafirishwa pamoja na masanduku ya soda kwenda visiwani.
 Feburuari mwaka 2012,  Mv. Pacific iliyokuwa ikisafiri kati ya Mwanza na kisiwa cha Ghana ilizama, ilikuwa na abiria 17, mmoja alifariki wengine wakaokolewa.
 Kwa mujibu wa SUMATRA, Boti nyingine iliyokuwa na abiria 31 ilizama huko Musoma,mkoani Mara,abiria   wote wakaokolewa kwa kutumia zana za uokozi.
 Kwa mujibu wa Alfred Wariana, Ofisa Mwandamizi wa SUMATRA, katika ajali tatu za mwaka jana 2012, kati ya watu 81 waliokuwemo katika boti hizo,ni mmoja tu aliyefariki dunia,na anasema hii huonesha kwamba sheria zimeanza kufuatwa.
  Kabla ya vyombo vya majini kuanza safari ni sharti kukaguliwa ili kuthibitishwa usalama wake.
Hata hivyo, Wariana anasema bado usafiri wa majini Ziwa Victoria ni salama zaidi kuliko barabarani.
“Usafiri wa barabarani hata wa ndege hapa Afrika ndiyo ‘Moving Coffins’ (majeneza yanayotembea),Barabarani kuna magari kuna pikipiki zinazochinja watu kila siku”, anasema Wariana.
Akizungumza kuhusu ushindani wa kibiashara, Ofisa huyu wa SUMATRA amesema, kuimarishwa kwa miundombinu ya barabara, hususan kutoka   Mwanza hadi Musoma, Tarime na hata Kenya,kumesababisha abiria wengi kususia usafiri wa meli.
 Tangu barabara ya lami ya Mwanza hadi Musoma ikamilike mwaka 1985, hakuna tena abiria wanaosafiri kwa meli kwenda Musoma,Shirati au hata Kisumu,Kenya.
    Upungufu huu ni wa abiria wa meli ni wa takriban asilimia 50.
  Kaimu Meneja Masoko na Biashara wa Kampuni ya Meli(MSC)Kapt. Obedi Nkongoki, anasema mwaka juzi,Kampuni hii ilisafirisha jumla ya abiria 235,794 tu ambao ni chini ya uwezo wake. Mizigo iliyosafirishwa ni tani 54,212.
  Kulingana na Kapt. Nkongoki, MSC ina jumla ya meli 15 zinazosafirisha abiria na mizigo kati ya Mwanza na  Musoma,Bukoba,Kemondo,Jinja(Uganda),Kisumu(Kenya),Port Bell Uganda, na Ukerewe.
 Mv.Victoria ndiyo meli kongwe kuliko zote; ilijengwa mwaka 1960. Imekuwa ikifanyiwa matengenezo na ukarabati mkubwa na mdogo.
 Kaimu Meneja Mkuu wa Marine Services Company(MSC)Projest Kaija, anasema Mv..Victoria ina umri wa miaka 52, lakini imefanyiwa ukarabati mkubwa na mdogo mara nyingi. Mara ya mwisho ilifanyiwa ukarabati mkubwa(Major Rehabilitation) mwaka 2008 ambako ilikaa miezi sita katika Bandari ya Mwanza South Port bila kufanya huduma.
  Ina uwezo wa kuchukua abiria 1,200 na tani 200 za mizigo;lakini kufuatia abiria kupungua siku hizi inachukua abiria 500-800,chini ya uwezo wake. Inafanya safari zake kati ya Mwanza-Kemondo-Bukoba-Mwanza.
 
 
 
 

No comments:

Post a Comment