Friday, December 28, 2012

MAKABURU WANGALIPO TANZANIA

Juni 16) mwaka 2013 itakuwa siku ya Kumbukumbu ya  miaka 37 ya mauaji ya vijana wa Kiafrika(Weusi) wa kitongoji cha Soweto ( South West Township ), Afrika ya Kusini.

  Seweto, ni kitongoji nje ya Pretoria , ambako Juni 16, mwaka 1976 wanafunzi zaidi ya 20,000 wa Kiafrika walifanya maandamano kupinga mitaala ya elimu ya kibaguzi, enzi za utawala wa Makaburu.
   Polisi wa Makaburu waliwafyatulia mabomu ya machozi ili kuwatawanya, bila mafanikio. Walifyatua risasi za moto katika kundi hilo kubwa la waandamanaji, vijana wa Kiafrika, pasipo huruma, pasipo kicho, wala bila kutoa hadhari.
 Juni 16, pia ni siku Rais Mstaafu, Thabo Mvuyelwa Mbeki aliapishwa kuwa Rais wa Afrika Kusini, mwaka 1999.
   Waliwafyeka waandamanaji vijana wadogo mithili ya nzi.
Yakageuka mapambano ya vijana wenye mawe, fimbo, matofali na hata mifuko ya daftari zao dhidi ya polisi wa makaburu wenye silaha za moto.
  Mwisho wa mapambano, walikufa vijana zaidi ya 250 katika vitongoji, mitaa na vijiji vya Weusi.
  Mwaka huo wa 1976 tu, inakisiwa Wabantu 600 waliuliwa kinyama na Makaburu. Naam, siku hizi, siku hiyo ya Juni 16 ati inaitwa, ‘SIKU YA MTOTO WA AFRIKA’.
Hapa kwetu Tanzania , inaadhimishwa na kulipana posho, wakati akina Waziri Mkuu, Johannes Vorster hawapo; umesalia ukaburu mamboleo nitakaobainisha hapa.
   Leo, tunatazama matatizo, changamoto na hali ya motto wa Kitanzania, ambamo tunasema serikali katili kama ile ya Makaburu wa Afrika ya Kusini, iliwafyeka kwa risasi za moto.
   Siku hizi, Makaburu mamboleo wanawafyeka watoto wa masikini kwa elimu duni, na kuwageuza manamba katika nchi yao , kama nitakavyobainisha.
  Akina P.W. Botha, walishaondoka tangu Agosti 14 mwaka 1989, akaingia F.W. de Klerk mwaka 1990.
   Nelson Rolihlahla ‘Madiba’ Mandela, aliachiwa huru Feburuari 11, mwaka 1990 baada ya kifungo cha  miaka zaidi ya 27 katika Kisiwa cha Robben.
   Siku hizi, Afrika Kusini ni nchi huru chini ya watu Weusi, akina Jacob Zuma ‘Mushorozi’ lakini Tanzania kuna ubaguzi wa matabaka wa watoto wa masikini, wanaopewa elimu duni, na watoto wa vigogo wanaosoma shule bora, ili wapate elimu safi, waje kuwa warithi wa vyeo na madaraka.
  Naam. Tanzania ungalipo mfumo katili wa kibaguzi dhidi ya watoto wa masikini. Tunasema Tanzania nchi huru inayotawaliwa na Waafrika wenzetu.
 Kwamba, hakuna Pierre Botha na F.W de Klerk, lakini watazame watoto wa masikini wanavyosoma katika shule duni katika vitongoji na vijiji vya masikini kuzidi Soweto ya enzi za Makaburu.
  Wanaketi chini mavumbini wawapo madarasani. Shule eti hazina madawati hata kama kulikuwa na Mpango wa Maendeleo ya Elimu(MMEM) ambao uliishia kujaza matumbo ya vigogo;wakanunua magari ya fahari na kujenga makasri mijini.
   Madarasa ya watoto wa masikini, hayana viti, meza, vitabu vya kiada na ziada. Wengine hukalia mawe na matofali. Walimu wamekwenda zao.
  Hawa walimu wako katika vyumba vyao vya kupigia soga vinavyoitwa ofisi za walimu; wengine wanadiriki kucheza bao, karata n.k
  Walimu wengine wako kwenye biashara zao za baa na vilabu vya ulanzi, wanzuki, mataptap na hata pombe haramu ya gongo, kwa sababu wanasema mishahara haiwatoshi.
   Walimu wengine wa kike wanafuma vitambaa vyao madarasani, wanauza vitumbua vyao, maandazi, karanga, kashata n.k saa za masomo.
  Ni nadra kumkuta mwalimu akifundisha kwa moyo kama zama za Mkoloni.Wakaguzi wenyewe hawafiki shuleni, hadi zitolewe taarifa na walimu waandae mbuzi na sufuria kadhaa za wali.
   Laiti Bwana Mkubwa, Albert Mnali angepandishwa cheo kuwa Mkaguzi wa Elimu, labda wangeogopa na kuingia madarasani.
  Ni kama walishagoma kufundisha siku nyingi, ingawa tulitangaziwa juzi kwamba, sasa watagoma kwelikweli.
   Siku hizi mwanafunzi akiwa mstarini, aghalabu hutangaziwa kwamba,
  “Kesho msipoleta hela ya Ankara ya maji, umeme, mshahara wa mlinzi, hela ya ubani ya mwalimu kufiwa shemejie, ya upotevu wa kitabu n.k mtakiona kilichomnyonyoa kanga manyoya”
  Hata ripoti za mtihani wa mwisho wa mhula hatupewi hadi wazazi tulipe pesa za mwalimu.
   Nachukua nafasi hii kuwahoji wanaharakati wa Haki za Watoto: Hivi, ukaburu unaovuka unyama mithili ya ule wa Soweto , siyo huu wa watoto vijijini kwetu kukalishwa mavumbini tangu saa 2.00 Asubuhi hadi saa 9.00 Alasiri?
Hawa wanaofanya hujuma,husaidiana na makaburu na wakoloni mamboleo kuididimiza Afrika.Zama hizo walishirikiana na majasusi wa Marekani(CIA) na makaburu(BOSS) kuhujumu uhuru wa Afrika,leo ni uhuru wa masikini unaohujumiwa.
   Watoto wanaketi mavumbini bila mwalimu kuingia darasani, na hakuna anayejali. Vijijini, wanafunzi wa shule hizi hubebeshwa majembe begani ili kulima mashamba yakiwemo ya walimu.
 Hawa, ni mithili wa manamba wa mashamba ya mkonge Tanga, enzi za Jarumani. Watoto wakiwemo wa darasa la kwanza, hubebeshwa mizigo, matofali, vyuma n.k utadhani guta au matrekta.
  Ukiuliza, unaambiwa ni mradi wa shule wa kupatia chaki, daftari, kalamu ya mwalimu n.k
 Hivi serikali inapotutoza kodi sisi wazazi, kwa nini watoto wetu wakabebe mizigo kama makuli wa Bandari ya Dar es salaam?
  Je, hali iko hivi katika shule za masikini kwa sababu watoto wa vigogo wao husoma International schools? Watoto wao husoma Uganda , Kenya , Uingereza n.k wakati elimu ya hapa ilishavuugwa.
  Kila siku utasikia migomo ya walimu, wakati hakuna anayehangaika na migomo ya watoto wa masikini wanaobebeshwa mizigo wakati wa vipindi, na kulimishwa mashamba, achilia mbali kuketishwa mavumbini.
  Kila kunapokucha, watoto ni amri moja ya “Majembe beganiii weka!!”
Utadhani watumwa, au wafungwa huko Robben Kisiwani. Ukiuliza kulikoni? Unaambiwa ni miradi ya shule maana serikali haijaleta fedha za chaki, kalamu n.k
   Sasa, mwalimu anapohamishiwa kituo kingine cha kazi, hawa wanafunzi hugeuzwa malori na maguta ya kubebea samani za mwalimu hadi kituo kipya cha kazi. Sijui fedha za uhamisho huenda wapi?
  Huu ni unyanyasaji na ukaburu wa hali ya juu sana , watoto chini ya miaka 17 kulimishwa mashamba ya walimu na wana vijiji.
  Tazama sare zao za shule, utaona hawa  watoto wana matatizo. Wamegeuzwa malori ya kusomba samani za walimu wa Prof. Jumanne Maghembe.
 Hapa lazima niondoe shilingi katika bajeti ya Waziri wa Elimu , hadi atakapokubali kutangaza marufuku wanafunzi wa shule za msingi kulima vibarua na kubeba mizigo kama matofali, kuni, samadi n.k
  Naam, walimu huwalazimisha watoto wa kike kuwatekea maji majumbani mwao, kuwapigia deki, kutwanga nafaka na kuwatandikia vitanda!
  Huko majumbani mwa walimu, watoto wa kike hubakwa na kugeuzwa vimada, walimu ‘mafataki’ huwanyanyasa watoto, hadi wazazi wanapolalamika walimu hulindwa katika mbawa za maofisa elimu na maofisa wa wizara, wasichukuliwe hatua.
  Kama Msumeno unasema uongo, Waziri husika aende kijiji cha Nyawa, katika Shule ya Msingi ya Nyawa A aulize kisa cha wasichana watatu kutorokea Mwanza,miaka michache iliyopita
   Bila shaka ataambiwa hadithi za mwalimu kubaka wanafunzi na kulipa mahali ya shilingi 100,000 ili aoe mwanafunzi chini ya umri wa miaka 16. Je, huu si ukaburu? Amepewa adhabu gani? Walimu wanawapa ujauzito wanafunzi, na kuishia kuhonga na kurejeshwa kazini.
  Mwisho, kama hakuna ukaburu Tanzania , basi serikali iseme leo kwamba watoto wa masikini vijijini ni marufuku kuketi sakafuni au mavumbini; kasha kwamba ni marufuku kuwahamisha walimu wao au kulima mashamba ya walimu.
  Basi serikali itamke tangu sasa kwamba walimu lazima waingie madarasani na kufundisha kila kipindi, hata bila kutishiwa na akina Albert Mnali.
   Kama Tanzania kuna usawa na umoja, basi serikali leo itangaze kwamba, watoto wa vogogo nao watasoma shule kama za Saragana, Rusoli, Bugoji, Kanderema n.k
 Na kwamba ni marufuku kigogo kupeleka watoto wake kusoma Uingereza na Afrika Kusini!
  Kama hili halifanyiki, ndiyo maana shule za maskini ni mavumbi tupu, hakuna kitabu wala dawati.Hii nini kama siyo Soweto tu?
Wakati huo,Marekani iliwaunga mkono Makaburu wa Afrika ya Kusini,kuikandamiza demokrasia na haki za binadamu.Hata sasa wanaofanya hivi hapa Tanzania na Afrika ni makaburu na wakoloni mamboleo ambao hatunabudi kuwapinga.
 Mungu wabariki watoto wa masikini.
     0786-324 074



No comments:

Post a Comment