Friday, May 25, 2012

MELI ZA ZIWA VICTORIA NI MAJENEZA YANAYOELEA?


                   

                    *Kununua tiketi  ya usafiri katika boti hizo, ni kununua tiketi ya kuzimu!
          
                 Na Conges Mramba, Mwanza
   NI SAA nane mchana, Alhamisi,Mei 24. Niko Mwaloni,Kirumba,Jijini Mwanza,katika moja ya Bandari bubu zilizomea kama uyoga, kandoni mwa Ziwa Victoria.
 Mbele yangu kuna boti iliyojengwa kwa mbao na mabati; imechakaa. Inapakia abiria na mizigo,tayari kung’oa nanga kuelekea katika moja ya visiwa vingi vidogo vidogo vya Ziwa Victoria.
   Nachungulia ndani ya boti hii, Mv. Maisha, nabaini kuna maboya machache yameputikwa ndani ya gunia kuu kuu.Sioni vifaa vya kuzimia moto(Fire Extinguishers), sioni kisanduku cha Msaada wa Kwanza(First Aid).
 Kama ada, makuli wanaendelea kupakia ndani ya Mv.Maisha mizigo; viroba vya sukari,chumvi,maboksi ya sabuni. Pia wanapakia magudulia ya mafuta ya taa na hata petrol! Wanachanganya abiria na mizigo? Abiria na petroli?
  Naam, hii ni boti iitwayo, Mv.Maisha inapakia abiria na mafuta ya taa na petrol, abiria wameketi botini kimya,hakuna anayeshangalia kitisho cha ajali ya moto, pindi petrol ikichokozwa kwa moto wa injini ya boti, ama moshi wa sigara!
  Abiria wanazidi kuingia na kuketi. Hawana muda kuhoji ikiwa boti hii ina maboya ya kutosha? Ina Bima? Ina vifaa vya kuzimia moto, au vile vya uokozi pindi ajali ikitokea?
   Alfred Wariana, ni Afisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini(SUMATRA), Mkoani Mwanza, ambaye anasema Ajali ya Meli ya Mv.Bukoba,Mei 21,mwaka 1996,iliizindua serikali katika usingizi wa pono,imetunga sheria za Usalama Majini!
  “Kufuatia Ajali ile. Sheria ya Kuongozea vyombo vya majini, The Merchant Shipping Act, imetungwa mwaka 2003,ikaanza kutumika mwaka 2004 ili kudhibiti Ajali”,Wariana anasema katika Mahojiano Maalum ofisini mwake.
   Kulingana na Wariana, Ofisa huyu  Mfawidhi wa SUMATRA, Mwanza kuna jumla ya Meli 47 ambazo zote zimesajiliwa, zina BIMA kwa sababu mtu hawezi kuendesha biashara ya huduma za Usafiri pasipo kuzingatia taratibu, sheria na kanuni.
  “Changamoto ya SUMATRA,Mwanza kuna boti zaidi ya 10,000 zinazosafirisha abiria na mizigo kwenda visiwani na Sengerema,Ukerewe na Geita. Huwezi kusema, asilimia mia zote hufuata sheria, na kuzingatia maelekezo.SUMATRA Mwanza, tuna wakaguzi watatu tu,lakini tunao mtandao(usiotosha) wa kuwadhibiti wasafirishaji wasiopenda kutii sheria pasipo shuruti. Kumbuka, Ziwa siyo barabarani ambako utaweza vizuizi njiani na kufanya ukaguzi ili kuwabaini wakosaji”, anafafanua Wariana.
  Polisi na Watendaji wa vijiji wapo katika maeneo ya vituo vya kibiashara,ambako boti hizi hutia nanga na kupeleka bidhaa,wanapaswa kuwatia mbaroni wasafirishaji wasiozingatia sheria za Usafirishaji wa Majini.
Kulingana na SUMATRA,Mwanza, ziko changamoto kuwafikia wamiliki wote wa vyombo vya majini,hususan vidogo vidogo,na kuvikagua kila mara.
 “Hata hivyo,mtandao wetu wapaswa kukagua na kuhakikisha kila chombo ni salama kabla ya kuanza safari,na kila chombo cha usafiri chapaswa kuwa na cheti cha kufaa-sea worthiness.
 Katika Ziwa Victoria,SUMATRA wana ofisi Mwanza, Bukoba na Musoma. Ziwa Victoria kuna visiwa takriban 60, Ukerewe pekee kuna visiwa 38 vingine hukaliwa na wavuvi tu.
  Mei 21, mwaka 1996,Meli iliyomilikiwa na lililokuwa Sherika la Reli(TRC) ilizama umbali wa mail inane(kilomita 12) za majini, jirani na Bandari ya Mwanza, uelekeo wa Bwiru.
 Mv. Bukoba, ilipinduka kasha kuzama,ikasababisha vifo vya zaidi ya watu 800.Wengine zaidi ya 100 walijeruhiwa,wakipoteza mali nyingi za mamilioni ya shilingi,hususan mikungu mingi ya ndizi.
 Kwa mujibu wa Ripoti ya Tume ya Jaji Robert Kissanga, iliyochunguza chanzo cha Ajali hiyo,usiku wa kuamkia siku ya ajali,Mv.Bukoba ilipakia abiria kati ya 750 na 800 pamoja na wafanyakazi 37 wa Meli hii.
  Kati ya hao, 114 waliokolewa wakiwa hai, wakati 391 waliopolewa wakiwa   wamefariki wakazikwa katika Makaburi ya Igoma,nje kidogo ya Jiji la Mwanza. Miili mingine ilichukuliwa na jamaa zao kwenda kuzikwa kwao. Jumla ya miili 332 haikupatikana.
      Kila mwaka, ifikapo Mei 21, serikali inayosema Haina Dini, huongozana na viongozi wa madhehebu ya dini na waganga kwenda eneo la ajali,kufanya ‘matambiko’ na kumwaga mchanga eneo  majini!
  Serikali iliwashitaki  katika Mahakama Kuu  aliyekuwa Nahodha wa Mv.Bukoba, Jumanne Rume-Mwiru, (ambaye sasa ni Marehemu),Mkaguzi wa Mamlaka ya Bandari(wakati huo THA),Gilbert Mokiwa, aliyekuwa Meneja wa Bandari ya Bukoba, Alphonce Sambo, na aliyekuwa Maneja wa Bandari ya Kemondo, Prosper Lugumila.
  Kesi hiyo Nambari 22 ya mwaka 1998, ilianza kusikilizwa Mei 14 mwaka 2001. Miongoni mwa waendesha mashitaka katika kesi hiyo ni Eliezer Feleshi, ambaye sasa ni Mkurugenzi wa Mashitaka nchini(DPP).
  Hukumu ya kesi hii ilitolewa Ijumaa, Novemba 29 mwaka 2002,majira ya saa sita mchana hadi saa 9 na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Juxton Mlay(amestaafu).
 Washitakiwa wote walishinda kesi hiyo,kufuatia Hukumu yenye kurasa 118 iliyosomwa kwa dakika 160 na Jaji Mlay,kusema Mv.Bukoba ilizama kwa sababu haikuwa na uwiano wa majini, na siyo uzembe wa washitakiwa.
 Serikali ikakata rufaa, hadi leo majaliwa na rufaa hiyo hayajulikani,na baadhi ya washitakiwa wamefariki dunia,bila kujua hatma ya kesi hiyo na stahili zao.
   Mv.Bukoba ilikuwa ‘Kaburi’ lenye kuelea Ziwa Victoria. Ilikwishapigwa marufuku,kwa kuwa haikuwa na viwango vya ubora-sea   worthiness.

Ilijengwa na Kampuni ya Kibelgiji,ikazinduliwa  Julai 27 mwaka 1979.Siku ya uzinduzi, ilibainika haikuwa thabiti,na ilikosa uwiano,ilitaka kumtosa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere ambaye alikuwa Rais wan chi wakati huo.
   Miaka michace iliyopita, meli nyingine ya MSC, Mv. Butiama, ilizimika injini zake jirani tu na Bandari ya Mwanza, lakini ikaelea kwa zaidi ya saa mbili,huku abiria wakihaha bila msaada. Ilikuja kufahamika kwamba, meli hiyo haikuwa na mawasiliano!
 Meli nyingine ya mizigo, Mv.Nyamageni,ilizama ziwa Victoria ikiwa na abiria zaidi ya 20 waliosafirishwa pamoja na masanduku ya soda kwenda visiwani.
 Feburuari mwaka huu,  Mv. Pacific iliyokuwa ikisafiri kati ya Mwanza na kisiwa cha Ghana ilizama, ilikuwa na abiria 17, mmoja alifariki wengine wakaokolewa.
 Kwa mujibu wa SUMATRA, Boti nyingine iliyokuwa na abiria 31 ilizama huko Musoma,mkoani Mara,abiria   wote wakaokolewa kwa kytumia zana za uokozi.
 Kwa mujibu wa Alfred Wariana, Ofisa Mwandamizi wa SUMATRA, katika ajali tatu za karibuni, kati ya watu 81 waliokuwemo katika boti hizo,ni mmoja tu aliyefariki dunia,na anasema hii huonesha kwamba sheria zimeanza kufuatwa.
  Kabla ya vyombo vya majini kuanza safari ni sharti kukaguliwa ili kuthibitishwa usalama wake.
Hata hivyo, Wariana anasema bado usafiri wa majini Ziwa Victoria ni salama zaidi kuliko barabarani.
“Usafiri wa barabarani hata wa ndege hapa Afrika ndiyo ‘Moving Coffins’ (majeneza yanayotembea),Barabarani kuna magari kuna pikipiki zinazochinja watu kila siku”, anasema Wariana.
http://upload.wikimedia.org/wikipedia/commons/thumb/7/7b/Liemba1.jpg/238px-Liemba1.jpg moja ya meli za MSC ziwani Victoria
 
Akizungumza kuhusu ushindani wa kibiashara, Ofisa huyu wa SUMATRA amesema, kuimarishwa kwa miundombinu ya barabara, hususan kutoka   Mwanza hadi Musoma, Tarime na hata Kenya,kumesababisha abiria wengi kususia usafiri wa meli.
 Tangu barabara ya lami ya Mwanza hadi Musoma ikamilike mwaka 1985, hakuna tena abiria wanaosafiri kwa meli kwenda Musoma,Shirati au hata Kisumu,Kenya.
    Upungufu huu ni wa abiria wa meli ni wa takriban asilimia 50.
  Kaimu Meneja Masoko na Biashara wa Kampuni ya Meli(MSC)Kapt. Obedi Nkongoki, anasema mwaka jana Kampuni hii ilisafirisha jumla ya abiria 235,794 tu ambao ni chini ya uwezo wake. Mizigo iliyosafirishwa ni tani 54,212.
  Kulingana na Kapt. Nkongoki, MSC ina jumla ya meli 15 zinazosafirisha abiria na mizigo kati ya Mwanza na  Musoma,Bukoba,Kemondo,Jinja(Uganda),Kisumu(Kenya),Port Bell Uganda, na Ukerewe.
 Mv.Victoria ndiyo meli kongwe kuliko zote; ilijengwa mwaka 1960. Imekuwa ikifanyiwa matengenezo na ukarabati mkubwa na mdogo.
 Kaimu Meneja Mkuu wa Marine Services Company(MSC)Projest Kaija, anasema Mv..Victoria ina umri wa miaka 52, lakini imefanyiwa ukarabati mkubwa na mdogo mara nyingi. Mara ya mwisho ilifanyiwa ukarabati mkubwa(Major Rehabilitation) mwaka 2008 ambako ilikaa miezi sita katika Bandari ya Mwanza South Port bila kufanya huduma.
  Ina uwezo wa kuchukua abiria 1,200 na tani 200 za mizigo;lakini kufuatia abiria kupungua siku hizi inachukua abiria 500-800,chini ya uwezo wake. Inafanya safari zake kati ya Mwanza-Kemondo-Bukoba-Mwanza.
 Kwa mujibu wa Kaija, meli nyingine za MSC zinazofanya huduma Ziwa Victoria, ni Mv. Butiama,Serengeti,Clarias ambazo hubeba abiria na mizigo kati ya Mwanza,Bukoba na hata Nansio-Ukerewe.
 Meli za mizigo ni pamoja na Mv. Umoja, Mt. Nyangumi ambayo husafirisha mafuta kutoka Mwanza hadi Kisumu,Kenya na Jinja na Port Bell huko Uganda.
 Mv.Ukerewe, MI wimbi na Malindi husafirisha mizigo,wakati Tanganyika Sea Warrior ni  boti mpya ya kusafirisha watalii wapatao 15 kwa wakati mmoja.
 Mt(Motor Tug) HUVUTA MATISHARI.
  Ziwa Victoria lina eneo la kilomita za mraba 68,800. Ni ziwa la pili kubwa duniani lenye maji baridi na ni nyumba ya sangara ambao sasa wamekaribia kwisha. Ni ziwa kubwa kuliko yote Afrika, Tanzania inamiliki asilimia 49 ya ziwa hili, Kenya asilimia 6 na Uganda inamiliki asilimia 45.
  Kulingana na Wariana, Ofisa Mfawidhi wa SUMATRA,Mwanza, mabaharia wote wa meli wanapaswa kuwa na viwango na wawe wamehitimu katika Chuo cha Mabaharia, Dar es salaam Maritime Institute,(DMI) ambacho hutambuliwa kimataifa.
 “Hakuna meli inayoendeshwa na Nahodha asiye na sifa”, anasema Wariana wa SUMATRA.Vyo mbo vyote vinapaswa kuwa na BIMA na vifaa vya uokozi,lakini boti chache na mitumbwi midogo na majahazi husafirisha abiria pasipo mamlaka kubaini,na ni changamoto zilizopo, wanapaswa kufuata sheria”, anasema Wariana wa SUMATRA.
Vyombo hivi vispofuata sheria,kanuni na taratibu za usafirishaji salama majini, Wariana anasema ndiyo hufanya kununua tiketi za usafiri katika vyombo hivi kuwa tiketi za kuendea KUZIMU!
  “Kwa bahati, shughuli za uvuvi ziwa Victoria zimepungua sana katika visiwa hakuna tena watu wengi wanaoenda huku na huko,kwa sababu samaki wamepungua sana ziwani,na ajali za majini zimepungua”, anasema Alfred Wariana, Ofisa Mfawidhi wa SUMATRA,Mkoani Mwanza.


No comments:

Post a Comment