Friday, December 28, 2012

AFRIKA UTUMWANI?

LEO,kuna mjadala mkali wa kwanini Bara la Afrika ni tajiri,lakini watu wake masikini?
Lawama zinakwenda kwa vyama vilivyoko madarakani, ama na watawala.
Inawezekana vyama hivi huchangia,lakini tatizo kubwa ni ujinga wa kutekeleza masharti ya wakoloni yanayoletwa kupitia ubinabsishaji.
Vyama vya ukombozi na viongozi wa Ukombozi walitaifisha makampuni ya mabepari kwa manufaa ya nchi.sasa hawapo na wameondoka kwa vifo na wengine kuhujumiwa kama tulivyomwona Lumumba.
SAFARI ya Bara la Afrika kutoka Uhuru kurejea Utumwani,ilianza kushika kasi mara baada ya viongozi waliopigania uhuru kuondoka.
 Ahmed Sokou Toure,Kwame Nkrumah, Gamal Abdel Nasser,Julis Nyerere, Patrice Emery Lumumba,n.k walioondoka madarakani wengine kwa hujuma za mabeberu,Afrika ikarudi kule ilikotoka.
Fikra huru za kuendeleza Afrika kwa maliasili zake nyingi zilihafifsishwa, ama na        Madola makubwa kwa njia za vikwazo,au fikra hizi pevu ziliyeyushwa na kutiwa kiza hadi tukakubaliana na utumwa na kuwategea wakoloni na mashirika yao waliyoanzisha baada ya Vita Vikuu vya pili vya Dunia, kwamba ndiyo utakaokuwa ufumbuzi wa matatizo ya maendeleo yetu.
 Abdul Rahman Mohamed Babu,katika kitabu kiitwacho,
“African Socialism or Socialist Africa?”(Tanzania Publishing House,1981), anasema katika ukurasa wa 35 kwamba, kuwategemea wafadhili hawa kulikuwa kujiingiza kichwa-kichwa katika ukoloni mamboleo, neo-colonialism.
Wapo viongozi wa Afrika waliogoma kunyoosha mikono ya urafiki kwa hawa wakiloni:Agostino Neto, Cabral, do Santos, Samora Machel na wenzao wakadhaniwa ni wajamaa wa Ki-Marx, waliopinga ukoloni na kutaka kueneza siasa hatarishi za kijamaa kwa madola ya Magharibi.
Walihujumiwa, hawapo na mawazo na njozi zao zilishapotezwa na hawa viongozi wa leoambao hawana jipya,sispokuwa kutenda kama mawakala wa ukoloni.
 Afrika, haina tena njozi za kuendelea kwa kutumia maliasili zake au rasilimali zake. Bali, ni kutegemea misaada ya tashtiti(myth of aid) kutoka Ulaya,Marekani kwa upande mmoja, na Japan,Uchina ama Urusi,kwa upande wa pili.
 Tumewekewa akilini kasumba na wakoloni,kwamba, “If no Aid, No Development” sasa, tunadhani misaada yao ni Haki Yetu, kumbe ni utumwa kwetu.
    Nimewahi kuwasikia viongozi wa Tanzania wakijisifu mno kwa ‘kusaidiwa’ sana na kufutiwa misaada, badala ya kujisifu kwa kuwaendeleza wananchi kwa kutumia fursa zetu na rasilimali zetu wenyewe.
 Hawa vigogo wetu, wanaona kiongozi anayesaidiwa sana kupita wenzake, ndiye ‘kipenzi’ cha Mabwana Wakubwa,kumbe ndiyo “Uchangudoa” mamboleo unaowauza       Waafrika, kwa kutumia utajiri na mitaji wakoloni waliyopora kwetu zama za Ukoloni mkongwe.
 Misaada kwa Bara hili ina makusudi mahsusi: Kwa njia za moja kwa moja au kupitia kwingine,misaada na hisani,huwanufaisha zaidi hawa wafadhili na wahisani,wakiloni mamboleo,kuliko sisi.
 Taasisi za Breton Woods,Fuko la Fedha la Kimataifa(IMF)na Benki Kuu ya Dunia(WB) wamegeuka miungu kwa kutuamria kila kitu. Nasi tunafuata bila kupinga,hata kama ni kubinafsisha mashirika yaliojiendesha kwa faida,viwanda vilivyoongeza thamani ya mazao yetu na kutupa ajira, matokeo yake tumefilisika,tunauza mazao ghafi kwa bei chee bila kuyachakata.
 Viwanda vya ngozi vimegeuka maghala, viwanda vya kusindika mazao vimekufa, na vingine kama Bora Shoe Company,vilivyoleta tija kwa Watanzania,vilishakwenda kuzimu.
 Imekuwa sasa, hawa wakoloni kwa kutumia IMF na Benki ya Dunia,wamejivika jukumu letu la kufikiri na kuamua kwa niaba yetu,nasi tumeaachia jukumu hilo la msingi-tumejiuza mithili ya machangudoa katika soko la matajiri.
Siku hizi tunaitwa, Nchi za Dunia ya Tatu(Third World Countries) ingawa tuna rasilimali nyingi na muhimu sana, kama tulivyoona katika sehemu ya kwanza ya makala hii.
 Tuna mafuta,gesi,uranium,dhahabu,almasi,maziwa makubwa,mito,Bahari,milima mirefu,wanyamapori na misitu isiyopatikana popote duniani ila hapa Afrika.
 Naam, Wakoloni wanafikiri na kuamua chochote watakacho kwa niaba yetu. Hii ni kusema kwamba,ubongo wetu wa mbele(The Frontal Lobe) umeshindwa kufikiri na kuamua kwa niaba yetu wenyewe, tumewaachia Marekani na Ulaya waamue mustakabali wetu!
 Rasilimali zetu wanachukua bila sisi kujua, wanauza na kutulipa mrabaha kidogo wanapojisikia, au wanatukopesha pesa za kununulia chandarua,na ujenzi wa zahanati, barabara,hospitali n.k huku tukiwashangalia na kuwachezea ngoma!
 Afrika tajiri, watu wake ni masikini, wenye njaa na wanaoingiliwa kisiasa,kiuchumi,kijamii na kijeshi na Ulaya na Mrekani na Asia.
 Mapinduzi,yalishashindwa kwa sababu wanamapinduzi walishatoweka,wenye fikra huru walishanyofolewa ubongo wa mbele-Frontal L obe-sasa tumekabidhi maamuzi na hatima yetu kwa Marekani na washirika wake!
 Nyerere, Patrice Lumumba, wa Congo, Ben Barka wa Morocco, Amilcar Cabral wa Guinea Bissau na wenzao wametoweka,jua limekuchwa.
 Afrika, ime ‘asilishwa’ hadi kubatizwa utoto bandia wa Ulaya na Marekani, wanaita “Africa Europeanized”.
 Kinachoangaliwa siku hizi,ni maslahi ya Ulaya hapa Afica, na siyo maslahi ya waafrika. Hakunavyama kama TANU, FRELIMO, M.P.L.A,UNIP na ANC vyenye kupinga utumwa na ubaguzi wa rangi na matabaka ya watu.
Matokeo yake, Umoja wa Afrika(AU) hauna turufu katika masoko, hauna maamuzi wa kura moja katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, hivyo hauna meno waka kauli hata juu ya yanayotokea hapa Barani.
   Ikitokea vita Somalia na Darfur,mpaka Marekani watutume kulinda amani na wanatulipa posho,utadhani wao walituzaa sisi!
 Marekani ndiyo yenye kusema kwa sababu ya MITAJI YAKE iliyowekeza hapa. Marekani inaweza kusema, “Gaddafi Must Go!” A.U ikiwa kimya! Ikisema ‘ Kikwete Must Go!” hata hakuna wa kupinga.
 Marekani ikiona aibu kwa kauli hizi za ubabe katika macho ya kimataifa, basi inajivua gamba,na kuwaachia washirika wake,hususan Umoja wa Kujihami wa Ulaya Magharibi(NATO), wanatushambulia tunapojidai kichwa ngumu.
   Jumatano ,Machi 30 mwaka  2011,nilipokuwa nikitazama kipindi kiitwacho, STRAIGHT TALK AFRIKA kinachorushwa na luninga Sauti ya Amerika(VoA) nikapatwa kichefuchefu,na kupiga chafya.
 Niliaona kwamba Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Rodham Clinton, alipokuwa akizungumzia Majuma Sita ya Vita nchini Libya’ hatimaye alisema, “Gaddafi Must Go!”
 Kwamba, Gaddafi lazima aondoke Libya,utadhani Marekani ndiye mwamuzi na ofisa     habari wa watu wa Libya!
Lini Walibya walimpa Clinton ubongo wao wa kufikiri na kutoa maamuzi(Frontal Lobe) ili aamue mustakabali wao kwa niaba yao?
 Kudhihirisha kiburi hiki cha Marekani, Machi 17 mwaka 2011, Marekani chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa(UN) wakatoa Amri ya ndege zote za Libya kutoruka katika Anga ya Libya, ”No Fly Zone!”
  Ati, hii ni Amri ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya kiongozi wa Libya,Kanali Mouammar al-Gaddafi, asiendelee kuwashambulia waasi wan chi hiyo kwa madege ya kijeshi,ama kusababisha maafa makubwa.
   Gaddafi, kawaita wanaompinga(Waasi) kwamba ni mende, panya,mijusi,pusi-paka nyau!
 Ndipo sasa, Umoja wa Mataifa umeruhusu NATO kuishambulia Libya,utadhani Libya imetangulia kuzishambulia nchi wanachama wa Umoja wa Kujihami wa Ulaya Kaskazini mwa Bahari ya Atlantic, yaani NATO!
 Tukubaliane kimsingi, kwamba Gaddafi kakaa kwenye uongozi tangu mwaka 1969,na kwamba ni Dikteta anayewaita wapinzani,mende,panya n.k
Tuchukulie kuwa kweli kwamba, Gaddafi nawaburuza raia wa Libya na wamemchoka.Sasa, Marekani,Ufaransa na Uingereza,ama NATO wamekujaje katika mgogoro huo?
 Ati, Gaddafi anatishia maisha ya watu na utu? Mbona Umoja wa Mataifa haujachukua hatua madhubuti za kuondoa vita Cote d’ Ivoire? Mbona hata huko kuna vita vinasambaa,na watu wanakufa?
Sasa,kwa akili tulizonazo na kuomba omba kwetu,kukaribisha Marekani na Ulaya kuamua lolote na kuingilia Afrika kijeshi,ndiyo Ukooloni tunaokaribisha Afrika.Afrika haijawahi kulaaniwa,kama wengine wasemavyo,ni kushindwa kuwa huru kifikra tu.
 Mtayarishaji wa kipindi cha Straight Talk Africa,Dk. Shaka Ssali, Jumatano hiyo alimuuliza swali mgeni wake studioni, Profesa Dk. Abdul Karim Bangura, ambaye ni Profesa  wa Uhusiano wa Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Howard.
 “Kwanini Marekani ichukue hatua Libya,na siyo Cote d’ Ivoire?”
    “ Ni mafuta” Prof. Abdul Karim Bangura alijibu, kwamba sababu ya Marekani kuiingilia kijeshi Libya kabla ya Cote d’ Ivoire ni mafuta ya Libya!
  Mafuta ya Libya,yanawavuta kunguru,tai, mainzi ya kijani na nyang’au wengi ili kuja kula mizoga!
 Ndivyo nilivyosema katika makala iliyotangulia,juma lililopita,kwamba mgogoro mmoja unaachwa ili kuingilia mahali kuliko na ‘uhondo’ wa mafuta.
 Wameacha suala la Laurent Gabagbo, wakaenda Libya,kwa sababu ya tabia yao ya upendeleo na macho yao yana makengengeza,ndiyo wanaita ‘double standards’.
  Suala la Marekani na Washirika wake kuona kwamba Cote d’ Ivoire hakuna taabu, wakakimbilia Benghazi na Tripoli ili kukamata visima vya mafuta, kwa visingizio kwamba Gaddafi ana madege mengi ya kijeshi na vifaru kuliko Gbagbo…ndiyo maana UN wakatuma NATO kushambulia Libya,ni uhuni na usanii ulioje?
 Kwa sababu gain Amri ya “No Fly Zone” ITANGAZWE LIBYA na wala siyo Abidjan ama Yamoussoukro?
Sasa wako Congo na wanawatumia akina Museveni na Jen.Kagame
  Ati, Libya hakuna demokrasia,hakuna katiba,kwa hiyo ni vita vya kuleta demokrasia na Haki za Binadamu. Vita dhidi ya ugaidi….Gaddafi ni gaidi kuliko akina Laurent Koudou Bagabgo, wanaoshindwa uchaguzi wanagoma kuondoka mamlakani.
 Umoja wa Afrika,mjini Addis Ababa umeshindwa kusema kwa sauti kubwa. Ulikuwa kimya wakati Hosni Mubarak akitimuliwa mjini Cairo. AU hawakusema kitu wakati Zine El Abidine Ben Ali akitimuliwa na wamachinga huko Tunis, Tunisia.
  Sasa, AU inasema polepole ikiwa chini ya makomeo ya milango na nondo za madirisha mjini Addis Ababa,kwamba Gaddafi anaonewa.Kesho watasema kiongozi mwingine kaonewa. Halafu hii AU haina chake,imejengewa hata ofisi zake Addis Ababa na Uchina kwa dola Milioni 200,kwa hiyo China itatazamwa kama Baba yetu,hata kama wachina wanakosea!
 Ni kwa sababu hii, Marekani inaidhihaki AU,kwamba  “Mfalme wa Wafalme” wa Afrika, GADDAFI alipaswa kutimuliwa tangu Libya hadi Afrika yote.
Gaddafi hakuwa Mfalme wa Afrika,upuuzi tu. Ulaya mbona kuna wafalme na malkia?
    Kanali Mouammar al-Gaddafi, “King of African Kings” kama wanavyomkebehi, ilikuwa  lazima aondoke!
 Hii ni Amri ya Marekani iliyojaa dharau na kiburi dhidi ya Waafrika wa rangi zote(Pan Africanism) ili Mzungu arudi kutawala?
 Gaddafi, “King of Kings” akiwa Mwenyekiti wa AU alitaka  Afrika iwe dola moja kubwa(UNITED STATES OF AFRICA) ili yeye awe rais kwa kwanza awatoe kamasi mabeberu,na kuwanyima rasilimali tete wanazotolea udenda!
  Gaddafi, ‘King of African Kings’ aliwakufuru hawa UNITED STATES OF AMERICA kwa kutaka kuwe na USA nyingine Africa?
 Mimi najiuliza, haya mapinduzi yaliyoanzia Tunisia,Misri, sasa Libya,Yemen na Syria zinawaka moto,yakivuka   Jangwa la Sahara na kufika Kusini, Robert Mugabe atapona kweli?
 Ataendelea kuwanyang’anya walowezi mashamba na kuwagawia Waafrika?
 Hili Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,lenye wajumbe wa kudumu,Marekani, Ufaransa,Uingereza(wanaoongoza kuivamia Libya) pamoja na Uchina na Russia, wakimwondoa Gaddafi,wakapora mafuta watakwenda Cote  d’ Ivoire na kutwaa kakao, kasha watakuja Zanzibar, Uganda,Musumbiji na kwingine kwenya harufu ya mafuta,na kuleta migogoro!
 Ni kwa sababu hii,tunauona ukoloni na utumwa mpya ukirejea Afrika kwa nguvu za kijeshi, huku wakijidai kuleta Haki za Binadamu na demokrasia,kumbe ni ‘Militarization and Human Right Abuses!”.MZUKA WA GADDAFI utazidi kuitafuta Afarika,na kifo chake na kufungwa kwa baadhi ya viongozi madikteta hapa Barani,siyo kheri ni mwanzo wa utumwa mpya
 Waafrika tuamke.
 0754/0786-324 074
 

No comments:

Post a Comment