Monday, December 31, 2012

MWANZA NJAA KALI BWANA

MWAKA 2012 umepita, umefika mwaka mpya 2013. Hurree!
Lakini…cha moto tutakiona!
 shida ni zile zile,matazizo yale yale ya miaka yote. Katika jiji hili kuna hatari kubwa kiuchumi.
Ripoti iliyotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuhusu Umasikini na Maendeleo ya Watu,mwaka 2011(Poverty and Human Development Report 2011) iliyotolewa Mei  mwaka jana 2012, imesema sekta ya uvuvi nchini imeporomoka kwa kiwango cha kutisha.
Wakazi wa Mwanza ni wavuvi; naam wafanyabiashara wa samaki.Asilimia kubwa ya wakazi wa mji hupata kipato chao kutokana na samaki.
Sasa,  “ Poverty and Human Development Report 2011” inasema, nchini Tanzania sekta  ya uvuvi imeporomoka kutoka asilimia 6.7 mwaka 2004 hadi asilimia 1.5 mwaka 2010.
Ripoti hiyo inasema, hiki ni kiwango cha chini sana kulinganisha na kingine chochote katika muongo mmoja uliopita.
Sababu za sekta hii ya uvuvi,hususan katika Ziwa Victoria kuporomoka ni uvuvi haramu:makokolo,uvuvi wa sumu hata dawa za kuoshea maiti,vilipuzi majini na usafirishaji  wa magendo ya samaki na mazao yake nje ya nchi.
Uvuvi wa sangara wadogo umekuwa ukifanywa hata na viwanda vya kusindika samaki,hadi wakati Fulani,John Pombe Magufuli aliwaposimama kidete,wakaogopa kidogo. Nyavu haramu yakiwemo makokolo hukamatwa hapa na kuuzwa pengine na hao maofisa uvuvi.
Wakenya waliwahi kukamatwa wakivua samaki katika visiwa vya Mwanza na Sengerema.Walipovua walisafirisha samaki pasipo kulipa ushuru na tozo nyingine.Wazawa wa eneo hili hutozwa tozo anuwai, hadi wamefilisika na kushindwa kushindana na wageni hawa katika soko.Weshindwa kurejesha mikopo katika taasisi za fedha,wamefilisika.
Matokeo yake, wageni kutoka Shirikisho la Afrika Mashariki(EAC)sasa wanamiliki soko la samaki,wana mitaji mikubwa,nao kufuatia ulegelege wa Mamlaka za serikali,wanavua visiwani na kusafirisha samaki nje,pasipo kulipa kodi na ushuru.
Wakazi wa Mwanza wanafukuzwa pole pole katika soko,wanashindwa kushindana kwa sababu ya mitaji yao kuwa midogo. Hiki ndicho kilichosemwa katika Ripoti hiyo.
Tanzania,kipato cha familia kimeporomoka,kutoka asilimia 18.7 hadi asilimia 16.6. Inasemwa kwamba Pato la Mkazi wa Mwanza ni shilingi 800,000 kwa mwaka.Ni kama shilingi 2,200 tu kwa siku.
Hii ni kusema kwamba,familia nyingi katika Jiji hili,hushindia chai,andazi moja la mitaani ama hupa mlo mmoja kwa siku.Maisha ni magumu katika Jiji hili,kuashiria maangamizi-Financial  Doom!
Vijijini, kilimo hususan cha pamba kimekufa,tunaposema, “Mtikisiko wa Uchumi(Global Economic Crisis) sasa ndiyo huonekana Mwanza.Majogoo yameshindwa kuwika alfajiri,mbwa hawabwekei tena adui.
Mfumuko wa bei umepanda kutoka “Single Digit” yaani kutoka asilimia chini ya 10(mwaka 2008) hadi asilimia 12.1 mwaka 2009. Hata leo hakuna nafuu ya maisha.
Chakula huuzwa bei ghali.Mwanza huletwa ndizi kutoka Uganda(za Bukoba zimepatwa Ukimwi wa migomba!)Mchele unauzwa kwa zaidi ya shilingi 2,000 kwa kilo,nao mwingine feki,umechanganywa na viazi mviringo!
Mwanza, viazi mviringo huletwa kutoka Molo, kule Misitu ya Mao,Jamhuri ya Kenya.Huku walishafyeka misitu hadi mvua zimekoma kunyesha.
Leo, katika kila familia kuna nakisi(deficit) ya Bajeti. Utaona Siku kuu za Noeli na Mwaka Mpya watoto wakiishia kula maembe.Mwanza,Shinyanga na Mara, Desemba uliopita, ni msimu wa maembe.
Tanzania Bara ina eneo la kilomita za mraba 881,000. Hatuitumii ipasavyo,badala yake tumeanza kuiuza kwa wawekezaji,ili walime sisi tununue kwao!
Watani zangu Wahaya,wameuza ardhi huko Bukoba na huzidi kuingia Jijini Mwanza na kununua Pikipiki,ili kufanya biashara ya ‘Bodaboda’.Kila mahali ni pikipiki,ni kelele za ving’ora,ni fujo.Mwanza ni Jiji la kelele utadhani,Rome,Italia.
Umeme unakatika kila wakati. Maji yamepungua Mtera,sijui Kihansi. Biashara za vinywaji baridi ziko mashakani.Watu wamefyeka misitu ili kuchoma mkaa. Jangwa la Kalahari,lililopo Kusini,na lile Sahara lililoko Kaskazini,limekuja kukutana huku Ziwa Victoria,sasa mvua imekoma kunyesha jangwani-Njaa!
“Hydropower” inayopatikana sasa ni asilimia 55 tu nchi nzima,Mwanza ni zaidi. Hata mitaa muhimu  ya ofisi na viwanda,hakuna umeme. Siyo mgawo, tuseme ukweli umeme hakuna huku.Unakatika zaidi ya dazeni kutwa.
Matokeo yake,uhalifu umeongezeka.Kesi 567,288 ziliripotiwa nchi nzima mwaka 2009.Ziwa Victoria limevamiwa na majambazi wenye silaha.Mwaka 2010 kesi zilikuwa 543,358 nchi nzima. Hii ni kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alipotoa hotupa ya Bajeti ya 2011/2012.
Kufuatia hali hii,Mwanza kuna machangudoa, “Commercial Sex Workers” lukuki,na ukija mgeni ukawakurupukia,utapeleka habari kwenu.Wengine ni wakwapuzi wa hatari.
Mtunzi wa Filamu ya Darwin’s Nightmares,Hubert Sauper alisema,machangudoa wa Mwanza hujiuza kwa Dola moja tu ya Marekani,kwa Wazungu,hasa wale marubani wa madege ya Kirusi waliofika Mwanza zama hizo kuchukua minofu ya sangara.
Machi 24 mwaka 2005, Ilyushin 76 ya mizigo, ya Shirika la Air Trans Inc, la Moldova huko Ukraine, ilianguka Ziwa Victoria, na kuua wafanyakazi saba wa ndege hiyo na rubani
.Wote walikuwa raia wa wa mataifa ambayo zamani  iliyokuwa Jamhuri ya Kisovieti: Belarus, Russia, Moldova n.k
 Ilikuwa ikiruka kutoka Mwanza, ikiwa na zaidi ya tani 50 za minofu ya sangara,kutoka viwanda vya Mwanza. Ilikuwa safarini kwenda Croatia,kupitia Benghazi(Libya) na Osijek.
 Visanduku vyeusi(Black Box) Viwili vilipatikana majini:
Cockpit Voice Recorder,kinachonasa sauti na Flyght Data Recorder,viliandikwa Kirusi,vikawashinda wataalamu wetu hapa kubaini chanzo cha ajali.
Bado nayakumbuka majina ya Warusi(waporaji wa minofu yetu ya sangara) waliozama Ziwani na dege lao na kufariki dunia katika ajali ile: Znak,Kapteni wa ndege na raia wa Belarus, Nesterenko,Nikolaev, Pabaruyev, Markevich,Liakh,Pulin na Pereglida.
 Nataka nikwambie msomaji. Dege lile lilizidisha uzito wa sangara wetu.
Wenye viwanda walikula njama kuzidisha uzito ili kuwakwepa maofisa wa serikali wa Forodha ama Mamlaka ya Mapato(TRA), wasijue ni kiasi gani cha sangara walisafirishwa kwenda Ulaya,ili tusilipwe mrahaba stahili.
Tanzania inaibiwa sana rasilimali zake.
Wenye viwanda vya samaki walihaha pale uwanja wa ndege,wakati wa ajali ile ya Ilyushin 76.
Nilikuwepo wakati Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Peter Toima Keroya, alipowaambia waandishi wa habari kwamba uwanja wa ndege wa Mwanza haukuwa na tatizo hadi ndege ile itumbukie ziwani wakati ndege inaanza kupaa.
     Hapa kuwa na mvua siku hiyo, maana mvua ikinyesha uwanja huo hujaa maji.

“Runway ni nzuri…'standard' ni ya kimataifa. Ubalozi wa Urusi, wataalamu kutoka Moscow na Moldova wa Air Accident Commission,watakuja kuchunguza chanzo cha ajali”, alisema Kaimu Mkuu wa mkoa wa Mwanza wakati huo.

Siyo madege ya Ilyushin 76 tu yaliyokuwa yakitua Mwanza kusomba samaki,hata BOEING 707, DC-8 ambayo katika ‘documentary’ ya Darwin’s Nightmare marubani walisema walitangulia kushusha silaha katika nchi za migogoro,kabla ya kutua Mwanza na kupakia sangara,huku wakizidisha uzito ili kukwepa kutulipa mrabaha.
Kitendo cha Wazungu kuleta silaha na kuondoka na  sangara wetu-Guns For Fish –kilisemwa na marubani hawa kwamba wakati nyakati za Krismasi na Mwaka Mpya, KAMA HUU, Watoto wa Ulaya walipelekewa samaki, zabibu,dhahabu na almasi, watoto wa Afrika waliletewa Automatic Kalashnikov 47(AK-47) ili wauane! Aibu.
Ulaya kuna shibe,kutokana na sangara za zabibu za hapa kwetu,Afrika kuna njaa,kuna vita,maandamano na migomo!

Mnofu  wa sangara aliyesindikwa wenye uzito wa Gramu 200-400 tu, uliuzwa kwa euro 12.9 ambazo wakati huo zilikuwa sawa na shilingi 18,800 za hapa.
 Hii maana yake ni kwamba, ‘Fillet’ ya sangara yenye uzani wa kilo moja iliuzwa Ulaya kwa zaidi ya euro 38 ambazo zilikuwa sawa na shilingi za hapa  Tanzania 58,050 hivi.

Wakati kilo moja ya sangara inauzwa Ulaya kwa takriban shilingi 60,000, mvuvi alilipwa kati ya shilingi 1,200 na 2,000 kwa kilo ghafi.
Kilo mbili za   sangara ghafi huzaa kilo moja ya Filleti.
Kwa hiyo, mvuvi alilipwa kati ya shilingi 2,000-4,400/= wakati Mzungu akiuza kilo moja ya Filleti kwa takriban shilingi 60,000.Siku hizi euro moja ni shilingi 2000 za Tanzania.
 Sangara wa Tanzania wanawatajirisha Wazungu!!
Mwaka 2003 Tanzania iliuza nje minofu(Fillet) yenye thamani ya euro milioni 100 sawa na shilingi za hapa bilioni 146.8.
Tanzania pekee iliuza karibu asilimia 60 ya sangara Ulaya.
Samaki wamekwisha,njaa ingalipo Musoma, Bukoba na Mwanza, inatishia uhai wa wananchi,wakiwemo wavuvi.
 Masoko makubwa ya sangara Ulaya yalikuwa Ubelgiji, Uholanzi,Ufaransa, Uingereza  hadi Marekani, ni Hukumu ya Ulimwengu,kwamba Tanzania iliwauzia Wazungu hawa chakula(samaki) wakati watu wake wakiwa na njaa-wakila ‘mapanki’.
 Tujisaili: Kama kilo moja ya sangara Ulaya iliuzwa kwa euro kama 40 ambazo kwetu hapa zilikuwa kama 60,000 hivi, kwa kijipande,ilikuwaje wavuvi wetu walipwe 2000 hadi 4,000 tu? Kwa nini Watanzania wananyimwa ajira viwandani humu, na wanaoajiriwa wanalipwa kiduchu,kulinganisha na wageni?
Wageni hulipwa maradufu kuliko wazawa..kisa,hawajui Umombo! Halafu wabishi,wazembe!

Wazungu waliooneshwa katika Filamu ile ya ‘Mapanki’ walisema Weusi hawataki kazi,hupenda kukaa tu vijiweni, “These black people do not work”!
 Tuna akili mgando,ndiyo maana Dawin’s Nightnmare, ikatushauri kutazama Biblia(Marko 6:34-44) kwamba Yesu aliwalisha zaidi ya watu5,000 kwa visamaki viwili na mikate mitano tu, wakala wakashiba na kusaza vikapu 12!
 Sisi Tanzania tulikuwa na sangara wakubwa(siyo visamaki) wangapi?
Tuna dhahabu kiasi gani? Almasi kiasi gani? Tuna tanzanite,ruby, wanyamapori,milima mirefu, mabonde, mito,maziwa, ardhi yenye rutuba na fusa tele!
 Tumwite Yesu wa Nazareti aje mioyoni mwetu na mioyoni mwa viongozi wetu ili waache wizi na ubinafsi ili kuwatumikia watu kwa uzalendo,ubunifu na upendo.
 Nchi tajiri Tanzania inakuwaje na raia masikini?
Kitu hiki kinaitwa The Shame of Poverty in the midst of Plentiful-aibu ya umasikini katika wingi wa rasilimali?
Tutakuwaje na nchi tajiri ya rasilimali,halafu tukawa ‘Highly Indebted Poor Countries’(HIPC) wakati sangara wetu wanatumbukia ziwani?
 Mchanga wa madini unatumbukia baharini?
 Tuna Mlima Kilimanjaro, madini hata tuna uranium lakini hatuna umeme! Mwanza tuna ziwa Vitoria,lakini twafa njaa!
Tuna mbuga za Serengeti,lakini twafa njaa-Hii ni HUKUMU YA ULIMWENGU!
 WWW.congesmrambatoday.blogspot.com
0786/0754-324 074





No comments:

Post a Comment