Tuesday, December 11, 2012

serikali ilivyobwabwaja kuhusu sangara kutoweka

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, alisema mwaka 2007 kwamba, sangara walioliingizia Taifa mabilioni ya fedha za kigeni, sasa wametoweka.
 
  " Wanapungua kwa kasi sana . Kama hatua za dharura hazitachukuliwa, watakwisha; wananchi watateseka kwa kukosa kipato. Viwanda wa samaki vitafungwa na kuathiri mapato ya nchi na ajira muhimu." Alisema Prof Maghembe, mwaka huo 2007
 
    Prof. Magembe, ambaye alikuwa akifungua kikao-kazi kwa viongozi wa mikoa na wilaya kuhusu uvuvi endelevu Ziwa Victoria , Juni 11 mwaka  2007 katika Ukumbi wa Chuo cha Benki Kuu Mwanza, ameonya kuwa maisha bora kwa Watanzania hawa yanaweza kuwa pwaji, ama porojo tupu.
   Lishe kwa wakazi milioni 30 wanaozunguka ziwa hili, wa Tanzania , Kenya na Uganda , itaporomoka; wakati fedha nyingi zikiwemo za kigeni, zitakosekana. Prof. Maghembe aliagiza, angalau ifikapo Juni mwaka 2007 ufanywe mkakati kuhakikisha sangara waliobaki wanazaa japo uzazi mmoja tu!
    Akasema, kitu kimoja muhimu sana , ambacho ni muktadha wa makala hii leo: Kwamba, bila kufanya mkakati wa kuepusha sangara ama samaki kutoweka Ziwa Victoria , Tanzania haitaepuka ‘Hukumu ya Ulimwengu’ kwa kuruhusu rasilimali zake wakiwemo sangara, kutoweka, na hivyo maisha ya watu wake kuathiriwa vibaya.
    “Hili, inabidi litimie. Vinginevyo, hatutaepuka hukumu ya Ulimwengu kwa kuruhusu rasilimali hii kutoweka, na hivyo watu wetu kuathirika vibaya”, alisema Profesa Maghembe.
   Aliweka kipindi cha nusu mwaka, kuhakikisha taarifa ya kazi inatolewa. Kwamba jambo hili si muhali; hivyo kushindwa kulitekeleza ili kuondoa kitisho hiki si chaguo la serikali yetu.
    Kwa upande mwingine, ‘Hukumu hii ya Ulimwengu’ aliyosema Prof. Maghembe, ilikwisha tolewa na Hubert Sauper, yule Mtunzi wa Filamu ya tashtiti, ya Mapanki(The Darwin’s Nightmare), serikali ikabisha!
   Kwamba, sangara wa Ziwa Victoria walikuwa wakiliwa Ulaya, wakati wazalendo wa nchi hii wakiambulia vijisenti kidogo vya kikunjajamvi, wakati wengine wakiambulia vichwa na mifupa-mapanki!
  Jinamizi la Darwin;Charles Robert Darwin (1809-1882) lililosimuliwa na Hubert Sauper, kwa njia ya kejeli, miaka michache iliyopita, kupitia filamu iliyomfedhehesha hata rais wetu, lilikuwa onyo tosha.
   Onyo kwa serikali yetu kuwamaizi Pwagu,(wezi na wadanganyifu), Pwaji(wapiga porojo) na Pwaguzi(wajanja zaidi kuliko Pwagu), waliokuwa wakikomba sangara wetu na kutuacha  masikini.
     Filamu hii iliwataka Watanzania kuondoka usingizini mara moja na kuepuka kugombea ubwabwa kidogo katika sufuria chafu, kula mapanki yenye funza, na kunywa pombe haramu ili kupata tafaraji, baada ya kuvua sana na kuuza samaki wengi sana kwa  Pwagu, yaani wakala wa   Pwaguzi, bila faida!
   Watanzania tulionywa na filamu hiyo kuwa na akili; yaani kuvua kwa tija, badala ya kuvua sana tukiishi katika makambi mithili ya manamba, ambako wavuvi huishia kufa kwa Ukimwi, na  dada zetu huishia kuwa machangudoa wanaopigwa ‘kipopo’  mithili ya wezi, na Wazungu kwa ujira wa dola dola 10 tu.
   Athari hasi za utandawazi, muktadha wake ni pamoja na kugombea maisha(struggle for existance); ni harakati zinazowafanya viumbe dhaifu kushindwa mapambano; na hivyo kuishia kuliwa mithili ya mchwa, panzi na kumbikumbi.
   Falsafa ya ya Charles Robert Darwin, mwanasayansi maarufu sana wa Kiingereza(alizaliwa Feburuali 12 mwaka 1802 na kufa Aprili 19, mwaka 1882) iitwayo Darwinism, huonya kwamba, katika maisha viumbe dhaifu ikiwemo mimea, abadan havishindani na vyenye nguvu.
    Katika zama hizi za utandawazi, mataifa dhaifu kama Tanzania ,  hujikuta yakinyang’anwa chakula, maji, hewa na mwanga wa jua, ili kuyapisha yenye nguvu kustawi.
    Tanzania kama mmea, itanyauka baada ya kuzongwa na magugu(Super powers), au baada ya kutafunwa kama sangara anavyowatafuna samaki wadogo, ama kama simba anavyowatafuna swala,pofu, nyumbu na palahala porini.
   Kitu hiki, ndicho Darwinism; yaani kwamba wenye kupona ni wenye nguvu tu(survival of the fittest).
     Kitendo cha sangara wetu kuuzwa Ughaibuni kwa vijisenti kidogo na kuwalisha Wazungu na Wahindi huku Watanzania wakihangaika kwa njaa kali, ni athari yakinifu za utandawazi unaoruhusu wakubwa kuwatafuna wadogo.
     Yesu wa Nazareti aliwalisha watu zaidi ya 5,000 katika kijiji cha Bethsaida kama miaka 2010 iliyopita, kwa visamaki viwali vidogo, ukilinganisha na sangara wa Ziwa Victoria, na mikate mitano.
   Katika Darwin’s Nightmare, muujiza huu unaosimuliwa katika Injili ya Mtakatifu Luka 9:10-11 na Marko 6:34-44 umeonyeshwa.
     Bila shaka, muujiza uliwekwa ili kuwakumbusha Watanzania kwamba, kama Yesu aliwalisha watu hao(walihesabiwa wanaume pekee, bila wanawake na watoto) kwa visamaki viwili; wakala hadi wakasaza vikapu12, Watanzania hushindwaje kujilisha kwa mabilioni ya sangara, dhahabu, almasi, tanzanite, ruby,  wanyamapori, misitu,shaba, pamba, kahawa, katani, korosho na rasilimali zingine anuwai?
 Kwa upande mwingine, hofu ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Maghembe, kwamba samaki wetu(si visamaki) watatoweka na kuwafanya wananchi kuathiriwa vibaya, ni sawa na kilio cha uchungu kuashiria maombolezo ya taifa.
    Sauper, alitaka kuwasagua Watanzania, tena kuwagutua kwamba umasikini na njaa yetu wakati sangara mabilioni wakitoroshwa Ulaya na akina Pwagu, bazazi, dumizi na pwaguzi kwa mrabaha kidogo, ulikuwa umbumbumbu.
    Hata rasilimazi nyingine kama madini, wanyamapori na mazao ya kilimo hutoroshwa hivihivi na ma-Pwagu, Pwajizi na mapwaguzi, pasipo sisi kunufaika na chochote. Sisi ni ng’ombe wa maziwa-watu wa kukamuliwa hadi tone la mwisho la damu.
    Pwagu, Bazazi na Pwaguzi wanavyowanyonya wavuvi. Wanasomba sangara kwa ujira kidogo.
    Hushirikiana na Maofisa uvuvi,polisi, maofisa wa Forodha, TRA, na hata baadhi ya Mawaziri husafirisha sangara kwa magendo!
Kama Profesa Maghembe na  aliyekuwa Mkurugenzi wa Uvuvi,Geoffrey Nanyaro walikuwa hawajui, shime wamaizi kuwa sangara wetu hukombwa na'pwaguzi’ kwa ujira kidogo wanaolipwa akina Pwagu!
    Katika biashara hii, wamo bazazi na dumizi wanaojipendekeza kwa Pwagu, ili kujipatia makombo!
    Naam. Hapa, Tanzania inaliwa na kubakizwa mifupa mitupu-mapanki. Mapanki nayo huuzwa nje yakaliwe na kuku, wakati Watanzania wakibaki  kugombea fadhila na chakula cha wahisani.
    Masikini wavuvi wanapofikisha sangara kiwandani, huambiwa na Mapwaguzi kwamba ni ‘reject’ kisha huambulia kipeto na kuondoka na njaa yao.
   Kitengo cha samaki (Globefish)cha Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa(FAO), Agosti mwaka jana kilisema kwamba sangara walikuwa wakitoweka kwa kasi Ziwa Victoria.
   Ni taathira kwa Watanzania watakaobaki hawana chakula, wakiomba msaada Ulaya na Marekani, ili kujiepusha kupotea katika uso wa dunia. Tunaambiwa Watanzania huambulia milioni 500 kwa siku kutokana na biashara ya samaki kila siku
     Kwamba kila mwaka wavuvi na wachuuzi wa samaki hupata sh. Trilioni176.
Kwa mwaka Wazungu hutafuna minofu maelfu ya tani kutoka Tanzania , wakati samaki wao wakiachwa akiba.
Vya walevi huliwa na mgema.
    Wavuvi wadogo leo husukumiwa laana ya kusababisha sangara kutoweka; kwamba wanavua kwa kutumia nyavu haramu. Hizi nyavu haramu hukamatwa hapa na maofisa uvuvi, kisha huuzwa pale, baada ya kuchoma  moto chache tu, mbele ya polisi na waandishi wa habari!
    Nyavu au makokoro hayo ya polisi na maofisa uvuvi ndiyo yanayoharibu mazingira ya ziwa na mazalia ya samaki.
 Leo,Maofisa wanadanganywa kwamba wavuvi haramu ni wananchi vijijini! Wakale wapi sasa?
Samaki wawili wa kitoweo wanapunguza samaki?
    Sangara wadogo wanaosafirishwa nje ya nchi, wanavuliwa na nani kama si na hao maofisa uvuvi na ndugu zao?
     Kwanini wasikamatwe? Watanzania masikini wanaovua bila leseni, huvua tani ngapi kama si kitoweo? Wanayuga-yuga kuepuka mhali, ama njaa inayowakabili. Kwanini akina Pwagu na Pwaguzi wanaachwa kuvua na kusafirisha  mamilioni ya sangara kwa magendo?
     Tatizo si wavuvi wadogo, ni mapwagu, mabazazi,dumizi na pwaguzi wanaokomba samaki Ziwa Victoria na kuwauza nje kwa magendo, lakini hawakamatwi. Vigogo, wakiwemo hata baadhi ya Mawaziri wana vikampuni hewa, wanapewa mgawo wao na akina Pwagu na Pwaguzi.
   Waziri Maghembe anawataka wabadilike! Waache kuimumucha Tanzania ? Hizi ni porojo, pwaji na soga! Waondolewe katika madaraka, tena wafilisiwe. Je, viongozi watazinduka? Wataweza? Shime wawafunge mikatale ili kuinusuru Tanzania.
    Wanao ubavu wa kuwakomesha akina Bazazi, pwajizi, pwagu na pwaguzi wasilikaushe ziwa Viktoria? Labda.
   0754 324 074
   0715 324 074.
 

No comments:

Post a Comment