Tuesday, May 29, 2012

SUMATRA DAR NOMA!!

*Abiria wahofia kitisho cha Al Shabaab
Na Conges Mramba, Nansio
MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Nchi Kavu na Majini(SUMATRA) inadaiwa kushindwa kusimamia ukaguzi wa vyombo vya majini Ziwa Victoria, hivyo kusababisha hofu ya kuweza kutokea   ajali.
  “Maofisa wa SUMATRA wanapotoka Dar es salaam kuja Ziwa Victoria kuendesha zoezi la ukaguzi,wanawashurutisha wamiliki wa vyombo vya majini kuwalipia gharama za chakula na malazi hotelini”, Gazeti hili limedokezwa.
Nahodha wa Meli moja ya kampuni binafsi, ameliambia Gazeti hili kwamba,kitendo cha maofisa wa SUMATRA kupewa hisani ya gharama za chakula,malazi na maburudisho wakati wanapofanya ukaguzi wa vyombo vya usafiri majini Ziwa Victoria,huhafifisha ubora wa vyombo husika,na changamoto kwa manahodha na mabaharia.
“SUMATRA, wanapofika Mwanza,toka Dar es salaam, wanakula na kulala kwa gharama za wamiliki wa meli na boti hapa Ziwa Victoria, sasa watakagua nini kama siyo kulipa fadhila kwa yale waliyotendewa na wamiliki wa meli ama boti?” Amehoji Nahodha wa Meli moja kwa masharti ya kutotajwa jina wakati wa mahojiano na gazeti hili.
 Tumemtafuta    Ofisa Uhusiano wa SUMATRA, David Mziray, kwa takriban juma zima,ili kujibu tuhuma hizo, lakini simu yake ya mkononi ama iliita pasipo majibu, ama ilikuwa imefungwa.
 Hata hivyo, Ofisa Mfawidhi wa SUMATRA,Mkoani Mwanza, Alfred Wariana, amesema maofisa wa SUMATRA kutoka Dar es Salaam,hufika Mwanza kufanya ukaguzi wa kila mwaka,na hulipiwa gharama za usafiri,malazi na chakula na Mamlaka, na wala siyo wamiliki wa vyombo vya usafirishaji Ziwa Victoria.
  Jumapili, Mei 27 mwaka huu,mwandishi wa makala haya alisafiri kutoka Jijini Mwanza,kwenda Nansio,Ukerewe kwa Meli ya Mv. Samar II inayomilikiwa na Kampuni na Kampuni ya Samar Filling Station,ya Mwanza.
Hii ni meli iyojengwa mwaka 2009 na Kampuni ya Songoro Marine Transport pia Jijini Mwanza,kama meli ya mizigo. Ilikuwa ikifanya safari zake kati ya Mwanza na Uganda.
 Meli hiyo ilibadilishwa matumizi mwaka huu, ikawekewa viti na kuanza kusafirisha abiria kutoka Mwanza hadi Nansio,Ukerewe. Uwezo wake ni kuchukua abiria 248 na tani kati ya 101 na 138 za mizigo.
 Nilimuuliza Nahodha wa meli hii,Kapteni Adam Andrew Alex, “Meli ina vifaa vya uokozi kwa kiwango gani?”
“Ina maboya(life rings) 60 na life jackets 350.Tuna mashua moja na vifaa 10 vya kuzimia moto”, Kapteni Alex alisema.
Kutoka Jijini Mwanza hadi Nansio, mji mkuu wa wilaya ya Ukerewe yenye visiwa 27 na vingine 11 visivyokaliwa na watu kuna umbali wa mali 29 za majini.
Kapt.Alex anasema alihitimu katika Chuo cha Mabaharia, Dar es salaam Maritime Insitute, na alikuwa na uzoefu wa mwaka mmoja kazini. Akasema meli yake ilikuwa na mabaharia tisa wenye uzoefu wa kati ya miezi sita na mwaka mmoja kazini.
 Akizungumzia mazingira ya kazi, amesema mikataba ya ajira katika vyombo hivi vya binafsi haiendani na kazi, “Hakuna hata malipo ya muda wa ziada wa kazi(over time),wala hakuna usafiri baada ya kazi”, Kapt. Alex amedai.
 Eferi Bulongo(75) ni miongoni mwa abiria waliosafiri na meli hiyo, Samar II kwenda Nansio. Nilimuuliza, “Una maoni gani kuhusu usafiri Ziwa Victoria?”
 “Sipendi kusafiri kwa meli binafsi;zinasumbua, ratiba ya safari haieleweki,ni namna wanavyojisikia wao, na melini hakuna mahitaji ya lazima ya kuaminika kama chakula na vinywaji;kuna chai”, Bulongo amedai.
 Amesema, meli za Mashirika ya Umma,kama Marine Services Company(MSC) ni bora kabisa, ratiba ya safari huzingatiwa.
“Hizi meli za MSC zinahujumiwa na baadhi ya wafanyakazi wake.Labda wanapewa rushwa na wamiliki wa meli za binafsi ili meli za MSC ziache kufanya huduma ili  wafanye biashara, abiria wengi hawazipendi hizi meli binafsi”, Bulongo amesisitiza, huku akihoji, “Kwanini Meli za MSC ndizo ziharibike kila kunapokucha? Mv.Clarias haijafanya kazi kwa zaidi ya miezi minne; sasa wamesikia Bunge la Bajeti karibu kuanza, ndiyo tunasikia itaanza kati ya kesho(Mei 27) na kesho”, anasema Bulongo.
  Nikampigia simu Kaimu Meneja Mkuu wa MSC,Projest Kaija kujibu tuhuma hizo.
“Leo, Jumapili Mei 27, tunaifanyia majaribio Mv.Clarias. Baada ya siku chache itaanza safari zake kwenda Ukerewe”, Kaija anasema.
 Anakanusha kuwepo kwa tuhuma zenye lengo la kuhujumu Kampuni ya umma kwa nia ya kuwanufaisha wenye meli binafsi.
“Wafanyakazi wa MSC wanawezaje kuhujumu kampuni inayowapa mshahara?” Anahoji,huku akisisitiza kuwa tuhuma hizo zitachunguzwa,kwa kuwa uongozi wa kampuni hiyo ya umma umebadilishwa siku chache zilizopita; kampuni inafanya matengenezo(reform) anuwai.
 Nikampigia simu  Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Everest Ndikilo,ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mkoa,  kumsaili:
“Kwanini abiria wanapopanda katika vyombo vya majini Ziwa Victoria hawakaguliwi, ili kubaini uwezekano wa kuwepo kwa magaidi kama  Al-Qaeda na Al-Shabaab, wanaotishia maisha ya watu nchi jirani ya Kenya?”
Magaidi waliwahi kuteka nyara ndege ya Air Tanzania(ATC)mwaka 1988 , yenye maandishi ubavuni, ‘Tango Charlie” wakati ikipaa kutoka uwanja wa ndege wa Mwanza,ikalazimishwa kwenda Jijini London ambako hatimaye jumla ya wateka nyara watano raia wa Tanzania walihukumiwa kifungo cha kati ya miaka mitatu na mitano jela,Jijini London.
 “Ulinzi na Usalama ni Ajenda ya  kudumu na siyo majini tu, hata kwenye majengo,mahoteli na makazi ya raia”, Mkuu wa Mkoa Ndikilo anasema.
Kuhusu maofisa wa SUMATRA,kutoka Dar es Salaam kulazimisha kulipiwa gharama za ukaguzi na wamiliki wa vyombo ziwa Victoria, Ndikilo akasema, “Kama jambo hilo lipo,basi ni tatizo kubwa,nitafuatilia ili hili likemewe”, Ndikilo akasema.
 Gazeti moja litolewalo kila siku hapa nchini kwa lugha ya Kiingereza, katika toleo lake la Mei 23 mwaka huu lilisema kwamba,mwaka 1996 Mv.Bukoba ilipozama na kupoteza maisha ya abiria wake takriban 1,000; miongoni mwao alikuwemo Abu Ubaidah al-Banshiri, ambeye alikuwa nambari mbili wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda.
Naam, kundi hili la AlQaeda, lilianzishwa na Osama bin Muhammad bin Awad bin Laden,Feburuari mwaka 1998 kwa jina la WORLD ISLAMIC FRONT,ili kuhujumu maslahi ya Marekani na washirika wake mahali popote duniani,hata kama ni Ziwa Victoria,
Osama alikuwa mshirika wa Marekani na shirika lao la Ujasusi(CIA) mwaka 1979 wakati majeshi ya Warusi walipovamia Afghanistan.CIA walimfadhili mabilioni ya Dola za Marekani kuanzisha kambi ya mafunzo ya Makhtab al-Khidamat(MAK).
Lakini,baada ya Urusi kuondoka Kabul mwaka 1989, Osama akageuka kuwa adui wa MAREKANI na washirika wao, akaungana na Taliban na Mullah Muhammad Omar kuendesha ‘Jihad’ dhidi ya Marekani na washirika.
Nataka kusema kwamba,mwaka 1996 wakati Mv.Bukoba inazama ziwa Victoria, al-Qaeda tayari walikuwepo,na wangeweza kufanya madhara hapa nchini kwa mashambulizi yenye kulenga shabaha Wamarekani ama maslahi yao hapa Tanzania.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Everest Ndikilo, amesema serikali imeimarisha ulinzi katika Ziwa Victoria,kwa kuwa zipo boti za doria zinazozunguka ziwani, na raia wanapaswa kutoa taarifa pindi wanapoona mienendo yenye mashaka ama kitisho cha magaidi wa al-Qaeda ama al-Shabaab!
0786 324 074
  
         

No comments:

Post a Comment