Friday, December 28, 2012

NUSU KARNE YA UHURU WA AFRIKA

Mei 25 mwaka huu, wa  2013 Afrika itaadhimisha miaka  50 ya kuanzishwa kwa Umoja wa Nchi huru za Afrika(OAU), mamilioni ya watu wake wakiwa bado maskini sana , na wengine wakilazimika kula mbwa ili kujinusuru wasife kwa njaa.
  Umoja huo wa OAU, ulianzishwa Mei 25 mwaka 1963 ukiwa na kusudi la  kuinua maisha ya watu wake, baada ya kunyonywa na wakoloni kwa karne nyingi, ambao walichota nguvu na rasilimali zetu ili kujenga kwao.
   Kulingana na viongozi 30 wa Afrika, waliokutana mwaka huo wa 1963 mjini Addis Ababa, Ethiopia, OAU ilikusudiwa kuondoa mifumo ya aina zote za ukoloni na pia kupinga ubaguzi wa aina zote, ukiwemo ule ulioendeshwa na Makaburu wa Afrika Kusini.
  Swali la kujiuliza leo, miaka 50 baada ya Umoja huo( kama angezaliwa binadamu angekuwa mtu wa makamo), Waafrika tuko huru leo? Hatuwategemei wakoloni?
 
  Wakoloni walioitawala Afrika ni pamoja na Wafaransa, Waingereza, Wahispania, Wareno Wabelgiji, Wajerumani na Waitalia: Tumekoma kusubiri shuruti kutoka kwao sasa?
Kama bado, kwanini? Kwa sababu gani Afrika yenye umri wa mtu mzima mwenye wajukuu, kuendelea kuwa tegemezi kwa wakoloni tuliofukuza miaka 50 iliyopita, tukisema walitudhoofisha? Kwanini Afrika imeshindwa kusimama yenyewe?
 
   Kulianzishwa juhudi za makusudi kuhakikisha yanaundwa mashirika ya kutukomboa kiuchumi. Mashirika hayo ya kiuchumi ni pamoja na Jumuia ya Uchumi Afrika Magharibi(ECOWAS), ya Kusini mwa Afrika(SADC), Jumuia ya Afrika Mashariki inayoharakishwa kuwa Umoja wa Afrika Mashariki(EAC) n.k.
  Julai 9, mwaka 2002 Ukaanzishwa Umoja wa Afrika(AU), lengo likiwa kuona Afrika inakuwa Nchi moja, pengine yenye nguvu za Kiuchumi, Kijeshi na Kisiasa kama Marekani, United States of America.
  Afrika yenye utajiri wa rasilimali: Ardhi, mito , maziwa, bahari, milima mirefu, mabonde, watu wenye nguvu na akili nyingi, madini ya kila aina na yenye thamani n.k imesalia duni, watu wake ni fukara, tena hawana chakula, kuna maradhi ya kuangamiza kila ustaarabu wa Mwafrika, Afrika imesalia Bara la Giza , pasipo tumaini.

Afrika ina ukubwa wa maili za mraba 11,667,000(kilomita za mraba 30,218,000). Kuna milima mirefu sana kama Mlima Kilimanjaro wenye urefu wa futi 19,340 sawa na mita 5,895. Mlima Kenya una urefu wa futi 17,058 sawa na mita 5,199.
   Kuna maziwa makubwa kama Victoria, lenye ukubwa wa maili za mraba 26,418, Tanganyika (maili za mraba 12,700), Nyasa(11,430); kuna mito kama Congo , Limpopo , Zambezi , Niger , Nile , Orange , Senegal na mingine kama Kagera, Tana, Ruvuma n.k.
    Bonde la Mto Nile hujumuisha nchi za Misri,Sudan,Ethiopia, Kenya, Tanzania, Uganda, J K Congo, Eritrea, Rwanda na Burundi.
   Hata hivyo, Afrika ilikuwa ikikatazwa na mikataba ya kikoloni kama ule wa mwaka 1929 uliokuwa ukizikataza nchi hizi kutumia maji ya Ziwa Victoria ama Mto Nile kwa miradi ya kilimo, bila idhini ya Misri na washirika wake!
   Afrika kuna madini: Asilimia 70 ya  almasi yote Duniani hutoka Afrika(J K Congo, Afrika Kusini , Botswana , Namibia , Ghana , Angola na Tanzania ). Asilimia 55 ya dhahabu yote Duniani hutoka Afrika: Afrika Kusini , Ghana , Zimbabwe , J.KCongo, na Tanzania .
    Afrika kuna Nickel au shaba , kuna Tanzanite inayopatikana Tanzania tu(lakini Kenya inaongoza kwa mauzo Duniani, na Marekani , India , Japan n.k hufuata). Afrika kuna mafuta, Nigeria , Libya , Algeria na Misri na nchi nyingine kama Tanzania , Kenya , Uganda , Zanzibar ziko katika mchakato wa kutaka kuchimba mafuta na gesi.
   Kuna madini mengine kama Ruby na Uranium. Uranium yanaweza kutumiwa kwa nishati ya umeme, na wala si kutengeneza mabomu ya Nyuklia pekee. Wamiliki wa madini haya, mafuta, mbuga za wanyama, shughuli za utalii n.k ni wageni, wakoloni wetu wa zamani, Waafrika, hususan weusi ni watazamaji na washangaaji wa utandawazi na sera zake za uporaji rasilimali.
  Naam, Afrika bado inawategemea akina Tony Blair kuunda Tume zao za kuchunguza umasikini wetu, ili  ripoti iwasilishwe kwenye Mkutano wa Mataifa makubwa ya viwanda(G-8) ili isaidiwe.
    Afrika bado hakuna utawala wa sheria, hakuna amani, ni vita na machafuko kila kunapokucha. Rushwa imefanywa kama biashara. Afrika ni kichwa cha mwendawazimu, kila tapeli hujifunzia kwetu.
    Matapeli wa Ulaya hunufaishwa na rasilimali za Afrika kwa miradi ama bidhaa feki,tena hewa! Miradi hii ni kama Richmond , IPTL, Rada na mingine mingi. Afrika ina makovu usoni yanayongoja akina Tony Blair, George W. Bush pengine na Gordon Brown, ili kuyatatua!
    Waafrika, wanapopigana wao kwa wao, kama J.K Congo , Sudan , Somalia , Sierra Leon, Rwanda , Burundi n.k Umoja wa Afrika huwasubiri akina Bush kulinda amani, au kulipa mishahara ya askari wetu wanaokwenda kulinda amani! Afrika humtegemea Blair na Bush kutupa silaha ama vifaa kwenda kulinda amani.
 
  Ndio hawa hawa wakoloni wanaochochea vita Afrika, ili Waafrika wapigane, wao warejee kutubadilishia bunduki za rashasha kama A K 47 kwa dhahabu kama si almasi! Juzi, vikosi vya Pakistan vya Jeshi la Umoja wa Mataifa(UN) nchini Congo , walibabwa wakibadilisha bunduki kwa dhahabu!
  Yaani, wageni hawa wanachochea Waafrika waendelee kuuana, halafu wao wawauzie bunduki kwa kubadilishana na madini; dhahabu au almasi! Hali hii si tofauti sana na Sierra Leone , ambako Waasi wa RUF wakisaidiwa na Charles Taylor, walikuwa wakibadilisha almasi kwa bunduki. Katika biashara hii haramu, Marekani haikosi kulaumiwa.
    Wakati wa mjadala mkali wa Filamu ya Mapanki(The Darwin’s Nightmare) ilielezwa kwamba mabeberu wa Magharibi walikuwa wakibadilisha madini ama sangara kwa bunduki! Watoto wa Afrika walikuwa wakiletewa bunduki toka Ulaya ili wauane, wakati Ulaya walipelekewa zabibu, dhahabu, almasi na nyama toka Afrika.
   Naam, miaka 50 baada ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika kasha Muungano wa Afrika, bado tunawategemea akina Blair na Bush kutupa fedha za Bajeti  ili kuondopa kansa nyusoni mwetu.
   Afrika ni Bara pekee fukara sana Duniani kwa miaka 25 sasa, inajipatia chini ya asilimia moja kutokana na vitega uchumi vyake.
 Watoto milioni 44 hawaendi shule; wengine wanakufa kwa njaa na vita vinavyochochewa na wageni ili waendelee kuiba madini.
 
 Afrika, licha ya utajiri wa rasilimali zake, imeshindwa kabisa kuinua hali ya maisha ya watu wake.Kupitia sera za ubinafsishaji katika mchakato wa ukoloni mamboleo uitwao utandawazi, fursa zote wanarejeshewa wakoloni.Afrika inasubiri kupangiwa kila kitu na Taasisi za Breton Woods, kama IMF na Benki ya Dunia. Benki ya Maendeleo Afrika(ADF) haijaweza kuwakopesha watu wa Bara hili kufanya miradi ya maendeleo, ili kuondokana na utumwa wa Taasisi zilizoundwa na Wazungu, kuwarejesha Waafrika utumwani.
  Kwa upande mwingine, miaka 50 baada ya Umoja wa Afrika, bado Waafrika hawana makazi, hawana maji, hawana shule, barabara, hospitali na hata hawana tumaini kutokana na biashara kusimamiwa na wageni kote Barani.Je, umoja huu ni mtego ama mkataba wa faida?
   Mbona dhahabu, almasi, tanzanite, sangara, wanyamapori wetu na misitu, havituletei neema?
Mbona wanaturoga kwa takwimu tu kwamba tunauza nje madini?
Misamaha ya kodi, mrahaba wa asilimia karibu na bure katika madini yetu, samaki na rasilimali zingine, vitatuepusha kula nyama za mbwa ili tusife njaa
Tanzania pekee miaka ya nyuma ilikuwa ikipoteza Dola milioni 200 kutokana na misamaha ya kodi kwenye dhahabu. Afrika inadanganyika kupakwa wanja wa mdomo, wakati ina kansa ya uso?
 
 Afrika ipo miradi mingi ya wazungu ya Ukimwi, viwanda vya pombe, miradi ya wakimbizi n.k ili isifike siku sisi wenyewe tusimame kujisimamia. Kauli mbiu ya Afrika inahusu kuisimika Afrika kwa nguvu katika nafasi ya Dunia kupitia mkakati bora wa Umoja wenye nguvu.
   Juni 25 hadi Julai6 mwaka 2007, Wakuu wa Afrika chini ya Mwenyekiti wao , Rais John Kufour(Mstaafu) wa Ghana , walikaa mjini Accra , kujadili serikali ya Afrika, yaani United State of Afrika.
Itaweza kuondoa migogoro Afrika? Serikali mpya ya Afrika, itawakemea mafisadi, wala rushwa, madikteta, wezi wa kura na wanaokaidi Haki za Binadamu?
 Baadaye, Kanali Muammar al Qaddafi naye aliiongoza AU kutaka Afrika iwe na serikali moja na taifa moja, United States of Africa, leo Qaddafi amewindwa na NATO na akapinduliwa na kukamatwa kisha kuuliwa kama Osama bin Laden.
 
    Serikali Mpya Afrika, inalenga kuikomboa Afrika mara ya pili kutoka utumwa wa utegemezi na wizi wa rasilimali zetu?
Wapiga kelele wa Afrika, wazungumze juu ya ukombozi wa mara ya pili kutoka Ukoloni mambpleo,lakini wanaingia katika mtego ule ule wa ugomvi na kufarakana,fujo na mauaji sisi kwa sisi.
   Mwandishi wa makala hii hupatikana kwa simu 0754 324 074, 0786- 324
www.congesmrambatoday.blogspot.com


No comments:

Post a Comment