Monday, January 28, 2013

TUMKUMBUKE KABILA WA CONGO HII JANUARI

Tumkumbuke Hayati Laurent Desire Kabila na Patrice Lumumba, na tujiulize nani aliwaua?
 
 Januari 16 mwezi huu, Rais wa zamani wa J.K. Kongo, Laurent Desire Kabila, alitimiza miaka 12 kamili tangu auliwe na mlinzi wake, Meja Rashid Kasereka katika Ikulu ya Kinshasa .
  ‘Papa’ Kabila, alikufa Jumanne, Januari 16 mwaka 2001, kwa kupigwa risasi ndani ya Ikulu hiyo, kufuatia mgogoro baina yake na washirika wake waliomwezesha kuwa kiongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Waliomwezesha Kabila kuingia Ikulu walimuua na sasa wanautafuta uhai waaaaa Kabila mtoto!
  Kabla ya mauaji hayo, nchi hiyo maarufu sana Barani Afrika, ilikwisha geuka uwanja wa vita vilivyosababisha  Mataifa ya kigeni: Rwanda , na Uganda kujipenyeza ndani yake kwa kisingizio cha usalama wan chi zao.
 Sambamba na kuyasaidia majeshi ya waasi wa serikali katika harakati zao za kutaka kuipindua serikali kwa madai kuwa ilikithiri kwa rushwa, ukabila,upendeleo na utawala mbovu.
   Naam. Miaka 12 kamili baada ya kifo cha ‘Papa’ Kabila, roho mchafu wa rushwa, ukabila, upendeleo na utawala wa hovyo, angali akitafuna mataifa haya yote ya Maziwa Makuu; hata kama mengine yana amani ya kuegesha.
    Rwanda , Burundi , Kongo yenyewe na sasa Kenya hutafunwa na ukabila; wakati majirani zetu kama Somalia na Sudan , hususan Darfur, tatizo hilo linafanya nchi kuvunjika vipande, na maelfu ya watu kufa, wengine makazi kutafuta hifadhi ya ukimbizi katika mataifa  mengine,
   Angola , Zimbabwe na Namibia zilijitosa kumsaidia Hayati Kabila asipinduliwe mapema na vikosi vya waasi wakiongozwa na Watutsi wa ‘Banyamulenge’.
 Licha ya kukubaliana kuacha mapigano katika majadiliano ya siku 13 mjini Lusaka , Zambia yaliyofanyika tangu Julai 10 mwaka 1999; vita vikaendelea katika nchi hiyo ya tatu kwa ukubwa Afrika; na yenye utajiri wa madini ya thamani kubwa.
   Mahali penye utajiri wa nishati na madini kama almasi na dhahabu ndipo mafisadi huchochea ukabila na vita vya kila mara ili wananchi wa kawaida, wasije wakapata fursa kusaka maendeleo huru nay a dhati. Naam,makampuni ya Magharibi.
   Kati ya Feburuari 24 na Juni 16 mwaka 2000, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliingilia kati mgogoro wa Kabila na Banyamulenge, na kuamuru majeshi ya kigeni kuondoka.
    Tumeona Rwanda na Uganda wakiwasaidia Banyamulenge kumwondoa ‘Papa’ Kabila madarakani, na tumeona Namibia , Zimbabwe na Angola yakisaidia majeshi ya serikali kuvitimua vikosi vya waasi
Hapakuwa na mafanikio.
   Basi, Baraza hilo likaamuru kupelekwa askari wa Umoja wa Mataifa wapatao 5,537 ili kusaidia kutekeleza makubaliano na kusitisha vita.
Katika jitihada za kumwokoa Kabila, alikutanishwa na Rais wa Rwanda , Meja Paul Kagame nchini Kenya ambako nako siku hizi baadhi ya watu, wakiwemo watoto na akina mama wanateketea katika miali mikali ya moto na maiti zao kuwa majivu. Unakumbuka vita vya baada ya uchaguzi,mwaka 2007?
   Kagame alikutana na Kabila nchini Kenya Juni 13 mwaka 2000.
Mapigano yakaendelea; yakasambaa hadi katika roho ya nchi penye utajiri wa madini na shughuli za kiuchumi.Siku hizi wanakutana Kampala.
   Naam. Utawala wa Kabila ulikoma Januari 16, mwaka huo 2001; yeye mwenyewe akauliwa kwa risasi kutoka kwa mlinzi wake ndani ya ikulu. Mlinzi huyo, Rashid Kasereka, aliuawa punde.
Kabila akarithiwa na mwanaye, Meja Joseph Kabila Kabange(42), anayejaribu kurejesha amani na kuleta maelewano miongoni mwa makabila yote ya ‘Bacongo’.
   Bado kuna vita na mauaji; na majeshi ya kigeni yangali yakichochea migogoro Kongo.
Naam, migogoro ya Kongo huchochewa na baadhi ya waafrika wenzetu, vibaraka wa Wakoloni wa zamani, kwa tamaa ya rasilimali za nchi.
  Kabila alifanya kazi moja…kukomesha utawala wa kibaraka mkongwe wa wazungu Afrika, Marehemu Dikteta Kuku Mbendu wa Zabanga wa Zaire ,maana yake Buldoza,linakopita hakibaki kitu!
, koplo wa zamani Seseseko Joseph Desire Mobutu!
Ilikuwa Mei 17, mwaka 1997.
   Kabila, akaibadili Zaire kuwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, baada ya kushika hatamu zote, kufuatia ushindi katika vita ‘laini’ dhidi ya serikali taabani ya Mobotu.
Baadaye, Banyamulenge waanzisha uasi dhidi ya ‘Papaa’ katika miji ya Bukavu na Goma mnamo Agosti Pili, 1998. Vikosi vya waasi vilipata nguvu kutoka nadharia ya Kitutsi ya majeshi ya Rwanda na Uganda .
   Inadaiwa, utawala wa Kabila uligubikwa chuki, mafarakano na uchoyo uliozaa mauti yake mwenyewe.
   Alirithi utawala wa choyo na rushwa toka kwa Mobutu, aliyesimikwa madarakani kwa masaada wa Mabeberu wa Magharibi, baada ya mauaji ya Waziri Mkuu, Patrice Emery Lumumba, mwaka 1961.
Tumekwishaona jambo hili,usikose safu hii.
   Kabila alipiga marufuku vyama vya siasa Mei 20 mwaka 1997. Akamweka kizuizini mwanasiasa aliyempinga, Etiene Tshisekedi. Tshisekedi alizuiliwa kijijini kwao Kasai, Feburuali 12, mwaka 1998 kwa sababu zili walizonazo watawala wetu hadi sasa- za hofu ya kuondoshwa mamlakani.
   Hayati Kabila alikuwa na uhusiano na Rwanda na Uganda tangu zamani. Biashara ya magendo ya almasi na dhahabu pengine ilifanyika wakiwa pamoja, ili kuimarisha vikosi vyao.
Kabila aliipinga serikali ya Kongo, Museveni alimpinga Obote na baadaye Tito Okello, na Kagame aliwahi kwenda msituni na waasi wa RPF dhidi ya serikali ya Rwanda .
    Walihitilafiana.
Museveni na Kagame wakaanza kumpinga Kabila, wakasaidia waasi ili kumwondoa huku kukiwa na madai ya kuiba madini.
 Baadaye majeshi ya Rwanda na Uganda yalichapana ndani ya Kongo kwa sababu zinazofahamika. Kumbukumbu ya hayati Kabila itufundishe kujua aina ya viongozi tulionao Afrika. Ni vibaraka wa adui wa Afrika.
   Uganda iliingiza jeshi lake Kongo mwaka 1998 kwa kisingizio cha kuharibu makambi ya waasi wa serikali wa Allied Democratic Front.
Ilidaiwa, walipata msaada toka Sudan .
Serikali ya Kampala ikihofia kwamba kulikuwa na makambi ya mafunzo ya waasi katika Kabaya, Kanyabayonga, Kibumba na maeneo ya jirani  na Goma.
    Majeshi ya UPDF na RPA yaliingia Kongo kupigana bega kwa bega  na waasi dhidi ya serikali ya Kabila.
Umoja wa Mataifa uliweka sharti majeshi hayo kuiacha Kongo chini ya Jeshi lake, UN Military Observer Mission for Congo (Monusco).
   Uganda na Rwanda zilionyesha kudharau amri hiyo wakaendelea kuwalea waasi wengi, akina Mbusa Nyamwisi(baadaye alijiunga na serikali), Profesa Ernest Wamba dia Wamba, na wale wa RCD Kisangani.
Mbusa Nyamwisi alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje  baadaye. Ni vita,ili kugawana madini ya Afrika.
   Hata baada ya Kongo kufanya uchaguzi wa Kidemokrasia, na  Rais Kabila kushinda, Kongo kungali na vita ya kikabila.
Yamefanyika mapatano kati ya Marais Kabila na Yoweri Museveni yaliyosimamiwa na Rais Kikwete katika hoteli ya Ngurdoto, Arusha. Hakuna kitu,vita vinaendelea kwa miaka 51.
   Inadaiwa, licha ya mapatano ya kuacha chokochoko, Rais Kabila hajamwamini sana Museveni.
   Kongo, kungali na Waasi wa Kitutsi kama, Laurent Nkundabatwale, wanaojaribu kukalia milima ya  Rumuhe na Mumba, Kaskazini mwa mji wa Ngundu. Kuna akina Bosco Ntaganda na wenzao wa M 23.
   Joseph Kabila, ambaye aliwahi kusoma Tanzania na kupata mafunzo ya kijeshi, JKT Makutupora, na baadaye Uchina, alimrithi babaye Januari 24, akaapishwa siku mbili baadaye, mwaka huo wa 2001.
    Baada ya kushinda uchaguzi na kuunda serikali, anaongoza nchi kubwa yenye watu zaidi ya milioni 60.
Hii ndiyo nchi mabeberu walimuua Patrice Lumumba Januari 17 mwaka 1961.
    Ndiyo, mwezi huu unaokwisha tunamkumbuka pia mwanamapinduzi Patrice Emery Lumumba, katika mapambano ya kudai uhuru wa kweli,  na njama za vibaraka.
 Ni kipindi cha kukumbuka urais wa akina Moise Tshombe, Juni 30 mwaka 1964.
    Jenerali Mobutu alitawala 1965, Congo ikawa Zaire mwaka 1977 kutoka Jamhuri ya Kongo toka 1966.
 Kabila, aliwatumia Watutsi kupindua serikali ya Mobutu ambaye alikuwa akitibiwa saratani, Ughaibuni, Mei 17, mwaka 1997.
   Mobutu alikwenda uhamishoni, na baadaye akafariki mjini Rabat Morocco , Septemba 7 mwaka huohuo.
 Mobutu ametawala Congo miaka 33; lakini ameondoka bila heshima sawasawa na Idi Amin, Jean Bedel Bokassa, na wengine wa kariba hiyo. Mafisadi wanaojifanya vibaraka wa Mzungu hapa nyumbani.
 Historia haiwaheshimu watawala mafisadi wa dunia, japokuwa wataiba sana na kuwa matajiri.
  Hawa hawana heshima kama akina Nyerere, Nkrumah, Samora, Gamal Abdel Nasser, Mandela na wengine.
   Tunapomkumbuka Kabila na Lumumba, tuitazame Afrika inavyoteketea katika moto baada ya madai ya mbinyo wa demokrasia na wizi wa kura.
Tuwatazame raia fukara dhidi ya watawala matajiri walioshiriki kuiuza Afrika vipande thelathini vya fedha.
    0786 324 074’0754 324 074

 

No comments:

Post a Comment