Friday, December 28, 2012

kaburu BOTHA NA TANZANIA YETU

KATIKA uhai wake, Kaburu Botha,  aliwahi kusema:
  “Mungu ninaye mwamini ni mkuu kiasi kinachotosha kuwa Mungu wa watu wengine,lakini aslani si Mwafrika!”
 
Alitetea nguvu za Jeshi imara la Afrika Kusini, lililokuwa na nguvu kuliko majeshi yote Afrika,kuilinda Katiba iliyokuwa ikitetea maslahi ya Wazungu ambao wakati huo walikuwa asilimia takriban sita tu, ya idadi ya watu wote Afrika Kusini.
 
 Aliamini kuwa,  mtu Mweusi, aslani hawezi kutawala nchi, ikawa na maendeleo, ikawa na amani, ila kuchinjana, dhuluma inayotokana na ufisadi uliotamalaki,  pengine na ubaguzi!
 Ni kauli mithili ya Dk Watson dhidi ya Mwafrika; kwamba hawezi kujitawala na kujiletea maendeleo; kwa hiyo eti Mwafrika hakustahili kuwa huru milele?
  Alitabiri hata vita  Afrika  nyakati za amani.
   Naam, wakati anafariki Jumanne, Oktoba 31, mwaka 2006, unabii wake ulikwisha timia; Afrika ingali inagugumia ukoloni wa aina yake, kiasi cha watu wengine kudhani, “Mungu wa P(ieter) W(illem) Botha, aliyemsukuma kutumia jeshi lenye nguvu kuendesha ubaguzi wa rangi Afrika, ni wa kweli, na yungalipo!”
Mtu mmoja kanipigia simu kusema Waafrika tumelaaniwa!
Kufikiri hivi tu,ni kuunga mkono akina Kaburu BothamDk.Watson na wajinga wengine wanaodhani Mwafrika kalaaniwa.
  Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Mzee Nelson Rolihlahla "Madiba" Mandela,alikuwa bado kifungoni enzi za utawala huo wa Botha, Rais wa kwanza Mtendaji, Afrika Kusini.Mandela, sasa ameruhusiwa kutoka hospitalini,lakini afya yake ni ya tashtiti.
        Mandela, “Gaidi” wa utawala wa Makaburu, aliyeswekwa  kizuizini tangu mwaka 1964, alikuja kupigiwa kura Aprili 1994, takriban miaka mitano baada ya P.W.Botha kuondoka madarakani, akaja kuwa Rais Mzalendo wa Tifa hilo lenye bendera ya rangi ya upinde wa mvua.
   Hili ni somo la kwanza kwa viongozi wa Bara hili kwamba, Mungu wa P.W.Botha awe amekufa, au bado yu hai, wapinzani wa serikali iliyoko madarakani hufika muda wakaaminiwa na umma  kushika madaraka ya nchi, kama haki haitendeki.
    Mandela alikuja kuachiliwa huru na De Clerk, Feburuari  11 mwaka 1990.
 Kwake, Mzee Mandela, uhuru binafsi toka gerezani haukuwa jambo la msingi kuliko uhuru wa Waafrika waliokuwa wakibaguliwa katika nyanja zote, na hivyo kusalia duni kulinganisha na Wazungu, Wahindi, Waarabu na watu wengine.
 Licha ya  Makaburu kutangaza kuwa Afrika Kusini ilikuwa  nchi Huru toka mikononi mwa Waingereza mwaka 1961.
    Mandela alikataa “Offer” ya uhuru wake, akakataa kutoka gerezani. Aliona ni heri abaki jela kuliko kupewe uhuru bandia wenye masharti kwamba  asijishughulishe na harakati za Ukombozi zilizoitwa na Makaburu, “Violence”. Yaani, kwa Makaburu, harakati za Mtu Mweusi kujikomboa ilikuwa machafuko; "VIOLENCE" na ilikuwa kinyume cha “Mungu” wa akina P.W.Botha!
    Naam, Mandela alikataa uhuru aliopewa na Marehemu P.W.Botha.
Nasi leo tunapoadhimisha miaka 49 ya uhuru tuliopewa na mkoloni, tumekataa uhuru gani bandia?
Uhuru chakupewa usiowaruhusu walio wengi kujiamulia mambo yao wenyewe, uhuru uliokuwa ukiruhusu Wazungu wachache kama asilimia sita kuneemeka zaidi wakati wengi wakitengwa na kuonwa kama majambazi katika nchi yao wenyewe!
    Mandela, hakuwa tayari kupewa kazi au cheo chochote ‘bandia’ na Weupe,wabaguzi wa rangi wa Afrika Kusini, wakati maslahi ya Weusi walio wengi yakikanyagwa chini kwa ridhaa ya 'miungu' ya akina P.W. Botha.
    Hakuwa tayari kupewa rushwa ya “nafasi nzuri” kulinganisha na watu wake. Maisha yake hayakuwa kitu cha thamani kuliko ya watu wake.
Utajiri kutoka kwa mabeberu haukuwa chochote kwake, zaidi ya unyama, usaliti, ushenzi na kutokuwa na msimamo kwa watu wake.
Mandela aliyefunguliwa kesi na utawala wa Makaburu Oktoba 9, mwaka 1963 alikubali kukosa raha za kitambo hadi watu wake wote watakapokuwa huru kujiamuria mambo yao wenyewe, bila kujali kama ingefika siku jeshi bora la Makaburu lingedhoofika, wanaharakati , weusi wakasimika bendera ya uhuru.
     Kwa viongozi wazalendo wa matumbo yao wenyewe(PATRIOTIC OF THEIR STOMACHS), watoto wao na jamaa zao, roho ya Mandela katika utawala imara wa akina P.W.Botha, ulikuwa ujinga!
 
  P.W.Botha aliyefariki Oktoba 31, miaka sita  iliyopita, alizaliwakijijini katika Jimbo la Orange Free State Januari 12,mwaka 1916.
  Katika umri wa miaka 20 alikwishahamasisha wenzake katika harakati za chama cha National.
Miaka 12 baadaye yaani mwaka 1948 aliingia Bungeni; na akapewa uwaziri.
   Mwaka 1976 alikuwa Waziri wa Ulinzi kwa miaka miwili,mwaka 1978 alichaguliwa Waziri Mkuu; na baadaye alichaguliwa Rais Mtendaji wa Afrika Kusini, Septemba 1984 hadi 1989 alipomwachia De Clerk.
    Wakati wa utawala wa Botha, angalau katiba ilianza kutambua uwakilishi wa rangi mbalimbali, wakiwemo weusi, hususan Bungeni ambako hata hao weusi waliwakilishwa kikabila.
   Kwa kiasi kidogo P.W.Botha alikataa jamii za watu weupe wa Afrika Kusini kujiona wateule kuliko weusi.
Hili ni somo kwa viongozi wa sasa wa Afrika, waliojigeuza watawala, kuacha kujenga matabaka katika nchi.
  Siku hizi matabaka yanaonekana dhahiri kwa rangi kwa cheo, kwa walio nacho-mabwana na watwana!
Naam, matabaka ya walionacho na wasio nacho. Watawala na watawaliwa.Walanchi,wananchi na wenye nchi!
  Siku zote watawala hujiona daraja la kwanza, matajiri daraja la pili, na walalahoi ambao ndio wengi katika nchi husalia watu wa chini wasio na mtetezi.
    Kama alivyofanya P.W.Botha, na wenzake waliomtangulia, baadhi ya watawala wa Afrika huthubutu kutumia jeshi kuua raia wanapoamka kupinga uonevu na unyang’au sawa sawa na unyama wa Afrika Kusini enzi za mauaji ya SOWETO , na hata mauaji ya wazalendo kama Chris Hani, na wenzao lukuki.
  Mwaka 1984 Botha aliondoka kutafuta uungwaji mkono kwa mataifa ya Magharibi, lakini akakataliwa kwa sababu ya siasa za kibaguzi.
 Leo Afrika inao viongozi kama P.W Botha, kasoro rangi, lakini wabaguzi, watesaji wa raia wao; wanaowapendelea wageni,na  matumbo yao , ndugu na jamaa zao, lakini wanapofika huko Ulaya na Marekani  hutandikiwa zuria jekundu, na kuidhinishiwa misaada!
Iko wapi roho ya mataifa iliyoiwekea vikwazo Afrika Kusini enzi za akina Botha leo?
 Kwa nini wanaowabagua raia wao katika nchi yao wenyewe, wasibaguliwe na Jumuia za Kimataifa na kunyimwa misaada leo?
   Leo viongozi huwekewa “Bingo” ya mamilioni ya Dola  za Bwana Mo Ibrahim, pindi wamalizapo mihula yao kwa kutekeleza utawala bora, wakati ni wajibu wao!
Kila Rais wa nchi huapa kufanya yaliyo mema kwa raia wao wakati wa utawala wao, sasa 'rushwa' kutoka kwa Mo Ibrahim za nini?
  Nani alisema anayetimiza wajibu apewe zawadi?
Rushwa hutolewa kwa viongozi ili wawatendee raia wao mema?
Si kwamba, kuwatendea mema raia ni wajibu; na ni haki kiongozi kutekeleza wajibu, haki na utawala bora kwa watu wake?
    Kwa nini kuweka Bingo kwa watawala wanaokula rushwa ambao ni wabaguzi sawa sawa na akina P.W. Botha, wakati Botha alipokea vikwazo kwa mataifa?
   Msomaji mmoja aliniletea ujumbe wa maandishi kupitia simu yangu ya mkononi, kwamba katika nchi zetu, raia wamegeuka mateka wa mfumo “twawala” hadi mategemeo na jukumu la  uhuru vimeachwa mikononi mwa vyombo vya habari, na si kwa viongozi mithili ya Nelson Mandela!
 Kwa mawazo ya wasomaji wangu kama huyu, japo Mandela yu hai na amemzika Kaburu P.W.Botha, lakini atakapokufa, Mandela ataondoka na roho yake.
 Hakuna tena akina Mandela, Julius Nyerere, Kwame Nkrumah, Gamal Abdel Nasser, Patrice Lumumba, Samora Machel n.k.
 Viongozi waliobaki ni "Makaburu" waliojivika koti la Vyama “Twawala” vinavyowaweka vigogo wake daraja la kwanza, wageni na matajiri daraja linalofuata, huku wakiwabagua na kuwanyanyapaa raia waliobaki!
 Kama nasema uongo, mbona vigogo watoto wao wanasoma International schools,nje ya nchi,wakati watoto wa masikini wanasoma shule za kata zisizo na walimu na miundombinu?
 Ni kama madai yale yale ya ya watoto 250 waliouawa Soweto(South West Township)Afrika ya Kusini mwaka 1976.
   Katika AWAMU  hii ya Nne, Rais Jakaya Kikwete ameahidi kuondoa matabaka haya na kuleta MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA.
     Swali linaloulizwa ni Je, Watanzania wote watakula ' matunda' ya CCM,  ifikapo 2015 au tutaambulia majani na mizizi ya sumu?
   Watanzania leo wanaomba kupata viongozi shupavu kama Waziri Mkuu wa zamani wa Singapore , Lee Kuan Yew, alivyowalinda watu wake kutoka katika Dunia ya Tatu hadi ya Kwanza .
Watanzania wanamtaka Rais Jakaya Kikwete amuige Lee Kuan Yew, ili mambo yaende!
    Kinyume cha haya tutakuwa tukitimiza unabii wa P.W.Botha, kwamba Waafrika tukipewa madaraka, hatuwezi kujitawala, badala yake tutaishia kuuana, kujilimbikizia mali , au kung’angania madaraka!
  Pengine unabii wa Marehemu Botha ulikwisha timia.  Ama, unatimia hata Ivory Coast, siku hizi.
  Tumeona watawala wa Afrika kama akina Mobotu, Idi Amini, Sani Abacha na wengine wakiwaua raia wanaopinga utawala wao ili wabakie  madarakani milele.
  Tawala zao ziliandamana na ufisadi licha ya unyama, na ubaguzi wa matabaka, huku ndugu zao wakitajirika kwa muda mfupi sana kwa fedha walizopata kwa njia za magendo na rushwa, na kuzificha hukohuko kwa hao wanaoimba wimbo wa utawala bora Afrika!
 
 Kulingana na kauli za wasomaji, viongozi wetu wanapaswa kumpinga Kaburu Botha, kwa vitendo, kwa kuendesha utawala bora kwa vitendo, 'To walk the talk' na wala si kwa vishawishi kutoka kwa matajiri, kama Mo Ibrahim kwa ahadi ya kitita cha dola za Marekani, wanapostaafu.
 
  Watanzania wanamaoni kuwa Tanzania inao Watanzania bado; ila wamekuwa wakibaguliwa na mfumo wa waliobahatika kuingia madarakani kwa njia za rushwa, ambao hutumikia zaidi njaa zao kuliko raia wanaowaongoza.
   Watanzania sasa wameanza kuhoji uzalendo wa viongozi: Kwamba kwa nini wauze mashirika ya umma kitapeli?
Kwa nini mikataba hewa?
 Kwanini kuuziana nyumba za umma kindugu, kwa madai kuwa ni ‘sera’ ya chama chenu?!
 Watanzania wa leo wanamtaka rais Kikwete kufanya mapinduzi makubwa ya kuondoa ubaguzi mamboleo ili kuwaondolea mbali viongozi magaidi waliojipenyeza katika utawala wan chi.
    Kama , Mandela alivyojitoa mhanga kuikomboa Afrika Kusini , Tanzania inawahitaji akina Mandela watakaozika fikra za akina Botha.
 Vinginevyo utabiri wa Kaburu huyu utakuwa kweli kwamba viongozi wa Bara hili hawana cha kuwafanyia watu wao, ila kuwabagua, kuwaua na kula rushwa!
 Ilifika wakati utawala wa makaburu uliokuwa na jeshi imara, ukapisha mabadiliko kwa walio wengi kujitawala wenyewe.
Makaburu mamboleo waliojipenyeza katika tawala za Afrika, iwe kimwili au kiakili, wanapaswa kupisha utawala wa watu na watu kwa ajili ya watu!
   Anapozikwa P.W.Botha, wazalendo wa Bara hili wanapaswa kupinga unabii wake ili viongozi wawe watumishi badala ya wachuuzi wa watu wao, ambao hawana tofauti na magaidi!
Je, Botha kafa na roho yake, ama roho ile ingalipo,au wangalipo  Makaburu wengine?
Je, I wapi roho ya akina Mandela, Nyerere na Lee Kuan Yew?
 Mwandishi anapatikana kwa simu 0754 324 074

No comments:

Post a Comment