Thursday, May 31, 2012

Kuelekea Olimpic London, 2012


 
MASHINDANO ya Olimpiki ya majira ya kiangazi yanayotarajiwa kufanyika London, mwezi Julai,  mwaka huu, yalianza zamani sana, karne tano kabla ya Kristo.
   Yale mashindano ya Olimpiki tunayoshuhudia siku hizi, yalianza Athens huko Ugiriki mwaka 1896
.Hufanyika kila baada ya miaka minne, wakati leo wanariadha wanaoshiriki wameongezeka kutoka nchi 13 mwaka 476 BC hadi zaidi ya 200 hii leo.
    Alama ya mashindano haya ya Olimpiki ni miduara mitano iliyoungana; inayowakilisha urafiki na udugu wa kimichezo wa watu wa mabara yote.
Miduara hii pia huwakilisha mabara natano ya kijiografia, ambayo ni Afrika, Asia, Ulaya, Australia na Amerika.
  Kila mduara una rangi tofauti kulingana na rangi ya watu wake. Miduara hii ina rangi nyeusi(Afrika), bluu(Ulaya), njano(Asia),kijani( Australia ) na Amerika wanawakilishwa na rangi nyekundu.
 Miduara hii mitano huwa katika bendera nyeupe ya Olimpiki.
   Madhumuni ya ushiriki wa mashindano haya si kushinda medali peke yake, bali ni kushiriki. Maisha ya kawaida ya mwanadamu si shangwe ya ushindi; ni kupambana.Yaani, kitu muhimu si kushinda bali ni kupambana kwa ari kubwa.
    Kauli mbiu ya mashindano ya Olimpiki ni “Citius, Altius, na Fortius” ambayo ni maneno ya Kilatini, maana yake, ‘Kupaa haraka, Juu na kwa Nguvu’. Afrika haina budi kushinda mafashisti mamboleo na kupaa juu kwa haraka na nguvu katika nyanja zote za maendeleo.
   Kiapo cha kila mwanamichezo anayeshiriki kushindana katika mashindano ya Olimpiki, ni kushindana kwa heshima kulingana na sheria na kanuni zinazoongoza mashindano; kuwa na uanamichezo na utukufu wa kweli wa mashindano, bila kusahau kuipa heshima timu ya kila mwanamichezo anayehusika.
    Mwenge wa Olimpiki uliotua Dar es salaam mwaka 2008, ukishuka kutoka dege kubwa la rangi ya ‘Pinki’ hivi, ulianza kukimbizwa mwaka 1936. Tayari mwenge huu umewashwa huko Athens.
.Zamani, mwenge huo uliwashwa kwa miali ya jua huko Olimpia(asili ya mashindano yenyewe), huko Ugiriki. Badaye, mwenge ulichukuliwa kupelekwa uwanja wa mashindano kwa meli au ndege.
    Dar es salaam mwenge huo ulikimbizwa kwa amani bila kitisho cha waandamanaji, ama al-Qaeda. Mashindano ya kisasa ya Olimpiki yalianza Athens mji mkuu wa Ugiriki mwaka 1896; miaka minne baadaye yalifanyika jijini Paris.
    Mwaka 1904 mashindano haya yalifanyika  St. Louis , Marekani. Mwaka 1906 yalifanyika Athens , lakini hayakutambuliwa na Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa(IOC). Mwaka 1908 yalifanyika mjini London kwa mara ya kwanza.
   Mwaka 1912 mashindano ya Olimpiki yalifanyika Stockholm nchini Sweden , 1920(Antwerp-Ubelgiji); 1924(Paris-Ufaransa);1928(Amsterdam-Uholanzi);1932(Los Angeles-Marekani);1936(Berlin-Ujerumani ya enzi ya Hitler);1948(London- Uingereza);1952(Helsinki-Finland);mwaka 1956 yalifanyika Melbourne-Australia, 1960 yalifanyika Rome mji mkuu wa Italia.
   Mwaka 1964 mashindano yalifanyika Tokyo , Japan , wakati yale ya 1968 yalifanyika Mexico City nchini Mexico . Mwaka 1972 mashindano yalifanyika jijini Munich , Ujerumani Magharibi wakati huo; yaliacha alama ya kitisho cha magaidi, kama ilivyo zama hizi za al-Qaeda.
   Septemba 5, mwaka huo wa 1972 magaidi wanane wa Kipalestina kutoka kundi liitwalo, Black Septemba, walidhamiria kulipa kisasi dhidi ya adui zao Waisraeli.
Walijipenyeza katika mabweni ya wanariadha katika kijiji cha Olimpiki(wakati wa ufunguzi wa mashindano); wakiwa wamevalia viruwiruwi(mask) nyusoni mwao, waliwatwanga risasi wanariadha wawili wa Israeli, kabla ya kuwateka nyara wengine tisa.
   Magaidi hao wa Black September walikuwa wakiwadai Waisraeli kuwaachia huru mateka wanamgambo 200 wa Kipalestina waliokuwa wamekamatwa na majeshi ya Israeli wakati huo.
    Black September, wakaitaka serikali ya Ujerumani Magharibi kuwasafirisha kwa helkopta wao na mateka wao hadi katika uwanja wa ndege ulio nje ya Munich.
Waliitaka serikali baadaye iwapeleke katika nchi yoyote ya Kiarabu, iliyokuwa ikiunga mkono Wapalestina kujitawala katika ardhi yao .
   Naam.Wapalestina waliwateka nyara wanariadha wa Uzayuni kama kisasi cha kutaka mateka wa Kiarabu kuachiliwa huru; wakijua wakati huo wa michezo ya Olimpiki, suala lao lingetangazwa sana na vyombo vyote vya Habari vya dunia nzima.
   Baada ya majadiliano makali Wajerumani waliamua kuwachukua magaidi wale(nisihukumiwe kuwaita hivi hata kama ni wanaharakati) na mateka wao hadi katika uwanja wa Furstenfeldbruck.
   Vikosi vya usalama vya Ujerumani vilifanya ujanja wa hali ya juu, vikauzingira uwanja huo na kuwasubiri. Walipotua tu uwanjani, kabla ya kushuka ndegeni, mapambano ya silaha yakaanza.
    Magaidi watano wa Kiarabu waliuliwa, wengine watatu wakatiwa  mbaroni. Hata hivyo, walikwisha waua wale wanariadha wote tisa wa Israeli, waliotekwa nyara mabwenini, kule Munich katika kijiji cha Olimpiki.
    Tukio hilo liliidhalilisha sana serikali ya Ujerumani Magharibi, baadhi ya mataifa yakatishia kususia mashindano. Huu ni wakati gaidi la kale sana la kimataifa, Carlos The Jackal, linalotumikia kifungo cha maisha Ufaransa, lilipotuhumiwa kupanga mashambulizi hayo.
   Sakata hilo lilipita, mashindano hayo ya Munich yakaendelea kama ilivyopangwa.
 Mwaka 1976 mashindano ya Olimpiki yalifanyika Montreal Alberta Canada .
Mwaka 1980 yalifanyika Moscow Urusi ya zamani, ambako Tanzania iliwakilishwa na mabalozi wengi wakiwemo akina Luliga Musa, Mwinga Mwanjala n.k
   Mwaka 1984 yalifanyika Los Angeles, Marekani. Mwaka 1988(Seoul-Korea Kusini); 1992(Barcelona-Uhispania); mwaka 1996(Atlanta-Marekani);mwaka 2000(Sydney-Australia); mwaka 2004 yalifanyika tena Athens, Ugiriki yalikozaliwa; lakini chini ya ulinzi mkali sana, kufuatia kitisho cha magaidi wa al-Qaeda.
   Mwaka huu wa 2008 mashindano haya yalifanyika Beijing nchini Uchina, huku kukiwa na kitisho cha matetemeko na magaidi wa al-Qaeda na wa Tibet.
 Mwaka 2012 mashindano haya yatafanyika mjini London. Hata huko London kitisho cha magaidi kingalipo…Afrika haijawahi kuandaa mashindano haya adhimu duniani. Kwa nini na kwa sababu gani? Kama ni suala la usalama, mbona hata Munich magaidi walitamba? Afrika itaandaa mashindano haya lini?
    Zamani, mabingwa wa Olimpiki walituzwa taji ya majani ya mizeituni
.Leo, mashindano haya huandamana na tuzo za kitajiri. Mashindano ya sasa yanapoteza maudhui ya Olimpiki, kama tulivyokwishakuona. Uzalendo unapotea, Olimpiki ni mnada tu wa kusaka utajiri.Mabingwa wa Afrika hurubuniwa kwa rushwa na Wazungu!
   Mraba huu unawakumbuka mabingwa wa Olimpiki, hususan askari shujaa sana wa Kigiriki aitwaye, Pheidipides.
Huyu, alitimka umbali wa mali kama 29 hivi, kutoka mahali paitwapo Marathon kwenda mjini Athens.
   Mwaka 490 BC Majeshi ya Waperizi(Iran ya leo) yalikwenda mahali paitwapo Marathon na kutaka kuivamia Ugiriki. Walikuwa na majeshi makubwa sana, kwa bahati jeshi dogo la Ugiriki likafanikiwa kuwapiga na kuwafukuza kabisa.
   Jemadari wa Jeshi la Ugiriki akamtuma Pheidipides kwenda mjini Athene(wakati huo) kwenda kupeleka Habari njema za ushindi.Ulikuwa wakati wa Mfalme Dario wa Umedi-Soma kitabu cha Danieli sura 2-3
  Basi, alipofika mjini Athens, sokoni kwenye mkusanyiko wa watu wengi, alifanikiwa kusema kwa shida sana kwamba jeshi lao lilikuwa limelishinda jeshi la wavamizi.
   Alipomaliza kusema, akaanguka mchangani na kufa!
 Mbio za Marathon zikaanzishwa kwa lengo la kumkumbuka shujaa, Pheidipides.Hizo zilikuwa enzi za Mfalme Dario anayesimuliwa Habari zake katika Biblia, katika Danieli.
 Utaona kuwa neno Olimpiki limetokana na Olympia, neno Marathon ni mahali alipoanza kutimka shujaa huyo kwenda Athens.
    Mabingwa wengine wa Marathon ni pamoja na Joan Benuit wa Marekani mwaka 1984,Rosa Mota wa Ureno(1988); Valentina Yegorova(1996), Fatuma Roba wa Ethiopia(1996) na Naoko Takahashi wa Japan mwaka 2000.
   Afrika inang’ara ipasavyo katika bendera nyeupe ya OIlimpiki. Mabingwa wa Marathon wa Afrika ni pamoja na  Abebe Bikila wa Ethiopia(1960,64); Marmo Wolde wa Ehiopia(1968);Josia Thugwane wa Afrika Kusini(1996); na Gezahgne Abera wa Ethiopia mwaka 2000. Rekodi za 2004 hazikuwekwa.
   Waama, mraba huu unamkumbuka sana kaka yetu, Jesse Owens, Mmarekani mwenye asili ya Afrika aliyeshinda medali nne za dhahabu katika mashindano ya Olimpiki ya mwaka 1936 mjini Berlin.
 Jesse Owens, alitimka kwa dakika 45 akawa na medali hizo nne,  pamoja na kushinda mita 200.Aliyekuwa mgeni wa heshima wa mashindano hayo, Dikteta Adolf Hitler, aliamua kususa kutazama mtu mweusi akishinda
 Aliondoka uwanjani hapo na kusema kwamba hakuwa tayari kuona ‘mnyama’ Owens, akiwanyanyasa binadamu(Wazungu).Wangalipo wenye mawazo kama Hitler hata sasa, wengine wamezaliwa Afrika.
   Hitler, ndiye mjenzi wa uwanja huo wa Berlin ilikokuja kuchezwa fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2006(miaka 70 baadaye) kati ya Ufaransa na Italia.
Ufaransa iliyokuwa na Weusi wengi katika kikosi chake, ilitukanwa kwamba ilishindwa kwa sababu ya hao Weusi!
   Tena, Michael Materrazi alimtukana Zenedine Zidane “Zizou” kwamba alikuwa gaidi, kutokana na asili yake ya Algeria.Zidane alimtwanga kichwa kikali, akatolewa nje kwa kadi nyekundu! Naam, mzimu wa unyanyapaa na  ubaguzi  wa rangi ungalipo mjini  Berlin hata baada ya Dikteta, Fashisti Adolf Hitler kujiua.
   Mabingwa wengine wa Olimpiki kutoka Afrika ni pamoja na Paul Erang wa Kenya aliyeshinda mita 800 mwaka 1988, William Tanui pia wa Kenya(1992). Mwaka 2000 Noah Kiprono Ngenyi wa Kenya alishinda mita 1,500, Mirutus Yifter wa Ethiopia alishinda mita 5000 mwaka 1980, Said Aouita wa Morocco alishinda 1984 hizo mita 5000, Venuste Niyongabo wa Burundi alishinda 1996 na Milton Wolde wa Ethiopia aliwika katika mashindano hayo mwaka 2000.
    Katika mita 10,000 Naftali Temu wa Kenya alishinda 1968, Miruts Yifter wa Ethiopia akashinda mwaka 1980. Haile Gebrselassie wa Ethiopia aliwika mita 10,000 mwaka 1996 na 2000.Nigeria ya akina Nwankwo Kanu ilipata kushinda kombe la Olimpiki la soka, kwa kuwachapa vigogo kama Brazil na Argentina. Afrika,  ni kichwa si mkia katika ramani ya Olimpiki.
    Mabingwa wengine wa Olimpiki ni Amos Biwott wa Kenya mwaka 1968, Kipchoge Keino pia wa Kenya mwaka 1972,Julius Korir wa Kenya mwaka 1984,Julius Kariuki wa Kenya mwaka 1988, Mathew Birir wa Nyayo mwaka 1996, Joseph Kater pia wa Nyayo mwaka 1996 na Robert Kosgei mwaka 1996. Maria Mutola wa Musumbiji alishinda mita 800 mwaka 2000. Afrika ni bara la mabingwa wenye ari ya kushinda.
    Tanzania imewahi kushiriki mashindano mengi ya kidunia; inajivunia rekodi za mabingwa wake kama Filbert Bayi, Suleiman  Mujaya Nyambui, Juma Ikangaa na wengine wengi.
    Afrika Kusini iliaandaa Kombe la Dunia mwaka 2010.
Baadaye Afrika itataka kuandaa mashindano makubwa ya kimataifa, licha ya kampeni chafu sana za Wazungu, kwamba Afrika hakuna usalama, hususan zama hizi za magaidi.
Mbona Black September waliteka wanariadha Munich ? Watasema, Afrika kuna miundo mbinu dhalili n.k
    Mwisho, Afrika si mshiriki bali mshindani wa dhati kama tulivyoona. Mtu mweusi si mtumwa, bali ‘championi’ katika nyanja anuwai kama tulivyoona akina Jesse Owens.
Wapo mabingwa wengine weusi katika nyanja tofauti za maisha-Afrika inastahili nafasi sawa.
    Shime, Waafrika wenye maradhi ya kutokujiamini ama kujidharau(inferiority complex) waone kuwa mtu Mweusi yuko juu sana .
Akina Hitler wa kizazi hiki wazomewe kwa sababu Afrika inakwea juu sana . Afrika, “Citius, Altius….Afrika Fortius”, ina  kwea Haraka, Juu na kwa Nguvu. Afrika  kilele cha utukufu.
Mwaka 2008 mashindano ya Olimpiki yalifanyika Uchina, mwaka huu 2012 yatafanyika London,siku chache zijazo kuanzia sasa. Je kutatokea ubaguzi wa rangi wa kuwabagua akina Caster Semenya?
     0786 324 074
   
   
   


No comments:

Post a Comment