Monday, January 28, 2013

afrika kizimbani 9

Novemba 10 mwaka 2004, askari wa Kiingereza, Brett Richard(20) na Nigel David(23) walidaiwa kumbaka kwa zamu na kumsababishia kifo msichana wa Kitanzania, Conjesta Ulikaye.
   Nigel David na Brett Richards, walikuwa mapumzikoni jijini Dr es salaam.
  Waitokea vitani, Irak, hivyo wakawa wanajiburudisha katika fukwe za jiji la Dar es salaam .
 Wakiwa katika fukwe za Hoteli ya Silver Sands, tukio la mauaji ya msichana huyo likatokea.Walitiwa mbaroni, shauri lao likashughulikiwa kwa siku 36 tu.
  Walifikishwa mahakani Novemba 16 mwaka huo; yaani kesi yao ilifika mahakani siku sita tu baada ya tukio.
 Ilipofika Desemba 22 mwaka huo wa 2004, kesi dhidi yao ikafutwa na Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP) kwa kile kilichoelezwa kwamba ni kwa mujibu wa  kifungu namba 91(1) cha sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 1985.
  Aliyekuwa DPP wakati huo, Godfrey Shaidi, alisema ushahidi uliokuwepo haukutosha, hivyo hao Wazungu, askari wa Uingereza vitani Irak wakaachwa huru huria.
  Ofisi ya DPP imekuwa ikisema kesi zinacheleweshwa mahakamani zinapokuwa zikingoja kupangiwa tarehe ya kusikilizwa, wala hazicheleweshwi na ofisi ya DPP.
   Mahakama inadaiwa kuchelewesha kusikiliza kesi hasa kwa watu Weusi tena masikini wasio na ukwasi na mvuto wowote katika jamii.
  Wakati, zile kesi zinazowahusu vigogo kama akina Marehemu ‘Ditto’, Abadallah Zombe na wengine wa kariba hiyo, na Wazungu kama hao askari wa Uingereza, kesi huendeshwa kwa kasi ya ‘supersonic’ hadi wanapoachiliwa huru.
  Ni hapa, inapokuja dhana kwamba, mfumo wa sheria wan chi hii, haujali usawa kwa raia, bali unazingatia rangi, kipato, vyeo n.k
  Pia, inasemwa magereza ni kama yalijengwa kwa ajili ya wahalifu masikini Weusi, na kamwe siyo kwa Wazunagu na wenye ukwasi.
!
  Mzungu, Yunus Santy(67) ambaye alikuwa Mmisonari wa Katoliki, alifunguliwa mashitaka jijini Mwanza kwa makosa ya kufanya ngono na wanafunzi wa kike wenye umri wa miaka 17.
 Pia, alikutwa na picha za uchi na viungo bandia vya shemu za    siri za kiume(toy boy). Badala ya kutiwa hatiani na kufungwa jela miaka 30 kwa kubaka wanafunzi hao huku wakichukuliwa mkanda wa video wa kitendo hicho kichafu, Yunus Santy aliamuriwa kuondoka nchini mara moja.Hiki ni nini kama siyo woga?
Ni wazi,serikali yetu iliogopa kuwatia mbaroni hawa na kuwafunga kwa sababu Afrika haijawa huru; na iko kizimbani.
   Idara ya Uhamiaji ikaamuriwa na mahakama kuhakikisha jamaa huyo anaondoka nchini mara moja, badala ya kufunguliwa mashitaka ya ubakaji na kufungwa miaka 30 jela akaenda kwao Italia, asikanyage jela za Tanzania, ambazo utadhani walijengewa masiki Weusi, wanaotenda wizi mdogo, uzururaji na umachinga tu.
  Miaka michache iliyopita, kulitokea ugomvi kati ya mwekezaji Muingereza, Stewart Middleton na mbia wake wa biashara, raia wa Tanzania , Benjamin Mengi.
   Vyombo vya dola vya Tanzania vilipomtia mbaroni Middleton, kufuatia ugomvi wa makampuni ya kilimo ya Silverdale Tanzania Limited na Mbono Farms ya huko Hai, Kilimanjaro, Bunge la Uingereza likachachamaa.
  Mbunge toka chama cha Mahafidhina(CONSERVATIVES),Bwana Roger Gale, akasema Bungeni Uingereza kwamba Tanzania ilistahili kunyimwa misaada kwa sababu huyo Middleton katiwa mbaroni na polisi huko Kilimanjaro.
  Ilidaiwa kwamba, kitendo cha Middleton kutiwa mbaroni na kushitakiwa kwa ugomvi wao na Benjamin Mengi, basi kulikuwa kuondoa mazingira bora ya uwekezaji yanayowanyanyasa wawekezaji, hususan mabwana wakubwa wa Uingereza!
 Uingereza, kupitia Shirika lake la misaada(DFID) ilikuwa ikiongoza kutupatia msaada kuliko nchi yoyote duniani.
 Mwaka 2003\2004 misaada toka Uingereza iliongezeka kutoka pauni milioni 80(sh. Bilioni 208) hadi pauni milioni 110(sh. Bilioni 286) mwaka wa 2005 na 2006. Asilimia 70 ya fedha zote hizo zilikuwa zikiingia moja kwa moja katika bajeti ya serikali.
  Nataka kusema kwamba, katika mazingira kama hayo, vyombo vya dola vya Tanzania na mfumo wa kutoa haki wan chi hii, ulikuwa na ubavu gain kuthubutu kuwatia mbaroni Waingereza hata kama walifanya uhaini hapa?
  Tunadhani, kwa sababu ya misaada tupewayo na mataifa ya Ulaya na Marekani, basi raia wao wameanza kuabudiwa kama miungu na mabunge yao na serikali zao huogopwa kama radi ama ngurumo na mafuriko.
  Ni kwa sababu hii tu, tunadhani wale Wazunagu wawili waliokuwa mapumzikoni, Silver sands, Dar es salaam (wakitokea vitani, Irak) waliogopwa kutiwa hatiani kwa kumbaka Conjesta Ulikaye kwa zamu hadi alipokata roho.
 Naam, Serikali ya mjini Dar es salaam, wakati huo ilichelea kuwatia hatiani na kuwahukumu Wazungu wale kutoka Uingereza kifo cha kitanzi hapa hapa jijini Dar, habari zisije kufika London, halafu misaada yote ikakatwa, na vigogo woote wa hapa wakazuiliwa kukanyaga London!!
 Ilikuwa siyo rahisi Nigel David na Brett Richards kutiwa hatiani na kunyongwa hata kufa kwa kamba jijini Dar, lisije Bunge la Uingereza likajua, likafoka, misaada huku ikakatwa na mashirika mengine kama Oxfam yakafunga virago hapa.
 Ni kwa sababu hii, tunadhani hakuna haki na usawa katika mfumo wa sheria wan chi hii iliyowahi kutawaliwa na wakoloni Waingereza.
 Bado mawaziri wakuu wa Uingereza:Harold McMillan,(waziri mkuu wa Uingereza 1957-63 wakati Tanzania inapata uhuru), Alec Douglas Home, Harold Wilson, Edward Heath, James Callaghan, Margaret Thatcher, John Major,, Tony Blair na Gordon Brown wanaogopewa bungeni na katika ikulu ya Dar es salaam kama mizuka.
Utadhani sisi siyo watu huru tuliopata uhuru toka Uingereza Desemba 9 mwaka 1961. Bado tunamwogopa sana Malkia wa Uingereza, Elizabeth II(alitawazwa Feburuari 6, mwaka 1952) kiasi kwamba tunaondoa haki na uhuru wa watu wetu ili kumpigia goti          Mzungu?
  Naam, tunawapigia goti Wazungu, makaburu na wenye pesa hadi raia masikini wan chi hii wananyimwa haki au kucheleweshewa haki zao, tangu polisi hadi mahakamani.
  Mzungu tapeli akionyesha pua yake polisi, hapo hapo anadhaminiwa asije kufikishwa nyuma ya nondo. Lakini, Mweusi fukara, mpaka utoe rushwa.
 Ikitokea masikini Mweusi umedhulumiwa na Mzungu au mwenye pesa, basi mfumo wetu wa sheria unawa ‘gwaya’ hawa, sheria zinapindishwa ‘fasta’ hadi wanaachiwa huru.
 Hapa jamii yetu inaona imetengwa katika madaraja kama zilivyokuwa zama za Ukaburu, Afrika ya Kusini.
Ziko wapi sheria zinazojali haki na usawa. Iko wapi Katiba ya haki na usawa wa binadamu sasa?
  Kwa majuma mawili tumejadili ushoga,shuruti za mataifa haya na usawa katika sheria za Tanzania unavyodhulumiwa na mahayawani wachache, kwa tama zao au kwa ubaguzi.
 Ni furaha kwamba wanasheria wameanza kujadili jambo hili kupitia kituo cha televisheni cha Star cha jijini Mwanza.
  Tunakusudia haki za waliowengi zinarejeshwa, na usawa uliowekwa na katiba kisha ukaporwa na baadhi ya watu, unarejeshwa haraka.
  Kwanini tutengwe katika madaraja ya walionacho na wasio nacho, Weusi, Wazungu, machotara, mabwana
na watwana n.k utadhani zama za       Ukaburu na ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini?
 Nakupongeza Rais Kikwete,kwa ushindi,lakini nimekukumbusha haya ili awamu hii Watanzania waheshimiwe na serikali yao inayopigia goti wageni na magabacholi, na kuwapuuza raia wazalendo.
Tunapaswa tangu sasa kukemea tabia hii ya ukaburu na ukoloni wa Wazungu kama  David Cameron na wenzao
Ni kwa sababu hii, mashirika ya misaada ya Uingereza na Bunge huwa na sauti kubwa sana hapa kwetu hadi kuingilia ‘mambo ya jikoni’ kwa maslahi ya Uingereza. Haya ndiyo Amin aliyokataa enzi zake.
 Nahitimisha Msumeno wangu leo, kwa kuwakumbuka Waingereza vijana wawili: Nigel David(23) na Brett Richard(20) waliotiwa mbaroni kwa tuhuma za kumbaka kisha kumuua msichana kigori wa Kitanzania, Conjesta Ulikaye, mnamo Novemba 10, mwaka 2004.
   Tukio hilo lilitokea katika ufukwe wa Bahari ya Hindi, katika hoteli ya Silver Sands, Dar es salaam .
   Shauri la kesi ya mauaji likashughulikiwa kwa siku 36 tu, Nigel na Brett wakafikishwa mahakamani ‘Fasta’ Novemba 16 yaani siku sita tu baada ya tukio. Vibaka wa hapa wanasota rumande hata miezi sita bila upelelezi kukamilika!
   Kesi hiyo ilifutwa Desemba 22 mwaka huohuo kwa mujibu wa kifungu 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 1985.
   Mraba   wangu, uliwahi kumuuliza Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP), Geofrey Shaidi(sasa Jaji), Machi Mosi mwaka 2005 alipokuwa jijini Mwanza:
    “Hao Waingereza wawili(walikuwa wanajeshi wan chi hiyo waliokuwa mapumzikoni Dar, wakitokea vitani Irak) waliachwa huru kwa maslahi ya umma wa Tanzania au maslahi ya Uingereza?”
    “Hawakuachwa huru kwa maslahi ya Uingereza au ya Tanzania …ushahidi uliokuwepo haukutosha!Wasingeendelea kung’ang’aniwa bila ushahidi” DPP Shaidi alisema.
   “Hata hivyo, kesi(dhidi ya raia) hazicheleweshwi na ofisi ya DPP, zinacheleweshwa mahakamani, zinaposubiri kupangiwa tarehe ya kusikilizwa. Hivyo, faili la Wazungu lilipofika kwetu, tukalishughulikia(fasta?) kama kawaida”,
  alifafanua DPP Shaidi wakati huo, huku akikanusha madai kwamba Waingereza hao hawakuachwa huru kwa sababu ya kuchelea kunyimwa misaada na Uingereza endapo wangehukumiwa kutiwa kitanzi.
    Laiti Nigel David na Brett Richard wangefanya unyama wao huo wa kumbaka msichana kwa zamu na kumsababishia kifo huko Uganda , enzi za Amin, bila shaka wasingeepuka kitanzi!
   Hata kama Mawaziri Wakuu kama Margaret Thatcher, James Callaghan, Edward Health, John Major, Tony Blair na Gordon Brown kwa pamoja wangemkoromea Amin, bila shaka Nigel na Brett wangenyongwa tu!
Afrika inazidiwa na Amin? Afrika iko kizimbani kwa kukosa sauti hadi sasa majeshi ya kigeni ya Kifaransa yanapoingilia mizozo Mali,Afrika ya Kati n.k Umoja wa Afrika(AU) ukiwa kimya!
      0786/0754-324 074
  
 
 
 0786-324 074
 
 
 

No comments:

Post a Comment