Monday, January 28, 2013

KAMBONA NA NYERERE NANI ALIKWAPUA MABILIONI YA WATANZANIA?

AZIMIO LA ARUSHA ,lilipoanzishwa mwaka 1967, liliwafanya baadhi ya mafisadi waliojichotea mali za mabilioni kutimkia uhamishoni?
Kwa sababu hiyo, miongoni mwa ‘mabilonea’ hao, labda ni Oscar Salathiel Kambona?
Tujadili msuala ya zamani kidogo,ili kutazama kwa kina ujanja wa siasa. Kambona alishika nafasi nyingi,nyeti sana serikalini na katika Chama cha Tanganyika National Union(TANU) zama hizo.
Alikuwa waziri katika wizara nyeti, tena akawa Katibu Mkuu wa TANU,kabla ya kutimkia Uingereza mwaka 1967 baada ya kukosana na Hayati Baba wa Taifa,Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Ilikuwa kuhusu Azimio la Arusha.
Kambona, ati alikuwa na mali nyingi za mabilioni ya fedha,majumba mengi ya kupangisha jijini Dar es salaam na kwingineko nchini.
Wakati wa Azimio la Arusha kumiliki mali nyingi ilikuwa kuhalifu sera za nchi,na ulikuwa Ubepari.Kambona alipingana na Nyerere.
Aliteuliwa kuwa waziri kwa mara ya kwnza katika serikali ya MADARAKA.Septemba 9 mwaka 1960 wakati Tanganyika ikijiandaa kupokea uhuru kutoka kwa ukoloni wa Kiingreza.
Aliteuliwa waziri wa Elimu,wakati huo Julius Kambarage Nyerere alikuwa waziri Kiongozi,wadhifa sawa na Waziri Mkuu.Aliendelea kuwa waziri wa Elimu chini ya Waziri Mkuu,Kambarage Nyerere,na baadaye Rashid Mfaume Kawawa.
Madaraka hayo yalimpa kuheshimiwa sana na kupendwa na wananchi.Baada ya nchi kuwa Jamhuri,Desemba 9,mwaka 1962,Kambona aliteuliwa kuwa waziri wa Mambo ya Nchi za Nje,baadaye tena akaongezewa  madaraka na kuwa waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ulinzi.
Alikuwa na kawaida ya kuchana nyewele zake akazipinda pembeni kidogo mwa uso wake.Mtindo huo ulijulikana sana miongoni mwa vijana wa wakati huo kama, “Kambona Style”,wakati huo kabla hujachana nywele kwa mtindo huo wa Kambona,basi ulionekana wa kuja.
Kambona,ndiye aliyezima uasi wa jeshi lililotaka kumpindua Mwalimu,Januari 20 mwaka 1964.Siku hiyo wakati Jeshi likiasi,Rais NYERERE,Makamu wa Rais Kawawa na mawaziri wengine walitimkia mafichoni kusikojulikana.
Baadaye,jeshi likavunjwa likaanzishwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ), lakini baadaye baada ya kuanzishwa Azimio la Arushwa,mwaka 1967 Kambona akapinga,kwa kile wanachosema, alikuwa na mali nyingi ambazo zilikuwa mbioni kutaifishwa na umma.
Alijifanya kuugua, akaenda Nairobi nchini Kenya kutafuta tiba. Akiwa Nairobi,yeye Kambona na mkewe,Flora na binti yao wakakwea ‘pipa’ kwenda London,Uingereza.
Alipofika London,akaomba ukimbizi wa kisiasa.Wakati huo,Mwalimu alikuwa amevunja uhusiano wa kibalozi na Uingereza,wakati huo ikiwa serikali ya Waziri Mkuu,Harold Wilson,kufuatia mgogoro wa Rhodesia, siku hizi ni Zimbabwe.
Uhusiano wa kibalozi wa Tanzania na Uingereza ulivunjwa kuanzia mwaka 1966 hadi 1969.
Kufuatia hali hiyo,Kambona alikubaliwa ukimbizi wa kisiasa Uingereza, huku byuma aliacha wafuasi ambao wengine walitiwa mbaroni na wengine kutimkia ng’ambo.
                            Dk.Masha mshirika wa Kambona?
Kambona akatimuliwa uanachama wa TANU,akaondolewa ubunge pamoja na wenzake  wanne.
Miongoni mwa wabunge waliotimuliwa mwaka 1968 ni Dk.Fortunatus Lwantyantika Masha(Mbunge wa Jimbo la Geita Mashariki zama hizo),Joseph Kaselabantu(Nzega Mashariki),Wilfred Mwakitwange(Taifa),Stephen Kibuga(Mufindi) na Modestus Chogga(Iringa Kusini.
Wengine ni Eli Anangisye(Rungwe Kaskazini),Gervas Kaneno(Karagwe) na Jeremiah Bakampeja(Ihangiro,Bukoba).
Januari 22,mwaka 1968,kikao cha kwanza cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kikatajiwa mali nyingi za Oscar Kambona,aliyetimkia Uingereza.
Kwamba,kabla hajatimkia London,aliingiziwa katika akaunti zake katika benki moja ya Uingereza shllingi 500,000 ambazo leo ni kama milioni 600 hivi.Ilikuwa Desemba 6,mwaka 1966 miezi miwili kabla ya Azimio la Arusha.
Kauli hiyo ilitolewa na Kawawa,wakati huo Waziri Mkuu, alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Rombo,Alphonce Maskini,bungeni.
                                             KAMBONA FISADI?
Baada ya Azimio la Arusha,ikatangazwa kwamba Kambona alimiliki majumba mengi ya kupangisha Dar es salaam,Morogoro,Songea ambayo thamani yake ilikuwa shilingi 485,612 sasa ni kama shilingi milioni 500 hivi.
Kawawa alisema pia kwamba,KATI YA Juni 1965 na Desemba 1966 Kambona aliweka katika akaunti yake ya Jijini Dar es salaam kiasi cha shilingi 896,800 ambazo leo zingekuwa na thamani  kama shilingi bilioni moja hivi.
Matokeo ya uchunguzi wa Benki Kuu(BoT)ULIBAINI PIA KWAMBA,Juni 1965 Kambona aliingiza Pauni za Uingereza 65,800 ambazo leo ni kama shilingi milioni 165.Julai 1967 eti aliweka Pauni 60,000 ni shilingi milioni 150 za sasa.
Na kwamba,alikuwa akiingiza pesa nyingi kwenye akaunti zake,na alimiliki majumba mengi yaliyojengwa Dar kwa mabilioni ya shilingi.
                        Ati, Mwizi Mkubwa?
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alimtaja Kambona kama ‘mwizi mkubwa’ leo tungesema Fisadi Kubwa lililojilimbikizia mali nyingi.Benki kuu ya Tanzania(BoT) Ikamwandikia barua aeleze alikopata fedha za kigeni kumwezesha kukwea ‘pipa’ kutoka Nairobi hadi London.Kumbuka wakati huo kupata fedha za kigeni ilikuwa ‘mbinde’ siyo kama siku hizi kuna Bureau De Change, tena kuna dola nyingi na Euro kwenye Black Market.
Haya yalielezwa Bungeni na Waziri Mdogo wa Fedha,Bwana S.Rashid alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Bagamoyo,Bwanga Mgaza.
Kambona akiwa Uingereza alishinda Bahati Nasibu, ‘Bingo’ ya kimataifa na kulipwa mamilioni ya pesa.
Wakati vyama vingi vikianzishwa hapa nchini mwaka 1992,Kambona alirejea nchini na mkewe,Flora na binti yao.
                               Bilionea,Masikini gani huyu?
Aliishi Sinza, katika nyumba ya kawaida sana.Alidai arejeshewe nyumba yake ya Msasani,ambayo ilidaiwa ilikaliwa na Rashida Kawawa.
Huyu anadaiwa kuongoza majaribio ya kutaka kumpindua Mwalimu Nyerere,mapinduzi ambayo aghalabu yalishindikana.Kambona alikanusha kuteka ndege ya abiria kutoka Mwanza hadi London,mwaka 1982,nilishasimulia kituko hicho.
Mwaka 1992, aliporejea Tanzania Kambona akachaguliwa kuwa Rais wa Chama cha TADEA.Alipokonywa uraia akaambiwa ni Mnyasa wa Malawi,akaamuliwa aondoke nchini.
Alikaidi, akabaki Dar lakini mwaka 1993 serikali ikamrejeshea uraia wake kwa sababu za kiutu.Alifariki akiwa London,Uingereza mwaka 1997,mwili wake ukarejeshwa Dar es salaam kwa mazishi.
TADEA Kimeongozwa muda mrefu na RIFA Chipaka,Mshirika wa Kambona aliyewahi kufungwa kwa makosa ya uhaini,mwaka 1971 baadaye alisamehewa.
Azimio la Arusha likatokomezwa miaka ya  karibuni,kwa sababu hiyo Kambona angekuwa hai na mali zake angekuwa ‘tycoon’ la Afrika kama siyo duniani.
Sasa jiulize,pesa zake zilikwenda wapi? Majumba yake yalikwenda wapi? Angekuwa mwekezaji!
Oscar Salathiel Kambona, alizaliwa Agosti 13, mwaka 1928 kandoni mwa ufukwe wa ziwa Nyasa ambalo linaleta kasheshe baina yetu na Joyce Banda,mjukuu wa Kana-Ka Mzizi,Banda.
Alizaliwa katika kijiji cha Kwambe,Mbamba Bay eneo la wilaya ya Mbinga.
                                       Rafiki Mkia wa Fisi?
Walikutana na Mwalimu,Julius(Butiama walimwita Kambarage tu)Nyerere katika sekondari ya Tabora Boys.Wakati huo,Mwalimu alikuwa akifundisha katika shule ya  St. Mary’s  ya Wakatoliki pale Tabora. Baadaye sasa ndipo Kambona aliteuliwa Katibu Mkuu wa TANU.
Wakati wa maasi ya jeshi la kikoloni,Januari 1964,Kambona alijitoa mhanga akawafuata wanajeshi Calito(Lugalo) jeshini;badala ya kurushwa kichura akaongea nao na wakakubaliana.Akina Nyerere na Kawawa na mawaziri walishajificha kabisa.
Askari walitaka nyongeza ya mishahara,na walitaka wale askari wa Uingereza wapishe vyeo askari Weusi wazalendo,ilikuwa ngoma nzito,Nyerere  na Kawawa walishatoroka-Mapinduzi!
Kambona katuliza fujo,mambo yakawa shwari,ukawa urafiki mkubwa na Mwalimu.Wakati Kambona anamwoa aliyekuwa Miss Tanzania,Flora,Nyerere alikuwa Best Man!
Kumbe,rafiki mkia wa fisi? Kambona na Nyerere wakakorofishana,Kambona katimkia London, Julai mwaka 1967akawa anafanya kazi ya mshahara mdogo,na nyumba ya kuishi alilipiwa na Uingereza kwa ruzuku ya serikali. Utajiri alipeleka wapi?
Kufuatia kuondoka kwake,nduguze,Mattiya na Otini Kambona walitiwa mbaroni na serikali. Unacheza wee!
Jaribio la mapinduzi la Oktoba 1969 alisemwa kuhusika,alihukumiwa akiwa uhamishoni,aliporejea nchini mwaka 1992 akaahidi ‘kutoboa siri’ mahali Nyerere na Kawawa walipoficha mabilioni ya fedha walizouibia umma wa Watanzania!!
Kumbe, ‘geresha’ tu, wanasiasa bwana! Kambona hakuwahi kuwatajia Watanzania fedha walizoiba Nyerere na Kawawa tangu Uhuru.
“Credibility” ya Kambona ilishuka,watu wakamwona aliyechanyikiwa tu,akazidiwa kete na akina Mtikila na Mrema, alisema uongo. Hadi anakufa London Julai mwaka 1997 hakuwa na mvuto tena katika siasa za Tanzania.
Atakumbukwa kama mkimbizi wa kwanza wa Tanzania London, alipigia debe mfumo wa vyama vya upinzani,na alijaribu kumpindua Mwalimu.
              Propaganda,chenga ya mwili ama Danadana?
Hayati Mwalimu Nyerere na Kawawa,walisema Kambona aliiba mabilioni ya shilingi na kutokomea nayo Uingereza.
Wakati Oscar Salathiel Kambona, alipofika uwanja wa ndege wa Dar wakati anarejea toka uhamishoni,akasema angemwaga mtama mahali Nyerere na Kawawa walipoficha pesa walizoiba nchini!
Hata hivyo, hawa wote watatu wamefariki.Nasi tungali tunajiuliza, “Hizo fedha zilizodaiwa kuibwa(na pande mbili za shilingi) na Nyerere,Kawawa na Kambona, zilifichwa wapi? Ama,ndiyo mabilioni ya Uswisi?
Bila shaka, hapakuwa na mwizi mahsusi kati yao wote watatu,bali propaganda tu kati yao na kuchafuliana majina!
0713 324 074
 
 
 
 
 
 

1 comment: